- Tanzania inaendelea kuimarisha sera na sheria za misitu, ikiwemo Sera ya Misitu ya 1998 (iliyoboreshwa 2017), pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza ukataji miti.
- Serikali inalenga kurejesha hekta milioni 5.2 za ardhi iliyoharibika na tangu 2023 inatekeleza miradi ya kuboresha mnyororo wa thamani wa nishati ya kuni kwa usimamizi endelevu wa misitu.
- Miradi ya serikali na asasi za kiraia imeongeza uelewa wa jamii, ikichochea upandaji miti, uvunaji endelevu na kuanzishwa kwa vyanzo mbadala vya kipato kama ufugaji nyuki.
- Ushirikishwaji wa jamii, elimu, na vyanzo vya kipato visivyotegemea misitu ni muhimu katika kupambana na ukataji miti, licha ya changamoto kama rushwa na utekelezaji dhaifu wa sheria.
Hili ni toleo la pili katika mfululizo wa makala kuhusu uharibifu wa misitu Tanzania. Soma toleo la kwanza hapa.
Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kupunguza au kumaliza kabisa ukataji ovyo wa misitu ambao kwa sasa ni tishio la kitaifa.
Jitihada hizo zinaongozwa na sera na sheria ikiwemo Sera ya Misitu ya Tanzania ya mwaka 1998. Sera hii imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto za wakati huu, na pitio la mwisho lilifanyika mwaka 2017.
Miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa, Kideghesho anasema ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama gesi na gesi asilia, gesi inayotokana na kinyesi cha wanyama.
Taarifa zaidi zinaonyesha serikali imedhamiria kurejesha misitu katika eneo la hekta milioni 5.2 ambalo ardhi yake imepoteza ubora kutokana na kukatwa miti hovyo.
Kuanzia mwaka 2023, serikali kwa kushirikiana na asasi za kiraia imekuwa ikitekeleza mradi mkubwa wa mageuzi ya matumizi ya nishati itokanayo na miti wenye lengo la kuboresha usimamizi na uvunaji endelevu wa misitu.

Mradi wa Mchakato Jumuishi wa Kuleta Mabadiliko Katika Mnyororo wa Thamani wa Nishati ya Kuni (Integrated Approach for Transformation of Tanzania Fuel Wood Value Chain Project), ni mmoja wa miradi inayolenga kuboresha ustawi wa jamii zilizo pembezoni na kuhifadhi na kulinda misitu.
Mradi huo unaotekelezwa katika wilaya 16 zilizopo kwenye mikoa ya Tabora, Dar es Salaam, Mwanza, Pwani, Tanga na Morogoro, unafadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya na utekelezaji wake ulianza tangu mwaka 2023 na utahitimishwa mwaka huu wa 2026.
Lengo la mradi huu ni kuboresha mfumo wa ikolojia ya misitu kwa kuzingatia utawala bora, sheria na kanuni ili kupata nishati endelevu ya kupikia kwa jamii zinazoishi pemebezoni mwa misitu.
Vyanzo mbadala vya kipato vimeanzishwa
Mradi huu umewasaidia wananchi kuelewa sheria za misitu na umuhimu wa uvunaji endelevu, ikiwemo kuchagua miti sahihi ili kupunguza upotevu. Pia wamehamasishwa kupanda na kutunza miti kwa matumizi yao bila kuathiri misitu ya asili, pamoja na kufahamu haki na wajibu wao katika kunufaika na rasilimali hizo kwa njia endelevu.
Ingawa mradi haujakamilika, tayari wananchi wamepata elimu ya utunzaji misitu na wameanza kuanzisha vyanzo mbadala vya kipato kama ufugaji nyuki ili kupunguza utegemezi wa misitu.
“Suala la kuboresha mnyororo wa thamani ya nishati itokanayo na miti siyo jukumu la watendaji wa idara ya misitu tu, linahusu wadau mbalimbali pamoja na Serikali kupitia wizara na idara zake.
Wote wanao wajibu wa kuhakikisha misitu inatunzwa na kuhifadhiwa ili jamii iweze kupata faida endelevu za kiuchumi na kijamii,” anasema Rajabu Hassan Rajab, Afisa Programu wa mradi kwa upande wa Chama cha Wanansheria wa Mazingira kwa Vitendo (Lawyers Environmental Action Team), taasisi mojawapo kati ya zile zinazotekeleza mradi huo.
Mbali na juhudi za Serikali, asasi za kiraia pia zinatekeleza miradi yenye lengo la kupambana na ukataji ovyo misitu.
Moja ya asasi hizo, ni Climate Action Network Tanzania (CAN Tz) ambayo inatekeleza Mradi Shirikishi wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Kupunguza Gesijoto Mijini, Vijijini na Mwambao wa Bahari kwa Kutumia Njia za Asili (Promotion of Participatory Processes for the Implementation of NDC through Nature-Based Solutions in Urban, Rural, Coastal Landscapes of Tanzania).
Mradi huu wa miaka mitatu unatekelezwa katika kijiji cha Vuma katika wilaya ya Same na vijiji vya Kigurusimba na Msaraza wilaya ya Pangani mkoani Tanga na unalenga kutumia mbinu shirikishi za kijamii katika kurejesha na kusimamia misitu kwa namna endelevu.
Pia unachangia jitihada za kitaifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia njia za asili hasa za utunzaji wa misitu.

Bonaventure Mchomvu, Meneja Miradi wa CAN Tanzania, anasema chini ya mradi huu, jamii inajengewa uwezo wa kuandaa vitalu vya miche ya miti ya asili, kupanda miche hiyo na kutunzaji miti ya asili ili kuboresha maisha yao na kuhifadhi baionuwai.
Wananchi wamepatiwa mafunzo ya utunzaji wa misitu na mbinu za kurejesha misitu ya asili, ikiwemo kubaini maeneo ya kupanda miti, kukusanya mbegu bora, na kuanzisha vitalu chini ya usimamizi wa wataalamu.
Pia wamehamasishwa kupanda miti katika mashamba na makazi ili kupunguza utegemezi wa misitu ya asili. Kutokana na hilo, wameongeza uelewa na baadhi wanapata kipato kwa kuuza mbegu na miche ya miti ya asili.
“Misitu ya asili inabeba jukumu kubwa la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga uchumi endelevu wa jamii na kuchochea ustahimili wa jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Misitu hii ikitoweka jamii itaathirika, hivyo tunawajengea uwezo wananchi wenyewe washiriki kikamilifu kupanda na kutunza miti ya asili ili waweze kuendesha maisha yao kwa uhakika kwa kutumia rasilimali za asili zilizopo katika vijiji vyao,” anaeleza Mchomvu.
Mradi huu pia umewasaidia wananchi kuelewa sheria za misitu ili kuepuka uvunaji usio endelevu na uvunjaji sheria, utunzaji misitu, uvunaji endelevu wa misitu na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ikiwemo ufugaji nyuki ili kuepuka kutegemea misitu moja kwa moja pamoja na uvunaji wa mpango ambao unazingatia uchaguzi wa miti sahihi iliyokamaa ili kupunguza upotevu wakati wa kutengeneza mkaa, anasema.
Hali ya wananchi kutotegemea misitu ya asili kwa mahitaji yao yote, inaelezwa kuwa njia mojawapo itakayosaidia kupunguza vitendo vya ukataji miti ovyo na kufanya vita dhidi ya uharibifu wa misitu kuwa nyepesi.
Changamoto ni kubwa
Susan Danda kutoka International Union for Conservation of Nature (IUCN), taasisi ya kimataifa inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira, bioanuwai, na matumizi endelevu ya maliasili, anasema: “Uhakika wa kipato kisichohitaji kukata miti kitawafanya jamii washiriki kikamilifu kulinda na kuhifadhi misitu, na hivyo kupata manufaa endelevu kutokana na rasilimali za misitu.”
Susan alisema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa Bonde la Kilombero uliofanyika hivi karibuni kujadili hali ya mazingira, umiliki wa ardhi na usalama wa wanyama pori katika Bonde la Kilombero ambalo ni Ardhi Oevu ya Kimataifa (Ramsar Site).

Kwa mujibu wa Susan, uhifadhi na ulinzi wa misitu lazima utilie maanani mahitaji ya jamii.
Anasema: “Ni muhimu wananchi washiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kupanga mipango ya uhifadhi na utekelezaji wake, kwani mawazo na maoni yao lazima yazingatiwe katika kufanya uamuzi wa mwisho”.
Alifafanua kuwa ushirikishwaji unapozingatiwa, vijiji vinakuwa na dhima ya kupanga mipango ya kuhifadhi na kulinda misitu na kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo ili kuhakikisha kuwa inapata manufaa endelevu kutokana na misitu.
Novemba mwaka 2025 katika Mkutano wa 30 wa Mabadiliko ya Tabianchi unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa (UNFCCC), wajumbe walikubaliana kuanzisha mfuko wa utunzaji misitu (The Tropical Forest Forever Facility (TFFF) wenye lengo la kukusanya fedha kwaajili ya kulinda na kuhifadhi misitu ili iendelee kutoa faida za kiuchumi, kimazingira na kijamii kwa nchi zinazoendelea ambazo bado zina misitu ya asili.
Mfuko huo ambao uko katika hatua za awali za kuanzishwa, unatarajiwa kukusanya kiasi cha fedha ili kusaidia kulinda na kuhifadhi misitu katika nchi 70 zinazoendelea. Miongoni mwa nchi hizo ni pamoja na Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Fedha zitatolewa kwa nchi ambazo zimehifadhi misitu yake kwa kupunguza ukataji ovyo na uharibifu na wanufaika wakubwa watakuwa jamii zinazoishi kando ya misitu kwani ndizo zinazobeba jukumu la kuhifadhi na kulinda misitu.
Mfuko huu unalenga kuzinufaisha nchi 70 ambazo zina jumla ya zaidi ya hekta bilioni moja za misitu ya asili. Nchi zitakazoanza kunufaika na mfuko huo ni pamoja na Brazil, Colombia, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Ghana, Indonesia, Malaysia, Kenya, Papua New Guinea na Peru.
Matumizi endelevu ya misitu
“Lengo kubwa ni kusisitiza matumizi endelevu ya misitu kwa faida ya vizazi vya wakati huu na wakati ujao. Katika kutoa elimu, ni muhimu jamii ikasaidiwa kupata chanzo mbadala cha kipato ili kupunguza kutegemea miti kutoka misitu ya asili,” anasema Kideghesho.
Elimu ya kutosha kwa wananchi ni suala lingine ambalo litasaidia juhudi dhidi ya ukataji misitu. Umuhimu wa kutoa elimu umesisitizwa pia katika Sera ya Misitu ya Tanzania ya mwaka 1998 ambayo inasema kuwa kukosekana kwa elimu kumesababisha mwamko mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu haja ya kuhifadhi miti na ufahamu wa kutosha kuhusu umuhimu wa kupanda miti na hivyo kukosekana misingi ya usimamizi endelevu wa misitu.
Kideghesho anadai kuwa sekta ya misitu kama sekta nyingi hapa Tanzania, imegubikwa na wimbi la rushwa.
Ili kupambana na hali hiyo anasema ni muhimu serikali na wadau wa misitu kutambua hilo na kutafuta njia sahihi ikiwa ni pamoja kuhakikisha usimamizi wa sheria na utawala wa sheria vinazingatiwa.
Petro Nyiti, ni mtaalamu wa misitu kutoka Reforest Africa, shirika linalofanya kazi kuhamasisha wananchi vijijini kutunza misitu na kuivuna kwa namna endelevu ili kuendelea kunufaika nayo.
Anasema mipango ya matumizi bora ya ardhi ni muhimu kwani huisaidia jamii kutenga ardhi kwa matumizi mbalimbali.

“Kukiwa na mipango bora ya ardhi, jamii inaweza kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji ambavyo ni mahitaji ya msingi kwa maisha yao. Ni muhimu pia kuhamasisha kutumia majiko banifu ambayo hutumia mkaa kidogo au kuni chache na kuokoa misitu,” anasema Nyiti.
Anafafanua kuwa iwapo jamii itapatiwa taarifa za mara kwa mara juu ya teknolojia bora isiyo na gharama kubwa pamoja na upatikanaji wa nishati safi mbadala, vitawasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kama vyanzo muhimu vya kupikia.
“Kutokana na mahitaji haya, ni muhimu Serikali na wadau wengine kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme, gesi asilia na umeme jua kwa jamii za vijijini ili kupunguza kasi ya upotevu wa misitu lakini pia kulinda afya za wananchi,” anasema Nyiti.
Anaongeza kuwa mipango ya matumizi bora ya ardhi ni muhimu kwani huisaidia jamii kutenga ardhi kwa matumizi mbalimbali.
“Wote tunaelewa, kupata kipato kwa ajili ya kujikimu kimaisha, ndiyo sababu kubwa ya watu kujihusisha na ukataji misitu. Kama watu watapata shughuli nyingine inayowaingizia kipato, na wakawa na uhakika wa familia zao kuishi, vita hii inaweza kufanikiwa,” anasema Nyiti.
“Pamoja na jitihada zinazofanywa kunahitajika utashi wa kisiasa kwa nchi na kimataifa ili kuchochea ushiriki wa wanufaika wote katika kulinda na kuhifadhi misitu, hasa jamii zinazozunguka misitu, kwani ndiyo wanufaika wakubwa wa kwanza.
“Kwao uhifadhi na ulinzi wa misitu huleta faida zinazodhihirika katika kuondoa umaskini, kuboresha afya na huduma za kijamii,” anasema Kideghesho.
Picha ya Bango: Wanakijiji wa Msaraza Wilaya ya Pangani wakiandaa udongo kwaajili ya kutengeneza vitalu vya miche ya miti ya asili. Picha kwa hisani ya CAN Tanzania.