- William Lukuvi alifariki Machi 25, 2026, akiacha pengo kubwa katika siasa na uhifadhi wa mazingira nchini Tanzania.
- Alijulikana kwa mchango wake katika kusuluhisha migogoro ya ardhi, hasa kati ya wakulima na wafugaji.
- Akiwa Waziri wa Ardhi, alisimamia mageuzi muhimu ya usimamizi wa ardhi, ikiwemo urasimishaji na matumizi bora ya rasilimali.
- Atakumbukwa kwa uongozi wake wa kushirikisha jamii na juhudi za kuunganisha maendeleo ya binadamu na uhifadhi wa mazingira.
Kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania, William Vangimembe Lukuvi, si tu pigo la kisiasa bali pia pengo kubwa kwa juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini humo.
Alipofariki dunia Machi 25, 2026, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, alikuwa bado anahudumu. Aliacha nyuma urithi unaotambulika katika kusuluhisha migogoro ya ardhi katika eneo nyeti linalogusa moja kwa moja mustakabali wa rasilimali asili, hifadhi za taifa, na maisha ya jamii zinazozitegemea.
Mjane wake amepoteza mume, watoto wamepoteza baba na Watanzania wamempoteza mbunge na mwanasiasa maarufu na mkongwe.
Lakini kwa wapenda mazingira nchini, kifo chake kinaamsha kumbukumbu za matumaini kuhusu mafunzo aliyoyaacha katika usuluhishi wa migogoro ya ardhi, hasa kati ya wakulima na wafugaji na katika maeneo yanayopakana na hifadhi za taifa.
Taarifa ya kifo cha Lukuvi, ambaye alikuwa pia Mbunge wa Jimbo la Isimani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), ilitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.
“Kwa wengine, Lukuvi alikuwa na kofia nyingi tofauti. Lakini kwetu wapenda mazingira, tunamwona kama shujaa wa usimamizi endelevu wa raslimali asili. Wote tunafahamu migogoro ya ardhi mara nyingi husababisha matumizi mabaya ya maeneo ya hifadhi, uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu. Lakini pia hupelekea kupotea kwa makazi ya wanyama pori au mimea ya asili.
“Kwa ujumla, usuluhishi wa migogoro ya ardhi ni kiini cha usimamizi endelevu wa rasilimali asili. Ndiyo maana tunamuona Lukuvi kama shujaa, kwa kutambua na kuyasimamia yote hayo,’’ anasema Paul Mphizi, mwanaharakati wa masuala ya mazingira.
Katika nafasi yake ya uwaziri katika wizara tofauti, Lukuvi alisimamia kikamilifu masuala ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kama msingi wa uhifadhi bora wa mazingira, ulinzi wa hifadhi za taifa, matumizi endelevu ya mali asili, na pia kama njia ya kuwaonyesha wakulima na wafugaji kwamba wanaweza kuishi kwa amani wakitumia raslimali zilizopo.
Hata hivyo, nafasi yake kama Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi (2015-2020) ndiyo iliyokuwa na mchango mkubwa zaidi katika masuala ya mazingira, hasa kupitia usimamizi wa matumizi ya ardhi na mipango ya makazi ya watu.
Pia aliongoza mawaziri wenzake wanane wa kisekta kufanya ziara katika mikoa 10 kwa ajili ya kutoa matokeo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kabla ya kuanza kwa ziara hiyo, Lukuvi alisema ziara hiyo ilikuwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu migogoro ya matumizi ya ardhi kwa kwa vijiji ambavyo wananchi wake walivamia maeneo ya hifadhi za misitu, mashamba na mifugo.
Wakati akiwa katika wizara hiyo, Lukuvi alichukua hatua kubwa za kusuluhisha migogoro ya ardhi ndani ya maeneo ya hifadhi. Aliweka pia utaratibu rasmi wa kuruhusu baadhi ya vijiji kubaki vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro, akihakikisha shughuli za wananchi zinakuwa chini ya mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Aidha, aliongoza timu ya mawaziri na wataalamu kutembelea vijiji vilivyopakana na Hifadhi ya Selous na misitu ya miombo mkoani Ruvuma ili kutambua changamoto, kutoa mwelekeo wa suluhu na kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Rais.
Leonard Chakupewa Soza, mwanaharakati na mchambuzi wa masuala ya Mazingira, anasema ukubwa wa utumishi wake wa miongo zaidi ya mitatu unaashiria pia jitihada zake kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Itakumbukwa kwamba katika kipindi hicho, akihudumu katika wizara hiyo, ndipo mfumo wa usajili wa taarifa ulibadilika kutoka analojia hadi dijitali.
“Hiyo ilisaidia kumaliza rushwa na urasimu uliokuwepo; utoaji wa hatimiliki kwa wakulima wadogo na wamiliki wa ardhi wadogo ulishamiri.
“Kadhalika ilisaidia kupungua sana kwa mlundikano wa mashauri ya ardhi, ambayo awali yalijazana katika mahakama mbalimbali na mabaraza ya usuluhishi kote nchini.
“Kwa ujumla, alileta ufanisi wa urasimishaji wa matumizi ya ardhi na kuufanya uendane na kasi ya ukuaji wa majiji kama Dar es Salaam na Dodoma,” anasema Soza.
Anasema Lukuvi pia alishughulikia pakubwa migogoro sugu baina ya wafugaji na wakulima kwa kutosubiri tu taarifa ofisini bali kufika maeneo husika, kusikiliza pande zote na kutoa maamuzi.
“Tunapaswa kumuenzi Lukuvi kwa kuendeleza jitihada na kuhakikisha migogoro ya ardhi inasuluhishwa mapema kabla haijawa mikubwa na kuleta athari kubwa kwa taifa letu,” anasema Soza.
James Nikombwa, mkulima kutoka kijiji cha Kibati wilaya Mvomero mkoani Morogoro, alisema: “Tunapaswa kuendelea kumuenzi Lukuvi kwa jitihada zake za kuhakikisha migogoro ya ardhi inasuluhishwa, na kuwawezesha wakulima na wafugaji kuishi kwa amani bila migongano.”
Michael Mwambande, mfugaji katika eneo la Chimala, wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, anasema mtindo wake wa ushirikishwaji wa wahusika wakuu wakati wa utatuzi wa migogoro, ni mfano halisi unaokumbukwa na wengi.
“Pande zote zinazohusika katika mgogoro, zinapopata uwakilishi katika mijadala ya kutafuta suluhisho, inachangia kwa kiasi kikubwa kufikia maamuzi mazuri na hata suluhisho la kudumu.
“Huu mtindo alioutumia sana Lukuvi unadhihirisha kwamba suluhisho la migogoro ya ardhi linaweza kupatikana kwa njia ya amani kupitia ushirikishwaji na uwajibikaji. Alituonyesha njia ya amani ya kumaliza tofauti zetu. Ni jukumu letu kuhakikisha tunaiendeleza kazi hii,’’ anasema Mwambande.
Lukuvi hakuwa nyuma katika ulingo wa kimataifa. Mwaka 2025, akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu),
Lukuvi alimwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kikao cha ngazi ya juu cha Mkutano wa Saba wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA-7). Jijini Nairobi, Kenya. Katika hotuba yake alitoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa Tanzania yasihi dunia kukabili changamoto za mazingira – HabariLeo kuchukua hatua za haraka, shirikishi na zenye matokeo katika kukabiliana na changamoto za mazingira zinazoendelea kuikabili dunia.
Kadhalika, alisema kwa nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, changamoto za mazingira mara nyingi huzidi uwezo wa kukabiliana nazo, hivyo, aliziomba nchi washirika kutimiza ahadi zao katika kuzisaidia nchi hizo. Katika mkutano huo pia aliwahimiza vijana kuendelea kujijengea uwezo ili kuwa na uelewa kuhusu mazingira.
Lukuvi ambaye alizaliwa Agosti 15, 1955, alikuwa Bungeni kwa vipindi saba, tangu mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi wa Mfumo wa Vyama Vingi nchini.
Alianza ngazi ya uwaziri akiwa Naibu Waziri, wa wizara ya Viwanda na Biashara (2000–2005). Pia alitumikia taifa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) (2010–2015).