- Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani tarehe 23 Machi 2026 yamefanyika huku yakisisitiza umuhimu wa sayansi ya hali ya hewa, lakini pia yakifunikwa na maafa ya mvua kubwa nchini Kenya.
- Licha ya tahadhari za mapema kutoka Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya, athari zimechangiwa na mabadiliko ya tabianchi, mipango duni ya miji, na changamoto za utawala.
- Mvua kubwa imesababisha vifo (takribani 81), mafuriko, maporomoko ya ardhi, na kuhamishwa kwa watu wapatao 70,000 katika kaunti 21, ikiwemo Nairobi.
- Serikali na wadau wanachukua hatua za dharura kukabiliana na maafa, huku wakisisitiza umuhimu wa utabiri sahihi wa hali ya hewa na uhifadhi wa mazingira ili kupunguza madhara ya baadaye.
Machi 23, 2026 ni siku ya kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa kutambua mchango wa sayansi katika kusaidia binadamu kuelewa na kutabiri hali ya hewa.
Huku maadhimisho haya yakiendelea, familia kadhaa kutoka Mashariki mwa Kenya zinaomboleza vifo vya ndugu zao. Watu wawili waliopoteza maisha baada ya ukuta uliolowa kwa maji ya mvua kuwaangukia, na msichana mdogo pia akachukuliwa na maji alipokuwa akichunga mifugo katika eneo hilo.
Katika Kaunti ya Baringo, iliyoko Bonde la Ufa, mwanamke mmoja na mtoto wa miaka minne walifariki baada ya maporomoko ya ardhi kuisomba nyumba yao.
Vifo vingine vinavyohusishwa na msimu huu wa mvua vinaendelea kuripotiwa kote nchini, huku matukio ya karibuni yakifanya idadi ya vifo vilivyotokea hadi sasa kufikia 81. Kwa mujibu wa taarifa za ReliefWeb, takribani kaunti 21 kati ya 47 za nchini humo, ukiwemo mji mkuu Nairobi, zimeathirika. Taarifa hiyo imefafanua kuwa “takribani watu 70,000 wamehamishwa makazi yao”.
Kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua, Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya ilitoa tahadhari. Idara hiyo ilitabiri mvua kubwa, zaidi ya milimita 20 ndani ya saa 24 katika maeneo mbalimbali, na kutoa onyo kuhusu mafuriko, maporomoko ya ardhi, na mwonekano hafifu. Idara hiyo imeendelea kutoa utabiri zaidi wa hali ya hewa kila siku.
Athari za mvua kubwa zinahusishwa na sababu mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upangaji wa miji, na mabadiliko ya matumizi ya ardhi. Pia kumekuwepo madai ya mapungufu katika utawala bora, kama ilivyoripotiwa Gazeti la The Daily Nation.
Wakati wa maadhimisho ya jana, Edward Muriuki, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya, alisema taasisi hiyo ina imani na utabiri wake kwa kuwa sasa umekuwa ukitolewa kwa wakati, unaolenga maeneo maalum, na unakaribia kuwa sahihi kwa karibu asilimia 100.
Athari za mvua kubwa zinahusishwa na sababu mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upangaji wa miji, na mabadiliko ya matumizi ya ardhi. Pia kumekuwepo madai ya mapungufu katika utawala bora, kama ilivyoripotiwa Gazeti la The Daily Nation.
Katika hafla hiyo ya kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani iliyofanyika Kaunti ya Nakuru, katika Bonde la Ufa, Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu Deborah Barasa, alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi vyanzo muhimu vya maji kama Msitu wa Mau na kuhamasisha matumizi ya utabiri wa msimu na ushauri wa hali ya hewa kwa kilimo ili kuboresha mipango na uzalishaji. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuchunguza leo, kulinda kesho”.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo Festus Ng’eno, alisema taarifa sahihi na za kuaminika za hali ya hewa na tabianchi ni muhimu katika kulinda maisha ya watu. “Kenya inaendelea kushuhudia mabadiliko ya tabianchi… yenye athari kubwa kama kuongezeka kwa kina cha maziwa… hivyo utabiri sahihi na unaotolewa kwa wakati muafaka ni muhimu katika usimamizi na kupunguza hasara zinazotokana na tabianchi,” alisema.
Katika msimu mfupi wa mvua zilizonyesha kati ya Oktoba na Desemba 2025, maporomoko ya ardhi katika eneo la Bonde la Kerio yalisomba makazi na kuua watu 39 nyakati za usiku.
Katika msimu huu wa mvua unaoendelea, jiji la Nairobi limeathirika zaidi, likiripoti angalau vifo 37.
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, amelaumiwa kwa kutokujiandaa ipasavyo kukabiliana na mafuriko kwenye jiji. Lakini katika video moja, mbunge wa Bunge la Taifa, James Nyikal, alisemwambia Sakaja kuwa tatizo hilo lilitambuliwa zaidi ya karne moja iliyopita.
“Mwaka 1908, Sir Winston Churchill alitembelea Nairobi, na baada ya kuichunguza akasema kulikuwa na makosa makubwa kwenye ujenzi wa jiji hilo,… kwani lilijengwa katika eneo la mkondo wa mafuriko.” Aliongeza: “Hili, kimsingi, ni tatizo la mifumo ya maji taka na mifereji ya maji.”
Hivi maajuzi Sakaja “aliagiza mpango wa dharura wa saa 48 kushughulikia kuongezeka kwa mafuriko, kushindwa kwa mifumo ya mifereji ya maji, na uharibifu wa barabara kote jijini,” kama ilivyoripotiwa na Kenyans.co.ke.
Mpango huo unajumuisha ukarabati wa barabara, kusafisha mifereji ya maji iliyoziba, na kubomoa miundombinu iliyojengwa kwenye njia za maji, kando ya mito, hasa katika maeneo ya hifadhi ya mito. Kaunti pia imeamuru baadhi ya maeneo kutokaliwa kutokana na hatari ya mafuriko.
Katika ngazi ya kitaifa, Wizara ya Mazingira, Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi inashirikiana na Kituo cha Kitaifa cha Operesheni za Maafa, vyombo vya usalama, pamoja na mashirika ya kibinadamu kama Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kukabiliana na janga hilo.
Wakati huohuo, hatari za ziada zinaendelea kuongezeka, zikiwemo magonjwa ya mlipuko yanayoenezwa kupitia maji machafu ya mafuriko na mifumo ya vyoo iliyoharibika.
Picha ya bango: Magari yaliyokuwa yamezama sehemu katika maegesho yaliyofurika maji huko Nairobi, Kenya, baada ya siku kadhaa za mvua kubwa tarehe 06 Machi 2026. Picha kwa hisani ya AA.com.tr