- Kutoka kula nyama ya kasa utotoni, Farid Abdallah sasa amebadilika na kuwa kinara wa juhudi za uhifadhi wa kasa katika eneo la Shimoni.
- Vijana wa Shimoni Turtle Watch wanatumia mbinu za kisasa za kidijitali kufuatilia mienendo ya kasa na kulinda viota vyao dhidi ya uharibifu.
- Kasa wanakabiliwa na vitisho vingi ikiwemo uchafuzi wa plastiki, shughuli za uvuvi, mabadiliko ya tabianchi na ujenzi wa miundombinu ya pwani.
- Juhudi za uhifadhi zimeanza kuzaa matunda, huku mwamko wa jamii ukiongezeka na matukio ya uvuvi wa kasa kupungua.
KWALE, Kenya – Akiwa na umri wa miaka nane, na akiwa katika darasa la pili, ilikuwa kawaida kwa familia ya Farid Abdallah kula nyama ya kasa. Hii ni kutokana na kwamba baba yake alikuwa mvuvi.
“Baba yangu alikuwa akija nyumbani na nyama ya kasa karibu kila siku. Kama sio yeye aliyemshika, basi ni wavuvi wenzake. Nyama yake ilikuwa ikigawanywa kwa jamii kama ilivyokuwa desturi. Nyama ya kasa ni tamu sana, na tulikuwa tunafurahia sana kitoweo chake,” alisema Abdallah.

Miaka 35 baadaye, Abdallah, ambaye amefanya uvuvi kwa miaka tisa sasa katika eneo la Shimoni, amekuwa mkereketwa mkubwa wa masuala ya kuhifadhi kasa katika kijiji chake.
Abdallah pia anashirikiana na kikundi cha vijana cha Shimoni Turtle Watch kilichoko wadi ya Pongwe-Kikoneni, Shimoni, eneo bunge la Lunga Lunga katika Kaunti ya Kwale, ambacho kimefanya kazi hiyo ya uhifadhi wa kasa kwa miaka saba sasa.
Hii ni kutokana na tishio la kupotea kwa kasa kutokana na uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi, shughuli za uvuvi na ujenzi kwenye fuo za bahari.
Wavuvi wanaochinja kasa waliokufa
Zaidi, Abdallah na kikundi hicho walisema wamechukua hatua hiyo ya kumlinda kasa kutokana na tishio kwamba kuna wavuvi wengine ambao wanapokutana na kasa amekufa humchinja na kugawia watu nyama yake, hatua ambayo inahatarisha afya ya jamii.

Kasa ni aina ya kobe wakubwa wanaoishi baharini. Mnyama huyo hutaga mayai yake ardhini hasa katika ufukwe wa bahari, na kuyafukia humo kwa kati ya siku 45 na 70, hadi yaanguliwe.
Kote duniani, kunao aina kadha wa kadha za kasa, wakiwemo Kasa wa Ngozi (Leatherback), Kasa wa Kijani (Green), Kasa wa Hawksbill, Kasa wa Loggerhead, Kasa wa Kemp’s Ridley, Kasa wa Olive Ridley, na Kasa wa Flatback.
Kati ya hao, walio hatarini sana, kwa mujibu wa IUCN, ni Hawksbill, Loggerhead, Olive Ridley na Leatherback. Aidha, kuna wasiwasi mdogo sana kuhusu uwepo wa kasa wa kijani (Green), kwani idadi yao inaongezeka, kwa mujibu wa IUCN.
Kwa mujibu wa matoleo ya WIOMSA, shirika linalokuza maendeleo ya kielimu, kisayansi na kiteknolojia katika nyanja zote za sayansi ya bahari katika ukanda wa Bahari ya Hindi ya Magharibi, kuna hadi spishi tano za kasa Zanzibari na barani Afrika kwa ujumla. Spishi tano za kasa zinapatikana nchini Kenya. Wametajwa kama kasa wa kawaida, n’gamba, kigange au kigamba, kasa duvi au kasa mtumbi na kasa ilazi/Kasa ngozi/Kasa noa/Kasa tasa.
“Jamii zilizo mashuhuri sana ni zile za kasa wa kawaida na ng’amba. Ingawa kasa hutaga mayai kwenye fukwe takriban kwa kipindi chote cha mwaka lakini msimu mkubwa wa utagaji ni wakati wa kaskazi [Novemba hadi Machi],” WIOMSA inasema.
Mkondo tofauti wa uhifadhi
Ili kuendelea kuhifadhi kasa hao wasipotee hasa eneo la Shimoni kaunti ya Kwale, Pwani ya Kenya, kutokana na ujenzi wa bandari ya kisasa eneo hilo, Shimoni Turtle Watch wanaendeleza juhudi hizo kwa kutumia njia ya kisasa ya kidijitali.
Omar Salim ni mwanzilishi wa kikundi hicho. Alisema ili kuhakikisha kuwa wamehifadhi kasa na viota vyao katika eneo hilo la bandari, kikundi hicho chenye vijana 35, ambapo 15 ni wanawake, kimechukua mkondo tofauti wa uhifadhi.
Wao huzamia baharini, kuwatambua kasa, na kuangalia mienendo yao. Pili, kwa ushirikiano na wavuvi wa eneo hilo, wao hushika doria kila siku kwenye viota vya kasa ili wavuvi na waendesha mashua wasiviharibu.
“Njia tunayotumia ni ya chini ya maji. Wanachama wetu 12 wamebobea kwa maswala ya uzamiaji, kwenda chini ya maji kufuatilia vile kasa wanavyoendelea.

“Wao huchukua picha na video za kasa na kuziweka katika takwimu zetu. Tunashirikiana na baadhi ya wataalamu wa mitandao ambao wanatusaidia kuangalia mienendo ya kasa wanapokua baharini wasipotee,” Salim aliiambia Mongabay.
Mbali na mbinu hizo, pia wanatoa hamasa kwa washikadau, ikiwemo wakuu wa bandari na jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi kasa na viota vyao.
“Mara nyingi sisi hutoa hamasa kwasababu mambo mengine hatuna uwezo wa kuamua sisi. Kwa hivyo, kama jamii, tunapozungumza na wakuu mbalimbali kuhusu chenye tunataka, huwa wanatusikiliza,” alisema Salim.
Zaidi wao hutembelea shule za msingi eneo hilo mara mbili kwa wiki na kutoa hamasa za uhifadhi wa kasa kwa wanafunzi. Lengo lao ni kukuza kizazi ambacho kitajua umuhimu wa kuhifadhi kasa na kutoharibu viota vyao.
Juhudi zimeanza kuzaa matunda
Juhudi zao zimeanza kuzaa matunda katika eneo hilo la Shimoni, Kijiji cha kihistoria kilichoko kusini mwa Kaunti ya Kwale, karibu na mpaka wa Tanzania na mkabala na Kisiwa cha Wasini.
Eneo hilo linajulikana sana kwa shughuli za uvuvi na utalii wa baharini.
Mbarak Kombo ni muongoza watalii katika eneo la Shimoni na Wasini hususan katika hifadhi ya Kisite Mpunguti. Mtazamo wake kuhusu kasa unaegemea katika uhifadhi.
Alisema kikundi hicho cha vijana, wakishirikiana na Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS), waliwapatia mafunzo kuhusu uhifadhi wa mazingira na viumbe wa baharini, ikiwemo kasa. Pia wamekuwa wakiwakataza watalii kubeba chupa za plastiki baharini ili kuzuia madhara kwa chakula au makazi ya viumbe hao.
“Nilipoanza kupeleka watalii kuzamia ndani ya maji, ilikuwa nadra sana kuona kasa. Lakini kwa sasa, niko na ujasiri wa kuwaambia watalii twende mahali fulani na kwa hakika tutawaona kasa.
“Mwaka huu pekee nimezama na watalii baharini mara tatu, na tuliona kasa. Hivyo ni muhimu kuendeleza hamasa hizo kwa wananchi wajue ni kwa nini kasa wanapaswa kulindwa,” alisema Kombo.
Adballah naye alisema juhudi hizo za kuhamasisha jamii na wavuvi zimeanza kuzaa matunda kwani sio rahisi kwa sasa kuona wavuvi wakivua kasa na kuuza nyama yake.
Usemi huu uliungwa mkono na Omar Salim.
“Tunapata habari kupitia wavuvi ambao ni washikadau wakubwa katika uhifadhi kwa sababu hao ndio hukutana na kasa mara kwa mara wanapokuwa katika shughuli zao.

“Wanapotupatia ripoti, tunaenda kuwachukua kasa hao na kuwazika. Lakini kabla ya kuwazika huwa tunachukua vipimo vyao, urefu, upana, na uzito. Pia tunatathmini kilichosababisha vifo vyao na kunakili takwimu hizo kisha tunawapelekea KWS,” aliongeza Salim.
Takwimu za kikundi hicho kuhusu kasa waliopatikana wamefariki katika eneo hilo la Shimoni kutoka mwaka wa 2023-2025, ni 12. Kati ya hao, tisa walizikwa na watatu kuripotiwa katika taasisi za serikali husika.
Aina ya kasa waliopatikana wamekufa katika eneo hilo walikuwa ni Green turtle na Hawksbill.
Vyanzo vya vifo vya kasa
Kulingana na uchunguzi wao, sababu ambazo zilisababisha vifo vya kasa hao ilikuwa ni pamoja na vifo vya kawaida, kugongwa na mashua, kunaswa kwenye nyavu za wavuvi, na kula plastiki.
Ali Shehi ni afisaa wa afya ya umma kutoka Kaunti ya Kilifi. Alisema kuna hatari kubwa ya watu kula kasa aliyekufa na kupata sumu ya chakula.
“Kasa ambaye amekufa mwenyewe huwa hamwagi damu, na ni rahisi sana kuoza, hasa huku pwani, kutokana na joto jingi. Akioza anaweza kuwa na sumu ambayo ni hatari.
“Pia kasa anaweza kuwa amekula sumu kutokana na uvuvi haramu ambao pengine huendelezwa baharini, hivyo basi wanapokula kasa yule watakuwa wanakula sumu moja kwa moja,” Aliongeza Shehi.
Afisaa huyo wa afya alitoa wito kwa jamii kukoma kula kasa ambao wamefariki na badala yake kuwachukua na kuwazika.
Lilian Mulupi ni Afisa wa Mipango, Kitengo cha Uhifadhi wa Bahari kutoka shirika la International Fund for Animal Welfare (IFAW) linalohusika na uhifadhi wa wanyama wa nchi kavu na baharini, makazi yao. Juhudi zao zimelenga wanyama wakubwa baharini, wakiwemo kasa.

Kwa mujibu wa Mulupi, kasa ana umuhimu mkubwa kwa ikolojia ya bahari, na anapoonekana inaashiria kuwa bahari iko na afya nzuri.
Mulupi hata hivyo alisema licha ya juhudi za kumhifadhi kasa kuendelezwa na mashirika, jamii na serikali, bado kuna upungufu wa takwimu kujua idadi yao baharini.
“Idadi kamili ya kasa baharini ni ngumu kupata kwa sababu kufanya utafiti wa baharini unahitaji pesa nyingi sana na utapata mara nyingi tuko na mapungufu. Sasa yule ambaye anakuja kutaga kwenye viota ndio tunamlinda vizuri, tuhakikishe hauliwi ama kushikwa,” Mulupi aliambia Mongabay.
Shirika hilo, kwa ushirikiano na Olive Ridley, wanatumia mbinu ya kidijitali kuwatambua kasa. Mbinu hiyo pia inatumiwa na Shimoni Turtle Watch, ili kujua takwimu za kasa baharini.
Kutambua kasa eneo la Diani
“Tangu mwaka wa 2018, tumekuwa tukifanya kazi ya kutambua kasa eneo la Diani na takriban kasa 1,000 wameonekana katika sehemu hiyo,” alisema Mulupi.
Kwa mujibu wa Dr Gladys Okemwa, ambaye ni mwanasayansi na mtafiti wa maswala ya bahari na uvuvi katika Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Samaki ya Kenya KMFRI, kasa ni muhimu sana katika ikolojia ya bahari.
“Kasa wa kijani [Green turtle], kwa mfano, wako na umuhimu katika kusawazisha mfumo wa ikolojia. Kasa hula nyasibahari na wanapokula kinyesi chao ni mbolea na huchangia lishe ya maji.

“Kasa pia hula samaki aina ya kiwanvi, ambao huwa wengi sana baharini, kwa hivyo husaidia kusawazisha na kudhibiti kuongezeka kwa aina hii ya samaki,” alisema Okemwa.
Kuhusu athari za miradi mikubwa kama vile ujenzi wa bandari, Okemwa alisema bado kuna haja ya kufanya utafiti kutathmini athari za miradi hiyo katika viumbe kama kasa.
Taarifa kutoka kwa Mamlaka ya Bandari ya Kenya hata hivyo inasema licha ya ujenzi huo wa bandari ya Shimoni kufanyika, bado haijaanza kazi rasmi. Inasema kwamba kuna mikakati ambayo itawekwa kwa kuzingatia maoni ya wakazi na wavuvi wa Shimoni ya jinsi ya kuhifadhi kasa na kuhakikisha kuna uvuvi endelevu.
Juhudi za Mongabay kupata usemi kutoka kwa mkuu KWS eneo hilo la Shimoni hazikufaulu. Hadi taarifa hii ikichapishwa, mkuu huyo alikuwa hajajibu maswali ya mwandishi mwetu ili kupata ufahamu zaidi kuhusu juhudi zao za kulinda kasa eneo hilo.
Hata hivyo, nchini Kenya, sheria za KWS chini ya kifungu cha uhifadhi wa wanyamapori na usimamizi, Sheria ya 376 iliyokarabatiwa 2013 (CAP376), inawataja kasa kama viumbe wanaolindwa na kuharamisha uwindaji, uuaji ama kuwasumbua.
Miongoni mwa vigezo vya kulinda kasa nchini Kenya ni kwamba sheria inaharamisha uwindaji, utegaji, kushika na kusafirisha kasa na viungo vyake kama vile mayai, nyama na magamba, akiwa amekufa ama akiwa hai bila ya kibali maalum kutoka kwa KWS. Adhabu ni kali, ikiwemo faini ya $154,799 [KSh20 milioni] na kifungo cha maisha.
Pia iwapo kasa ameshikwa bila kukusudia wakati wa uvuvi, sheria inasema kwamba aachiliwe mara moja kurudi baharini akiwa hai ama hata kama amekufa.

Sheria hiyo ikiendana sawa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa, nambari 14, inazungumzia kuhusu kulinda uhai wa viumbe vya majini.
Kupata ufadhili
Licha ya changamoto wanazozipitia katika juhudi za uhifadhi wa kasa bandarini, kikundi cha Shimoni Turtle Watch, chini ya uongozi wake Salim, kimepata kutambulika hata kufikia hatua ya kupata ufadhili.
Kwa mfano, Salim alisema walipata ufadhili kupitia kwa Shirika la Maendeleo la Umoja Mataifa [UNDP] kupitia mradi wake wa GEF SGP ili kuendeleza harakati hizo wa $21,746 ili kuendeleza juhudi hizo za kuhifadhi mazingira ya baharini, kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi kasa na mbinu endelevu za uvuvi.
Pia ufadhili huo unawapatia mafunzo vijana 30 ujuzi wa kupiga mbizi baharini na kufuatilia, kutambua kasa, pamoja na kunakili vifo vya kasa ili kuchangia ukusanyaji wa takwimu za kasa.
“Jambo lililochangia sisi kutambulika ni swala la kujitolea na kuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kwamba kasa wanapokua wengi wanachangia mambo mengi kama vile utalii na hiyo inamaanisha kuongeza kipato kwa wakaazi.
“Kasa wakiwa sawa, matumbawe yanakua mazuri na samaki wanaongezeka na kuongeza mapato kwa wavuvi,” alisema Salim.
Picha ya bango: Kasa akiwa baharini shimoni. Mnyama huyo hutaga mayai yake ardhini hasa katika ufukwe wa bahari, na kuyafukia humo kwa kati ya siku 45 na 70, hadi yaanguliwe.