- Utafiti wa miaka 30 unaonyesha mgawanyiko wa aina yake ndani ya jamii ya sokwe katika Mbuga ya Kitaifa ya Kibale nchini Uganda, ulioibua vita vikali.
- Makundi mawili hasimu ya sokwe yamefanya uvamizi wa kuratibiwa uliowaua wanaume na watoto wachanga.
- Watafiti walirekodiangalau mashambulizi 24 kati ya mwaka 2018 na mwaka 2024, ikipendekeza kuwa vurugu kali si jambo la kawaida.
- Matokeo yanaonyesha namna kuhama kwa uhusiano wa kijamii kunawezakutia dosari katika jamii za wanyama na kusababisha vurugu za pamoja.
Jamii ya sokwe katika Mbuga ya Kitaifa ya Kibale nchini Uganda iligawanyika katika makundi hasimu na kushambulia washirika wa zamani, katika kile watafiti wanakifafanua kuwa ni “vita vya wenyewe kwa wenyewe” vya nadra vya sokwe.
Utafiti huo mpya, uliochapishwa kwenye jarida la Science, unaangazia uchunguzi wa takriban miongo mitatu kwenye tovuti ya utafiti wa sokwe wa Ngogo, ukiongozwa na mtaalamu wa wanyama Aaron A. Sandel wa Chuo Kikuu cha Texas huko Austin, nchini Marekani. Yeye na wenzake wanasema hili ni tukio la nadra linaloweza kutokea mara moja tu kila baada ya miaka 500. Limezingatiwa mara moja tu awali na wanadamu.
Kabla ya mgawanyiko huo, jamii ya Ngogo ilikuwa kubwa isivyo kawaida, ikiwa na takriban sokwe 150 hadi 200 (Pan troglodytes), na kuifanya kuwa mojawapo ya makundi makubwa zaidi ya sokwe kuwahi kurekodiwa porini. Baada ya mpasuko huo, jamii iligawanyika katika makundi mawili, ambayo watafiti wameyaita makundi ya Kati na Magharibi, yaliyopewa jina la sehemu za misitu walimoishi.

Kati ya mwaka 2018 na mwaka 2024, kundi la sokwe wa Magharibi lilifanya mashambulizi 24 kwenye kundi la sokwe wa Kati, na kuua angalau wanaume wazima saba na watoto wachanga 17. Sandel aliiarifu Mongabay kuwa mzozo huo bado unaendelea na huenda ukawa na matokeo ya kudumu kwa idadi ya sokwe.
“Kundi la sokwe wa Kati liko hatarini – wamekuwa na ongezeko kubwa la vifo,” Sandel alisema. “Swali kuu ni: Je, watahimili vipi hali hii?”
Tofauti na makundi mengi ya nyani, mgawanyiko wa Ngogo ulihusisha “mauaji yaliyoratibiwa ya washirika wa muda mrefu,” Sandel na wenzake waliandika. Viwango vya mauaji pia vilizidi makadirio ya uvamizi kati ya makundi katika sokwe. Watafiti wanakadiria kuwa sokwe wa eneo la Kati walifariki kwa kiwango sawa cha takriban 3,376 kwa kila sokwe 100,000 kwa mwaka, zaidi ya mara 30 ya kiwango cha wastani cha takriban 100 kwa 100,000 kilichoripotiwa kwa idadi ya sokwe wengine.
Watafiti wanasema uhasama huo unaweza kutoa ufahamu adimu wa jinsi vurugu zinaweza kuibuka ndani ya jamii za wanyama zenye uhusiano kwa karibu. Utafiti huo unapendekeza kuwa mabadiliko katika mahusiano ndani ya mtandao wa kijamii yanaweza tosha kuvunja jamii iliyokuwa imeshikamana, wazo lililochunguzwa kwa umakini kwenye uchambuzi wa kina wa watafiti wa mgawanyiko wa Ngogo.
Kutoka kwenye mgawanyiko wa kijamii hadi uhasama mkali
Dalili za mgawanyiko mwanzo zilionekana mwaka wa 2015, wakati sokwe wa Ngogo walipoanza kuubuni makundi mawili tofauti ya kijamii. Watafiti waligundua mabadiliko hayo kwa kutazama kwa muda mrefu, rekodi za idadi ya sokwe na mabadiliko katika mitandao ya kijamii kulingana na sokwe waliotumia muda pamoja au walitunzana. Kutunza ni kiashirio kikuu cha uhusiano wa kijamii.
Baada ya muda, mwingiliano ndani ya kila kikundi uliongezeka huku mwingiliano kati yao ukipungua.
Ulipowadia mwaka 2017, vikundi vya sokwe wa eneo la Magharibi na sokwe wa sehemu ya Kati vilikuwa vikitumia sehemu tofauti za msitu, na kuligeuza eneo lao la zamani kuwa mpaka.
Uzazi baina ya washiriki wa vikundi viwili ulisita: Mtoto wa mwisho wa kikundi cha muingiliano alitungwa mnamo Machi 2015, na tangu wakati huo, watoto wote walio na kizazi kinachojulikana walitungwa ndani ya kundi moja.
Ilipofikia mwaka 2018, watafiti walihitimisha kuwa jamii ilikuwa imepitia mgawanyiko wa kudumu, ikigawanyika katika vikundi viwili ambavyo havikuimarisha tena uhusiano wa kijamii.

Watafiti walirekodi doria za maeneo kuanzia mwaka wa 2016, doria nyingi zikihusisha sokwe wa Magharibi. Doria zilizidi kila mara katika miaka iliyofuata. Mengi yalitangulia mashambulizi mabaya dhidi ya kundi la sehemu ya kati baada ya mgawanyiko wa kudumu mnamo mwaka wa 2018.
Kilichowashangaza watafiti wengi ni uhusiano kati ya washambuliaji na waathiriwa. Sokwe ambao “waliishi, walikula, walitunzana na kufanya doria pamoja kwa miaka mingi, kisha wakalengwa na mashambulizi mabaya kwa msingi wa uanachama wao mpya wa kikundi,” waandishi waliandika.
Kutokana na sokwe kuorodheshwa kuwa kwenye hatari katika Orodha Nyekundu ya shirika la IUCN, kupotea kwa hata sokwe wachache tu, kunaweza kuwa na athari kubwa kwa maisha yao ya siku za usoni.
Sababu halisi za mgawanyiko
Sababu za mpasuka wa Ngogo hazijabainika. Hata hivyo, waandishi wa utafiti na wataalam wanaashiria sababu kadhaa zinazowezekana za kijamii na kiikolojia.
Sandel na wenzake waliandika kwamba uchunguzi wao unaunga mkono kile wanachokiita “dhahania ya mienendo ya uhusiano,” nadharia inayopendekeza kwamba mabadiliko katika mahusiano ndani ya mtandao wa kijamii yanaweza kubuni upya utambulisho wa kikundi, na hatimaye kuzalisha ghasia za pamoja.
Kama waandishi walivyoandika, “mitandao ya kijamii inaweza kugawanyika, na mipaka mipya ya kundi inaweza kuchipuka, na kusababisha vurugu za pamoja.”
Michael L. Wilson, ni mtaalamu wa tabia za wanyama katika Chuo Kikuu cha Minnesota nchini Marekani, ambaye hakuhusika katika utafiti huo, alisema mabadiliko katika mahusiano ya kijamii pekee yanaweza yasieleze kikamilifu mgawanyiko huo.
“Hapa, kubadilisha mahusiano ya kijamii ni muhimu,” Wilson alisema. “Ila inanifanya nijiulize ni nini kingesababisha uhusiano huo wa kijamii kubadilika.”
Wilson alipendekeza kuwa shinikizo la kiikolojia linaweza kuwa na jukumu, ikiwa ni pamoja na ushindani juu ya eneo au sehemu zenye vyakula vingi. Tofauti za umri wa sokwe wa kiume au mifumo ya undugu ndani ya vikundi vipya inaweza pia kuathiri jinsi miungano inavyobuniwa na uhasama kutokea, alisema.
Wilson pia aliuliza iwapo mzozo huo unapaswa kuelezewa kama “vita vya wenyewe kwa wenyewe.” Kwa maoni yake, matukio yanafanana kwa ukaribu zaidi na “mgawanyiko wa kikundi unaofuatiwa na mapigano,” badala ya vita ndani ya jamii yenye angalau upande mmoja unaojaribu kusalia pamoja.
Sandel alisema wanaendelea kupeleleza uwezekano huu wakitumia seti za data za muda mrefu za tovuti hiyo, zilizorudi nyuma kwa miongo kadhaa iliyopita: Wanasayansi walianza kuwachunguza sokwe wa Ngogo mwaka wa 1995.
“Hii ni dhana kubwa,” Sandel aliiambia Mongabay. “Maoni yangu ya awali ni kwamba sokwe hawakuwa na chakula cha kutosha, lakini tuna timu za watafiti wa Uganda na wa kimataifa wanaoshughulikia maswali haya sasa.”
Kubainisha sababu halisi ya uhasama huo huenda isiwe rahisi, aliongezea. “Itakuwa vigumu sana kuthibitisha sababu. Lakini kwa kuchanganya data ya muda mrefu na mbinu mpya za takwimu, nadhani tutaweza kufichua mengi.”

Tukio adimu, lakini si la kipekee
Ingawa si kawaida, uhasama wa Ngogo haukosi mfano.
“Kumbukumbu ya mgawanyiko mwingine pekee wa jamii ya sokwe ulitokea katika Hifadhi ya Kitaifa ya Gombe nchini Tanzania mapema miaka ya 1970,” Wilson alisema.
Mgogoro huo, na aina ya vikundi vya sokwe wa Kasekela na Kahama, ulielezewa kwa umaarufu na mtaalamu wa tabia za wanyama marehemu Jane Goodall kama “Vita vya Miaka minne.”
Sandel alisema upelelezi wa Ngogo unaimarisha tafsiri zilizofanywa miongo kadhaa hapo awali huko Gombe, ambako timu ya Goodall iliandika kwa mara ya kwanza mzozo mbaya kufuatia mgawanyiko wa jamii.
Wilson alibainisha kuwa kisa cha Ngogo kinafaidika kutokana na nyaraka nyingi zaidi kuliko mgogoro wa Gombe, ambao ulitokea wakati wa miaka ya awali ya utafiti wa sokwe.
Hii inaangazia umuhimu wa utafiti wa muda mrefu wa viwanjani, Sandel alisema, ambao uliwezesha kufuatilia mgawanyiko wa kijamii kama ulivyotokea Ngogo.
Wana miongo mitatu ya data asili ya historia na upelelezi wa kitabia wa muda mrefu. “Hii ni taarifa inayoendelea. Kwa kutumia data ya muda mrefu, tutaelewa sababu na matokeo.”
Eneo la utafiti la Ngogo pia si la kawaida kwa sababu sokwe hawa kwa kiasi kikubwa wamekingwa dhidi ya shinikizo la binadamu. Tofauti na Gombe ambako sokwe hao walipewa ndizi na kutangamana karibu na makazi ya binadamu na shughuli za kitalii, sokwe wa Ngogo wamefanyiwa utafiti katika mazingira ya misitu ambayo kwa kiasi kikubwa haina usumbufu.
“Eneo hili lipo katikati ya msitu na limekuwa likilindwa na Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda kwa miaka 30,” Sandel alisema. “Ulinzi huo ndio uliouwezesha utafiti wetu wa muda mrefu na kufichua taarifa hii.”
Kufahamu historia yao huenda kukawasaidia wanasayansi kuelewa vyema jinsi migogoro hutengeneza upya jamii.
“Uchunguzi wetu ni mwanzo tu,” Sandel alisema. “Tunahitaji njia za takwimu za maamuzi ya ni watu gani ni muhimu sana kwa kudumisha mshikamano katika mtandao.”
Ingawa sokwe wa Ngogo wanaishi katika msitu uliohifadhiwa ndani ya Hifadhi ya Kitaifa ya Kibale, bado wanakabiliana na maradhi yanayoenezwa na binadamu. Kuwalinda sokwe kutokana na maradhi ya binadamu ni jambo jingine muhimu kwa watafiti wanaofanya kazi katika eneo hilo. Maradhi ya kupumua yaliyosababishwa na binadamu mwaka 2017 yaliua sokwe 25 huko Ngogo.
Tangu kipindi hicho, watafiti wametekeleza kanuni kali za afya kwa ushirikiano na Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda, ikiwemo na karantini ya siku saba kwa binadamu wanaotaka kuingia msituni.
Kulingana na Sandel, hatua hizo zinaonekana kusaidia. “Tangu karantini kutekelezwa Ngogo, tumeona kupungua kwa wingi wa virusi miongoni mwa sokwe.”
Aliongeza kusema, “Tunafurahi kuona kile tunachojifunza katika miaka 30 ijayo.”
Picha ya bango: Sokwe mzee, BF, alikuwa mwanamume wa mwisho kwenda kati ya vikundi viwili. Picha na Aaron Sandel
Nukuu:
Sandel, A. A., He, Y., Ren, J., Kei, Y. L., Lee, K. C., Clark, I. R., … Mitani, J. C. (2026). Lethal conflict after group fission in wild chimpanzees. Science, 392(6794), 216-220. doi:10.1126/science.adz4944
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 17/04/2026