- MKWC kupokea swala 4 wa milimani kutoka Ulaya kuongeza idadi yao.
- Uhamisho ni matokeo ya ushirikiano wa kimataifa na mpango wa miaka 11.
- Idadi porini imeshuka sana kutokana na ujangili na uharibifu wa makazi.
- Teknolojia na uzalishaji hifadhi kusaidia kuongeza idadi hadi 2050.
NYERI, Kenya – Hifadhi ya Wanyamapori ya Mount Kenya (MKWC) iko mbioni kupokea swala wa milimani wanne kutoka bustani za wanyama za Ulaya, hatua inayolenga kuongeza idadi ya miongoni mwa swala walio hatarini zaidi kutoweka barani Afrika.
Uhamisho wa swala hao wa kiume uliongozwa na wataalamu kutoka bustani ya Wanyama ya Chester nchini Uingereza, kwa ushirikiano na Shirika la Huduma za Wanyamapori la Kenya (KWS) pamoja na European Association of Zoos and Aquaria (EAZA), na the European Association of Zoos and Aquariums.
Katika taarifa iliyotumwa kwa Mongabay, Bustani ya Chester ilisema wataalamu wake walitumia zaidi ya miaka 11 kuratibu mpango wa uzalishaji (breeding program) katika bustani za uhifadhi barani Ulaya.
“Swala hawa wanne wa kiume walioteuliwa kwa kuzingatia umri, afya na vinasaba: watakuwa wa kwanza kabisa kuhamishwa kutoka bustani za wanyama za Ulaya kwenda Kenya kama sehemu ya juhudi za kurejesha spishi hii porini.”
“Ushirikiano kama huu ni muhimu sana ikiwa tunataka kuzuia spishi hii adimu kutoweka kabisa,” Nick Davis, Meneja Mkuu wa Mamalia katika Bustani ya wanyama ya Chester na mratibu wa mpango wa uzalishaji wa Ulaya, alisema katika taarifa hiyo.
“Unaonyesha jinsi bustani za kisasa za wanyama zinazoongozwa na sayansi zinavyochangia kwa kiasi ikubwa urejeshaji wa spishi hizi zilizo katika hatari ya kutoweka”.
Tathmini ya mwaka 2016 ya IUCN ilibainisha kuwa swala hawa wanaoishi misituni walikuwa katika hatari kubwa ya kutoweka ambapo idadi ya wale waliofikia umri wa kukomaa waliobaki porini walikuwa kati ya 70 hadi 80. Idadi hii ilikuwa ya wanyama wote wa aina hii walioko nchini Kenya.
Katika muongo uliopita, swala wa milimani (Tragelaphus eurycerus ssp. isaaci) waliongeza idadi yao ndani ya kipindi kifupi. Ripoti ya sensa ya kitaifa ya wanyamapori Kenya inaonyesha kuwa mwaka 2021 kulikuwa na takriban swala 150 porini, lakini kufikia mwaka 2025 walikuwa wamepungua hadi 66.
Wataalamu wa Kenya wanahusisha kupungua kwa spishi hii na mchanganyiko wa uharibifu wa makazi yao pamoja na ujangili.
Wakati idadi ya waliopo porini ikipungua, wale walioko katika hifadhi (captivity) wanaongezeka. Kulingana na sensa hiyo, idadi yao iliongezeka “kutoka 54 mwaka 2021 hadi 93 kufikia mwaka 2025.” Aidha, swala wengine 17 walirudishwa kutoka Marekani.
Baada ya swala hao wanne wa kiume kukamilisha “uchunguzi mkali wa afya na karantini,” watasafirishwa kwa ndege hadi Kenya, ambapo watafuatiliwa kwa karibu kabla ya kuingizwa katika mpango wa uzalishaji.
“Hawa swala wa kiume ni sehemu muhimu ya mpango wetu wa kurejesha spishi hii porini,” alisema Robert Aruho, mkuu wa hifadhi ya MKWC.
“Kwa sasa MKWC ina zaidi ya swala 100 katika mpango wa uzalishaji, huku mwelekeo ukiwa uzalishaji endelevu chini ya malengo ya muda mrefu ya taifa ya kuongeza idadi ya swala hadi angalau 750 ifikapo mwaka 2050,” alisema Aruho katika taarifa yake kwa Mongabay.
Teknolojia pia inaendelea kusaidia juhudi za uhifadhi. Chester ilisema ilishirikiana na wadau, wakiwemo Chuo Kikuu cha Liverpool John Moores, “kuunda mfumo wa kwanza duniani wa utambuzi wa swala wa milimani unaotumia akili bandia (AI), kamera zinazotoa taarifa za wakati halisi kuhusu tabia, mienendo na afya ya wanyama hao bila kuwasumbua.”
Maendeleo kama haya ya teknolojia ya uhifadhi, pamoja na mafanikio ya programu za uzalishaji na juhudi za kimataifa za kurejesha spishi, “yataweza kubadilisha mwelekeo wa hatma ya swala wa milimani,” alisema Stuart Nixon, Meneja Mwandamizi wa Programu wa Chester, barani Afrika katika taarifa yake kwa Mongabay.
Picha ya Bango: Swala wa milimani aliye hatarini kutoweka akiwa kwenye Bustani ya Chester, Cheshire, Uingereza. Picha kwa hisani ya Chester Zoo.
Taarifa hii ilichapishwa hapa kwa mara ya kwanza kwa Kiingereza mnamo 03/04/2026.