- Umeme wa jua ni nishati safi isiyo na madhara kwa mazingira.
- Upanuzi wa wigo wa nishati jadidifu utachangia ujenzi wa mfumo wa nishati unaostahimili mabadiliko ya tabianchi.
- Nishati ya umemejua inapunguza kutegemea umeme wa maji ambao mara nyingi huathiriwa na ukame.
- Matumizi ya umemejua yamewapa fursa wananchi kufungua biashara ndogo ndogo.
Serikali ya Tanzania imekamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa kuzalisha umeme wa jua wenye uwezo wa kutoa megawati 50 uliogharimu Shilingi za Tanzania Bilioni 118.6 (Dola za Marekani Milioni 47.44).
Mradi huo uliojengwa katika kijiji cha Ngunga, wilaya ya Kishapu, mkoa wa Shinyanga, unalenga kuongeza uzalishaji wa nishati safi na kuimarisha uthabiti wa gridi ya taifa. Ulianza kutumika rasmi Februari, mwaka huu.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Tamko la Dar es Salaam la Misheni 300 la mwaka 2025, ambapo Tanzania iliahidi kuongeza mchango wa nishati mbadala katika uzalishaji wa umeme kwenye gridi ya taifa hadi asilimia 75 kufikia mwaka 2030, kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 61.8.
Tamko la Misheni 300 ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2025, inayosisitiza matumizi ya nishati safi endelevu na Mpango wa Kitaifa wa Mchango wa Taifa (NDC) katika Mkataba wa Paris.
Mkataba wa Paris ni makubaliano ya kimataifa yaliyoanzishwa mwaka 2015 chini ya Umoja wa Mataifa, yakilenga kupunguza ongezeko la joto duniani hadi chini ya nyuzi joto 2°C, na ikiwezekana 1.5°C, kwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.
Kupitia mkataba huo, nchi wanachama, ikiwemo Tanzania, hutakiwa kuandaa na kutekeleza mipango yao ya kitaifa ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi (NDCs).
Chini ya mpango huo, Tanzania imeahidi kukuza matumizi ya teknolojia za nishati safi katika uzalishaji wa umeme na shughuli za viwanda, kwa lengo la kupunguza utegemezi wa nishati chafu kama mafuta, gesi na kuni, ambavyo huchangia uchafuzi wa mazingira na kuongeza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, anasema kuwa kuwepo kwa mitambo ya umemejua Kishapu kumeongeza mchango wa nishati ya umemejua katika gridi ya taifa kutoka asilimia 0.37 hadi asilimia 1.33.
Kwa mujibu wa Twange, ongezeko la megawati 50 kutoka mitambo ya kuzalisha umemejua ya Kishapu kumeongeza uwezo wa kuzalisha umeme kwenye gridi ya taifa kufikia megawati 4,450 kutoka 4,400. Lengo ni kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Anasema malengo ya mitambo ni kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja cha nishati ya umeme, hususan umeme wa maji, kwa kuongeza mchanganyiko wa vyanzo vya nishati. Inalenga pia kuimarisha ustahimilivu wa gridi ya taifa, kukuza matumizi ya nishati safi, kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme kwa muda mrefu, pamoja na kuongeza upatikanaji wa umeme nchini.
Kupitia Mkataba wa Kitaifa wa Nishati, Tanzania imeweka malengo ya kuongeza kwa kiasi kikubwa ujenzi wa vituo vya umeme wa jua ili kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini. Takriban megawati 463 za umeme wa jua zinatarajiwa kuongezwa ifikapo mwaka 2030 kutoka 50 za sasa.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza mchango wa nishati mbadala hadi asilimia 75 ya uzalishaji wa umeme, kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyo na uhakika kama maji na gesi, pamoja na kukuza matumizi ya nishati safi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kaimu Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umemejua, Kishapu, Mariana Mark Mroso, anasema kuwa mtambo wa kuzalisha umemejua Kishapu una uwezo wa kuhudumia nchi nzima wakati wa mchana kama jua likiwa la kutosha.
“Megawati 50 zina uwezo wa kuhudumia taifa wakati wa mchana. Tunaweza kutumia uzalishaji wa hapa kupunguza matumizi ya baadhi ya mitambo ya gesi katika masaa yenye jua la kutosha,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa nishati ya jua haiwezi kutegemewa peke yake kwa kuwa uzalishaji wake hutegemea mwanga wa jua.
“Ni muhimu kuwa na mchanganyiko wa vyanzo vya nishati. Sola inafanya vizuri wakati wa jua kali, lakini mfumo wa taifa unahitaji vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha umeme unapatikana masaa 24,” anasema.
Muktadha wa mabadiliko ya tabianchi
Wataalam wa mazingira wanasema kuwa hatua hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa uzalishwaji wa umeme kutoka vyanzo vya mafuta ambavyo ni chanzo kikuu cha uzalishwaji wa hewa chafu inayochochea mabadiliko ya tabianchi.
Mtaalam wa Mabadiliko ya Tabianchi, Pius Yanda, anasema umeme wa jua ni miongoni mwa nishati safi zaidi ambayo uzalishaji wake hauna madhara kabisa kwa mazingira na kwamba kuongezeka kwa miradi ya kuzalisha umeme huo kutapunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kama tunazungumzia nishati safi, basi hii ni miongoni mwa nishati safi zaidi kwa sababu haitoi kaboni wala gesi joto nyingine wakati wa kuzalisha umeme,” anasema Yanda.
Anataja mafuta ya dizeli na petroli, makaa ya mawe, pamoja na matumizi ya kuni na mkaa kuwa ni vyanzo vingine vya nishati ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa gesi joto.
Kwa mujibu wa Yanda, matumizi ya nishati hizo huchangia kuongezeka kwa joto duniani, mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa hewa na madhara ya kiafya kwa binadamu.
Aidha, matumizi ya kuni na mkaa huchochea ukataji miti na uharibifu wa misitu, hali inayopunguza uwezo wa mazingira kufyonza kaboni na kuongeza hatari ya ukame, mmomonyoko wa udongo na kupotea kwa bioanuai.
Anasema kuwa ongezeko la umemejua kwenye gridi ya taifa kutatoa hamasa ya kutumia nishati ya umeme kupikia kwa sababu adha ya umeme kukatika mara kwa mara itapungua.
Yanda anaongeza kuwa mradi wa Kishapu umeonyesha mwanzo mzuri, lakini anasisitiza umuhimu wa kuendelea kupanua wigo wa nishati jadidifu ili kujenga mfumo wa nishati unaostahimili mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hatari za kutegemea chanzo kimoja cha uzalishaji.
Ili kuongeza uzalishaji wa umeme huo, Yanda anashauri serikali kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika utekelezaji wake kama inavyofanyika katika nchi nyingi za Ulaya na Skandinavia na imeleta mafanikio makubwa.
“Nchi nyingi za Ulaya zimefanikiwa kuongeza uzalishaji wa sola kwa kutumia mifumo ya PPP, ambapo sekta binafsi huwekeza katika mitambo na serikali huweka sera rafiki na miundombinu ya gridi. Tanzania inaweza kujifunza kutoka katika mifano hiyo,” anasema.
Anashauri pia serikali kuhamasisha uzalishaji wa umemejua katika viwanda vidogo akiamini kuwa njia hii inaweza kuleta matokeo ya haraka zaidi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu na gridi ya taifa. Anatolea mfano mkoa wa Kigoma, ambapo anasema taasisi binafsi zimewekeza katika viwanda vidogo vya umemejua katika vijiji ambavyo gridi ya taifa bado haijafika.
Moja ya vijiji vinavyonufaika na umemejua katika mkoa wa Kigoma ni Kalya, ambapo takribani nyumba 283 zimeunganishwa kusaidia wananchi kubadilisha matumizi ya mafuta kwenye taa kwenda umeme wa jua.
Aidha wamewekeza kwenye biashara ndogo kama saluni, kuchaji simu na shughuli nyingine za kiuchumi, huku wakilipia gharama ndogo ya kuanzia Shilingi za Tanzania 10,000 (Dola za Marekani $3.89) kwa mwezi.
“Nimeshuhudia uwekezaji mdogo katika Mkoa wa Kigoma. Mfano huko Kigoma Ujiji, taasisi nyingi kama shule, hospitali na watu binafsi wamefungiwa mifumo midogo ya umemejua na wanautumia katika shughuli zao za kila siku,” anasema.
Kwa muda mrefu, uzalishaji wa umeme nchini umeegemea zaidi katika vyanzo vya maji na gesi asilia. Hata hivyo, vipindi vya ukame vilivyoongezeka katika miaka ya karibuni vimeathiri mabwawa ya kuzalisha umeme wa maji, na kusababisha changamoto za upatikanaji wa umeme.
Mkurugenzi wa taasisi ya Endelevu Consults na mtaalam wa mabadiliko ya tabianchi, Franklin Masika, anasema miradi ya umemejua kama wa Kishapu ni hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa nishati ya umeme wa maji ambao kwa sasa unaathiriwa na ukame.
“Kama teknolojia ya umemejua ikipanuliwa, itasaidia kukabiliana na athari tunazozipata kutokana na kutegemea umeme unaozalishwa kutokana na nguvu za maji. Hiyo ni kwa sababu wenyewe pia unaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, kwa hiyo tunatakiwa tuache kabisa kutegemea zaidi umeme unaozalishwa na maji,” anasema.
Anasema hatua hiyo ni muhimu kwa Tanzania, ambayo licha ya kuwa miongoni mwa nchi zenye mchango mdogo katika uzalishaji wa hewa ukaa duniani, inaathirika kwa kiwango kikubwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame, mafuriko na mabadiliko ya mifumo ya mvua.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Benki ya Dunia, Tanzania inazalisha takriban tani milioni 30 hadi 35 za hewa ukaa kwa mwaka, ambayo ni chini ya asilimia 0.1 ya uzalishaji wa dunia.
“Kwa kuwekeza katika miradi ya aina hii, Tanzania inaonyesha utekelezaji wa ahadi zake za kupunguza uzalishaji wa gesi joto chini ya Mpango wa Kitaifa wa Mchango wa Taifa (NDC) katika Mkataba wa Paris,” anasema Masika.

Kupunguza gharama za usafirishaji wa umeme
Kwa mujibu wa Mroso, kabla ya mradi huo, Kanda ya Ziwa ilikuwa ikitegemea umeme unaosafirishwa kutoka mitambo ya maji ya Kihansi, Mtera, Kidatu, Hale, Nyumba ya Mungu na Mradi wa Julius Nyerere, pamoja na mitambo ya gesi iliyopo Dar es Salaam.
Hali hiyo inaipa serikali mzigo wa gharama za usafirishaji kwa kuwa inalazimika kujenga vituo vya kupokea na kuchakata umeme na kuweka wafanyakazi katika njia ambazo umeme huo unapita mpaka kufikia eneo husika.
Kwa hiyo uwepo wa mradi huo wa umemejua unapunguza gharama za kuutoa umeme huo Dar es Salaam na kuufikisha katika Mkoa wa Shinyanga na ya jirani.
Hata hivyo, Msoro anasema kuwa ongezeko la megawati 50 katika gridi ya taifa hakutapunguza gharama za umeme majumbani kwa kuwa gharama za uendeshaji wa mitambo ya kuzalisha umeme wa nishati jadidifu bado ni kubwa.
“Matarajio ya serikali ni kuwa kadri miradi ya umemejua itakavyoongezeka, gharama za uzalishaji kwa kila uniti ya umeme zitapungua,’’ anasema.
Mtazamo wa kiuchumi
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, anasema mradi huo umenufaisha moja kwa moja kaya 109 za kijiji cha Ngunga ilipofungwa mitambo ya umemejua, kaya ambazo hazikufikiwa na umeme wa gridi ya taifa kwa kukosa fedha za kulipia gharama.
Anasema tangu kuunganishwa na umemejua, wananchi wa kijiji hicho wanafanya biashara ndogondogo za kujiingizia kipato kama vile kuuza maji ya baridi na barafu, na kuendesha maduka ya kutoa huduma za kifedha, ambayo awali hayakuwa mengi kutokana na ukosefu wa umeme wa kuchajia machine za kuhamishia pesa.
Mariam Bakari, mmoja wa wanufaika wa umeme wa jua, anasema mara baada ya kufikishiwa umeme, alifungua duka la kuuza vinywaji baridi, ikiwemo maji, soda, barafu, biashara ambayo imemuongeza kipato na kuboresha maisha yake.
Naye Charles Nshoka anasema anafurahia sana kuunganishwa na umeme huo kwa sababu watoto wake wanasoma na kufanya kazi za shule usiku kwa kuwa wanapata mwanga wa kutosha kutoka kwenye umeme, tofauti na awali walipokuwa wakilazimika kutumia vibatari.
Picha ya Bango: Mitambo ya kuzalisha umemejua iliyojengwa katika kijiji cha Ngunga, Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga. Picha kwa hisani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).