- Mkakati mpya wa taasisi za serikali, wanasayansi na wananchi kutoka maeneo ya Pwani unapendekeza mpango wa kazi wenye malengo 19 ya kudhibiti kupungua kwa kasi kwa idadi ya papa na samaki jamii ya papa pweza nchini Kenya.
- Kwa kuwa wavuvi wadogo wana ushawishi mkubwa na uelewa kuhusu idadi ya viumbe hao wa baharini, malengo mengi yanawahusisha moja kwa moja, au yanakusudia kuwashirikisha,au yanajaribu kuwaweka karibu ili kuhakikisha mafanikio ya mkakati huo.
- Miongoni mwa malengo hayo ni pamoja na matumizi ya zana mbadala za uvuvi, kuanzisha vyanzo mbadala vya kipato ili kupunguza shinikizo la uvuvi, kuongeza maeneo ya bahari yanayosimamiwa na jamii, kuwashirikisha wavuvi katika maamuzi ya uhifadhi pamoja na kuimarisha utekelezaji wa sheria.
- Wawakilishi wa wavuvi wanasema wanaunga mkono mpango huo, lakini wanasisitiza kuwa baadhi ya mambo kama upatikanaji wa vyanzo mbadala vya kipato vinavyotekelezeka pamoja na mbinu bora za uvuvi, vinapaswa kuimarishwa ili kufikia malengo ya uhifadhi.
NAIROBI, Kenya — Katika pwani ya mashariki mwa Kenya, mvuvi mdogo hubeba samaki waliovuliwa siku hiyo na kuwaweka mezani kwa ajili ya kuwakatakata tayari kwa kuuzwa. Kuna uwezekano mkubwa miongoni mwa samaki hao zimo spishi zilizo hatarini zaidi kama papa aina ya scalloped hammerhead na samaki aina ya white-spotted guitarfish.
Huu ni mfano mmoja tu wa mwenendo mpana zaidi, ambao kulingana na wahifadhi wa mazingira, unaoonyesha jinsi hatma ya papa na samaki jamii ya pweza walio hatarini, ilivyofungamana kwa karibu na maisha ya wavuvi wanaojitafutia kipato katika Bahari ya Hindi ya Magharibi.
Mnamo Februari, ili kuweka mpango kazi unaotekelezeka wa uhifadhi wa papa na samaki jamii ya pweza nchini Kenya, kundi la watunga sera, wanasayansi na viongozi wa jamii walichapisha mkakati wenye malengo 19. Kati ya hayo, zaidi ya malengo 12 yanawahusisha moja kwa moja wavuvi wadogo au yanakusudia kuwashirikisha ili kuhakikisha mafanikio yake.
Malengo hayo yanajumuisha kuanzisha maeneo zaidi ya bahari yanayosimamiwa na jamii, kuwashirikisha wavuvi katika maamuzi ya uhifadhi, na kuimarisha utekelezaji wa sheria kuhusu zana za uvuvi na uvuvi wa spishi zilizo hatarini.
Tangu mwaka 2023, Kenya tayari ina sera ya uhifadhi wa papa na samaki jamii ya pweza — Mpango wa Kitaifa wa Hatua za Uhifadhi na Usimamizi wa Papa (NPOA-Sharks). Hata hivyo, mpango huo bado unasubiri kuidhinishwa rasmi na serikali. Mkakati uliopendekezwa na wadau unatoa njia ya jinsi ya kuutekeleza.

Baadhi ya wadau pamoja na kikosi cha wataalamu kutoka Huduma ya Uvuvi ya Kenya na Mipango ya Uhifadhi wa Spishi wa IUCN, walishiriki kuandaa mkakati huo kufuatia kupungua kwa kasi kwa idadi ya spishi nyingi za papa na samaki jamii ya pweza.
Kulingana na CORDIO Afrika Mashariki, shirika la utafiti na uhifadhi lililoongoza uandaaji wa mkakati huo, Kenya sasa ni miongoni mwa nchi 10 duniani zenye idadi iliyopungua zaidi ya papa wa maeneo ya pwani.
Wadau wanasema wavuvi wadogo wana mchango mkubwa katika mifumo ya ikolojia ya baharini na uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Rhett Bennett, Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Afrika wa Kundi la Wataalamu wa Papa la IUCN SSC (SSG), alisema wavuvi wa jadi huchangia hadi asilimia 75 ya samaki wote wanaovuliwa. Hata hivyo, sehemu kubwa ya samaki hao ni spishi zilizo hatarini.
Uvuvi kupita kiasi unaofanywa na wavuvi wadogo, sera zisizo imara na ukosefu wa utekelezaji wa sheria dhidi ya uvuvi haramu na matumizi ya zana zisizofaa vimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa papa na samaki jamii ya pweza nchini Kenya na katika Bahari ya Hindi ya Magharibi.
Orodha Nyekundu ya IUCN ya Spishi Zilizo Hatarini inakadiria kuwa karibu asilimia 40 ya spishi zote za papa na rays katika eneo hilo ziko hatarini kutoweka.
Said Mote, ambaye ni mvuvi mdogo na mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe cha Ngomeni (chama cha jamii kinachojumuisha wavuvi, wafanyabiashara na wamiliki wa boti kinachoshirikiana na serikali kusimamia uvuvi), alisema wavuvi wadogo hawalengi papa na pweza moja kwa moja.
“Wanatupa tu nyavu zao, na chochote wanachokamata ndicho wanachochukua nyumbani kama chakula au kukiuza sokoni,” alisema.
Mbali na masoko ya ndani, pia kuna soko la kimataifa tayari kwa papa na pweza. “China, Singapore na nchi nyingine za Mashariki zina mahitaji makubwa sana ya mapezi ya papa na bidhaa nyingine,” aliongeza.
Huduma ya Uvuvi ya Kenya iliripoti kuwa mwaka 2022, jumla ya tani za metriki 1,080 za papa na pweza zilivuliwa katika pwani ya Kenya. Hii ilikuwa asilimia 4 ya samaki wote waliovuliwa na wavuvi wadogo mwaka huo.

Ni mbadala gani uliopo?
Mote, ambaye alishiriki katika kuandaa mkakati huo, alisema anasubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa mkakati huo. Hata hivyo, aliiambia Mongabay kuwa ili kufanikisha uhifadhi wa papa na samaki jamii ya pweza, wavuvi wanahitaji mbadala unaotekelezeka.
“Wavuvi wadogo hawana tatizo. Wanahitaji kufundishwa na kuelimishwa kuhusu kilicho sahihi. Ikiwa tunaambiwa tuache kutumia mbinu fulani ya uvuvi, basi tupewe mbadala wake,” alisema.
Moja ya malengo ya mkakati huo linahusu zana za uvuvi. Kuhusu hilo, mkakati unapendekeza “kudhibiti au kubadilisha zana kuwa zile endelevu kupitia: kuweka viwango vya ukubwa wa matundu ya nyavu; kufunga uvuvi kwa misimu pamoja na kuanzisha maeneo yasiyoruhusiwa kuvua na maeneo yenye vikwazo vya matumizi ya zana.”
Ukubwa unaopendekezwa wa matundu ya nyavu, kulingana na CORDIO Afrika Mashariki, ni sentimita 10.2–15.2 (inchi 4–6). Ukubwa huu unasaidia kukamata spishi zinazokua haraka na kufikia ukomavu mapema bila kuwakamata wadogo, na pia hupunguza kiwango cha papa na pweza wanaovuliwa.
Ingawa wavuvi wengi hawalengi papa moja kwa moja, Bennett alisema wengi hupata papa kama samaki wanaonaswa kwa bahati mbaya kutokana na mbinu kama uvuvi wa tuna kwa nyavu za kuzingira, ndoano ndefu na nyavu za kuvulia.
Utafiti mmoja wa CORDIO Afrika Mashariki ulibaini kuwa hadi asilimia 79 ya samaki wanaovuliwa nchini Kenya wako katika kundi la spishi zilizo hatarini. Takriban papa wote (asilimia 97) na karibu nusu ya pweza (asilimia 46) waliovuliwa walikuwa bado hawajakomaa.
Kwa mujibu wa Benedict Kiilu, Naibu Mkurugenzi katika Huduma ya Uvuvi ya Kenya, hali hii inachangiwa na shinikizo kubwa la uvuvi kwa viumbe hao. Kiilu alikuwa miongoni mwa wadau waliounda mkakati wa uhifadhi wa papa na pweza pamoja na Mpango wa Kitaifa wa Uhifadhi wa Papa (NPOA-Sharks).

“Wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na mzunguko wa maisha yao. Huishi kwa muda mrefu, na kwa kawaida, kiumbe kinachoishi sana ukuaji wake huwa ni wa taratibu. Wanakabiliwa na changamoto kubwa, na pale wananusurika, tunawaweka chini ya shinikizo lingine linalosababishwa na uvuvi,” alisema Kiilu.
Ili kupunguza shinikizo kwa papa na pweza, moja ya malengo yenye uwezekano mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya kupitia mkakati huo, kulingana na maoni ya wadau, ni kuanzisha njia mbadala za kuwaingizia wavuvi kipato cha kuendesha maisha yao.
Lakini, vyanzo vinasema lazima kitu kitakachoanzishwa kiwe kinakubalika kiutamaduni, kiendane na fursa zilizopo na pia kihamasishe uhifadhi.
Melita Samoilys, mkurugenzi wa CORDIO Afrika Mashariki, aliambia Mongabay kuwa kutafuta njia mbadala za maisha kwa wavuvi kama ilivyopangwa katika mkakati, lazima zitekelezwe kwa ushirikiano na mashirika mbalimbali, serikali na asasi zisizokuwa za kiserikali.
Vyanzo vya habari havikutaja shughuli maalum inayoweza kuwa mbadala kwa wavuvi kuendesha maisha yao. Lakini kulingana na Samoilys, CORDIO huwafundisha wavuvi kuhusu “masuala ya kifedha, kuhusu akiba, kisha kufuatilia biashara ndogondogo ambazo wanaweza kuzifanya kujiingizia kipato.”
Baadhi ya mapendekezo ni pamoja na uvuvi wa kaa, ufugaji wa samaki baharini na ufugaji wa samaki majini.
“Tunaweza kumfundisha mvuvi hadi akafahamu kwa undani biolojia ya papa, lakini kama hana njia nyingine ya kuishi, hali itamlazimisha abaki ndani ya mzunguko wa uvuvi,” alisema Charles Makio, meneja wa uvuvi wa Bahari Hai, shirika la kijamii linaloendesha mpango wa uhifadhi wa papa na samaki bapa huko Kilifi.
Kulingana na Mote, jamii na wavuvi wadogo anaowajua wako tayari kubaini na kulinda maeneo ya kuzaliana ya papa na samaki bapa kwa kuyatenga kama maeneo yasiyoruhusiwa kuvuliwa kwa misimu fulani, kama ilivyo katika moja ya malengo ya mkakati.
“Mara tutakapofanya hivi kwa kudhamiria, tuseme labda kuanzia Aprili hadi Agosti, papa huzaliana kwa wingi kwenye eneo hilo, wavuvi watajua kwamba hawapaswi kuchukua samaki katika maeneo hayo au kutumia tu zana za uvuvi zilizoruhusiwa, ambazo haziwezi kumkamata papa na hasa wale wadogo,” alisema.

Pwani ya Kenya imeshuhudia kuanzishwa kwa maeneo kadhaa ya baharini yanayosimamiwa na jamii (LMMAs), yanayojulikana kama maeneo ya usimamizi shirikishi tangu mwaka 2015, ambapo kulikuwa na maeneo 24. Mkakati huu unahimiza kuongezwa kwa maeneo zaidi.
Kulingana na Samoilys, kuongeza LMMAs kutawapa wavuvi na jamii uwezo pamoja na kuwaongezea fahari ya umiliki na udhibiti wa mbinu za uvuvi na rasilimali za baharini katika maji ambayo wameyatumia kwa miongo mingi. Mtazamo huu pia unahusisha kuwashirikisha wavuvi moja kwa moja katika shughuli za utafiti.
Pia unalenga kuunganisha maarifa ya kienyeji ya mazingira ili kubaini makazi muhimu ya viumbe wa baharini. Hatua hii inaweza kuongeza utayari wao kushiriki katika juhudi za uhifadhi wa papa na samaki jamii ya bapa.
“Unaweza kuwa na maeneo ambayo hayaruhusiwi kabisa kufanya uvuvi, yanayojulikana kama ‘maeneo yasiyoruhusiwa uvuvi’ (no-take zones), na njia bora ya kuyatekeleza ni kupitia sheria za usimamizi shirikishi,” alisema.
“Kilichojitokeza kutoka kwenye warsha na kazi na wavuvi ni kwamba wavuvi wanataka kuchukua jukumu hilo wenyewe, na kufuata juhudi zitakazoboresha hali ya papa na samaki jamii ya bapa.”
Kama kiongozi wa wavuvi wadogo, Mote alisema hapingi kuanzishwa kwa LMMAs zaidi.
“Katika kaunti ya Kilifi pekee, tuna maeneo ya uvuvi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,339.15. Eneo hili ni kubwa sana. Tunaweza kukubaliana kutenga Ghuba ya Ungwana kwa miezi sita au kuacha eneo la Sabaki kwa mwaka mzima kwa sababu ni eneo la kuzaliana, huku tukivua katika maeneo mengine,” aliiambia Mongabay.
LMMAs kwa kiasi kikubwa hufanya kazi kama maeneo yaliyofungwa (ya kudumu au ya msimu), lakini pia hujumuisha miradi ya usimamizi wa bahari. Kwa mfano, katika Wasini na Mkwiro (kaunti ya Kwale Kusini) na Kuruwitu (Kilifi Kaskazini), hufanya urejeshaji wa matumbawe katika maeneo yao ya tengefu.
Baadhi pia hufanya urejeshaji wa mikoko kupitia miradi ya mikopo ya kaboni, huku wengine wakijihusisha na shughuli za utalii.


Mkakati huo pia unahamasisha kuchorwa kwa ramani ya LMMAs zote zilizopo ili kuelewa vyema kama zinapaswa kupanuliwa ukubwa wake au kuunganishwa ili kuunda maeneo makubwa zaidi.
Kuimarisha utekelezaji wa sheria
Ili utekelezaji ufanyike kama ulivyopangwa kwenye mkakati, Makio alisema kunahitajika “uwazi kamili kuhusu kanuni za uvuvi.”
Alisema kwa sasa bado haijulikani wazi kutokana na Sheria ya Uvuvi na Sheria ya Wanyamapori (uhifadhi na usimamizi), pamoja na marekebisho yake, ni aina zipi za samaki jamii ya elasmobranch (papa na samaki bapa) zimelindwa. Kitu kingine kinachohitaji uwazi ni pamoja na masharti ya ukubwa wa matundu ya nyavu kwa maziwa, lakini si kwa bahari.
“Ni ipi tafsiri mahsusi ya samaki wachanga (juveniles) ambao hawapaswi kuvuliwa, au ni adhabu gani itatolewa kwa wale watakaovunja sheria?” Aliuliza kisha akanyamaza. Alisema kuwa kama sheria hazieleweki au hazitekelezwi ipasavyo, papa ndio wanaoumia zaidi.
Kwa upande wa Samoilys, mbinu yenye unafuu zaidi ni ile inayotoa elimu kwa wavuvi kupitia mafunzo, inayoweza kusaidia kufuata sheria na hivyo kulinda papa na samaki bapa.
“Mimi binafsi ninaamini kujenga utii wa sheria ni muhimu sana, kwa sababu mara wavuvi wanapopata maarifa na kuelewa kilicho bora kwa maisha yao na rasilimali wanazotegemea, watafanya jambo sahihi,” alisema.
Hata hivyo, katika kutekeleza mbinu mbadala kama matumizi ya zana za uvuvi, Kiilu alisema anaona changamoto.
Mkakati huo unaonyesha matatizo yaliyopo ya utekelezaji wa sheria na serikali, na una malengo ya kuyashughulikia kupitia taasisi husika. Lakini hata kama BMUs (vyama vya usimamizi wa fukwe vinavyoongozwa na jamii) vitaongeza juhudi, bado kuna changamoto, aliiambia Mongabay.
Kwa maoni yake, kwa kuwa wanachama wa BMUs ni watu wa jamii moja wanaofahamiana, utekelezaji wa sheria unaweza kuwa mgumu, jambo ambalo linaweza kudhoofisha juhudi za uhifadhi.

“Bado wana mtazamo wa kindugu katika kushughulikia mambo, kwamba huyu ni ndugu yangu, huyu ni jirani yangu, nitatekelezaje sheria dhidi yake? Lakini tunajaribu kubadilisha hilo kupitia uhamasishaji,” aliiambia Mongabay.
Bennett alisema nguvu ya mkakati huu itategemea jinsi utakavyotekelezwa “na utayari wa wadau wote kuona uhifadhi wa papa na samaki jamii ya bapa unaimarishwa.”
Kiilu alisema ana uhakika utekelezaji utaanza mara moja, na serikali itajikita katika kuimarisha utekelezaji wa sheria.
Mkakati huu unahitaji hatua kutoka taasisi zake, Huduma ya Uvuvi Kenya, kwa kushirikiana na Huduma ya Wanyamapori Kenya na Walinzi wa Pwani ya Kenya, aliiambia Mongabay.
Kwa upande wake, Samoilys alisema moja ya nguvu kuu ya mkakati huo ni kuongeza uelewa miongoni mwa wavuvi na jamii za pwani kwa ujumla.
“Hili ni jambo tunalolifanyia kazi kwa dhati,” alisema. “Tunatoa mafunzo mengi na kufanya uhamasishaji kwa jamii za pwani kuhusu masuala mbalimbali ya mazingira ya pwani, hasa kuhusu papa na samaki jamii ya bapa.”
Picha ya bango: Mvuvi Chapoka Miongo akizungumza akiwa ndani ya mtumbwi wake wa jadi katika eneo la mkondo wa Shimoni, kaunti ya Kwale, Kenya, mwaka 2022. Picha na AP/Brian Inganga.
Taarifa hii ilichapishwa hapa kwa mara ya kwanza kwa Kiingereza mnamo 27/03/2026.