- Kenya imeanza kusafirisha kahawa inayokidhi viwango vya EUDR, lakini wakulima wengi wadogo bado hawajajiandaa au hawana uelewa wa masharti hayo mapya.
- EUDR inahitaji kahawa iwe haina uhusiano na ukataji miti, ikiwa na ufuatiliaji wa kina wa mashamba (ikiwemo data za kijiografia), jambo linaloweka shinikizo kwa wakulima.
- Ukataji miti unaendelea kuwa changamoto kubwa nchini Kenya, huku maelfu ya hekta za misitu ya asili zikipotea kutokana na upanuzi wa kilimo.
- Wakulima na wataalamu wanaona kilimo mseto (agroforestry) kama suluhisho muhimu la kukidhi masharti ya EUDR huku wakikabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
NYERI, Kenya – Wakati Kenya ilipoadhimisha usafirishaji wake wa kwanza wa kahawa inayokidhi viwango vya EUDR kwenda nchini Poland tarehe 25 Machi, hali halisi kwenye maeneo ya uzalishaji ilikuwa tofauti huku ikigubikwa na ugumu usioelezeka.
Huku serikali ikisherehekea kusafirisha mzigo wa magunia 320, kila moja likiwa na uzito wa kilo 60 na kutoka katika vyama 13 vya ushirika, hatua hii iliashiria mafanikio, lakini pia shinikizo. Wakulima wengi bado hawajajiandaa kwa masharti makali dhidi ya ukataji miti ambayo sasa yanaamua upatikanaji wa soko lenye faida la Ulaya. Hili ni jaribio.

Chini ya jua kali la mchana katika kijiji cha Gaturere, Kaunti ya Nyeri, takribani maili 95 kaskazini-mashariki mwa Nairobi, Nichodemus Muchangi, baba ya watoto wanne, yuko shambani, akili yake ikiwa imetawaliwa na kuhudumia kahawa, jambo ambalo amefanya kwa zaidi ya miongo mitatu.
Akiwa na miti 400 ya kahawa katika shamba lake la nusu ekari, Muchangi anasema hajawahi kufanya kazi nyingine tangu aliporithi ardhi hiyo kutoka kwa baba yake alipokuwa na umri wa miaka 13. Sasa ana umri wa miaka 43.
Kwa mujibu wa Bruno Linyuri, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kilimo na Chakula ya Kenya, Kenya ina takribani wakulima wadogo wa kahawa 800,000 walioko katika maeneo 33 ya uzalishaji. Wakulima hawa huzalisha takribani asilimia 70 ya kahawa ya Kenya, ambayo pia ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato ya fedha za kigeni nchini.
Maeneo ya kilimo cha kahawa nchini Kenya yanajumuisha baadhi ya maeneo muhimu sana kiikolojia, ikiwa ni pamoja na safu za milima ya Aberdare, misitu ya Mlima Kenya, miteremko ya Mau, na mifumo ya ikolojia ya nyanda za juu za Bonde la Ufa. Maeneo haya yanahifadhi vyanzo muhimu vya maji, hifadhi za kaboni, na bioanuwai.
Katika baadhi ya maeneo, mipango isiyo rasmi ya kilimo inaathiri uhifadhi wa misitu, huku wakulima wengi wakilima karibu na mipaka ya misitu ambako shinikizo la ardhi ni kubwa na uvamizi, mmomonyoko wa udongo, pamoja na uharibifu wa makazi ya viumbe tayari vinatishia ustawi wa misitu.
Kwa mujibu wa Global Forest Watch, Kenya ilipoteza hekta 54,000 za misitu ya asili yenye unyevunyevu kati ya mwaka 2002 na 2024, ikiwa ni asilimia 14 ya upotevu wote wa uoto wa miti katika kipindi hicho. Upotevu wa miti umetajwa kuwa mojawapo ya sababu kuu za ukataji miti katika kipindi hicho, huku eneo la misitu ya asili yenye unyevunyevu likipungua kwa asilimia 8.0.
Mwaka 2024 pekee, Kenya ilipoteza hekta elfu 7,400 za misitu ya asili, sawa na uzalishaji wa tani milioni 3.0 za hewa ukaa (CO₂).

Ripoti ya Hali ya Misitu ya mwaka 2024 inaonesha kuwa Kenya hupoteza takribani hekta 84,700 za misitu kila mwaka kutokana na ukataji miti, huku hekta 15,000 zikiharibiwa kila mwaka. Uchambuzi wa hivi karibuni wa Global Forest Watch unaonesha kuwa asilimia 92 za ukataji miti barani Afrika kati ya mwaka 2021 na 2024 ulisababishwa na upanuzi wa kilimo cha kudumu na kilimo cha kuhamahama.
Sheria ya Umoja wa Ulaya kuhusu ukataji miti
Mwaka 2023, Bunge la Umoja wa Ulaya lilipitisha sheria inayolenga kuongeza matumizi ya bidhaa zisizohusishwa na ukataji miti (deforestation-free) na kupunguza mchango wa Umoja wa Ulaya katika ukataji miti na uharibifu wa misitu duniani. Kanuni ya Umoja wa Ulaya kuhusu Ukataji Miti (EUDR) inalenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafu (GHG) na upotevu wa bioanuwai. Kanuni hii ni sehemu muhimu ya mpango wa EU wa kukabiliana na ukataji miti.
Kanuni zenyewe zinahusu mazao na bidhaa kama mifugo, kakao, kahawa, mafuta ya mawese, soya, mbao na mpira.
EUDR inawataka wakulima kutoa taarifa sahihi za kijiografia (GPS) za mashamba yao ya kahawa. Hii inawezesha wasimamizi wa EU kupitia picha za satelaiti na kutathmini kama kumekuwa na ukataji miti au uharibifu wa ardhi.
Hata hivyo, marekebisho ya hivi karibuni yamebadilisha ratiba ya utekelezaji wa sheria hiyo, kwa mara ya pili sasa. Utekelezaji kamili sasa unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka 2026 kwa makampuni makubwa, na katikati ya mwaka 2027 kwa waendeshaji wadogo.
Pamoja na hayo, baadhi ya wakulima wadogo wa kahawa bado hawajui uwepo wa EUDR na athari zake, kiuchumi na kimazingira. Kushindwa kuzingatia masharti kunaweza kuwa na madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kufikia soko la EU, kutozwa faini, na kutengwa kibiashara.
Kwa mujibu wa ODI Global, “EUDR inahitaji kahawa inayouzwa au kusafirishwa kwenda EU isiwe na uhusiano na ukataji miti, izalishwe kisheria kulingana na sheria za kitaifa, na iweze kufuatiliwa kikamilifu hadi kwenye eneo halisi ilikolimwa.
“Kila mzigo lazima uambatane na ukaguzi wa kina, likijumuisha taarifa za kijiografia, tathmini ya hatari na hatua za kupunguza hatari. Kutokufuata masharti kuna gharama kubwa, ikiwa ni pamoja na faini hadi asilimia 4 ya mapato ya kampuni ndani ya EU, pamoja na kukataliwa kwa mizigo na kuharibika kwa sifa.”
Muchangi hana habari kuhusu EUDR. “Sijawahi kuisikia chochote kuhusu EUDR. Ninasikia kutoka kwako kwa mara ya kwanza, na sijui inahusu nini,” Muchangi aliambia Mongabay.
Licha ya kukosa uelewa kuhusu EUDR, Muchangi amekuwa akichanganya kilimo cha kahawa na miti ya Faidherbia albida na Moringa (Moringa oleifera), ambayo anaiita “miti rafiki kwa kahawa”.
Anasema alianza kupanda miti ndani ya mashamba yake ya kahawa ili kuboresha rutuba ya udongo, kuhifadhi unyevu na kulinda kahawa dhidi ya vipindi virefu na visivyotabirika vya ukame vinavyozidi kuongezeka.
Kwa Muchangi, mabadiliko haya si kwa ajili ya kufuata EUDR, bali ni njia ya kujinusuru dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema: “Nilipochukua shamba kutoka kwa baba yangu, hakukuwa na miti, na mavuno hayakuwa mazuri kwa sababu rutuba ya udongo ilikuwa imeshuka. Niliamua kupanda miche 200 ya miti ya Faidherbia albida, na ndani ya miaka mitano, ilikuwa kama msitu mdogo na mavuno ya kahawa yakaongezeka.”
Kahawa na Moringa zote ni chanzo chake cha mapato. “Nimekuwa nikiepuka kabisa kukata miti hiyo. Nina mpango wa kupanda mti mpya wa Moringa kwa kila mti mpya wa kahawa,” aliongeza Muchangi.
Kinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi
Kwa Agnes Wanjiku, mwenye umri wa miaka 45, kuwa na mchanganyiko wa miti ya makadamia na parachichi (Persea americana) pamoja na miti 1,400 ya kahawa katika ekari moja kumemsaidia kujikinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kama ukame wa muda mrefu.
“Miti yangu ya makadamia na parachichi pia ni chanzo cha mapato. Pia inalinda kahawa dhidi ya jua kali, na majani yanayooza kutoka kwenye miti hiyo husaidia kurejesha afya ya udongo na kuongeza bioanuwai,” alisema Wanjiku.

Wanjiku anasema hakupanda miti 200 ya makadamia na 100 ya parachichi kwa ajili ya kufuata EUDR, bali ilikuwa sehemu ya mfumo wa kilimo mseto unaoendana na uhifadhi endelevu wa mazingira.
Lalisa Duguma, mtaalamu wa ikolojia, mshauri wa programu na mtaalamu wa suluhisho zinazotegemea asili katika shirika la Global Evergreening Alliance (GEA), anaeleza kuwa EUDR inaweza kusaidia Kenya kupambana na ukataji miti kwa kuwa inahamasisha kilimo mseto kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Hii ni kutokana na wakulima wengi wa kahawa kuanza kupanda miti ya kivuli na kurejesha ardhi iliyoharibika ili kukidhi masharti ya sheria hiyo.
“Kenya imekuwa ikijitahidi kufikia malengo yake ya kitaifa ya kuwa na asilimia 10 ya uoto wa miti. Sera kama EUDR zinaweza kusaidia kuharakisha kufikiwa kwa malengo hayo,” alisema.
Aliiambia Mongabay kuwa EUDR ni chombo muhimu kinachoendana na malengo ya Kenya ya kurejesha misitu kwa kuimarisha mbinu endelevu kama kilimo mseto.
“Kimsingi, EUDR inawaambia wakulima wa kahawa waache kukata miti ili kupanda mazao ya biashara ya kuuza nje, na badala yake wapande vyote kwa pamoja,” alisema.
Mhifadhi Mkuu wa Misitu nchini Kenya, Alex Lemarkoko, anasema kuwa matakwa ya kuwa taarifa sahihi za kijiografia zinazoonyesha mahali kahawa inapolimwa, yatasaidia sio tu kuboresha ufuatiliaji wa matumizi ya ardhi, bali pia litazuia uvamizi haramu wa misitu.
“EUDR itaongeza nguvu juhudi za Huduma ya Misitu Kenya (KFS) katika kufuatilia uoto wa miti kitaifa, hali ya misitu na kulinda misitu ya umma,” alisema Lemarkoko.
Alisema kuwa kama kila mmoja wa wakulima wadogo wa kahawa wapatao 800,000 atapanda takribani miti 100 kila mwaka, Kenya itaongeza takribani miti milioni 80 kila mwaka kupitia wakulima wa kahawa pekee.
“Tunashirikiana na vyama vya ushirika vya wakulima wa kahawa kuwahamasisha wakulima kuchanganya kahawa na miti rafiki kama ya matunda, miti ya dawa na miti ya asili kwa manufaa ya kiikolojia na kiuchumi.”
Kwa mujibu wa Lemarkoko, sera ya EUDR inaendana na makubaliano ya kimataifa kama Mkataba wa Paris, na malengo ya urejeshaji wa ambayo Kenya ni mshiriki wake.
“EUDR inaendana pia na agizo la rais wa Kenya la kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032 kama njia ya kurejesha mazingira yaliyoharibika na kuhakikisha maisha endelevu. Wakulima wa kahawa wako katika nafasi nzuri ya kuendeleza juhudi hii,” Lemarkoko aliiambia Mongabay.
George Watene, Meneja wa Programu wa Jukwaa la Kahawa Kenya chini ya Jukwaa la Kahawa la Kenya Platform,anaona kuwa EUDR itahamasisha uendelevu kupitia uhifadhi wa misitu. Hata hivyo, anaonya kuwa kuwazuia wakulima wadogo wa kahawa kuingia katika soko lenye faida la EU kunaweza kuhatarisha juhudi za uhifadhi, kwani wengi wanaweza kugeukia njia mbadala kama kilimo ndani ya misitu, ukataji miti na uchomaji mkaa, hali itakayoongeza ukataji miti.
“Wakulima wengi wa kahawa ambao ni wadogo si lazima wahusike na ukataji miti, na wengi wao tayari wameanza kufuata ajenda ya uendelevu ambayo EUDR inahamasisha,” alisema Watene.
Aliongeza kuwa kwa kuwa asilimia 50 ya kahawa ya Kenya tayari imeidhinishwa kwa vigezo vya uendelevu wa mazingira, utekelezaji wa EUDR utahakikisha kuwa asilimia 100 ya kahawa ya Kenya inazalishwa kwa njia endelevu.
Wakati huo huo, anaonya kuwa ukosefu wa miundombinu ya kutosha na msaada wa kiufundi ni vikwazo vikubwa kwa wakulima wengi katika kufuata masharti ya EUDR.
“Wakulima wanakosa rasilimali muhimu za teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), kama vile intaneti ya uhakika na vifaa vya kidijitali vinavyofaa kama simu janja. Hali hii inapunguza uwezo wa kutekeleza mifumo ya ufuatiliaji wa mazao kwa ufanisi,” alisema Watene.
Hali ya utekelezaji
Bruno Linyuri, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kilimo na Chakula ya Kenya, aliiambia Mongabay kuwa kufikia Januari 2026, asilimia 30 ya mashamba ya kahawa nchini yalikuwa yamepimwa kijiografia katika maeneo 16 kati ya 33 ya uzalishaji kahawa nchini humo. Hii inamaanisha kuwa ni hekta 32,688 tu kati ya hekta 109,384 za mashamba ya kahawa nchini ndizo zimekidhi masharti ya EUDR.

Kwa kuwa Umoja wa Ulaya hununua asilimia 60 ya kahawa yote inayosafirishwa nje ya Kenya, Linyuri alisema: “EUDR haihusu kahawa na bidhaa nyingine pekee, bali pia ustawi endelevu wa mazingira ambamo bidhaa hizi huzalishwa.”
“Tunakabiliwa na changamoto ya watu kukata misitu ili kupanda kahawa na mazao mengine ya biashara. Sera hii itatusaidia kukabiliana na hali hiyo. EUDR ipo kusaidia kuboresha hadhi ya kilimo huku tukilinda mazingira,” alisema Linyuri.
Felix Mutwiri, mkuu wa Idara ya Kahawa nchini, alisema timu ya taasisi mbalimbali imeundwa kuhakikisha utekelezaji wa EUDR. Serikali tayari imeandaa mkakati wa utekelezaji wa kanuni hizi. Ili kuwasaidia wakulima kufuata masharti, tumeanza zoezi la kupima mashamba kwa kutumia taarifa za kijiografia pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo kuhusu mahitaji ya EUDR,” alisema Mutwiri.
Kupunguza uzalishaji wa kaboni
Matthias Reusing, Mshauri wa Kwanza wa masuala ya kilimo, mazingira, mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya kidijitali katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwa Umoja wa Afrika, aliiambia Mongabay kuwa EUDR inalenga kuhakikisha kuwa Umoja wa Ulaya hautoi soko kwa bidhaa zinazochangia ukataji miti na uharibifu wa misitu duniani.
Matthias alizungumza Februari 2026, wakati wa mkutano wa wadau uliowakutanisha maafisa wa Umoja wa Ulaya, wadau wa kahawa na maafisa wa serikali ya Kenya kuhusu utekelezaji wa kanuni za EUDR, uliofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Kilimo na Chakula ya Kenya jijini Nairobi.

“EU ina lengo kubwa la kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaotokana na matumizi na uzalishaji wa bidhaa kama mifugo, kakao, kahawa, mafuta ya mawese, soya, mbao na mpira kwa angalau tani milioni 32 kwa mwaka, na EUDR ni moja ya zana za kufikia lengo hilo,” Reusing aliiambia Mongabay.
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linaeleza kuwa kudhibiti ukataji miti na kurejesha mifumo ya ikolojia ni miongoni mwa njia bora za kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Reusing aliongeza kuwa EUDR “ni zaidi chombo cha tabianchi na mazingira kuliko biashara,” na inalenga kutimiza madhumuni yanayoendana na Mkataba wa Paris.
“Lengo kuu si kumzuia mtu au bidhaa yoyote kuingia katika soko la EU, bali ni kudhibiti ukataji miti na kupunguza mchango wa EU katika uzalishaji wa gesi chafu na upotevu wa bioanuwai duniani,” alisema Reusing.
Festus Ng’eno, Katibu Mkuu katika Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, alisema EUDR ni muhimu sana kwa bara la Afrika. “Itasaidia kushughulikia vyanzo vya ukataji miti vinazotokana na kilimo, ambazo ni muhimu katika kulinda misitu na kuhakikisha maisha endelevu.”
“Masoko mengine ya bidhaa kutoka Afrika yanapaswa kujifunza kutoka EU kupitia EUDR. Yanapaswa kusaidia Afrika kupambana na ukataji miti kwa kuhakikisha kuwa ni bidhaa zisizohusishwa na ukataji miti pekee zinazoingia katika masoko yao,” alisema Ng’eno.
Ili kuhakikisha wakulima wengi zaidi wa kahawa wanatimiza masharti ya kutohusishwa na ukataji miti, Mamlaka ya Kilimo na Chakula ya Kenya (AFA), kupitia Idara ya Kahawa na Umoja wa Kitaifa wa Vyama vya Ushirika vya Kahawa (NACCU), wamekuwa wakitoa miche ya miti na kahawa kwa wakulima kama sehemu ya juhudi za kurejesha mazingira nchini.
Mwenyekiti wa NACCU, Felix Mwai, alisema kuwa kwa kila mche mmoja wa kahawa anaouchukua mkulima, hupatiwa pia bure mche mmoja wa mti wa kupanda pamoja. “Kama mkulima atachukua miche 100 ya kahawa, lazima pia achukue miche 100 ya miti. Na hatuishii hapo; tuna mfumo wa ufuatiliaji kuhakikisha miti hiyo inapandwa na kutunzwa,” alisema Mwai.
Alisema lengo la kutoa miche ya miti bure ni kwenda zaidi ya EUDR na kuwafanya wakulima wa kahawa kuwa sehemu ya juhudi za muda mrefu za kurejesha mifumo ya ikolojia iliyoharibika, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kukuza utamaduni wa uendelevu wa mazingira katika maeneo ya uzalishaji kahawa.
“Lengo letu ni kuimarisha uendelevu wa muda mrefu wa kilimo cha kahawa kwa kuboresha afya ya udongo, kulinda vyanzo vya maji na kuhifadhi bioanuwai kupitia upandaji wa miti ndani ya mashamba ya kahawa,” alisema Mwai.
Usafirishaji wa majaribio wa magunia 320 unaonyesha kile kinachowezekana, lakini pia unaangalia ukubwa wa changamoto inayokabili sekta inayowahusisha karibu wakulima wadogo milioni moja.
Picha ya bango: Godfrey Mwangi, mkulima wa kahawa katika Kaunti ya Nyeri, nchini Kenya kwa miongo mitatau sasa. Picha na Jackson Okata, Mongabay.