- John Tanui alihudumu kwa zaidi ya miaka 30 katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa, akichangia sana katika mawasiliano na mapambano dhidi ya ujangili.
- Alitambulika kwa ujuzi wake mkubwa wa wanyamapori na mapenzi ya dhati kwa kazi yake, pamoja na ushirikiano wa kimataifa.
- Atakumbukwa kwa utu wake, uongozi na kujitolea, akiwahamasisha wengine hata katika nyakati ngumu.
Wakati mwili wa John Tanui unashushwa katika kaburi katika eneo moja la Bonde la Ufa nchini Kenya tarehe 25 Machi, 2026, simulizi kuhusu mwanamume ambaye wengi walitamani awe na maisha marefu duniani, ziliendelea kujadiliwa ndani na nje ya nchi.
Tanui alifanya kazi kama Afisa wa Mawasiliano ya Usalama katika Hifadhi ya Wanyapori ya Lewa kuanzia mwaka 1995 hadi 2024.
“Tanui amekuwa Lewa kwa zaidi ya miaka 23, akisaidia kuboresha operesheni za timu za kupambana na ujangili na wafanyakazi wa hifadhi. Kama mtaalamu wa teknolojia, ndiye aliyeongoza mawasiliano ya kupambana na ujangili Lewa,” Ripoti kuhusu Athari iliyochapishwa mwaka 2017 na hifadhi hiyo, ilieleza.

Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa ujuzi wa Tanui kuhusu wanyamapori na ndege ulikuwa wa kuvutia na kwamba alikuwa mahiri na mtu wa kujituma kuwasaidia wageni wa Lewa ambako alikuwa kama mwongozaji wao. “Kifaru wake aliyempenda zaidi ni Elvis.”
Tanui alikuwa mtu ambaye alivutiwa na kushangazwa na mandhari ya wanyamapori, japo walikuwa wale wale ambao amekuwa akiwashuhudia kwa miongo kadhaa.
Siku moja jioni, alipokuwa akizunguka hifadhi hiyo akiwa na mgeni, walitazama kundi la simba likipanda juu ya mti uliokuwa umeanguka. Jinsi ambavyo Tanui alishangazwa na ustadi wa simba hao kulimshtua mgeni huyo, zaidi ya kuwaona hao wanyama wenyewe. Wote wawili walitazama simba hao kwa takriban saa moja.
Mgeni huyo alikuwa mkurugenzi wa EarthRanger, Jes Lefcourt. “Sijawahi kumwona akifurahia kama alivyokuwa akitazama simba hao. Hapo ndipo unapoona upendo wa kweli na kujitolea,” alisema Lefcourt katika taarifa aliyoitoa baada ya kifo cha Tanui.
Tanui alikutana na kuwapa maelezo wageni wengi, kuanzia waigizaji na wanasiasa, hadi watu mashuhuri kama David Attenborough, mhariri, mwandishi na mtaalam wa masuala ya asili kutoka Uingereza.
Akiitwa kwa jina la utani la “Tango”, Tanui alitumia zaidi ya miongo mitatu kulinda wanyamapori chini ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa. Katika kipindi hicho, mchango wake katika kuunda na kuimarisha shughuli za uhifadhi ulivuka mipaka ya Kenya, hasa kupitia ushirikiano wake na EarthRanger, na Tusk.
Ujuzi alioukusanya ulimweka katika nafasi ya kipekee kati ya mila na ubunifu wa kisasa, huku akisaidia kuingiza teknolojia za kisasa katika kazi za askari wa hifadhi.
Kwa mujibu wa Lefcourt, kazi ya Tanui ya hivi karibuni ilimpa nafasi ya kusafiri katika maeneo mbalimbali barani Afrika, akiwafundisha askari wa hifadhi na timu za usimamizi wa maeneo ya uhifadhi.
Katika ujumbe wake mitandaoni, Tusk ilimkumbuka Tanui kwa ujuzi wake mkubwa kuhusu Lewa na mazingira yake mapana.
“Mapenzi yake kwa teknolojia, mawasiliano na ubunifu wa vitendo yalionekana wazi. John alikuwa mtu wa kipekee ambaye sisi Tusk tumemfahamu kwa miaka mingi, na tunajiona wenye bahati kumwona akiwa katika ubora wake, mwenye hamu ya kujifunza, mwenye kujitolea, na mwenye kipaji cha aina yake,” ilieleza taarifa hiyo.
Alipofariki, Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa ilisema: “Katika nyakati ngumu zaidi, ikiwemo vipindi vya ongezeko la ujangili, Tango alibaki imara. Hakuwahi kukata tamaa. Aliendelea kusonga mbele, na aliwapa wengine matumaini na kuendelea kuwa thabiti. Alijulikana kwa nidhamu yake, nguvu zake, na kujitolea kwake bila kuyumba katika kazi.”
Lakini mbali na mafanikio yake ya kitaaluma, Lewa ilisema Tanui atakumbukwa zaidi kwa utu aliokuwa nao. Alikuwa ni mshauri, rafiki, na kiongozi aliyejenga familia, na si timu tu.
Picha ya bango: Aliyekuwa Afisa wa Mawasiliano ya Usalama wa Lewa Wildlife Conservancy , John Tanui, (kushoto) alipokuwa akiikaribisha timu ya EarthRanger nchini Kenya mwezi Juni, mwaka 2024. Tanui alifariki mwezi Machi 2026. Picha kwa hisani ya timu ya EarthRanger.