- Jaribio lake halihusu kuweka rekodi mpya tu, bali kubadili mwenendo wa uharibifu wa misitu kabla haujafikia hatua ya hatari.
- Hii ni zaidi ya rekodi. Ni tamko la kile kinachowezekana pale jamii zinapoungana kurejesha mazingira.
- Mafanikio ya Antoine ni mchango katika mpango wa Kenya kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032.
Kenya wiki hii imekuwa kitovu cha harakati za kuvunja rekodi za dunia za Guinness baada ya mwanaharakati wa mazingira kutoka Canada, Antoine Moses, kuvunja rekodi yake mwenyewe ya kupanda miche 47,460 ya mikoko ndani ya saa 24 tu. Idadi hiyo ilithibitishwa Mei 1, saa 8:01, muda mfupi baada ya kukamilisha zoezi hilo.
Antoine alikuwa nchini humo kwa siku 10 kabla ya tukio hilo, ambapo alipanda miti mingine 13,600 ili kujenga stamina katika maandalizi ya rekodi mpya. “Tumekuwa Kenya kwa siku 10 zilizopita tukipanda mikoko, tukijifunza kutoka kwa jamii na kutengeneza kumbukumbu zisizosahaulika na marafiki wapya,” alisema kabla ya jaribio hilo, na kuongeza: “Baada ya kufikia miti 10,000 chini ya saa nne wakati wa mazoezi, nilijua tuko tayari kusonga mbele zaidi.”
Waziri wa Mazingira wa Kenya, Deborah Barasa, alimkaribisha Antoine na alikuwepo alipokuwa akipanda mche wake wa kwanza. Alisema: “Kenya imepata heshima kumkaribisha Antoine Moses… Jaribio lake la kijasiri la kupanda mikoko 40,000 ndani ya saa 24 katika eneo la Tudor Creek, Kaunti ya Mombasa, halimaanishi tu kuweka rekodi mpya, bali ni kubadili mwenendo wa uharibifu wa misitu kabla haujafikia hatua ya hatari. Uwepo wake unaimarisha nafasi ya Kenya kama kiongozi anayeaminika katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”
Timu iliyoratibiwa ya wanajamii, wahifadhi wa mazingira, maafisa wa Huduma ya Misitu Kenya, akiwemo Katibu Mkuu Gitonga Mugambi, pamoja na washirika kutoka Earthlungs, walimpa hamasa, wakitembea pamoja naye ili kumsaidia kutimiza malengo yake.
Awali, Antoine aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba malengo yake ni kupanda miche 35,500 ya mikoko.
“Hii ni zaidi ya rekodi. Ni tamko la kile kinachowezekana pale jamii zinapoungana kurejesha mazingira,” alisema Antoine baada ya kukamilisha zoezi hilo, mikono yake ikiwa imejaa matope.
Mchakato huo ulifuatiliwa kwa karibu na maafisa kutoka Guinness World Records pamoja na Huduma ya Misitu Kenya (KFS). Antoine pia alieleza kuwa alipanda aina mpya ya mikoko. “Leo tulikuwa tukijaribu aina mpya ya mikoko. Ni midogo na rahisi zaidi kuhudumia, ingawa pia huvunjika kirahisi, hivyo nahitaji kuwa mwangalifu ninapoipanda,” alisema siku moja kabla ya kuanza jaribio lake hilo jipya.
Hayo yanajiri wiki moja tu baada ya mwanaharakati wa mazingira kutoka Kenya, Hillary Kibiwott, kuvunja rekodi ya Antoine ya mwaka 2023 ya kupanda miti 23,060. Kibiwott alipanda miti 23,326 katika Bonde la Ufa ndani ya saa 24. Hata kabla ya Guinness World Record kuthibitisha rasmi mafanikio ya Kibiwott, Antoine alirejea tena, safari hii katika pwani ya Kenya, kando ya eneo lililoharibika la Tudor Creek, Mombasa kupanda miti zaidi.
Misitu ya mikoko ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia ya pwani na ni hifadhi bora ya asili ya kaboni duniani, ikiwa na uwezo mara nne zaidi ya misitu ya tropiki, jambo linalosaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pia ni maeneo muhimu ya kuzaliana kwa aina mbalimbali za samaki, hivyo kuwa nguzo muhimu kwa uendelevu katika utalii, uvuvi, uchumi na maisha ya jamii za pwani.
Mafanikio ya Antoine ni mchango katika mpango wa Kenya chini ya Rais William Ruto wa kupanda angalau miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032, kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kulikuwa na shamra shamra baada ya Antoine kuvuka lengo lake, huku wanajamii walioshiriki wakionyesha matumaini kwamba mpango huo utasaidia kurejesha mfumo wa ikolojia na kuboresha idadi ya samaki ambao wengi wanategemea.
Swalleh Mkamburi, mwanajamii kutoka Mombasa, alisema wamekuwa wakishuhudia mikoko ikipotea katika eneo la Tudor kutokana na uvunaji kupita kiasi. “Leo inatupa matumaini kwamba mikoko inaweza kurejea,” alisema.
Antoine sasa anasubiri uthibitisho rasmi kutoka Guinness World Records. “Mikoko ni muhimu kwa taifa letu. Inalinda fukwe zetu, inaunga mkono uvuvi, inaendeleza maisha ya watu, na ni miongoni mwa mifumo bora zaidi ya asili ya kufyonza na kuhifadhi kaboni, hivyo kuwa muhimu katika kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema Barasa.
Picha ya Bango: Antoine Moses akipanda miti ya mikoko katika eneo la Tudor, Mombasa. Picha kwa hisani ya Wizara ya Mazingira.