- Tume mbili za Rais Samia ziliwasilisha ripoti zikibaini kuwa zoezi la uhamaji Ngorongoro halikushirikisha wananchi kikamilifu na limefanikiwa kwa asilimia ndogo sana (takriban asilimia 7 tu ya kaya kuhama).
- Wananchi walikataa kuhama kwa hofu ya kupoteza utamaduni, maeneo ya ibada na mfumo wao wa maisha, huku pia wakilalamikia kuondolewa kwa huduma za jamii.
- Ongezeko kubwa la watu na mifugo limezidisha mgogoro wa matumizi ya ardhi, kuharibu mazingira na kusababisha kupungua kwa baadhi ya wanyamapori pamoja na migongano kati ya binadamu na wanyama.
- Tume zimependekeza ushirikishwaji zaidi wa wananchi, maboresho ya sheria na mifumo ya usimamizi, pamoja na kuanzishwa kwa chombo huru cha kuratibu uhamaji na takwimu sahihi za wakazi.
Hili ni toleo la kwanza katika mfululizo wa makala kuhusu mgogoro wa Ngorongoro, Kaskazini mwa Tanzania. Soma toleo la pili hapa.
Hatimaye tume mbili zilizoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan mnamo mwezi Desemba mwaka 2024, moja kuchunguza zoezi la kuhama kwa hiari kwa wakazi wa Ngorongoro, na nyingine kuchunguza migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo, zimewasilisha ripoti na kutoa mapendekezo yao.
Tume hizo ziliundwa kwa lengo la kufanya tathmini ya kina na shirikishi kuhusu hali halisi ya migogoro ya muda mrefu katika eneo la Ngorongoro na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupata suluhisho la kudumu.
Tume ya kwanza iliongozwa na Musa Iyombe ambaye ni Katibu Mkuu Mstaafu. Wajumbe wengine saba na nafasi zao ni; Sihaba Nkinga- Katibu Mkuu Mstaafu; Alphayo Kidata; Mohamed Mtonga; Valentino Mlowola, Balozi na Mkurugenzi wa Amani, PCCB; George Madafa, Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC); Edward Maura Nduleti na Rehema Moisare wote wakazi wa Ngorongoro.
Tume hii ilizinduliwa rasmi tarehe 20 mwezi Februari mwaka 2025 na kuanza kazi rasmi tarehe 25 Februari mwaka huo.
Tume ya pili iliongozwa na Gerald Ndika ikiwa na wajumbe wengine ambao ni Philemon Luhanjo ambaye ni Katibu Mkuu Mstaafu, Zakia Meghji ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Jaji George Masaju (Baadaye alijiondoa baada ya uteuzi wake kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani).
Wengine ni Richard Muyungi ambaye ni Mshauri wa Rais katika masuala ya Mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi, Salome Sijaona, Wilbard Kombe kutoka chuo Kikuu cha Ardhi; Emmanuel Luoga kutoka chuo Kikuu cha Kilimo cha SUA; Mollel James Moringe ambaye ni diwani na Katibu wa Baraza la Wafugaji pamoja na Moi Aprakwa Sikorei ambaye pia ni diwani.
Tume zote zilitarajia kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku 90 lakini katika hali iliyozua maswali mengi, hilo halikutokea hadi Machi 12, 2026, zilipowasilisha ripoti zake kwa Rais Samia, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Yaliyobainika: Tume ya kuchunguza kuhama kwa hiari
Mwenyekiti wa tume hiyo ya kuchunguza zoezi la kuhama kwa hiari kwa wakazi wa Ngorongoro, katika ripoti yake alibainisha mambo kadhaa ambayo uchunguzi wao ulibaini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, yafuatayo ni mambo makubwa yaliyobainishwa:
Zoezi la kuwahamisha wananchi halikuwa shirikishi
Zoezi la kuwahamishwa kwa hiari wakazi wa Ngorongoro kwenda katika vijiji vya Kitwai B kilichoko wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na Msomera na Saunyi vilivyoko wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga, lilifanyika bila kuwashirikisha wenyeji ili wafanye maamuzi.
Tume ilibaini pia kuwa wananchi hawakuhama kwa hiari yao bali kwa ushawishi wa serikali.
“Suala la ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi katika eneo la Ngorongoro wakati wa zoezi la uhamaji wa hiari halikuwa shirikishi katika kuandaa na kutekeleza mpango wa uhamaji. Zoezi liliendeshwa kwa mbinu ya ushawishi wa kuhama badala ya ushirikishwaji wa wananchi ili waamue wenyewe,” alisema Iyombe wakati akiwasilisha ripoti ya tume.
Zoezi halikufanikiwa kufikia malengo yake ya kuhamisha idadi kubwa ya wakazi wa Ngorongoro kwani hadi wakati ripoti ilipowasilishwa, ni asilimia 7 tu ya kaya zilikuwa zimehama licha ya zoezi hilo kuanza tangu mwaka 2022.
Mongabay imeelezwa kwamba wenyeji wa Ngorongoro wana sababu za msingi zilizowafanya wahofie kuhama kutoka eneo hilo. Sababu ya kwanza ni ya kiutamaduni ambapo ilidaiwa kuwa, wengi walihisi wakihama, utamaduni na asili yao vingepotea.
Sababu ya pili ni ya kiimani ambapo inaelezwa kuwa wakazi wa Ngorongoro wanafanya ibada zao za jadi katika baadhi ya milima, mchanga unaohama pamoja na kreta hasa kipindi ambacho vijana huhama rika. Katika hilo, hofu yao ilikuwa ni kupoteza maeneo muhimu ambayo kwao siyo tu ya kifugaji bali ya ibada.

“Wakati tume inatoka eneo walikohamishiwa kulikuwa na kaya 1,678 sawa na asilimia 7.3 tu ya kaya 23,000 zinazoishi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro. Hizo kaya 1,678 ndiyo zilizohamia makazi mapya zikiwa na mifugo 40,593 sawa na asilimia 5.7 ya mifugo 715,496 iliyokuwa ndani ya eneo la hifadhi. Kwa takwimu hizi, utaona kabisa kwamba zoezi halikufanikiwa kama ilivyotarajiwa, alisema Iyombe.
Nyumba zilizojengwa katika vijiji vitatu vya Msomera, Kitwai B na Saunyi zilijengwa bila kuzingatia uhalisia wa maisha ya jamii husika. Kulikuwa na kaya nyingine ambazo mwanamume mmoja ana wake zaidi ya watatu lakini walipofika makazi mapya, wakashangaa kukuta nyumba ni moja tu.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya wanaume waliohamia huko kukosa mahali pa kuwaweka wake zao wengine. Miongozo iliyotumika katika zoezi la kuhamisha wakazi wa Ngorongoro ilibadilika kila awamu. Changamoto hii ilisababisha kusuasua kwa zoezi la watu kuhamia maeneo yaliyoandaliwa.
“Moja ya masuala yaliyosababisha zoezi la uhamaji wa hiari kusuasua, ni kubadilika kwa muongozo uliohusu kutoa motisha kwa baadhi ya kaya zilizohama awamu ya kwanza na awamu ya pili. Katika awamu ya kwanza iliyohusisha nyumba 103, kila kaya ilipata nyumba na motisha ya shilingi milioni 10.
“Mabadiliko ya miongozo yaliyofanyika katika awamu ya pili, yalimtambua mkuu wa boma na kupewa motisha ya shilingi milioni 10, na nyumba moja tu hata kama huyu mkazi ana wake zaidi ya mmoja, ikimaanisha kwamba ana kaya zaidi ya moja,” alisema Iyombe.
Waliobaki Ngorongoro waliondolewa huduma za jamii
Suala lingine ambalo tume iligundua ni kuibuliwa kwa mambo kadhaa ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yakilalamikiwa na wenyeji waliobaki katika eneo la Ngorongoro.
Baadhi ya malalamiko kutoka kwa wananchi waliobaki ndani ya eneo la hifadhi ni kwamba waliondolewa huduma za jamii, kuhamishwa kwa fedha za miradi ya maendeleo, kufutwa kwa vijiji ndani ya eneo la Tarafa ya Ngorongoro (ambalo tayari serikali imelishughulikia), kufutwa kwa baraza la wafugaji, kubadilishiwa vituo vya kupigia kura (hili nalo tayari serikali imeshalifanyia kazi) na kuwekewa vikwazo vya kuingia ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
Kabla ya zoezi hilo kufanyika, hakuna tamko lolote lilitolewa na serikali kwa wananchi. Ilidaiwa kuwa Machi 14, 2022, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, alipokea barua kutoka TAMISEMI, ikielekeza kuwa pesa za maendeleo takriban milioni 160 zilizoingizwa katika Halmashauri ya Wilaya Ngorongoro, zinatakiwa kuhamishwa kwenda Wilaya ya Handeni kwa mujibu wa Wizara.
“Nimepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI yenye kumbukumbu namba BD.291,298/03/281 ya tarehe 14 mwezi wa tatu 2022 inayohusu mada tajwa hapo juu kuhusu pesa za miradi ya UVIKO-19 zilizoingizwa katika akaunti zenu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na bweni, kuwa fedha hizo zihamishiwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,” sehemu ya barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro kwenda kwa Wakuu wa shule za Msingi Endulen, Misigyo na Esero, ilieleza.
Idadi halisi ya wakazi wa Ngorongoro haijulikani
Kupata idadi halisi ya wakazi wa Ngorongoro ilikuwa changamoto kwani hata Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority), haina rejista maalum yenye orodha ya wakazi wa eneo hilo. Tume imetilia shaka takwimu zilizopo ambazo ni kutoka Mamlaka ya Takwimu Tanzania tu.
“Pamoja na uwepo wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tume ina maoni kuwa zipo changamoto za idadi halisi ya wakazi kutokana na kukosekana kwa rejista ya watu na mifugo. Vilevile, Ofisi ya Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro haina takwimu halisi za idadi ya watu wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi”.
Mapendekezo ya yume ya kutathmini uhamaji Ngorongoro
Kufuatia mambo yaliyobainika katika uchunguzi wa kutathmini zoezi la uhamaji Ngorongoro, tume ilitoa mapendekezo kadhaa.
Uandaliwe mpango unaoshirikisha wananchi, wadau muhimu
Suala la ushirikishwaji wa watu ambao ni wenyeji wa Ngorongoro pamoja na wadau wengine muhimu, litiliwe mkazo katika utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari.
Elimu ya kutosha itolewe kwa wakazi pamoja na viongozi wa kimila na kidini waliopo eneo la Ngorongoro. Mpango utakaoandaliwa uzingatie utoaji wa elimu katika ngazi zote muhimu, ikiwemo kuwashirikisha wananchi husika, viongozi wa kimila (malaigwanani), madiwani, viongozi wa Serikali, viongozi wa kisiasa na viongozi wa dini.
Kutokana na nyumba zilizojengwa Saunyi, Msomera na Kitwai B kutokuwa na wakaaji, tume ilipendekeza Serikali isitishe ujenzi wa nyumba hizo na badala yake wananchi wapewe kiasi cha pesa ambacho kimekubaliwa. Lengo ni kufanya wananchi kuamua wenyewe aina ya nyumba inayoendana na utamaduni na mila zao.
Kuhusu malalamiko ya wananchi ya kusitishwa kwa huduma za jamii katika eneo la Ngorongoro, tume ilipendekeza kuwa serikali inatakiwa iendelee kutoa huduma hizo kwa wenyeji waliobaki Ngorongoro. Lakini tume ilisisitiza kuwa huduma hizo zitolewe kwa kutumia miundombinu iliyopo na si kujenga mipya.
Kiundwe chombo kinachojitegemea kuratibu uhamaji
Kwa vile utaratibu wa uhamaji uliotumika haufanikiwa kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri, tume ilipendekeza kiundwe chombo kinachojitegemea kitakachoratibu zoezi la uhamaji wa wakazi wa Ngorongoro.
“Zoezi la uhamaji wa hiari liendelee kwa kuratibiwa, kusimamiwa na kutekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia maboresho yaliyoshauriwa na tume hii. Hivyo, uhamaji wa hiari uendelee kwa wananchi kwenye maeneo yaliyotengwa na serikali ya Kitwai B, Msomera, Saunyi na maeneo mengine,” alisema mwenyekiti wa tume hiyo.
Baraza la Wafugaji ambalo lilianzishwa rasmi mwaka 1998 lirudishiwe mamlaka yake ya kusimamia fedha zake. Ikumbukwe kuwa baraza hili liliundwa likiwa ni chombo cha jamii kusaidia uchumi wake pamoja na kuunganisha sauti za wafugaji.
Kwa sababu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro haina takwimu sahihi ya wenyeji wanaoishi katika eneo hilo, tume ilipendekeza kuwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa utaratibu wa kupata takwimu sahihi za wenyeji wa eneo la Ngorongoro.
Yaliyobainika: Tume ya Rais ya Kushughulikia Mgogoro wa Ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro
Mwenyekiti wa tume hiyo, Gerald Ndika katika ripoti yake alibainisha mambo kadhaa ambayo uchunguzi wao ulibaini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, yafuatayo ni mambo makubwa yaliyobainishwa:
Ongezeko la idadi ya watu na mifugo
Kuwepo kwa ongezeko la idadi ya watu ikilinganishwa na kipindi Hifadhi ya Ngorongoro inaanzishwa, jambo linaloongeza mahitaji ya ardhi kwa matumizi ya maendeleo ya jamii, utalii na shghuli zingine.
“Idadi ya watu ndani ya hifadhi imeongezeka kutoka takriban 8,000 waliokuwepo mwaka 1959, hadi kufikia watu 100,793 mwaka 2022. Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu za mwaka 2022, idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia watu 276,651 ifikapo mwaka 2050, wastani wa ukuaji wa asilimia 3.6 kwa mwaka.

Ongezeko hili la idadi ya watu linaenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya matumizi ya ardhi na hivyo kuongeza ushindani wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii, kwa kuwa ukubwa wa ardhi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hauongezeki,” alisema Ndika wakati akiwasilisha ripoti ya tume kwa Rais.
Kwa mujibu wa tume hiyo, ongezeko la watu katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro yaani NCA, licha ya kusababisha ushindani wa matumizi ya ardhi, limeleta uharibifu wa mazingira na kupungua kwa nyanda za malisho kutokana na ongezeko la makazi. Kwa mujibu wa tume hiyo, kuna ongezeko la makazi la asilimia 28.8 kutoka mwaka 2019 hadi 2025.
“Makazi yameongezeka ndani ya eneo la hifadhi kutoka 13,381 yaliyokuwepo mwaka 2019 hadi kufikia 17,784 kwa mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 28.8,” alisema Ndika wakati akiwasilisha ripoti.
Kuwepo kwa ongezeko la mifugo katika eneo hilo, jambo ambalo iwapo litaendelea hivyo hadi mwaka 2050, basi itakuwa ngumu kupata malisho.
“Kuna ongezeko la mifugo kutoka 261,723 mwaka 1960 hadi kufikia mifugo 715,466 mwaka 2022. Idadi hiyo ya mifugo iliyoongezeka inajumuisha ng’ombe 274,943, mbuzi 201,938, kondoo 226,553 na punda 11,032.
“Kwa mujibu wa tathmini ya Tume, inakadiriwa kuwa idadi ya ng’ombe pekee itaongezeka kutoka 274,943 takwimu ya mwaka 2022 hadi kufika ng’ombe 418,913 ifikapo mwaka 2050, wastani wa ukuaji ukiwa ni asilimia 2.7 kwa mwaka, na hivyo kuongeza mahitaji zaidi ya ardhi ya malisho.”
Tume ilisema kuwa inahofia kuwa hadi mwaka 2050, eneo lote la Hifadhi ya Ngorongoro haitatosheleza kwa matumizi ya mifugo pekee.
“Tathmini imeonesha kuwa mwaka 2022 mifugo ilihitaji eneo la kilomita za mraba 4579 sawa na asilimia 56.4 ya eneo lote la hifadhi ya Ngorongoro ya kilomita za mraba 8122.7.
“Mahitaji hayo yanakadiriwa kuongezeka hadi kufikia kilomita za mraba 8464.56, sawa na asilimia 104 ya eneo lote la hifadhi ifikiapo mwaka 2050. Hii ina maana kuwa hata kama wanyama pori na makazi vitaondolewa, eneo hilo halitatosha kwa matumizi ya mifugo pekee ifikapo mwaka 2050,” ilisema ripoti ya tume.
Baadhi ya wanyama wameanza kupungua
Tume hii ilieleza kuwa kutokana na ongezeko la watu pamoja na uhitaji wa eneo la makazi, kuna aina ya wanyama ambao wameanza kupungua katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kuanzia kuanzishwa kwake hadi hivi sasa. Baadhi ya wanyama hawa ni jamii ya swala pamoja na nyumbu.
“Swala jamii ya Thomson (Thomson Gazelles), wamepungua kutoka swala 5,000 mwaka 1965 hadi swala 1,500 mwaka 2019. Grant Gazelles nao wamepungua kutoka 1,700 mwaka 1965 hadi swala 400 mwaka 2019.
“Pia kuna upungufu wa nyumbu wenyeji (Resident Wildbeest) kutoka 1,600 mwaka 1960 hadi nyumbu 600 mwaka 2020. Kupungua au kutoweka huko kwa wanyamapori kunahusishwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi ndani ya hifadhi,” Ndika wakati akiwasilisha ripoti ya tume yake.
Ndika aliongeza kuwa kumekuwa na mgongano kati ya binadamu na wanyamapori, hali inayosababisha vifo pamoja na watu kuumizwa. Aidha alisema mwingiliano na mgongano huo pia umesababisha hasara kwa upande wa mifugo ambayo iliuawa na wanyamapori katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2015-2025.
“Takwimu zinaonesha kuwa wastani wa watu saba wamekuwa wakiuawa na wanyamapori kila mwaka kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana 2025, na kufanya jumla ya watu waliouawa katika kipindi hicho kufikia 77. Pia watu 274 walijeruhiwa, na pia mifugo 1,450 iliuawa na wanyamapori katika kipindi hicho,” alisema mwenyekiti wa tume hiyo.
Uharibifu wa mazingira
Kuwepo kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za binadamu katika maeneo haya kumeibuliwa na tume. “Changamoto nyingine ni uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ambao unasababisha kupungua kwa uoto wa asili ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro,” ripoti ya tume ilieleza.
Katika matokeo ya jumla ya uchunguzi wa tume hii, Ndika alibainisha kuwa mifumo ya Laigwanan kwa Wamasai, na mabaraza ya wazee kwa Wasonjo vinapishana na mifumo ya Serikali katika suala la ardhi. Tume zote zinasisitiza kutolewa elimu kwa viongozi wa kimila kwani ndiyo wanaosikilizwa na wananchi linapokuja suala la ardhi katika jamii za kifugaji.
Katika hatua nyingine, Tume imebaini kuwa huenda kuna mashirika yasiyo ya kiserikali, yaani yanasikilizwa sana katika eneo la wilaya ya Ngorongoro, na baadhi yake yanafanya kazi inayokinza na Serikali.
Tume hiyo ilipewa majukumu ya kuchunguza migogoro ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni pamoja na kubaini chanzo cha mgogoro katika eneo la Loliondo, eneo la Pori la Akiba la Parloleti.
Tume ilisema Wananchi wa Loliondo wanataka eneo la kilomita za mraba 1502 lililopandishwa hadhi kutoka Pori Tengefu la Loliondo la mwaka 1951 na kuwa Pori la Akiba la Parloleti mwaka 2022, lirudishwe kwa wafugaji kwani wananchi hawakushirikishwa katika mchakato huo.
Kuhusu eneo la Ziwa Natron ambalo Serikali inataka kulipandisha hadhi na kuwa Pori la Akiba, Tume imebaini kuwa wananchi wa maeneo hayo (Wilaya tatu za Ngorongoro, Longido na Mponduli) wanahofia kupoteza ardhi kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.
Mapendekezo ya Tume ya Migogoro ya Ardhi
Kufuatia mambo kadhaa yaliyobainika katika uchunguzi wa migogoro ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, tume ilitoa mapendekezo kadhaa.
Kufuatia tume kubaini kuwa mfumo wa matumizi mseto ya ardhi ndani ya Ngorongoro siyo endelevu, ilipendekeza mfumo wa ardhi mseto uondolewe kwa maelezo kwamba ndiyo unaowezesha watu kuishi ndani ya hifadhi wakifanya ufugaji huku shughuli zingine za utalii na uhifadhi zikiendelea.
Sheria ya Hifadhi ifanyiwe marekebisho
“Hivyo inapendekeza kuwa sheria ya hifadhi ya Ngorongoro sura ya 284 ifanyiwe mapitio na marekebisho kwa kuwashirikisha wadau wote muhimu, ili iendane na wakati na mahitaji ya sasa,” ripoti ya tume ilieleza.
Kuhusu idadi ya watu, tume inapendekeza kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iorodheshe na kujua idadi ya wenyeji licha ya kuwepo kwa takwimu zingine.
“Ili kuondoa uvamizi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro, Mamlaka ya Usimamizi ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro iwatambue na kuwaorodhesha kwenye kanzidata wakazi wote wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro, makazi yao, mifugo na kuwapa vyeti vya makazi (Certificate of residence), ” ripoti ya tume ilieleza.
Tume ilishauri kuimarishwa kwa uhusiano kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro NCAA na Baraza la Wafugaji katika eneo hilo.
“Uhusiano wa Baraza la Wafugaji na Mamlaka ya Usimamizi wa eneo hili la uhifadhi uimarishwe, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa matumizi ya fedha ndani ya baraza hilo kwa kuzingatia taratibu za matumizi ya fedha za umma,” ilisema ripoti ya tume.
Wakati zoezi la uhamaji linaendelea katika eneo la Ngorongoro, Serikali itekeleze wajibu wake wa kutoa huduma za jamii kwa wenyeji ambao bado hawajaondoka.