- Kiwango cha samaki kimezidi kupungua huku baadhi ya aina ya samaki wakitoweka kabisa.
- Kuwepo kwa maji machache husababisha joto kubwa wakati wa kiangazi na samaki hufa kutokana na joto kali.
- Uvuvi haramu unachochewa na mfumo wa kiutawala usiozingatia usimamizi jumuishi.
- Uvuvi endelevu hutegemea mfumo imara wa ikolojia ya mito, mabwawa na maziwa.
Ni Jumamosi alfajiri. Jamal, ameketi kando ya mtumbwi wake, akiwa ameshika tama, macho yake yametizama mto Kilombero ambao miaka yote umempa fahari mbele ya familia yake. Pembeni yake zimeegeshwa nyavu ambazo kwa miaka mingi zimekuwa tegemea la maisha yake, lakini safari hii zimerudi tupu.
Kwa muda mrefu uvuvi ulikuwa fahari yake kuu na chanzo cha mapato, lakini katika miaka ya hivi karibuni hali imebadilika, samaki wamepungua kwa kiasi kikubwa majini. Kimya kimya anaijuliza, ikiwa leo hakuna samaki, kesho kutwa, mtondo na mtondogoo hali itakuwaje? Mashaka haya hayamkabili Jamal pekee, bali pia wavuvi wengi nchini kote.
Kilio cha wavuvi
Kilio cha wavuvi nchini Tanzania ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yameitikisa vibaya sekta ya uvuvi kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusababisha kiwango cha samaki kupungua huku baadhi ya aina ya samaki wakitoweka kabisa.
Victor Tondelo, Mtaalamu Mtafiti wa Madiliko ya Tabianchi, aliiambia Mongabay kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zimejidhihirisha zaidi katika rasilimali za maji (water resources) hasa kwenye mito, mabwawa na maziwa.
“Kwa sababu ya kupungua kwa mvua inayonyesha na misimu inayotabirika, maji yamepungua na hivyo idadi ya samaki ambao maisha yao ni majini pia imepungua,” alieleza.
Aliongeza kuwa kuwepo kwa maji machache pia husababisha joto kubwa wakati wa kiangazi na samaki na viumbe wengine wa majini hufa kutokana na joto kali.
Uchunguzi wa Mongabay kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta ya uvuvi, ulijikita katika mikoa mitatu ya Morogoro, Iringa na Pwani. Katika mkoa wa Morogoro ulihusisha mto Kilombero, Luipa, Ruhudji na Mto Mnyera. Iringa ulihusisha Bwawa la Mtera huku katika mkoa wa Pwani, ulihusisha mto Rufiji. Mito yote hiyo ya Mkoa Morogoro huungana na kujenga mto Kilombero ambao nao huchangia asilimia 60 ya maji ya mto Rufiji.
Uchunguzi ulibaini kuwa kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kiasi cha samaki kinachovuliwa na wavuvi wadogo katika mito na mabwawa kimeshuka na hivyo kuathiri wanufaika wa mnyororo mzima wa thamani ya uvuvi wakiwemo wavuvi wenyewe, walaji wa samaki na wauzaji wa jumla na rejareja katika masoko ya vijijini na mijini.

Kupungua kwa samaki kumethiri pia uhakika wa chakula na kuwakosesha ajira baadhi ya wanawake na hivyo kuchoea umaskini katika familia zao.
Upungufu wa samaki
Tafiti zinaonyesha kuwa takriban asilimia 40 ya samaki wote duniani huvuliwa kutoka kwenye mito na maziwa yenye maji baridi ambayo hata hivyo imeendelea kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi na uharibifu wa mazingira na shughuli nyingine za kibinadamu.
Ripoti nyingine za watafiti zinaonyesha kuwa kumekuwa na upungufu mkubwa wa samaki katika Bonde la Kilombero kutokana na sababu mbalimbali hivyo kuwafanya wavuvi kuhamishia nguvu zao katika kilimo cha mazao ya chakula. Bonde la kilombero lina wavuvi wadogo wapatao 33,000 kutoka kaya zipatazo 110,000. Takriban kaya 50,000 huishi kwa kutegemea uvuvi. Wavuvi kati ya 1,500 hadi 2,000 hufanya shughuli zao katika bwawa la Mtera, wakati mto Rufiji una wavuvi zaidi ya 200 kati ya wakazi wapatao 150,000, takwimu zaidi za FAO, zinaonyesha.
Takwimu kutoka katika chapisho la Kilorwemp, zinaonyesha kati ya aina 49 za samaki zinazopatikana katika Bonde la Mto Kilombero, wavuvi hulenga kuvua kati ya aina 15 na 20 tu ambazo ni rahisi kuzipata kutokana na zana wanazotumia.
Tafiti za miaka ya nyuma zinaonyesha kuwa idadi ya samaki katika bonde la Kilombero imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, kati ya mwaka 1990 na 1999 idadi ya samaki ilishuka kwa asilimia 34.
“Kwa sasa, wavuvi wengi wanasema mapato yao yanaendelea kushuka kwa hiyo wameanza kilimo ili kufidia upungufu wa chakula na kipato,” anasema Renus Titus Mlindima, Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine wanasema kuwa takriban asilimia 64 ya wavuvi waliohojiwa katika utafiti wao, walikiri kuwa kuna upungufu wa samaki unaoendelea kwa miaka mingi.
Takwimu sahihi za uvuvi katika mito mbalimbali ukiwemo Mto Kilombero, ni vigumu kupatikana kwani wavuvi ni wadogo wadogo ambao hufanya shughuli zao katika maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia.
Mzizi wa tatizo
Katika mahojiano na wadau tofauti, Mongabay ilibaini namna mbalimbali ambazo sekta ya uvuvi imeathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi na athari nyingine zinazochochewa na matokeo ya mabadiliko hayo.

Tondelo anasema kutokana na mabadiliko haya mvua zinapungua na wakati mwingine misimu haitabiriki, hali ambayo inaathiri moja kwa moja kitendo cha samaki kuzaliana.
Aliongeza kuwa kwa vile mabadiliko hayo yanasababisha pia uhaba wa mvua, watu hujiingiza kwenye kilimo holela na kuathiri mito na mabwawa. “Wakulima na wafugaji wanafanya shughuli zao kandokando ya mito na kwenye ardhi oevu. Hii inasababisha mito na mabwawa kupoteza kina na samaki kushindwa kuishi,’’ anasema Tondelo.
Miongoni mwa mito ambayo imeathirika na hali hiyo ni Kilombero, ulioko mkoani Morogoro. Andrea Justine Mtolera ambaye amekuwa akivua samaki katika mto huo kwa miaka 42, ana simulizi ya kusisimua. Anasema, “Nimekuwa nikivua samaki katika huu mto huo tangu nilipokuwa darasa la sita, nikichanganya uvuvi na masomo. Kuna kipindi nilikuwa nikinunua samaki kutoka kwa wavuvi hapa katika mwalo wa Lipangalala na kwenda kuuza sokoni, baadaye nikaamua kuwa muuza samaki pale sokoni kwa miaka kadhaa, lakini nimerudi tena moja kwa moja kwenye uvuvi.”
“Ukweli ni kwamba maji yanapopungua ndivyo samaki wanavyopungua. Tazama zile nguzo ya daraja; pale yalipofikia maji kwa juu ndipo maji yalipokuwa mwaka jana wakati kama huu na alama ya juu zaidi ndiyo kiwango yalipokuwa mwaka juzi. Mwezi huu wa Aprili ndiyo upeo wa mvua za masika, kwa hiyo kwa sasa hakuna namna kina cha maji kitaongezeka zaidi ya hiki tunachoona,” Mtolera aliiambia Mongabay.
Dani Ling’ola, mvuvi katika Mto Kilombero katika mwalo wa Lipangalala uliopo umbali wa kilometa takriban saba kutoka mjini Ifakara, amekuwa mvuvi kwa miaka 25 na anakiri kuwepo kwa upungufu wa samaki katika mto huo.
Akieleza namna upungufu huo unavyojidhihirisha wakati wa masika na kiangazi pia, Ling’ola alisema, “Ni zaidi ya miaka kumi sasa tangu upungufu huu uanze na samaki wamekuwa wakipungua mwaka hadi mwaka. Wakati mwingine tunakuja kuvua kwasababu ya mazoea na hatuna kazi nyingine ya kufanya kwa sababu samaki wanaopatikana ni wachahche,” alieleza.

Katika chapisho lililoangalia mitazamo ya jamii kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi, wavuvi walisema kupungua na kutoweka kwa baadhi ya aina ya samaki kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi. Wakazi wa vijiji vya Mofu na Ikwambi katika Wilaya ya Kilombero nao waliunga mkono maoni hayo.
Uvuvi kutumia njia haramu
Licha ya mabadiliko ya tabianchi, taarifa zaidi zinaonyesha sababu nyingine zinazoathiri mito na mabwawa ni uvuvi wa kutumia njia haramu kama sumu, nyavu zilizopigwa marufuku na mabomu ambavyo vyote huua samaki wachanga na kuharibu mazalia ya samaki. Matokeo yake kiasi cha samaki wanaopatikana kimekuwa kikipungua pia.
Ling’ola anaunga mkono hoja kwamba uvuvi haramu ni sababu kubwa ya kupungua kwa samaki kwenye Mto Kilombero. Anadai kuwa mabadiliko ya tabianchi yangekuwa ndiyo sababu pekee basi mito mingi ingekauka na hata hii iliyopo ingekuwa na maji machache sana.
“Kwenye uvuvi haramu, watu wanatumia sumu, nyavu ndogo na makokolo ambayo siyo tu yanaua samaki wachanga bali pia huharibu maeneo ambayo samaki huzalia. Maeneo haya huchukua miaka mingi kurejea katika hali yake na kwakuwa uharibifu unaendelea siku hadi siku, hali hiyo haiwezi kurejea. Ukiua samaki wachanga na kuharibu mazalia yao, usitegemee kuona samaki wakiongezeka,” anaeleza Ling’ola.
Mtolera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Wavuvi katika mwalo wa Lipangalala aliiambia Mongabay kuwa kushamiri kwa uvuvi haramu kunachangiwa na udhaifu wa kiutawala unaofanya uvuvu halali kuwa ghali kuliko uvuvi haramu.
Sababu nyingine ya kupungua kwa samaki ni uharibu wa mazingira unaochafua maji na kufubaza mazalia ya samaki ukienda sambamba na matumizi ya njia haramu za uvuvi, (chapisho la Kilorwemp linaonyesha.
Mbolea zenye kemikali
Kilimo kinachotumia mbolea za kemikali na viwatilifu pia kinachangia uharibifu kwenye mito na mabwawa na hatimaye upungufu wa samaki. Hiyo inatokana na ukweli kuwa sehemu ya kemikali hizo hubaki ardhini na kusafirishwa na maji ya mvua hadi kwenye mito na maziwa ambako huua samaki wakubwa na wachanga.
Tafiti zinaonyesha kuwa takriban tani 800 za mbolea za kemikali na viwatilifu huingia kwenye mito duniani kote.
Chapisho kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, linataja upanuzi wa mashamba, kulisha na kunywesha mifugo kandokando ya mito na vyanzo vingine vya maji kama mambo mengine ambayo husababisha mmomonyoko wa udongo.
Kwa mujibu wa jarida hilo, udongo unapojaa kwenye mito licha ya hupunguza kina cha maji, huharibu mazalia yaliyoko kwenye kina kirefu na hatimaye kupunguza kuzaliana kwa samaki.
Julius Mhonda ambaye ni mtalaam wa masuala ya uvuvi aliiambia Mongabay kuwa Bonde la Kilombero limeshuhudia ongezeko la kilimo cha mpunga katika miaka ya hivi karibuni ambacho kinatumia mbolea za kemikali na viwatilifu.
“Baadhi ya viwatilifu na kemikali hubaki kuwa “hai” aridhini kwa muda mrefu na wakati wa masika husafirishwa kwa maji ya mvua na kuingia kwenye mito mbalimbali. Vyote hivi ni sumu kwa samaki na viumbe vingine vya majini. Samaki wasipozaliana lazima idadi inayovuliwa itapungua,” alisema.

Mwongozo kuhusu uvuvi endelevu unaonyesha ustawi wa samaki hutegemea mfumo imara wa ikologia ya mito, mabwawa na maziwa ambao ndiyo msingi wa maisha yao. Kwa mujibu wa mwongozo huo, mfumo huo ukitetereka, idadi ya samaki hupungua na baadhi ya aina ya samaki hutoweka.
Nini kinafanyika
Ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na vyanzo vingine, jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika ngani za vijiji, wilaya na hata taifa.
Renus Titus Mlindima ni Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara aliiambia Mongabay kwamba Halmashauri inafanya jitihada ya kuimarisha vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi (BMU) ili kuipa jamii fursa ya kutunza na kulinda ikolojia ya samaki na mazingira kwa ujumla na kujihakikishia upatikanaji endelevu wa samaki.
Aidha serikali ya Tanzania imeanza kuchukua hatua stahiki ili kuweka uwiano baina ya uhifadhi wa mazingira na mahitaji ya wakazi wa Bonde la Kilombero ambao wanakadiriwa kufikia 400,000.
Kupitia Mpango Jumuishi wa Usimamizi wa Bonde la Kilombero, serikali inakusudia kulinda na kuhifadhi eneo la Bonde la Kilombero ambalo ni ardhi oevu kubwa kuliko zote nchini yenye maji baridi, ili kuhimiza matumizi endelevu ya maliasili. Mkakati huu unajumuisha pia kutatua migogoro ya ardhi, kulinda ikolojia kutokana na ongezeko la shughuli za kilimo na kusimamia matumizi bora ya maliasili zilizomo katika bonde hilo.
Kwa mujibu wa mpango wa serikali wa kulinda bonde la Kilombero, baadhi ya hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kudhibiti eneo lipatalo kilometa za mraba 2,000 za bonde hilo kwa ajili ya kuhifadhi na kulinda mazalia ya samaki na shoroba za wanyama.
Kadhalika inaweka jukumu kubwa la usimamizi wa maliasili kwa mamlaka za wilaya, kata na vijiji ili kutoa fursa kubwa kwa wana vijiji kushiriki kikamilifu katika mchakato wote wa maamuzi kwa nia ya kuanzisha na kunufaika na vyanzo endelevu vya mapato.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa sera na mikakati mipya ya kuhifadhi Bonde la Kilombero inaunganishwa katika mpango wa utekelezaji wa Uchumi wa Bluu 2025 -2035 ukilenga usimamizi endelevu wa uvuvi.
Mpango huu ni mkakati unaolenga kuboresha matumizi ya maliasili za bahari na maji baridi kwaajili ya kukuza uchumi, kuboresha hali ya maisha ya wananchi, kuongeza uhakika wa chakula na kujenga ustahimilivu wa mazingira kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha Chapisho kuhusu ulinzi bonde la Kilombero linaonyesha kuwepo kwa miradi ya kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji na upandaji miti katika mkondo wa mto na kuzunguka maziwa na mabwawa.
Halmashauri ya Mlimba iliyoko Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro imetengeneza mpango mkakati 2021/2022 – 2025/2026 ili kuboresha uvuvi katika Bonde la Kilombero.
Kupitia mkakati huu, halmashauri inalenga kuhamasisha uvuvi endelevu na kuvijengea uwezo vikundi vya usimamizi wa uvuvi (Beach Managemnt Units) ili viweze kutekeleza sheria na kusimamia uhifadhi wa mazingira.
Katika hatua nyingine ya kudhibiti upungufu wa samaki na kutoweka kwa baadhi ya aina ya samaki, mashirika binafsi yamekuwa yakitekeleza miradi ikiwemo Kilorwemp yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa sheria na usimamizi endelevu wa mnyororo wa thamani wa uvuvi.
Changamoto
Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni ugumu wa kupambana na uvuvi haramu. Kwa mujibu wa Mtolera, changamoto ya kwanza katika utekelezaji wa hilo ni tozo kubwa ambazo kila mvuvi anatakiwa alipe.

“Ukiacha tozo ambazo tunatakiwa kulipa kwa mwaka, kila siku mvuvi akiingia mtoni anatakiwa kulipa ushuru wa shilingi 7,000. Anaweza kuingia mtoni akapata samaki wachache sana, kwa hiyo katika hali hiyo, anaamua kukwepa ushuru na kuingia mtoni usiku…atavua kwa kutumia sumu au nyavu zisizoruhusiwa na kuondoka na samaki wake. Ni njia rahisi ya kujipatia kipato lakini njia hii inaua samaki na kuharibu mazalia na kuathiri uvuvi endelevu,” anasema Mtolera.
Anasema kukosekana kwa ufuatiliaji ni tatizo lingine linalokwamisha jitihada za kupambana na uvuvi haramu. Kuhusu hilo anasema, “Kwa mfano mtu akishalipa ushuru huo wa shilingi 7,000, hakuna anayefuatilia kuona huyu mvuvi anavua katika sehemu gani ya mto au anatumia zana gani. Hali hii inatoa uhuru kwa wavuvi kuvua kwa namna wanayotaka kwani anajua hakuna mamlaka inayofuatilia shughuli zake.’’ anaeleza Mtolera.
Renus Titus Mlindima ni Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara ambako amefanya kazi kwa takriban miaka mitatu. Awali alkuwa Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Rufiji ambako alifanya kazi kwa miaka 12. Aliiambia Mongabay kuwa uvuvi haramu na matatizo mengine vinachochewa na mfumo wa kiutawala usiozingatia usimamizi jumuishi.
Anasema udhaifu huu ndio unaotoa mwanya wa kushamiri kwa uvuvi haramu na hatimaye upungufu wa samaki katika mito. Anafafanua, “Mimi ni mtaalamu wa uvuvi, ni afisa uvuvi wa mji wa Ifakara lakini siruhusiwi kwenda maeneo ya mto Kilombero ambayo yako chini ya halmashauri ya mji bila kibali cha mamlaka ya wanyamapori. Yaani ni kama mtu huwezi kuingia nyumbani kwako bila kibali. Sasa kwa vipi tutatoa elimu ya uvuvi endelevu? Kwa namna gani tutawashawishi wavuvi na wananchi wengine kuacha uvuvi haramu na kuwapa mbinu za utunzaji mazingira kwa ustawi wa rasilimali za uvuvi?”
Anasema ni kweli mabadiliko ya tabianchi yanaathiri upatikanaji wa samaki lakini tatizo limekuwa kubwa kutokana na kukosekana kwa usimamizi jumuishi (intergraded management) wa maliasili, jambo ambalo lingewajengea wavuvi na wananchi wengine uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Changamoto nyingine inayotajwa ni kutawanyika kwa wavuvi wadogo, hali inayoleta ugumu siyo tu wa kusimamia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali bali hata kuwasaidia ili waweze kufanya uvuvi kwa njia zitakazowafanya waweze kuihimili mabadiliko ya tabianchi. Kadhalika hakuna takwimu za kuaminika za idadi ya samaki wanaovuliwa katika bonde hilo.
Nini kifanyike
Ili kurejesha idadi ya samaki wanaovuliwa ni muhimu kuongeza jitihada za udhibiti wa njia haramu za uvuvi na kuvipa vijiji na vikundi vya uvuvi fursa ya kusimamia uvuvi kwa namna endelevu na kwa kuzingatia ubora wa mazingira, anasema Mtolera.
Picha ya Bango: Mabadiliko ya tabianchi ambayo hudhihirika zaidi raslimali za maji, yameitikisa sekta ya uvuvi nchini Tanzania kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusababisha kiwango cha samaki kupungua huku baadhi ya aina ya samaki wakitoweka kabisa.