- Wahifadhi wa mazingira na viongozi wa Kimasai wanaonya kuwa mradi huo unaweza kuvuruga uhamaji mkuu wa wanyamapori na kudhoofisha maarifa ya jadi ya ikolojia pamoja na maisha ya jamii.
- Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Narok ilitupilia malalamiko hayo, ikiamua kuwa mlalamikaji hakuwa ametumia njia zote zilizopo za kushughulikia malalamiko kabla ya kufikisha suala hilo mahakamani.
- Hata hivyo, mahakama haikutoa uamuzi kuhusu kiini cha kesi yenyewe.
- Mamlaka za Kenya zinasema kuwa ufuatiliaji unaonyesha hakuna athari hadi sasa katika njia za uhamaji wa wanyamapori, ingawa mtaalamu mmoja huru wa sayansi anatoa wito wa kufanyika kwa tafiti za muda mrefu zinazotegemea takwimu.
Huu ni mwisho wa sakata ambalo limevutia wapenzi wa mazingira na utalii nchini Kenya kwa miezi sita iliyopita. Mahakama ya Mazingira na Ardhi, ikifanya kikao chake mjini Narok, ilitupilia mbali ombi lililowasilishwa Agosti 2025 na Meitamei Olol Dapash, mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Wamasai, Utafiti na Uhifadhi. Mhifadhi huyo wa mazingira alikuwa akipinga ufunguzi wa Ritz-Carlton, Masai Mara Safari Camp, inayoendeshwa na Lazizi Mara Ltd.
“Mahakama inaona haina mamlaka ya kushughulikia suala hili kwa sababu kuna mifumo mbadala ya utatuzi wa migogoro ambayo haikutumiwa na mlalamikaji, hivyo kesi hii iliwasilishwa kabla ya muda wake, na mahakama imeondolewa mamlaka ya kuisikiliza. Bila mamlaka, mikono ya mahakama imefungwa,” uamuzi wa mahakama unasema.
Uamuzi wa mahakama unaeleza kuwa mlalamikaji, kabla ya kufungua shauri, alipaswa kuwasilisha malalamiko chini ya Kifungu cha 117 cha Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori, ambacho kinataka njia zote za utatuzi, ikiwa ni pamoja na zile za kijamii, zitumike, na pia kukata rufaa chini ya Kifungu cha 129 cha Sheria ya Usimamizi na Uratibu wa Mazingira.
Ili kupata taarifa zaidi, Mongabay iliwasiliana na mahakama ya Narok na mamlaka za kaunti, lakini hawakujibu ombi letu la kufanyiwa mahojiano.
Kwa mtazamo wa wahifadhi wa mazingira kama Johnson Yiamat, uamuzi huo unatuma ujumbe usio sahihi. “Ninahisi kwamba matokeo ya kiutaratibu hayapaswi kufunika kiini cha hoja zilizowasilishwa,” alisema kupitia ujumbe aliotuma kwa Mongabay.
Yiamat ni Mmasai na mwanzilishi wa Osotua Green Alliance, shirika linaloongozwa na jamii lililojikita katika masuala ya uhifadhi wa bioanuwai, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uwezeshaji wa jamii.
“Mjadala kuhusu Ritz-Carlton Masai Mara Safari Camp haukuwa tu wa kisheria, bali pia ulihusu uangalifu wa kiikolojia, sauti ya jamii na usimamizi wa muda mrefu wa Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara,” aliongeza, kabla ya kubainisha kwamba kwa uzoefu wake, mara nyingi walalamikaji huamriwa kulipa gharama za kesi nchini Kenya wanaposhindwa shauri.

Ritz-Carlton Masai Mara Safari Camp ina vyumba 20 vya kifahari vya kujitegemea, bwawa la kuogelea, huku bei ya kila usiku ikianzia $3,500, kiasi ambacho ni takriban asilimia 30 zaidi ya wastani wa kipato cha mwaka wa mtu, kulingana na Benki ya Dunia.
Hata hivyo, kiini cha utata uliopo siyo anasa hiyo ya kupindukia ya kambi hiyo. Badala yake, tatizo kuu ni eneo lake: ni ndani ya eneo lililohifadhiwa kando ya Mto Sand, kwenye njia ya uhamaji wa wanyamapori. Njia hii ya uhamaji ni miongoni mwa maeneo maarufu zaidi ya wanyamapori duniani.
Kila mwaka kati ya Juni na Oktoba, uhamaji mkuu wa wanyamapori hushuhudia takriban nyumbu milioni 2 na wanyama wengine wanaokula majani wakihama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara nchini Kenya kuelekea Tanzania kutafuta malisho mapya, huku wakiwa chini ya uangalizi wa mara kwa mara wa wanyama walao nyama.
Tukio hili ni la kuvutia kiasi kwamba watalii husafiri kutoka sehemu mbalimbali za dunia kulishuhudia, wakivutiwa na mwendo wa makundi ya wanyama pamoja na mwingiliano wa kusisimua kati ya wanyama wanaowinda na wanaowindwa, jambo ambalo ni chanzo kikubwa cha mapato katika sekta ya utalii ya Kenya.
Hifadhi ya Maasai Mara hupokea wageni zaidi ya 300,000 kila mwaka, na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka. Tangu baada ya janga la COVID-19, ongezeko la wageni wa kimataifa pamoja na wale wa tabaka la kati, linaloendelea kukua, limechochea ukuaji mkubwa wa sekta ya hoteli za kifahari nchini Kenya.

Goliathi anapomshinda Daudi
Lakini kulingana na mwongozo rasmi wa uendeshaji wa usimamizi wa hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara, hakuna hoteli inayopaswa kujengwa katika eneo hilo hadi itakapofika mwaka 2032.
Hata hivyo, kulingana na nyaraka rasmi ambazo kituo cha televisheni cha Citizen, cha Kenya kiliona, inaonekana kwamba ofisi ya Rais wa Kenya William Ruto yenyewe iliidhinisha ruksa inayoruhusu ujenzi wa hoteli ya kifahari katika eneo hili maalum, licha ya vizuizi vilivyo kwenye mpango wa usimamizi.
Shivan Patel, mkurugenzi mkuu wa Lazizi Mara, alijibu maswali ya kituo hicho cha habari akisema kwamba ruksa yao haikuwa tukio la kipekee, bali waliupata baada ya kufuata utaratibu rasmi, ikiwa ni pamoja na kuwa na Tathmini ya Athari kwa Mazingira.
Lakini kwa jamii ya wanasayansi, idhini ya rais haimaanishi kwamba hatari zote zimeondolewa.
“Ni dhahiri kwamba kambi hiyo ya kifahari imejengwa katika moja ya njia zinazopendwa zaidi na wanyama, kwa sababu wanahitaji watalii waweze kuona wanyama, nyumbu, wakivuka,” alisema Isla Duporge, msomi anayefanya utafiti, aliyepata shahada ya uzamivu katika Idara ya Ikolojia na Biolojia ya Chuo Kikuu cha Princeton, ambapo amechunguza Uhamaji Mkuu kwa kutumia teknolojia ya satelaiti na akili bandia.”


Kutokana na umuhimu wa kipekee wa eneo hilo, suala hili likiwa na taswira ya pambano la Daudi dhidi ya Goliathi, lilishika kasi haraka. Lilisambaa kupitia vyombo vya habari vya jadi na mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mkubwa kwa umma.
Kama ilivyo kwa Olol Dapash, wahifadhi wa mazingira wana hofu kwamba kuziba njia za uhamaji kunaweza kulazimisha wanyama kupita njia hatarishi, jambo ambalo linaongeza vifo na kuvuruga mifumo ambayo imekuwa ikiendeleza mifumo hii ya ikolojia kwa karne nyingi.
Jamii ya Wamasai, ambayo imeishi katika ardhi hizi kwa vizazi vingi, pia ina hofu kuhusu athari kulingana na maarifa ya jamii waliyo nayo.
“Tumeishi pamoja na wanyamapori wanaohama kwa karne nyingi, tangu enzi za mababu zetu wa zamani,” alisema Yiamat. “Mwendo wa wanyama unatupa maarifa ya kiikolojia; unatupa uwezo wa kuelewa mifumo ya mvua, urejeaji wa malisho, na upatikanaji wa maji pia.”
Kijadi, Wamasai ni wafugaji mashujaa wanaohamisha ng’ombe na kondoo wao kulingana na mizunguko ya malisho. Ikiwa Uhamaji Mkuu wa wanyama utabadilishwa, madhara yanaweza kuwa makubwa. “Maarifa ya jadi ya kiikolojia yatapotea, na hatutajua tena wapi pa kupeleka mifugo yetu kulisha kwa usalama. Kutakuwa na kudhoofika kwa mila zetu na vyanzo vyetu vya riziki,” alisema Yiamat.

Hata hivyo, miezi michache baada ya kesi hiyo kupata umaarufu, Olol Dapash aliacha kuizungumzia hadharani. Katika hotuba kwa njia ya video aliyoitoa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa Novemba, alisema: “Imetolewa amri ya muda ikinipiga marufuku kujadili baadhi ya masuala yanayohusiana na kesi hii.”
Huku akisisitiza msimamo wake wa kuheshimu mchakato wa mahakama wa Kenya, aliongeza: “Tutaendelea, hata baada ya kesi hii, kutetea usimamizi sahihi, ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori katika Hifadhi ya Wanyama ya Maasai Mara. Pia tunapaswa kuendelea kupigania haki za watu wa Kimaasai.”
Lakini tarehe 16 Desemba, mwaka 2025, Dapash aliamua kuiondoa kesi hiyo kabisa. Kufikia wakati huo, alikuwa tayari amechelewa, kwani suala hilo lilikuwa tayari limekuwa la maslahi ya umma.
“Maslahi ya umma yaliyowasilishwa awali katika kesi hayataathirika kutokana na kuondolewa kwa kesi,” mahakama ilitoa uamuzi wa awali kabla ya kuifuta kabisa tarehe 26 Februari. Mbali na kufuta kesi, mahakama ilimwamuru Olol Dapash kulipa gharama zote za kesi bila kubainisha kiasi. Mongabay ilijaribu kuwasiliana naye kwa maelezo zaidi lakini haikufanikiwa.
Kwa upande wake, Yiamat alisema anaona uamuzi huu kama aina ya vitisho, njia ya kunyamazisha jamii. “Katika mazingira ambapo jamii au watu binafsi wanajaribu kupinga miradi ndani ya mifumo nyeti ya ikolojia kama Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara, hatari ya kifedha ya kufungua kesi inaweza kuwa ya kutisha. Ikiwa mzigo wa gharama utakuwa mkubwa sana, unaweza kuwakatisha tamaa wananchi wa kawaida, viongozi wa jamii au watetezi wa mazingira kuibua masuala halali ya mazingira siku zijazo,” alisema.

Mamlaka zinasema wanyamapori hadi sasa bado hawajaathirika
Msimu mmoja wa kuvuka kwa nyumbu tayari umeshapita, na kulingana na Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS), ambalo ni shirika la serikali unaohusika na ulinzi wa wanyamapori, hakuna tukio lolote lililoripotiwa.
“Takwimu za ufuatiliaji wa muda mrefu zinaonyesha wazi kwamba eneo la kambi ya safari ya Ritz-Carlton na kambi nyingine tano za safari kando ya Mto Sand… halipo ndani ya, halizuii, wala haliingilii njia zozote za uhamaji wa nyumbu,” KWS ilisema katika taarifa yake.
Kwa upande wa Duporge, maoni ya KWS hayashangazi. “Nyumbu huvuka katika eneo kubwa sana, kama maili 42 (sawa na kilomita 68),” alieleza. “Kwa sababu wanavuka katika eneo kubwa hivyo, jambo hili halitakuwa na athari kubwa sana kwa uhamaji, kwani kuna maeneo mengine mengi kando ya mto wanayoweza kuvukia.”
Kutoka katika mtazamo wa kibaolojia, aliongeza, itakuwa jambo la kushangaza iwapo wanyama hawataweza kuzoea kizuizi hiki kipya. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kufanya tafiti za muda mrefu badala ya uchunguzi wa muda mfupi ili kujihakikishia kuwa wanyamapori hawaathiriwi na ujenzi wa kambi hiyo ya kifahari.
“Sijui ni kwa kiwango gani nyumbu wanatumia njia hii… nafikiri takwimu tulizonazo kuhusu hilo bado ni dhaifu,” alisema, akibainisha kuwa hajafanikiwa kuona tathmini ya athari za kimazingira na kijamii ya mradi huo ili kuthibitisha matokeo yake.

“Swali la msingi ni kama kambi hiyo ya kifahari imejengwa katika eneo muhimu la kuvuka linalotumiwa na makundi makubwa sana ya nyumbu,” alisema Duporge. “Nadhani kampuni zinapaswa kutumia data za satelaiti katika tathmini zao za athari za mazingira, kwa kulinganisha hali kabla ya ujenzi, wakati wa ujenzi, na baada ya mwaka mmoja ili kutathmini athari halisi kwa mtazamo mpana zaidi.”
Kwa upande wake, KWS linasema katika taarifa kwamba kambi hiyo ya kifahari haitendewi haki kwa kutwishwa malalamiko isivyostahili. “Kando ya Mto Sand pekee, kuna kambi tano za kudumu za safari na zaidi ya kambi mbili za msimu, na hakuna hata moja iliyopata kulalamikiwa kwa kiwango ilichofanyiwa Kambi ya Safari ya Ritz-Carlton,” shirika hilo lilisema, likiongeza kuwa nyaraka zote zinazohitajika, ikiwemo tathmini ya athari za kimazingira na kijamii, ziliwasilishwa kabla ya ujenzi.

Katika utafiti wa athari za kijamii na kimazingira, kampuni inapaswa kubainisha hatari zinazoweza kusababishwa na mradi wake kwa jamii ya eneo husika na kwa bioanuwai, pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kupunguza hatari hizo. Hata hivyo, nyaraka hizi bado hazijawekwa wazi kwa umma, jambo linaloendelea kuchochea mjadala na utata.
Tangu mwaka 2023, hadi 2032, ujenzi wa kambi mpya ndani ya hifadhi hiyo ulipigwa marufuku rasmi ili kupunguza athari za utalii kwa wanyamapori. Hata hivyo, kulingana na gazeti la Uingereza, The Times, “Mwezi Aprili mwaka 2024, Felix Koskei, mkuu wa wafanyakazi wa rais wa Kenya William Ruto, aliiomba Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kutoa ‘ruksa ya mara moja’ wa kusitisha marufuku hiyo ili kuruhusu maendeleo ya mradi wa Ritz-Carlton.”

Ruksa hii iliyotolewa licha ya kuwepo kwa katazo, imeibua maswali. “Nadhani kiwango cha uchunguzi kutoka kwa vyombo vya habari vya kimataifa ambacho mradi huu maalum umepata ni jambo zuri sana,” alisema Duporge.
“Katika siku zijazo, wao (waendelezaji) watalazimika kuhakikisha wanafanya vizuri tathmini ya athari za mazingira, na wanashirikisha jamii za eneo husika, vinginevyo watakumbana na tatizo hilo hilo. Lazima suala hili limeathiri sana sifa ya mradi huu kuona dunia nzima ikiutazama na kusema, ‘hili halikubaliki.’ Hivyo, huenda katika siku zijazo miradi mingine italazimika kufanya mambo kwa njia tofauti.”
Mongabay iliwasiliana na timu ya kambi ya safari ya Ritz-Carlton ili kupata maelezo zaidi. Walijibu kwa taarifa iliyoandikwa kupitia barua pepe wakisema: “Hatutoi maoni kuhusu tathmini za sifa au dhana zisizo na uhakika. Lengo letu linaendelea kuwa kuendesha shughuli kwa uwajibikaji, kutimiza matakwa ya sheria na kuendelea kufuata viwango vya kimazingira na kisheria vinavyotumika katika hifadhi. Kama sera ya kampuni, hatutoi taarifa kuhusu idadi ya wageni au utendaji wa kibiashara.”
Huenda kesi imefutwa, lakini wasiwasi wa kimazingira bado upo. Iwapo nyumbu wataendelea kuvuka bila kuathiriwa au watabadilisha njia zao taratibu kwa muda, huenda itajulikana wazi baada ya miaka kadhaa ijayo.

Picha ya Bango: Sehemu ya Uhamaji Mkuu, kundi la nyumbu wanajipanga kuvuka Mto Mara katika Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara. Picha na Danijel Mihajlovic kupitia Wikimedia Commons (CC BY-SA 4.0).
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 07/04/2026.