- Wanafunzi wanane nchini Uganda wamefikishwa mahakamani kwa kushiriki maandamano ya kupinga mradi wa bomba la mafuta la EACOP, wakiwa wamezuiliwa kwa muda tangu kukamatwa kwao.
- Kesi hiyo imeibua maswali kuhusu haki za binadamu, hususan uhuru wa kujieleza na kuandamana kwa amani miongoni mwa vijana na wanaharakati.
- Wanaharakati na mashirika ya kiraia wanadai kuwa kukamatwa kwa wanafunzi hao ni juhudi za kukandamiza sauti za upinzani dhidi ya mradi huo wa mafuta.
- Wakati huo huo, mjadala kuhusu athari za mazingira na kijamii za EACOP unaendelea kuongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki.
KAMPALA, Uganda – Wanafunzi wanane na wanaharakati wa mazingira wamehukumiwa kifungo cha miezi 11 jela nchini Uganda kwa kosa la kusababisha usumbufu wa umma baada ya kuandamana kupinga mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (East African Crude Oil Pipeline – EACOP), huku hukumu hiyo ikizua maswali mapya kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kuandamana.
Saa nne asubuhi, ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Buganda Road, Katikati mwa jiji la Kampala nchini Uganda, wanaharakati wa mazingira na wanafunzi wanane walifikishwa kizimbani.
Wanafunzi hao wanatoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Uganda, na wamekuwa gerezani tangu Agosti 1, 2025, baada ya kukamatwa wakiandamana kupinga mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la EACOP.
Nje ya Mahakama, kulikuwa na rasharasha za mvua. Wasiwasi ulitanda miongoni mwa wanafunzi wa vuguvugu la “Students Against EACOP” waliokuwa wamefika pale ili kuhudhuria hukumu ya Mahakama hiyo dhidi ya wenzao. Hakimu Mkazi alitangaza kuahirishwa kwa hukumu yao hadi saa nane mchana.
Lakini nyakati za chakula cha mchana, kabla ya saa nane, wanafunzi walio nje waliambiwa kwamba wenzao wanane wamehukumiwa kifungo cha miezi 11 jela kwa kosa la kusababisha usumbufu wa umma (common nuisance).
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Sylvia Muwonge katika chumba chake kwenye Mahakama ya Buganda Road. Mawakili, umma au hata waandishi wa habari hawakuhudhuria.
Upande wa utetezi umepinga hukumu hiyo, ukisema kuwa wanafunzi hao wamenyimwa haki ya kupewa dhamana, na vile vile kunyimwa nafasi ya kuridhisha kujitetea.
Kato Tumusiime, wakili wa wanaharakati hao, anaelekeza kidole cha lawama kwa upendeleo uliokuwepo katika kesi hiyo tangu mwanzo.
“Hukumu ya leo tunaamini si ya haki kabisa ikizingatiwa kwamba ushahidi ulioletwa na upande wa uendeshaji mashtaka haukuweza kuthibitisha madai yaliyowasilishwa mahakamani,” alisema.
Kundi la waliohukumiwa linawajumuisha wanaharakati wa mazingira na wanafunzi wakiwemo Keisha Ali, Shammy Nalwadda, Teopista Nakyambadde, Dorothy Asio, Shafik Kalayango, Noah Kafiiti, Ismail Zziwa na Akram Katende.
Aprili 10, 2026 siku ambayo walipatikana na hatia, upande wa uendeshaji mashtaka uliambia mahakama kwamba, kinyume na sheria, kundi hilo lilifunga barabara wakati wa maandamano yao ya Agosti 2025, kitendo ambacho kilisababisha hatari kwa watumiaji wengine wa barabara.
“Upande wa mashtaka umethibitisha kosa la usumbufu barabarani bila shaka yoyote,” Hakimu Mkazi Rophine Achayo alitoa uamuzi huo tarehe Aprili 10.
Wanaharakati hao walikamatwa wakiwa njiani kuelekea katika makao makuu ya benki ya Stanbic kuishinikiza kusitisha ufadhili wake kwa mradi wa EACOP.


Kato Tumusiime anasema hukumu hiyo inalenga kukatisha tamaa harakati za watetezi hao wa mazingira na kuminya uhuru wa kufanya maandamano ya amani, ameapa kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Uganda.
Licha ya kuwa tayari wametumikia takribani miezi tisa gerezani na sasa kuhukumiwa miezi 11, wanaharakati hao wameapa kutokata tamaa na harakati zao za kutetea mazingira ikiwemo kuendelea kupinga mradi wa EACOP, ambao wanasema unatishia mazingira, maisha ya wanyamapori na mfumo wa ikolojia.
Kayuda Thadeo, mhamasishaji wa vuguvugu hilo, anasema lengo la uamuzi wa Mahakama na hukumu yake ni kuwatia hofu.
“Hukumu ya Mahakama inaonekana kama ile inayotuvunja mioyo, lakini bado tunasalia imara sisi walio nje,” aliapa.
“Hukumu hii inalenga kututishia na kuhakikisha hakuna wanafunzi wengine wanaoweza kuthubutu kuandamana dhidi ya miradi isiyo ya haki kama EACOP, kwa hivyo hatujafurahia, lakini hatutasalia kimya,” Kajubi Maktoum, mwanachama wa vuguvugu hilo, aliongeza.
“Ukamatwaji na kuzuiliwa kwa kiholela, vitendo vya unyanyasaji wa kimahakama, pamoja na hukumu za jinai, ni sehemu ya mwelekeo endelevu na mkali wa ukandamizaji unaolenga watetezi wa mazingira na haki za binadamu pamoja na jamii zilizoathirika katika muktadha wa miradi ya maendeleo ya mafuta nchini Uganda,” Shirika la The Observatory for the Protection of Human Rights Defenders, ambalo ni ushirikiano kati ya Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH) na Shirika la Dunia Dhidi ya Mateso (OMCT), lilisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake.
Kuhusu mradi wa bomba la EACOP
EACOP, lenye urefu wa kilomita 1,443, litasafirisha mafuta ghafi kutoka eneo lenye mafuta nchini Uganda la Albertin Graben hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Mradi huo utagharimu $5 bilioni na unamilikiwa na kampuni ya mafuta ya TotalEnergies (asilimia 62), Kampuni ya Mafuta ya Kitaifa ya Uganda (asilimia 15), Kampuni ya Mafuta ya Kitaifa ya Tanzania, (asilimia 15), na kampuni ya mafuta kutoka nchini China ya CNOOC (asilimia 8).
Hata hivyo, kulingana na Shirika la OXFAM, takriban kilomita 460 za bomba hilo zitakuwa ndani ya bonde la maji safi la Ziwa Victoria, ambalo linasaidia moja kwa moja zaidi ya watu milioni 40 kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali.
Uchimbaji mafuta katika eneo la Albertine Graben nchini Uganda utaathiri vibaya maisha ya wanyamapori katika Mbuga ya wanyama ya Murchison Falls, na kutishia bioanuwai na spishi adimu, na zilizo hatarini kutoweka.
Thadeo anasema: “Kutokana na kwamba makazi ya wanyamapori yameharibiwa, baadhi ya tembo wameanza kuvamia watu. Mwaka uliopita waliwaua watu wanne”.
Mbuga ya Wanyama ya Murchison ndio mbuga kubwa zaidi na kongwe zaidi nchini Uganda, eneo muhimu zaidi la bioanuwai linalotoa makazi kwa aina mbalimbali ya wanyamapori, wakiwemo tembo, simba, viboko, na spishi nyingi zinazopatikana katika eneo hilo.
Nchini Tanzania, bomba la EACOP litapitia katika maeneo ya bioanuwai, ikiwemo Hifadhi ya Wanyamapori ya Biharamulo, ambayo inatoa makazi kwa simba, nyati, pofu, tandala, swalapala, viboko, twiga, na pundamilia.
Ukiukwaji wa Haki za kibinadamu
Katika miaka ya hivi karibuni, wanaharakati wa mazingira wanaopinga mradi wa EACOP wamekuwa wakilengwa kwa kukamatwa wanapofanya maandamano, na hata wengine kukabiliwa na mateso wakishikiliwa korokoroni.
Agosti 9, 2024 wanafunzi 47 walikamatwa katika mji wa Kampala walipofanya maandamano kupinga ujenzi wa bomba la EACOP.
Kati ya Mei hadi Juni 2024, wanaharakati wa mazingira, wakiwemo Adriko Sostein, Julius Tumwiine na Stephen Kwikiriza, pamoja na Jealousy Mugisha Mulimbwa pia walikamatwa na kufungiwa.
Licha ya hukumu dhidi ya wenzao, wanafunzi wa vuguvugu la Students Against EACOP wanasema wataendelea na harakati zao za kupinga mradi huo unaotishia mfumo wa ikolojia, maisha ya wanyamapori, na haki za kibinadamu.
Picha ya bango: Baadhi ya wanafunzi na wanaharakati waliohukumiwa kifungo cha miezi 11 kwa kosa la kusababisha usumbufu wa umma walipokuwa wakipinga mradi wa EACOP. Picha na Gerald Ahairwe.