- Badala ya mvua kuleta athari kama mafuriko, tujenge miundombinu ya kuvuna maji kwa ajili ya matumizi wakati wa ukame.
- Mafanikio ya uvunaji maji yatategemea zaidi uwepo wa mipango thabiti ya kuyafanyia tiba sahihi na usafi wa mifumo ya uvunaji.
- Mabadiliko ya tabianchi tayari yamejikita katika mifumo ya asili, na hivyo kuhitaji juhudi endelevu za kukabiliana na athari zake.
- Wananchi waelimishwe kuhusu dhana ya mabadiliko ya tabianchi na wajibu wao katika kujikinga na athari zake
DAR es SALAAM, Tanzania – Mvua imenyesha bila kukoma usiku kucha. Nyumba zimejaa maji, nyingine zimesombwa kabisa. Katikati ya taharuki hiyo, Salehe na familia yake wanajaribu kujiokoa kwa kushikilia chochote kilicho karibu nao, wengine wanashikilia miti, wengine magodoro na makabati yanayoelea juu ya maji.
Hata hivyo, taswira inayotia uchungu zaidi ni ya madumu yale yale ya njano ambayo hutumika wakati wa ukame kununulia maji, sasa yanaelea juu ya maji mengi kupita kiasi. Ni picha inayobeba ukweli mchungu: katika enzi ya mabadiliko ya tabianchi, jamii zinakabiliwa na ukame na mafuriko kwa wakati mmoja.
Swali la msingi ni: Ni kwa namna gani kero ya mvua kubwa inaweza kugeuzwa kuwa suluhisho endelevu la changamoto ya upatikanaji wa maji? Hilo ndilo swali la msingi kwa sasa, ambalo baadhi ya wataalam wanalijibu katika makala haya.
Taarifa za mamlaka kuhusu mvua za masika
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa kuhusu mvua za masika. Katika taarifa yake ya mwelekeo wa mvua za masika Machi-Mei, 2026 inasema kuwa mvua hizo katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (kanda ya Ziwa Victoria, nyanda za juu Kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini pamoja na maeneo yaliyopo kaskazini mwa mkoa wa Kigoma) katika kipindi cha miezi hiyo, vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ladislaus Chang’a anasema matukio haya yanaweza kuleta uharibifu wa miundombinu na mazingira, milipuko ya magonjwa, pamoja na upotevu wa mali na maisha.
Anahimiza Idara ya Usimamizi wa Maafa, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini, kuendelea kuratibu na kutekeleza mipango ya kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Aidha, Sekta ya Mazingira pamoja na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata/shehia, na kijiji/mtaa zinashauriwa kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu maafa kwa kuzingatia sera, sheria, taratibu na miongozo itakayosaidia katika kuzuia/kupunguza athari, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali pindi maafa yatakapotokea.

Aprili 7, 2026, TMA, ilitoa tahadhari ya siku tatu, ikionya kuhusu kutokea kwa mvua nyingine ambazo zingeleta mafuriko katika mikoa kadhaa ikiwemo ya Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani, Dar es Salaam pamoja na Unguja na Pemba.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) nalo limetoa tahadhari kuhusu hatari ya mvua kubwa na maporomoko ya ardhi yanayoweza kusababisha uharibifu mkubwa.
Mwanzoni mwa mwaka 2025, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Immaculate Semesi, alikaririwa na vyombo vya habari akisisitiza juu ya umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema wakati matukio ya hali mbaya ya hewa yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi yakiendelea kuongezeka.
Alikumbusha madhara ya majanga yaliyotokea awali, yakiwemo maporomoko ya ardhi ya Katesh (Manyara), Kawetere (Mbeya) na Mamba Miamba (Kilimanjaro), pamoja na mafuriko makubwa yaliyotokea Rufiji, Morogoro na Kilombero, yaliyosababisha vifo, uharibifu wa mali na kuathiri miundombinu muhimu kama barabara, madaraja na miundombinu ya umeme.
Aidha NEMC iliwataka wananchi kuzingatia miongozo ya mazingira, kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi ya mafuriko na maporomoko, pamoja na kufuatilia taarifa za hali ya hewa. Baraza hilo pia lilisisitiza umuhimu wa kutekeleza kikamilifu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, na kuzingatia mipango sahihi ya matumizi ya ardhi ili kuzuia uharibifu wa mazingira.
Badala ya mafuriko maji ya mvua yavunwe
Katikati ya hofu ya athari zinazochochewa na mabadiliko ya tabianchi kama mvua kubwa, mafuriko, maporomoko na upepo mkali, baadhi ya watalaam wanashauri kuwepo kwa mkakati wa kitaifa ambao utawawezesha Watanzania kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya matumizi wakati wa kipindi cha uhaba wa maji na kupitia mpango huo taifa likawa na chanzo endelevu cha maji.
Zakayo Mwamlima, Mkurugenzi wa taasisi ya Quality Water & Sanitation, anasema miongoni mwa matokeo ya mabadiliko ya tabianchi ni kuwa na vipindi virefu vya ukame, lakini pia vya mvua nyingi ambayo wakati mwingine huleta mafuriko, ambayo husababisha madhara makubwa kwa watu ikiwa ni pamoja na vifo, kuharibu mali, makazi na miundombinu.
Anasema kuwa msimu wa mvua unapoingia, badala ya maji kuleta athari kama mafuriko, ni vema kungekuwa na mkakati wa kujenga mabwawa ya chini ya ardhi ili kuvuna maji kwa ajili ya matumizi wakati wa kipindi cha ukame.
“Tungekuwa na mpango kama taifa wa namna ya kubadilisha changamoto za mvua nyingi zenye athari kuwa faida itakayotusaidia kumaliza shida ya maji. Wakati tunasubiri mipango ya muda mrefu, tunaweza kutumia njia hii ya haraka na ya gharama nafuu,” anasema.
Anasema Serikali ina nafasi kubwa ya kufanya hivyo na kwamba gharama za kujenga mabwawa ya chini ya ardhi yanayoweza kuvuna maji haya, ni nafuu. “Nimefanya kazi kwenye maeneo ya ufugaji na nimeona hilo la kuvuna maji linawezekana. Badala ya maji kwenda kwenye makazi ya watu na kuleta mafuriko ama athari nyingine, yanageuzwa mwelekeo.
Nchini Tanzania nyumba za bati ziko nyingi, zikiangusha maji yakakusanywa na kuhifadhiwa, halafu yanawekewa dawa ili kuua bakteria na kuondoa vimelea vingine vya hatari, yanaweza kuwa salama kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu,’’ anasema Zakayo.
Leonard Chakupewa Soza, mtalaam wa masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, anasema uvunaji wa maji ya mvua unawezekana iwapo wananchi wataelimishwa namna salama ya kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Leonard, ni muhimu wananchi wakajengewe uwezo wa namna ya kutumia njia za asili za kuvuna maji zilizokuwa zinatumika miaka ya nyuma.
Akisimulia namna njia hizo zinavyotumika anasema, “Hatua ya kwanza ni kuchimba shimo ili kupata tanki la asili, kisha nailoni pana na kubwa hutandikwa humo na kutokeza kwenye kingo za lile tanki na baadaye kupangwa mawe juu ili kuzuia ile nailoni isitumbukie ndani, maji yatakapokuwa yanaingia mle kwa ajili ya kutuama.
“Ili kuhakikisha maji yanaelekea kwenye matanki na si kwenye makazi ya watu au kwenye mashamba, mifereji inatengenezwa na kuwekewa sakafu ya saruji na kisha kuweka tena nailoni juu yake ili maji yanapotiririka kwenda kwenye matanki, yajichuje na kuacha uchafu juu. Hata hivyo, maji hayo, ili yaweze kufaa kwa matumizi ya binadamu, ni lazima yawekewe dawa za kuyatibu’’.
Sambamba na mpango wa kitaifa, Zakayo anasema zoezi la kuvuna maji ya mvua linaweza kufanywa hata na mtu mmoja mmoja au familia.
Sheria ya Usimamizi wa Raslimali za Maji namba 11 ya mwaka 2009 (Water Resources Management Act, 2009) inawapa wananchi haki ya kuanzisha mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua kwa matumizi ya nyumbani ndani ya maeneo yao bila kuhitaji kibali maalum kutoka serikalini, mradi tu anafanya hivyo ndani ya eneo lake (mfano kiwanja au nyumba yake).
Aidha, mwaka 2025, Serikali ya Tanzania ilifanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Maji kwa kujumuisha mikakati inayolenga kuboresha maendeleo ya rasilimali za maji. Toleo lililorekebishwa linahamasisha kuboresha mbinu za kuhifadhi na kutumia maji, ikiwemo uvunaji wa maji ya mvua ili kukabiliana na uhaba na mabadiliko ya tabianchi.
Tafiti kuhusu uvunaji wa maji ya mvua
Baadhi ya tafiti zilizofanywa nchini Tanzania zimebainisha kwamba uvunaji wa maji unawezekana na maji ya mvua yanafaa kwa matumizi ya binadamu iwapo yatawekewa dawa kuondoa bakteria na uchafu mwingine.
Utafiti uliofanyika Jijini Dar es Salaam, “Rainwater harvesting for domestic use in suburb areas of Dar es salaam, Tanzania: a case study of Wazo Hill, na matokeo kuchapishwa kwenye Journal of Science Tanzania mwaka 2025, ulionyesha kuwa uvunjaji wa maji ya mvua ni suluhisho linaloweza kusaidia kupunguza kero ya maji. Kwa mujibu wa utafiti huo, tayari baadhi ya maeneo yaliyo nje ya jiji la Dar es Salaam yanatumia utaratibu huo kujipatia maji.
Utafiti huu ulibaini kuwa sehemu kubwa ya kaya katika eneo la Wazo Hill hutegemea maji ya mvua yaliyovunwa kwa matumizi ya kunywa na ya nyumbani kutokana na uhakika wake pamoja na gharama zake kuwa nafuu.
Hata hivyo, matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa maji ya mvua yana kiwango cha uchafuzi wa vimelea vya magonjwa, hususan bakteria na vinyeshi vinavyosababishwa na uchafu kutoka kwa ndege na wanyama wanaofika maeneo ya kukusanyia maji pamoja na mifumo duni ya uhifadhi.

Ingawa uvunaji wa maji ya mvua ni mbinu muhimu ya kukabiliana na uhaba wa maji mijini, mafanikio yake yatategemea zaidi uwepo wa mipango thabiti ya kuyafanyia tiba sahihi pamoja na usafi wa mifumo ya uvunaji ili maji yawe katika kiwango na ubora unaotakiwa kwa usalama wa afya ya watumiaji, utafiti unabainisha.
Utafiti unapendekeza kuwa maji ya mvua yaliyovunwa ni lazima yatibiwe kabla ya matumizi kwa kutumia njia mbalimbali zinazopatikana kama klorini, kuchemsha na uchujaji (flocculation). Pia, mifumo ya gharama nafuu kama vifaa vya kuondoa maji ya awali (first flush diverters) na vichujio inapaswa kuingizwa katika miundo mbinu ya uvunaji wa maji ili kupunguza uchafu.
Mapendekezo ya kisera yanahusisha uandaaji wa miongozo ya usanifu, usakinishaji na matengenezo ya mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua majumbani, kuingizwa kwa viwango vya uvunaji wa maji katika kanuni za ujenzi na mipango miji, pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu usalama wa ukusanyaji, uhifadhi na matibabu ya maji ya mvua.
Pia, ufuatiliaji na upimaji wa mara kwa mara wa vyanzo vya maji vya majumbani na mamlaka za mitaa unapendekezwa ili kuhakikisha usalama wa afya ya wananchi.
Katika chapisho liitwayo, “Adaptive-Water-Governance-and-Climate-Change-Resilience-among-Rural-Communities-TZ, ilibainishwa kuwa jamii za Kilosa zimekuwa zikitegemea mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maji, ambapo uvunaji wa maji ya mvua hujitokeza kama suluhisho la vitendo na linaloendana na mazingira ya kijamii na kiuchumi ya wakazi wa vijijini.
Utafiti huo ulieleza kuwa mifumo ya usimamizi wa maji inayohusisha ushirikiano wa jamii na taasisi za serikali huongeza uwezo wa watu kukusanya na kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi ya nyumbani na kilimo kidogo.
Aidha, uvunaji wa maji ya mvua unasaidia kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyo vya uhakika, hasa wakati wa ukame, hivyo kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, utafiti pia unabainisha changamoto kama ukosefu wa miundombinu bora na uelewa mdogo kuhusu uhifadhi na matumizi salama ya maji.
Kwa ujumla, matokeo yake yanaonesha kuwa uvunaji wa maji ya mvua ni sehemu muhimu ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji na ni nyenzo ya msingi katika kujenga ustahimilivu wa jamii vijijini Tanzania.
Katika utafiti uitwao “Identification of suitable zones and sites for rainwater harvesting to ensure urban water security in Songea, Tanzania’’ , ambao matokeo yake yalichapishwa kwenye Journal of African Earth Sciences, mwaka 2026, mvua inaweza kuwa suluhisho la changamoto ya maji katika miji iwapo itakusanywa na kuhifadhiwa ipasavyo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, karibu asilimia 95 ya eneo la Songea linafaa kwa uvunaji wa maji ya mvua. Kadhalika, maeneo mengine ya mji huo yana uwezo wa kujengwa miundombinu ya kuhifadhia maji kama mabwawa madogo.
Kwa ujumla, ushahidi huu unaonesha kuwa changamoto ya maji si uhaba wa mvua pekee, bali ni ukosefu wa mifumo madhubuti ya kuyakusanya na kuyahifadhi, jambo linalofungua nafasi ya kubadili athari za mabadiliko ya tabianchi kuwa rasilimali endelevu ya maji.
Kuhusu uwezo wa kumudu gharama, utafiti huo unaonyesha kwamba uvunaji wa maji ya mvua ni suluhisho ambalo jamii nyingi zinaweza kumudu kwa sababu miundombinu inayohitajika, kama mabwawa madogo, mifereji ya kuelekeza maji na maeneo ya kuhifadhi maji, vina gharama ndogo ukilinganisha na miradi mikubwa ya maji kama mabwawa makubwa au usambazaji wa maji kutoka vyanzo vya mbali.
Kwa ujumla, matokeo ya tafiti hizo yanaonyesha kuwa uvunaji wa maji ya mvua si tu suluhisho la kiikolojia, bali pia ni mbinu nafuu, endelevu na inayofikika kwa watu wengi.
Mabadiliko ya tabianchi na mvua kubwa
Mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa changamoto inayoleta athari kwa mifumo ya hali ya hewa duniani. Moja ya athari hizo ni ongezeko la mvua kubwa na zisizotabirika, ambazo zimekuwa zikisababisha mafuriko na madhara kwa jamii na mazingira.
“Mabadiliko ya tabianchi tayari yamejikita katika mifumo ya asili, na hivyo kuhitaji juhudi endelevu za kukabiliana na athari zake badala ya kutegemea kuzuia kabisa kutokea kwake,’’ anasema Leonard.
Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi 2021-2026 unaelekeza jinsi Tanzania inavyoweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Unataja maeneo ya kuweka vipaumbele katika sekta muhimu kama kilimo, maji, nishati, afya na misitu, kwa kuhimiza matumizi ya teknolojia endelevu, utafiti na usimamizi bora wa rasilimali, lengo likiwa kulinda mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu licha ya changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi. Pia unasisitiza ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na jamii, pamoja na kuongeza uelewa na elimu kwa umma ili kujenga ustahimilivu wa kijamii na kiuchumi.
Mwanzoni mwa mwaka 2026, Chang’a alisema kuwa kwa sasa dunia inashuhudia ongezeko kubwa la matukio ya hali mbaya ya hewa yanayotokana na kuchagizwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ikiwemo mvua kubwa, mafuriko, vipindi virefu vya ukame, pamoja na matukio ya vimbunga na upepo mkali. Alisema hayo wakati akizungumza kwenye warsha ya mafunzo ya Rada za Hali ya Hewa na matumizi ya taarifa zinazotokana na rada, iliyofanyika mwanzoni mwa 2026 Jijini Dodoma.
Alisema matukio hayo yamekuwa ya mara kwa mara na ya hatari zaidi, na akaongeza kuwa katika kipindi hiki, huduma za tahadhari dhidi ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana, hususani kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Leonard anasema mabadiliko ya tabianchi yanatokea duniani kote na ndiyo maana mikutano yote ya nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, inafayonyika kila mwaka, hujadili namna ambavyo mataifa yanapambana na athari zake. Hii inadhihirisha kuwa kila taifa linatakiwa kujiandaa namna ya kukabiliana na athari zake.
“Wote tunafahamu kuwa miradi mingi ya mazingira ilikuwa inafadhiliwa na mataifa ya nje na hivi sasa ufadhili umesitishwa ama unachechea. Lakini mabadiliko ya tabianchi hayaangalii kama wafadhili wapo au wameondoka. Kwa hiyo kama taifa tunapaswa kujikita zaidi katika kuweka mikakati kujiepusha na majanga haya lakini pale yanapotokea kuhakikisha hayawi na athari kubwa kwetu,” anasema Leonard.
Aidha alisema kitu kingine muhimu ni kuwafikishia elimu wananchi katika maeneo mengi nchini, ili wafahamu kwa kina dhana nzima ya mabadiliko ya tabianchi na wajibu wao katika kujikinga na athari zake.
“Bado wananchi wengi uelewa wao katika masuala haya ni mdogo. Wengi hawawezi kuhusisha baadhi ya shughuli ambazo wanafanya na matokeo ya kimazingira ama yenye mafungamano na athari zinazojitokeza.
“Majanga kama maporomoko na mafuriko yanapotokea, kuna watu wanasema ni mpango wa Mungu, au ni uchawi. Pia kuna sehemu ambazo watu huwatuhumu wenzao kwamba wamezuia mvua ama wamesababisha mafuriko. Yote haya ni matokeo ya uelewa hafifu miongoni mwa wana jamii,” alisema Leonard.
Picha ya bango: Wasafiri walilazimika kuvuka mto kwa miguu baada ya daraja la mto Suguti lililoko barabara ya Musoma hadi Busekera mkoani Mara kukumbwa na mafuriko kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika sehemu mbalimbali nchini. Picha na Sabato Kasika, Mongabay.