- Maeneo yaliyotelekezwa yanapovamiwa na wachimbaji holela, mazingira hulipa gharama kubwa.
- Mvua inaponyesha, udongo husombwa na kuingia katika mito, hali inayoharibu mfumo wa ikolojia.
- Uchimbaji usio endelevu unazalisha mifumo kandamizi katika jamii.
- Sheria ichukue mkondo wake kuhakikisha urejeshwaji wa mazingira unafanyika ipasavyo.
Sekta ya madini nchini Tanzania imetikiswa na hatua ya Serikali kuzifutia leseni za utafiti wa madini kampuni 40 huku ikitoa muda wa siku 30 kwa kampuni nyingine 43 kurekebisha mapungufu yao, la sivyo nazo zitapoteza leseni zao. Wakati watu wengi wameunga mkono hatua hiyo kwa kuangalia matokeo ya uamuzi huo kwa mtazamo wa kiuchumi na uwajibikaji, watetezi wa mazingira wameibua hoja nzito kuhusu uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokea pindi leseni za utafiti zinapotelekezwa.
Waziri wa Madini Antony Mavunde, katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika katika makao makuu ya Tanzania, jijini Dodoma, alitaja mambo kadhaa ambayo kampuni hizo zimeshindwa kutekeleza licha ya kupewa onyo na muda wa kurekebisha kasoro zilizobainishwa.
Alibainisha kuwa leseni hizo zilifutwa kufuatia ukiukwaji mkubwa wa masharti, ikiwemo kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, kushindwa kulipa ada stahiki, kutotekeleza wajibu wa ushirikishwaji wa Watanzania pamoja na kupuuza miradi ya uwajibikaji kwa jamii.
“Tunashuhudia baadhi ya watu wanamiliki leseni kwa miaka mingi bila uwekezaji wowote unaoonekana. Hii si tu inapoteza fursa za kiuchumi bali pia inachochea uharibifu wa mazingira na migogoro katika jamii,” alisema Waziri.
Kwa mujibu wa waziri huyo, leseni 40 za utafiti wa madini zilizofutwa ni sawa na eneo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 900 sawa na hekari 188,163.
Uharibirifu wa mazingira
Simulizi za watu tofauti wakiwemo wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali zinaonyesha jinsi mazingira yanavyoharibiwa iwe katika hatua ya utafiti wa madini ama uchimbaji wenyewe.
“Usiku mvua ikinyesha kidogo tu… asubuhi tunakuta shimo limejaa maji na kuta zimeporomoka,” anasema Emmanuel Joseph, mchimbaji mdogo katika Mkoa wa Kimadini Mbogwe, kauli ambayo inafichua ukweli mchungu uliofichika nyuma ya harakati za kutafuta dhahabu katika maeneo yaliyotelekezwa na waliopewa leseni na serikali kuchimba madini au kufanya utafiti wa madini.

Katika maeneo hayo, Joseph aliiambia Mongabay kuwa kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaoambatana na uchimbaji usio endelevu.
Akiwa katika Mgodi wa Kanegere Na. 1, Joseph anakiri wazi kuwa kila wanapovamia maeneo yaliyotelekezwa na wenye leseni na kuanzisha uchimbaji holela, mazingira hulipa gharama kubwa.
Anasema madhara hayo yanajumuisha ukataji miti bila mpango na uchimbaji holela unaoacha mashimo yasiyo salama, mambo anayosema yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku, lakini yanayohatarisha si tu wachimbaji bali pia mifugo na wananchi wanaopita karibu na maeneo hayo.
“Mashimo mengi huachwa wazi bila kufukiwa. Mvua inaponyesha, ardhi huteleza na kuwa hatari kubwa kwa maisha yetu na ya wengine,” Joseph anafafanua.
Anabainisha kuwa huwa wanavamia maeneo yaliyotelekezwa na wenye leseni wakiamini kuwa yana uwezekano mkubwa wa kuwa na madini, lakini mara nyingi wanapokosa madini katika maeneo hayo, huondoka na kuyaacha mashimo wazi.
Mashimo hayo hugeuka mitego isiyoonekana kwa mifugo na hata binadamu. Hali hii, Joseph anasema, imekuwa ikisababisha ajali zisizo za lazima, huku ardhi ikiharibiwa na kupoteza thamani yake kwa matumizi mengine ya kiuchumi kama kilimo.
Athari hizo hazikomei ardhini pekee. Katika maeneo ya kuosha mchanga (mialo), Joseph anasema kuna matumizi holela ya maji bila mifumo rasmi ya uhifadhi au usimamizi. Hali hiyo husababisha maji hayo kusambaa ovyo, yakichanganyika na kemikali na tope, na hatimaye kuchafua vyanzo vya maji vinavyotegemewa na jamii zinazozunguka migodi hiyo.
“Hatuna miundombinu ya kudhibiti maji tunayotumia. Yanatapakaa ovyo na wakati mwingine huathiri hata makazi ya watu,” Joseph anafafanua zaidi.
Mbali na hilo, ukosefu wa huduma muhimu kama vyoo na maji safi katika hatua za awali za uchimbaji huzidisha hatari za kiafya. Wachimbaji hulazimika kujisaidia ovyo vichakani, hali inayochangia uchafuzi wa mazingira na kuenea kwa magonjwa ya mlipuko.
Hata hivyo, Joseph anaamini suluhisho lipo katika kuweka msisitizo wa elimu na usimamizi madhubuti. Anasema ni muhimu wachimbaji kufikiwa na mafunzo ya uchimbaji endelevu pamoja na uwajibikaji wa kisheria kwa wanaokiuka taratibu.
Hatua ya Serikali
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Mavunde alisisitiza kuwa hatua ya kufuta leseni 40 zinalenga kuondoa uzembe na kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya wananchi.
“Hatutaki kuona rasilimali zetu zinageuka laana. Uchimbaji lazima uende sambamba na uhifadhi wa mazingira,” Mavunde alisema, hatua inayotafsiriwa kama msukumo mpya wa kulinda rasilimali na mazingira ya nchi.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga pia kuzuia uchimbaji holela unaoambatana na uharibifu wa ardhi, uchafuzi wa maji na hatari za kiafya kwa wananchi.
Alionya kuwa serikali haitovumilia vitendo hivyo, akisisitiza kuwa ulinzi wa mazingira ni sehemu muhimu ya Sera ya Madini ya mwaka 2009, yenye dhima ya kuhakikisha rasilimali madini inatumika kwa manufaa ya taifa na wananchi kwa njia endelevu, huku ikichangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii.
Mbali na kufuta leseni 40, Waziri Mavunde alisema serikali imewapa siku 30 kuanzia Aprili 10, mwaka huu wamiliki wa leseni nyingine 43 (40 za utafutaji na tatu za uchimbaji wa kati) kurekebisha kasoro zilizobainika.
Endapo hazitatekeleza masharti hayo ndani ya muda uliowekwa, nazo zitafutwa na maeneo husika kutolewa kwa wawekezaji wengine wenye uwezo na dhamira ya kuziendeleza.
Alisema hatua hii inaendana na azma ya serikali ya kuhakikisha sekta ya madini inakuwa chachu ya maendeleo jumuishi, kwa kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu.
Waziri Mavunde alieleza kuwa sehemu kubwa ya leseni zitakazorejeshwa serikalini (leseni zilizokuwa zinashikiliwa na kampuni hizo 40) zitatengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (BMT).
Serikali hadi sasa haijatoa orodha ya kampuni hizo 40 zilizofutiwa leseni, majina ya wamiliki wala nchi wanazotoka.
Kadhalika mwandishi wa habari hizi alipotaka kufahamu kinachoendelea tangu leseni hizo 40 zilipofutwa na iwapo kampuni nyingine 43 zilizopewa muda wa kurekebisha mapungufu yao zimefanya hivyo, aliambiwa afuatilie baada ya siku 30, yaani muda uliotolewa, utakapotimia.
Ingawa hakuna takwimu rasmi zinazoonyesha mgawanyo wa moja kwa moja kati ya kampuni za ndani na za kigeni kwenye leseni 40 zilizofutwa, uchambuzi wa mienendo ya sekta na mwelekeo wa sera ya madini unaonyesha kuwa walioathirika zaidi ni kampuni za kigeni, hasa zile za utafiti zilizokuwa zinashikilia vitalu bila kuviendeleza kwa lengo la kusubiri kuuza au kupata faida baadaye.
Kauli ya Waziri kuhusu leseni hizo (zilizokuwa mikononi mwa kampuni 40) kukabidhiwa kwa aliowaita wawekezaji wengine wenye uwezo na dhamira ya kuziendeleza, inadhihirisha wazi utekelezaji wa sera ya serikali ya kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kikamilifu na kuongeza nafasi kwa Watanzania kushiriki moja kwa moja katika sekta hiyo.
Habari za ndani kuhusu hatua hiyo ya Serikali zinadai kuwa ufutaji wa leseni hizo na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya madini yanashinikizwa na malalamiko ya muda mrefu ya wadau kuhusu sekta hiyo kwamba imemezwa na wageni huku wazawa wakiwa vibarua.
Sauti ya wadau
Wachambuzi wa masuala ya mazingira wanasema kuwa iwapo hatua hizi za Serikali zitatekelezwa kwa uthabiti, zinaweza kusaidia kupunguza uharibifu wa ardhi, kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha sekta ya madini inakuwa rafiki kwa mazingira huku ikichangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mhandisi wa Migodi kutoka PaulSam Geo-Engineering Company Limited ya Chunya mkoani Mbeya, Maloda Mandago, anaeleza kuwa kuacha maeneo ya migodi bila kuyaendeleza ni chanzo kikuu cha uharibifu wa ardhi (land degradation). Mashimo haya, yasipofukiwa, hugeuka mitego hatari kwa binadamu na mifugo.
“Unakuta eneo zima limejaa mashimo na mitaro. Hakuna mpango wa kurejesha ardhi (rehabilitation). Hii ni hatari kubwa sana,” anasema.
Katika msimu wa mvua, Maloda anasema hatari huongezeka maradufu. Maji hujaa katika mashimo, udongo hulainika na kusababisha maporomoko ya ghafla, ajali zinazoweza kuepukika lakini zinaendelea kugharimu maisha.
“Mbali na ardhi, maji nayo yamekuwa mwathirika mkubwa wa uchimbaji usio endelevu. Mashimo yaliyoachwa wazi hukusanya maji yanayoweza kuchanganyika na kemikali hatari, zikiwemo metali nzito,” Maloda anasema na kuongeza: “Katika baadhi ya maeneo, hali hii husababisha kile kinachojulikana kitaalamu kama acid mine drainage (AMD), mchakato unaofanya maji kuwa na sumu kali kwa viumbe hai.”
Lakini hatari kubwa zaidi iko kwenye matumizi ya zebaki (mercury), kemikali inayotumika kinyume cha sheria na baadhi ya wachimbaji wadogo kunasa dhahabu.”
Anafafanua kuwa zebaki inapochanganyika na maji, huingia katika mnyororo wa chakula. Samaki wanapokula viumbe vidogo vyenye zebaki, na baadaye binadamu wakala samaki hao, sumu hiyo huingia mwilini.
“Matokeo yake ni mabaya, kuanzia matatizo ya mfumo wa fahamu hadi saratani. Wachimbaji wadogo pia huchoma dhahabu ili kuitenganisha na zebaki. Moshi wake unaingia moja kwa moja mwilini. Hii ni sumu kali sana,” anaeleza mtaalamu huyo.
Maloda anaungana na mchimbaji mdogo Joseph kuwa uchimbaji holela unaacha ardhi bila uoto wa asili. Miti hukatwa ovyo ili kupisha machimbo mapya, na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo.
Anasema mvua inaponyesha, udongo husombwa na kuingia katika mito na mabwawa, hali inayoharibu mfumo mzima wa ikolojia. Samaki hufa, vyanzo vya maji vinaziba na kilimo huathirika.
Zaidi ya hapo, makazi ya viumbe hai hupotea. Bayonuai ambayo ni urithi muhimu wa asili, hupungua kwa kasi, na baadhi ya spishi hutoweka kabisa.
Mhandisi Maloda anasema kuwa maeneo mengi yaliyotelekezwa hugeuka kivutio cha wachimbaji holela. Bila udhibiti, watu huingia kwa wingi wakifuata taarifa za kuwapo madini.
Hali hii husababisha msongamano mkubwa wa watu, kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko, migogoro ya kimiliki na hata uhalifu.
Ni katika muktadha huu ndipo hatua ya serikali ya kufuta leseni hizo inaonekana kuwa na uzito wa kipekee.
Jicho la LHRC
Akizungumzia mwenendo wa leseni za madini zinazofutwa, Ofisa wa Haki za Binadamu na Biashara kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Clay Mwaifani, anaweka bayana kuwa kiwango cha uharibifu wa mazingira kinategemea kwa kiasi kikubwa na shughuli zilizowahi kufanyika katika eneo husika kabla ya leseni kufutwa.
Anaeleza kuwa iwapo eneo lilitumika kwa uchimbaji wa moja kwa moja na kuachwa na mashimo wazi, madhara yake huwa makubwa zaidi kulinganisha na maeneo yaliyofanyiwa utafiti kwa kutumia teknolojia kama ndege au droni.
Hata hivyo, anatahadharisha kuwa hata leseni za utafiti, ambazo mara nyingi huonekana kuwa na madhara madogo, zimekuwa zikichangia uharibifu wa mazingira pale zinapotekelezwa bila usimamizi.
Katika muktadha huo, Mwaifani anasisitiza wajibu wa kisheria kwa wamiliki wa leseni kuhakikisha wanarejesha mazingira katika hali yake ya awali pindi wanaposhindwa kuendeleza maeneo waliyopewa.
“Aliyepewa leseni na akashindwa kuendeleza eneo, anapaswa kulirudisha kwanza katika hali salama. Sheria ichukue mkondo wake kuhakikisha urejeshwaji wa mazingira unafanyika ipasavyo,” anasema.
Kauli hiyo inaibua hoja ya uwajibikaji, hasa katika mazingira ambako maeneo yaliyotelekezwa hugeuka kivutio cha wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli bila udhibiti.
Ingawa haelezi moja kwa moja kama maeneo yote yaliyofutwa yalivamiwa, anaashiria uwezekano wa baadhi ya wamiliki wa leseni kuruhusu, kwa njia rasmi au isiyo rasmi, wachimbaji kuingia katika maeneo yao.
Kwa mtazamo wake, uvamizi wa aina hiyo haupaswi kuchukuliwa kirahisi, kwani unafungua mlango wa uharibifu mkubwa wa mazingira na kukiuka misingi ya usimamizi endelevu wa rasilimali.
“Eneo haliwezi tu kuvamiwa bila mmiliki kujua. Kuna wakati hali hiyo huashiria udhaifu au hata ridhaa ya mmiliki. Hivyo, uwajibikaji lazima uanze kwake,” anabainisha.
Kuwajibisha wamiliki leseni
Mwaifani anasisitiza kuwa serikali ina mamlaka ya kuwawajibisha wamiliki wa leseni pale inapobainika kuwa mazingira yameharibiwa, hata kama uharibifu huo umefanywa na wachimbaji wadogo waliovamia maeneo hayo.
Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa sheria na misingi ya usimamizi wa rasilimali, mmiliki wa leseni anabeba dhamana ya kulinda na kuendeleza eneo lake.
Zaidi ya athari za kimazingira, Mwaifani anagusia pia athari pana za kiuchumi, akieleza kuwa kushindwa kuendeleza leseni kunalikosesha taifa mapato na kuzuia wananchi kunufaika na rasilimali hizo.
“Unaposhikilia eneo bila kuliendeleza, unazuia fursa—si kwa serikali tu bali hata kwa wananchi wanaoweza kunufaika kupitia ajira na shughuli za kiuchumi,” anasema.
Ofisa huyo wa LHRC anaunga mkono hatua ya serikali kufuta leseni zisizoendelezwa, akiitaja kuwa ni mkakati muhimu wa kurekebisha mfumo na kuhakikisha rasilimali zinawanufaisha wengi badala ya wachache wanaozihodhi bila kuzitumia.
Katika mtazamo wa haki za kijamii, Mwaifani anaonya kuwa uchimbaji usio endelevu hauishii kuharibu mazingira pekee bali pia unazalisha mifumo kandamizi katika jamii.
Anataja kuwepo ajira za watoto migodini, mazingira hatarishi ya kazi, na ukosefu wa usawa wa malipo kati ya wanawake na wanaume kama baadhi ya changamoto zinazoibuka katika maeneo hayo.
“Unakuta watu wanafanya kazi zilezile lakini malipo yanatofautiana. Hakuna usalama na usawa kazini, hakuna huduma za msingi kama vyoo. Hii ni hatari kwa afya na utu wa binadamu,” anasisitiza.
Katika kutoa mwelekeo wa suluhisho, anashauri matumizi ya mbinu mbadala zisizoathiri mazingira, ikiwemo kuacha matumizi ya miti ya asili katika shughuli za uchimbaji na badala yake kutumia vifaa vya kisasa kama vyuma au rasilimali mbadala zisizo na athari kwa mazingira.
Mtazamo wa Mwaifani unaonyesha tatizo la leseni zilizotelekezwa si la kiutawala pekee, bali ni mnyororo unaounganisha uharibifu wa mazingira, upotevu wa mapato ya taifa na ukiukwaji wa haki za binadamu, hali inayohitaji usimamizi madhubuti na uwajibikaji wa kisheria ili kuurekebisha.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kampuni haiwezi kuanza shughuli za utafiti wa madini bila kukidhi masharti ya kimazingira yaliyowekwa chini ya mfumo wa kisheria wa nchi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake pamoja na Sheria ya Madini ya mwaka 2010, zinataka kampuni kuzuia na kudhibiti athari za mazingira kabla, wakati na baada ya utafiti. Kwa maneno mengine, kampuni haiwezi kuruhusiwa kufanya utafiti bila kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment – EIA), kupata cheti cha mazingira pamoja na kuwa na Mpango wa Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Plan – EMP) unaoeleza namna ya kusimamia na kurejesha mazingira. Taratibu zote hizi husimamiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Wadau wanasema shida hapa si ukosefu wa sheria bali utekelezaji wake na uwajibikaji wa watumishi kwenye wajibu wa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji. Kauli ya wachimbaji wadogo
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Hamza Tandiko, anasema juhudi zimeanza kuonekana katika kubadili mwenendo huo.
Anaeleza kuwa chama hicho kimeanza kuweka mifumo ya kudhibiti utiririshaji holela wa maji na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya migodi.
“Tunatambua kuwa uchimbaji wetu uko karibu na makazi ya watu, hivyo ni wajibu wetu kulinda vyanzo vya maji, mifugo na usalama wa jamii kwa ujumla,” Tandiko anasema.
Anaongeza kuwa kama wachimbaji wadogo wakipatiwa fursa ya kusimamia leseni zilizofutwa na serikali, watahakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa kuzingatia kanuni za uhifadhi wa mazingira ili kuepuka madhara yaliyoshuhudiwa hapo awali.
Kiini cha tatizo
Pantaleo Munishi, Profesa wa Mifumo ya Ikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Idara ya Mifumo Ikolojia na Uhifadhi, akichambua kwa jicho la kitaalamu hatua hiyo ya Serikali, anasema kuwa kiini cha tatizo si tu kuwepo uchimbaji, bali namna unavyofanyika bila kuzingatia misingi ya kisayansi na kimazingira.

Mchimbaji mdogo wa mgodi wa Nyamishiga, Joyce Andrew akiangalia wingi wa dhahabu kwa njia ya kienyeji kabla ya kununua mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu, katika mgodi ulioko Lunguya Msalala wilayani, Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Shaaban Njia.
Anasisitiza kuwa dhana ya “uchimbaji usio endelevu” mara nyingi huchanganywa, lakini kwa tafsiri sahihi ni ule uchimbaji usiopangwa, usiozingatia mazingira husika na usiofuata taratibu zilizowekwa kisheria.
Kwa mtazamo wake, uchimbaji wa aina hiyo huwa na athari hasi zisizoepukika kwa mazingira, hasa pale unapofanyika katika maeneo yenye bayonuai adimu ambayo haiwezi kupatikana kwingine.
“Si kila eneo linafanana kimazingira. Kuna mifumo ya ikolojia ambayo ni ya kipekee kabisa. Ukiharibu hapo, umeharibu kitu ambacho hakiwezi kurejeshwa kirahisi,” anafafanua.
Katika hilo, Profesa Munishi anaunga mkono hatua ya kufuta leseni zisizoendelezwa pale inapobainika kuwa sheria za mazingira, ardhi na madini hazikufuatwa.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa uwazi ni muhimu. Wamiliki wa leseni wanapaswa kuelezwa bayana ni masharti yapi hayakuzingatiwa na ni kwa namna gani yalikuwa na athari kwa mazingira.
Anahoji pia mfumo wa utoaji maonyo kwa baadhi ya wamiliki wa leseni, akieleza kuwa maonyo hayo yanapaswa kuwa na mwelekeo mahsusi. Yaainishe wazi nini kifanyike kurekebisha kasoro, badala ya kubaki kuwa maagizo ya jumla yasiyo na mwongozo wa utekelezaji.
Katika uchambuzi wake, Profesa Munishi pia anagusa kiini kingine cha tatizo, ambacho ni maeneo yaliyotelekezwa. Anaeleza kuwa pale leseni zinapotolewa lakini hazitekelezwi kwa wakati, maeneo hayo hubaki wazi na kuvutia wachimbaji wadogo.
Tofauti na wawekezaji wakubwa, anasema wachimbaji hawa huingia kwa wingi katika eneo dogo, wakifanya kazi bila uratibu, bila miundombinu ya kijamii na bila mwongozo wa kitaalamu. Matokeo yake ni mkusanyiko mkubwa wa watu katika mazingira yasiyo na huduma muhimu kama vyoo, maji safi na mifumo ya kudhibiti taka.
“Hapo ndipo hatari za kiafya zinaanza. Ukosefu wa usafi katika eneo lenye watu wengi unaweza kusababisha milipuko ya magonjwa mbalimbali yanayotokana na uchafu,” anabainisha, akirejea uwezekano wa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Kimazingira, Profesa Munishi anaeleza kuwa uvamizi huo huenda sambamba na uharibifu mkubwa wa ardhi na uoto wa asili. Kila mchimbaji anapojitafutia eneo lake, miti hukatwa ili kupisha uchimbaji na pia kupata nishati kama kuni. Matokeo yake, anasema ni kupungua kwa misitu, kuharibika kwa udongo na kupotea kwa makazi ya viumbe hai.
“Eneo linageuka kuwa uwanja wa vita. Kila mmoja anachimba anavyotaka. Hakuna utaratibu wa kudhibiti kemikali, hakuna mpango wa kurejesha mazingira,” anasema.
Anasisitiza kuwa hata kama sheria za madini zipo wazi kuhusu namna ya kuchimba na jinsi ya kudhibiti kemikali ili zisichafue mito na vyanzo vya maji, lakini changamoto kubwa ni utekelezaji wake, hasa katika maeneo yanayovamiwa.
Hata hivyo, Profesa Munishi anatambua ugumu wa hali halisi ya maisha kwa wachimbaji wadogo, kwamba wanatafuta riziki katika mazingira magumu. Lakini anasisitiza kuwa utafutaji huo wa maisha haupaswi kufanyika nje ya utaratibu.
“Maisha ni muhimu, lakini hayawezi kutafutwa kwa kuvunja sheria. Suluhisho si kuzuia tu, bali kuwaelimisha na kuwawezesha kufuata taratibu,” anashauri.
Anapendekeza kuwapo mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi na maeneo ya uchimbaji, ili iwe wazi ni wapi wachimbaji wadogo wanaruhusiwa kufanya kazi na kwa masharti gani.
Vilevile, anasisitiza umuhimu wa kuwasaidia kuelewa sheria na kanuni, kwani mara nyingi hawazijui.
Kwa upande wa wamiliki wa leseni za utafiti, Profesa Munishi anatoa msimamo mkali, kwamba leseni zisigeuke nyenzo za kuhodhi ardhi bila kuendelezwa. Badala yake, ziwe na muda maalumu wa utekelezaji, na wamiliki wawajibike kuanza shughuli ndani ya muda huo.
“Leseni si ya kushikilia eneo. Ni ya kufanya kazi. Ukishindwa, hatua zichukuliwe mapema ili eneo lisibaki wazi na kuvamiwa,” anasisitiza.
Anaonya kuwa kufuta leseni pekee hakutoshi kama hakutaambatana na mipango mbadala. Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa maeneo yanayorejeshwa yanapangiwa matumizi mapya kwa uwazi, ikiwemo kuwaelekeza wachimbaji wadogo maeneo sahihi ya kufanya shughuli zao.
Vinginevyo, anasema, mzunguko uleule utaendelea, akiwa na maana leseni kufutwa, maeneo kutelekezwa, uvamizi kuanza upya na hatimaye uharibifu wa mazingira na hatari za kiafya kuendelea bila kikomo.
Picha ya Bango: Mchimbaji mdogo wa mgodi wa Nyamishiga, Joyce Andrew akiangalia wingi wa dhahabu kwa njia ya kienyeji kabla ya kununua mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu, katika mgodi ulioko Lunguya Msalala wilayani, Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Shaaban Njia.