- Uchimbaji wa mawe kiholela huvuruga uwiano wa mifumo ya ikolojia na kuharibu mwingiliano wa viumbe na mazingira yao.
- Sauti za milipuko huwatisha viumbe hai, hasa wanaotegemea mazingira tulivu kuishi na kuzaliana.
- Kuondoka kwa tabaka la juu la udongo lenye rutuba, kunapunguza uwezo wa ardhi kuzalisha uoto wa asili.
- Sheria zinazomtaka kila mtu kulinda mazingira zipo lakini zinaendelea kupuuzwa.
Hili ni toleo la kwanza la mfululizo wa makala kuhusu uchimbaji holela wa mawe jijini Mwanza. Soma toleo la pili hapa.
Ni asubuhi, na kwa mbali jua linaanza kuchomoza juu ya vilima vya Jiji la Mwanza. Juma anaingia kazini, katikati ya miamba mikubwa ya mawe, mahali anapopaita ofisi yake. Kila siku hufika hapo kutafuta riziki kwa kuponda mawe na kuyauza. Kabla hajapiga nyundo yake kwenye jiwe la kwanza, anafunga macho kwa sekunde chache, moyo wake umejaa hofu na mashaka. Ameshuhudia wenzake wakipoteza maisha baada ya kupondwa na mawe au kufukiwa na vifusi bila msaada. Kwa Juma, maisha yake ni bahati nasibu. Kila siku ni uchaguzi kati ya uhai na kifo.
Juma ni miongoni mwa wakazi wengi wa Jiji la Mwanza ambao wanaishi kwa kujishughulisha na upasuaji na uuzaji wa mawe, shughuli ambayo licha ya kuwa na madhara mengi kwa mazingira, afya, jamii na hata kusababisha vifo, vita dhidi yake inaendelea kuwa ngumu kutokana na changamoto mbalimbali.
Mchakato hatari wa uchimbaji mawe
Jiji la Mwanza nchini Tanzania limeendelea kukua kwa kasi, likichochewa na ongezeko la watu na mahitaji ya makazi pamoja na miundombinu. Jiji hili lenye asili ya milima na miamba linafanya uchimbaji kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, ukitoa ajira na kuchangia upatikanaji wa malighafi za ujenzi zinazohitajika.
Hata hivyo, nyuma ya faida hizi za kiuchumi, shughuli hizi zinatishia utunzaji wa mazingira na jamii, kwa kuathiri ardhi, bioanuai, usalama wa wachimbaji wenyewe pamoja na wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya uchimbaji.
Hatari ya kwanza ya shughuli hii inatokana na namna kazi hiyo inavyofanywa. Shughuli hiyo inahusisha mchakato wenye hatua kadhaa, ikiwemo uchimbaji wa mawe, upasuaji, uchomaji pamoja na matumizi ya baruti, endapo jiwe linalopasuliwa ni kubwa.

“Hatua ya kwanza huwa tunachimba jiwe, mpaka tunalipata linapoishia, kisha tunaanza kuchoma kwa kutumia magogo na chenga,” anasema Joshua Masano, mkazi wa Ngw’ashi jijini Mwanza, alipozungumza na Mongabay. Joshua amefanya kazi hiyo kwa takriban miaka kumi na minne.
Msafiri Heneliko, mkazi wa Bulale jijini Mwanza, anafafanua zaidi kuhusu hatua hizo. Anasema: “Hatua inayofuata ni kulipua jiwe. Tunawaita wenzetu wenye baruti, wanatoboa, wanaweka unga (baruti), kisha wanalipua. Baadaye tunatafuta kuni na kuchoma. Yakipasuka tunapiga na kukusanya”.
Joshua, Heneliko na wenzao wanaofanya shughuli hiyo hivi sasa wamepata urahisi kwani kwa sasa mawe makubwa hawayachomi kwa moto tena, bali wanayalipua kwa baruti. Wakati kwa Joshua na wenzake hiyo ni ahueni, kwa wananchi wanaoishi jirani, hali ni mbaya.
Katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Mkolani, Nyakagwe, Ngw’ashi na Bulale jijini Mwanza, uchimbaji wa mawe unafanyika karibu na makazi ya watu. Uchimbaji huu umesababisha uharibifu wa mwonekano wa ardhi, mmomonyoko wa udongo, na umeathiri bioanuai pamoja na kuhatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo.
Athari za uchimbaji wa mawe kwa mazingira
Uchimbaji huu umesababisha madhara mbalimbali. Licha ya kuathiri mwonekano wa ardhi, kusababisha mmomonyoko wa udongo, uchimbaji huo huathiri bioanuai pamoja na kuhatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo.
“Uchimbaji wa mawe hupunguza na kuharibu bioanuai kwa kuondoa makazi asilia ya viumbe hai,” anasema Juvenary Matagili, mtaalamu wa mazingira ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Muungano wa Wavuvi (FUO) jijini Mwanza, katika mahojiano na Mongabay.
Kwa mujibu wa Juvenary, kitaalamu, bioanuai inahusisha utofauti wa viumbe (mimea, wanyama na wadudu) pamoja na mifumo yao ya ikolojia. Uchimbaji wa mawe husababisha uharibifu wa makazi, ambapo miti hukatwa, udongo wa juu ya ardhi huondolewa, na miamba kubomolewa.
Anasema hali hii hupunguza idadi ya spishi na hata kusababisha kutoweka kwa baadhi ya viumbe. Mtikisiko na vumbi hubadilisha mazingira na kuathiri mienendo ya uzalishaji na uhamaji wa viumbe.
“Kwa mujibu wa sayansi ya udongo, mimea na mizizi yake husaidia kushikilia udongo na kupunguza kasi ya maji ya mvua. Uchimbaji kiholela huondoa kifuniko cha mimea na kuacha udongo wazi. Hii huongeza kasi ya mtiririko wa maji ya mvua, ambayo hubeba chembechembe za udongo, na kusababisha mmomonyoko mkali. Pia, mashimo yanayochimbwa hubadilisha mtiririko wa maji na kuongeza uwezekano wa maporomoko ya ardhi,” anasema Juvenary.
Anafafanua kuwa uchimbaji wa aina hiyo pia huvuruga uwiano wa mifumo ya ikolojia na kuharibu mwingiliano wa viumbe na mazingira yao. Pia hubadilisha muundo wa ardhi, kuathiri mzunguko wa virutubisho, na kupunguza uzalishaji wa kiasili wa mfumo.
“Mabadiliko haya huathiri minyororo na mitandao ya chakula, ambapo spishi tegemezi hupoteza chanzo cha chakula au makazi. Hali hii inaweza kusababisha kuondoa uwiano kwenye mfumo wa ikolojia na kupungua kwa uthabiti wa mazingira. Kwa ujumla, uchimbaji wa mawe unavuruga kabisa uwiano wa ikolojia, kuathiri minyororo ya chakula na kupunguza uwezo wa mazingira kujirekebisha,” Juvenary aliambia Mongabay.
Madhara kwa viumbe wanaotegemea mazingira tulivu
Laurent Kitogo, Afisa wa Mazingira kutoka Environmental Management and Economic Development Organization (EMEDO), aliiambia Mongabay kuwa shughuli za uchimbaji na upasuaji wa mawe kwa kutumia baruti huleta kelele, tetemeko na kuathiri watu na bioanuai.

“Ile sauti inayotoka wakati wa mlipuko husababisha kitu kinachoitwa “sound pollution”, yaani kelele nyingi zisizohitajika. Hiyo milipuko inakosesha watu utulivu. Lakini pia bioanuai iliyopo katika eneo hilo zinapata sauti ambayo si rafiki,” anasema.
Akifafanua, anasema sauti kubwa na mitikisiko inayosababishwa na milipuko hiyo huwaathiri wanyama wadogo wanaotegemea mazingira tulivu kwa ajili ya kuishi na kuzaliana. Kufuatia kukosekana kwa utulivu, baadhi ya viumbe huhama au kupoteza makazi yao, huku wengine wakishindwa kuendelea na mifumo yao ya kawaida ya maisha kama kutafuta chakula na kuwasiliana.
“Pili, jiwe linapopasuka linasababisha mtikisiko wa ardhi. Hali hiyo hutengeneza hofu kwa bioanuai zilizoko pale, na binadamu. Jiwe linaweza likatoka pale katika mazingira ambayo hukuyatarajia, likaruka na kusababisha madhara mengine, ikiwemo mitikisiko kwenye nyumba zilizopo pembezoni. Maeneo ambayo uchimbaji unafanyika hayapo porini; ni sehemu ambazo watu wanaishi jirani,” anasema Laurent.
Mbali na matumizi ya baruti, wachimbaji huchoma mawe kwa ajili ya kuyalainisha ili iwe rahisi kuyapasua. Kuhusu madhara ya kitendo hicho, Laurent anasema; “Kwa wale wanaochoma kwa kutumia kuni, magogo au matairi ya magari, wanatengeneza sumu ambayo watu au wanyama wanapoivuta inawasababishia madhara ya kiafya”.
Uchomaji wa matairi huzalisha gesi na kemikali hatarishi ambazo zinaweza kuathiri ngozi, macho, pamoja na mfumo wa upumuaji na kusababisha matatizo kama kukohoa, kubanwa kwa kifua na ugumu wa kupumua. Vilevile, baadhi ya kemikali zinaweza kuongeza hatari ya kupata saratani.
Kwa mujibu wa utafiti, “Athari za uchimbaji wa malighafi za ujenzi kwa njia za kienyeji katika uhifadhi wa bioanuai na maisha ya jamii zinazoishi katika Jiji la Mwanza, Tanzania”, uliochapishwa mwaka 2022 na African Journal of Social Sciences and Humanities Research, shughuli za uchimbaji holela wa mawe na usiodhibitiwa jijini Mwanza umepelekea mmomonyoko wa udongo, uchafuzi wa hewa, kupotea kwa bioanuai pamoja na athari za kiafya kwa wakazi waishio karibu na maeneo uchimbaji unapofanyika.
Joshua Masano, ambaye ni mzoefu katika uchimbaji wa mawe jijini Mwanza amekiri juu ya suala la uharibifu wa ardhi akisema kuwa uchimbaji huo huacha mashimo na kuharibu ardhi. Anasema: “Mashimo yanakuwa ni mengi. Jinsi tunavyofanya kazi, mtu anachimba hapa, anaruka anaenda pale, ardhi inakosa mpangilio. Ndiyo maana ukija mlimani unakuta pamekaa vibaya sana.”
Licha ya kuendelea kwa shughuli ya uchimbaji, sheria inawataka watu walinde mazingira na si kuyaharibu. Kifungu cha sita cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 nchini Tanzania, kinachozungumzia wajibu wa kulinda mazingira, kimeeleza kuwa kila mtu ana wajibu wa kulinda mazingira.
Mtu yeyote anayeishi Tanzania anawajibika kutunza na kuendeleza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote linaloweza kuathiri mazingira, sheria hiyo inasisitiza.
Athari za uchimbaji wa mawe kwa jamii
Wakazi wanaoishi karibu na maeneo yanapofanyika shughuli za uchimbaji na upasuaji wa mawe wamesema kuwa uchimbaji huo umesababisha makorongo ambayo yanachochea mtiririko wa maji kutoka milimani na kuleta madhara kwao na mali zao.

Maji hayo yanapopita kwa nguvu kwenye makorongo huongeza mmomonyoko wa udongo, kubomoa makazi, na kuharibu miundombinu ya kijamii kama barabara na mashamba. Makorongo pia yamesababisha kuondoka kwa tabaka la juu la udongo lenye rutuba, hali inayopunguza uwezo wa ardhi kuzalisha uoto wa asili na kilimo.
Kevin Antony, mkazi wa Ngw’ashi jijini Mwanza, anasema: “Ardhi imemeguka na kuacha makorongo makubwa sana. Maji yakitoka huko juu mlimani yanakuja mpaka huku kwenye makazi ya watu, yanaharibu mali za watu.”
Licha ya uharibifu wa mali, Kevin anasema shughuli hizi za uchimbaji wa mawe ni hatari kwa maisha ya watu. “Mawe yanapoporomoka huwaangukia watu na kuwaumiza. Wakati mwingine hata wale wanaochimba huangukiwa na kuvunjwa baadhi ya viungo,” anasema Antony.
Winifrida Buganda anasimulia kisa cha kuhuzunisha kuhusu kijana mmoja aliyepoteza maisha wakati wa uchimbaji mawe. Anasema: “Mwaka juzi (2024) pale Mlima wa Nyuki, kuna kijana alikufa baada ya kuangukiwa na jiwe wakati anachimba. Mwingine alijeruhiwa na hadi sasa ni mlemavu.”
Joshua Masano, ambaye amefanya kazi ya kuchimba na kupasua mawe tangu mwaka 2012, anasema hadi sasa ameshapoteza rafiki na baadhi ya watu wake wa karibu baada ya kuangukiwa na mawe ama kufukiwa na kifusi.
“Ukiwa ndani unasikia ‘Puuh! Puuh!’ Yaani kama una shinikisho la damu, unakufa… Huwa hawatoi taarifa. Unasikia mtikisiko hadi ndani,” analalamika Rahma Harris.
“Mtikisiko ule wa baruti unapotokea, wakati mwingine unasababisha mipasuko kwenye nyumba. Kuna kipindi fulani mwaka 2024 walipasua jiwe likaruka hadi likatoboa bati la kanisani,” anasema Kevin Antony.
“Uchimbaji huu pia ni hatari kwa watoto kwa sababu wachimbaji wanaacha mashimo makubwa ambayo kipindi cha mvua kama wakati huu, maji ni mengi, watoto wanaweza kuzama humo na kufa ama kupata madhara mengine,” anasema mkazi mmoja wa Nyakagwe.
Itakumbukwa kuwa mnamo Desemba 03, 2023, takriban watu 89 walipoteza maisha baada ya kutokea kwa maporomoko ya udongo katika mlima Hanang mkoani Manyara baada ya mvua kubwa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali ya Tanzania, sababu iliyopelekea maporomoko hayo ni kumeguka kwa sehemu ya mlima huo ambao ulikuwa na miamba dhoofu iliyonyonya maji na kusababisha mporomoko, na hivyo kutengeneza tope.
Hatua stahiki zisipochukuliwa katika jiji la Mwanza, maafa kama haya yanaweza kutokea.
Picha ya Bango: Uchimbaji mawe katika mlima huu uliopo Mkolani jijini Mwanza ukiwa umefanywa karibu na nyumba inayoendelea kujengwa. Picha na Dominic Allen, Mongabay.