- Njia za asili zinasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa bioanuai.
- Kuna mabadiliko ya kijamii, hasa katika nafasi ya wanawake katika usimamizi wa ardhi.
- Zaidi ya vijiji 39 vimeanza kuwa na utaratibu wa mpango bora wa matumizi ya ardhi.
- Vijiji vimeweka sheria ndogo ndogo kuwachukulia hatua watu wanaokiuka taratibu.
Ukame unaochechewa na mabadiliko ya tabianchi unazidi kuathiri maisha ya wafugaji na mifumo ya ikolojia Kaskazini mwa Tanzania. Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma, safari hii, jamii za Kimasai hazina wasiwasi mkubwa wa kupoteza mifugo kutokana na kukosa malisho.
Mfumo wa jadi unaowawezesha kuhifadhi maeneo ya malisho wakati wa msimu wa mvua na kuyafungua wakati wa kiangazi, umekuwa mkombozi kwao na mifugo yao.
Mfumo huo wa malisho ya kuhamahama, unaojulikana kama Engaroni kwa lugha ya Kimasai, unawawezesha wafugaji kutenga ardhi katika nyanda mbalimbali. Ardhi hiyo hutumika kwa nyakati tofauti kulingana na msimu.
Chini ya mfumo huo, wafugaji hufunga baadhi ya maeneo wakati wa msimu wa mvua ili nyasi zikue na kurejesha rutuba na kuyafungua wakati wa kiangazi au ukame kwa ajili ya kulisha mifugo na kuiokoa isife kwa kukosa malisho.
Mfumo huo wa kugawa kanda za malisho pia unajumuisha kugawa kanda kwa ajili ya ndama au wanyama wengine ambao hawawezi kutembea umbali mrefu.
Mbinu ya kutenga maeneo kwa ajili ya ndama hujulikana kama Oloipolili. Mbinu zote mbili husaidia ardhi kujirutubisha na majani kuota vizuri baada ya kuacha kuitumia kwa kipindi fulani.
Akizungumza na Mongabay, Nyamyak Saibulu, mfugaji kutoka kijiji cha Orbamba wilaya ya Longido, mkoani Arusha, anasema desturi hii imekuwa ikitumika kwa muda mrefu katika jamii za wafugaji lakini hivi sasa utamaduni huo umehuishwa kwa kujumuisha mikakati ya kisasa kama upandaji wa miti na majani katika maeneo yaliyotengwa.

Wilaya za Monduli na Longido zilizoko mkoani Arusha ni miongoni mwa wilaya ambazo ni kielelezo cha mafanikio ya matumizi ya mfumo huo wa jadi ulioongezewa mbinu za kisasa katika kutoa suluhisho kwa maeneo ya wafugaji yanayokabiliwa na athari za ukame na mabadiliko ya tabianchi.
Jinsi Engaroni na Olopololi zinavyotekelezwa
Namyak anafafanua namna mbinu hii inavyofanya kazi. Anasema kipindi cha mvua, wanatenga maeneo na kisha kuyagawa katika makundi, kundi la kwanza likiwa la maeneo yatakayoachwa yapumzike na kustawi upya wakati wa kipindi cha mvua ya masika, na la pili likihusisha maeneo ambayo wanyama wataendelea kutumia kipindi hicho.
Wakati mifugo mikubwa huhamishiwa eneo la mbali kabisa, ndama na wanyama wengine ambao hawawezi kutembea umbali mrefu, hutengewa eneo lililo karibu.
“Tukishaona ile mvua kubwa imeanza kunyesha, haya maeneo tunayatenga. Kipindi hicho, ng’ombe hawaruhisiwi kukanyaga humo, mpaka vikao vikae tena kwenye tarafa yalimo maeneo na kuamua kwamba muda umefika wa kuruhusu mifugo iendelee kula majani kwenye maeneo yaliyotengwa na wafugaji,” anaeleza Namyak.
Anasema maeneo yaliyofungwa yanapofunguliwa na ng’ombe kuruhusiwa kuingia, zile sehemu walizokuwa wamehamia kwa muda, nazo hufungwa ili zipumzike na majani kukua tena.
Hali katika wilaya ya Monduli
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kuhusu makadirio ya idadi ya watu, Halmashauri ya Wilaya ya Monduli iliyoko mkoa wa Arusha ilikadiriwa kuwa na wakazi wapatao 248,860 hadi mwaka 2025, ambao wanaishi kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 6,993.
Shughuli kuu ya kiuchumi katika wilaya ya Monduli ni ufugaji wa wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo. Kilimo hufanyika kwa kiasi kidogo huku watu wachache wakijihusisha na biashara. Kutokana na asili ya wakazi wake, ardhi ndiyo utajiri muhimu kwa ajili ya mifugo yao.
Kanda za maalum katika kijiji cha Lengoolwa
Kijiji cha Lengoolwa kilichoko wilaya ya Monduli, mkoa wa Arusha, ni miongoni mwa maeneo yanayokaliwa na jamii za wafugaji wa Kimasai ambayo yamekuwa yakikabiliana na ukame. Matokeo ya hali hiyo yamekuwa ni ukosefu wa maji na malisho, na kuhatarisha maisha ya mifugo.
Hata hivyo, Tajiri Keshori Laizer, Mwenyekiti wa kijiji cha Lengoolwa, anasema wananchi wa kijiji hicho, kwa kutumia mbinu za Engaroni na olopololi pamoja na elimu ya kisasa, wamekuwa wakinusuru baadhi ya mifugo yao isife kwa kukosa malisho.
“Katika kijiji chetu tumekuwa tukitumia mbinu hii ya asili kuhakikisha mazingira yetu yanatunzwa na mifugo inapata malisho. Lakini pia tunazingatia matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia michoro inayoonyesha maeneo ya kuchunga, ya makazi pamoja na yale ambayo hayaruhusiwi kutumia,” anasema Laizer.
Anafafanua kuwa kwa zaidi ya miaka minane sasa wamekuwa wakifanya kazi na shirika la Ujamaa Community Resource Team (UCRT) ambalo huwapa elimu ya kisasa na kuwasaidia kutekeleza mfumo wa ugawaji ardhi kwa ajili ya malisho.

Ili kuhakisha elimu ya kisasa kuhusu utunzaji ardhi kutoka kwa taasisi mbalimbali inawafikia watu wengi zaidi, waratibu wa kanda za malisho pamoja na viongozi wa vijiji wamekuwa wakifikisha elimu hiyo kwa wananchi kwa njia mbalimbali, ikiwemo kupitia mikutano ya hadhara, mikutano ya halmashauri ya kijiji pamoja na kuwatembelea katika maeneo yao ya kufuga.
Akifafanua kuhusu njia za utoaji elimu ya mazingira kwa jamii za wafugaji, Laizer anasema waratibu wa kanda za malisho kutoka Serikali za vijiji na mikutano mikuu ya vijiji huenda moja kwa moja kwenye makazi ya muda ya wafugaji yanayojulikana kama ronjo na kukaa nao chini ya miti kwa lengo la kuwaelimisha.
“Kutokana na juhudi hizo, hivi sasa kuna waratibu wa kanda za malisho ambao tayari wana elimu. Pia baadhi ya wafugaji wana uelewa wa kutosha kuhusu namna ardhi inavyoweza kutunzwa na kurudisha ikolojia yake,” anasema.
Ili kuhakikisha makubaliano ya kugawa na kutenga maeneo ya malisho hayakiukwi, wameweka sheria ndogo za kijiji kwa ajili ya kuwachukulia hatua watu wanaokiuka mipango waliyojiwekea.
“Baada ya kupata elimu ya utunzaji wa mazingira, wananchi wamefanikiwa kutunza chanzo kimoja cha maji hapa kijijini kinachoitwa Lengolwa, ambacho kilikuwa hatarini kukauka lakini hivi sasa kina maji ya kutosha,” anasema Laizer.
Kwa mujibu wa Laizer, katika kijiji chao walitunga sheria ndogo ambazo zinasimamiwa na waratibu wa kanda za malisho, kamati ya mazingira ya kijiji pamoja na wafugaji.
Wale wanaovunja sheria hizo wanawajibishwa, hali inayosaidia eneo kuendelea kutunzwa.
Faida za mbinu za asili katika Wilaya ya Monduli
Mbinu ya asili ya kupumzisha ardhi katika ukanda mmoja na kutumia ardhi ya eneo lingine imeanza kuleta faida na mabadiliko kwa jamii za kifugaji.
Baadhi ya faida ni za wazi wakati nyingine haziwezi kuonekana moja kwa moja kwa sasa.

Kwa mujibu wa Laizer, kupitia mfumo huu, vyanzo vya maji vimelindwa, wanyama wanapata malisho mazuri, udongo unalindwa, miti na majani ya asili imeanza kustawi tena.
“Mfano mzuri ni wa kijiji cha Lengoolwa, ambako siku za nyuma, ufugaji ulikuwa ukifanyika karibu na chanzo cha maji cha Loisale, lakini hivi sasa mbinu hizi za asili zimekuwa na mchango mkubwa katika kulinda vyanzo vya maji na misitu ya asili,” anasema Laizer.
Anaongeza: “Msitu wa mlima Lokisale, ambao ni chanzo muhimu cha maji kwa watu, mifugo na mifumo ya ikolojia ya eneo hilo, hivi sasa umestawi kutokana na juhudi za watu”.
Anafafanua kuwa kupitia upangaji na matumizi bora ya ardhi, ikiwemo kugawa maeneo ya matumizi ya msimu wa mvua na yale ya msimu wa kiangazi, jamii imeweza kupunguza shinikizo kwenye misitu, chemichemi na maeneo nyeti ya ikolojia ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa maji na udhibiti wa athari za ukame.
Faida nyingine iliyotokana na elimu waliyopatiwa wananchi ni kitendo cha kuacha tabia ya kukata miti, tabia iliyokuwa ikileta uharibifu mkubwa awali.
Laizer anasema, “Kwa sasa uelewa wa watu umeongezeka, wakazi wengi wamebadilika na kupunguza ukataji wa miti katika msitu wa Lokisale”.
Marcel Kichumisa, ambaye ni mtaalamu wa mazingira, anasema njia hii ya asili ina faida nyingi.
Anasema: “Ni njia nzuri sana katika kutunza bioanuai na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kwanza ardhi inapata nafasi ya kupumzika na hivyo kurudisha rutuba katika udongo na kupunguza mmomonyoka wa udongo, lakini pia kurejesha uoto wa asili.
Kwa mujibu wa Kichumisa, kupitia njia hii wanyamapori pia hupata nafasi ya kurejea na kutumia maeneo hayo kwa malisho na makazi’’.
“Njia za asili zina nafasi kubwa katika kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa bioanuai. Uzuri ni kwamba hata katika sayansi zinatambulika sana.
“Kwa kutambua hilo, kuna mashirika mbalimbali ya kimataifa yenye miradi ambayo ni ya kuboresha na kuongeza matumizi ya njia asilia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” anasema Kichimisa.
Wilaya ya Longido
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Wilaya ya Longido hadi kufikia mwaka 2025, ilikuwa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu wapatao 191,761.
Wakazi hawa wanaishi katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 7,885. Kama ilivyo kwa Monduli, wakazi wengi wa Longido pia ni wafugaji.
Wilaya ya Longido ambayo iko karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya ni miongoni mwa wilaya zinazokaliwa na jamii za wafugaji hasa Wamasai.
Ardhi ya eneo hilo kwa kiasi kikubwa ni kame, jambo linalofanya jamii hizo kupangilia vizuri matumizi ya ardhi kwa miongo mingi sasa.
Mwaka 2022, mkuu wa wilaya ya Longido, Nurdin Babu aliwahi kukaririwa akisema kuwa ng’ombe 200 pamoja na mbuzi na kondoo 356 walikufa kutokana na kukosa malisho, tatizo alisema lilisababishwa na ukame.
Ripoti ya Ukaguzi wa Mpango wa Taifa wa Kupambana na Jangwa (Performance Audit Report on the Implementation of National Action Programme to Combat Desertification) iliyotolewa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, kuhusu utafiti uliofanyika katika Wilaya 12 za kifugaji nchini Tanzania zikiwemo wilaya za Monduli na Longido, ilionyesha kuwepo kwa vifo vya mfugo vilivyotokana na ukame.
Katika ripoti hiyo, ukurasa wa 35, ilionyesha Wilaya ya Longido kuongoza kwa idadi ya vifo vya mifugo ambapo idadi ya vifo ilikuwa asilimia 42.5 ya jumla ya mifugo wakati kwa upande wa Wilaya ya Monduli, idadi ya vifo vya mifugo kutokana na ukame ilikuwa zaidi ya asilimia 16.
Kutokana na hali hiyo, mbinu ya asili ya Engaroni pamoja na jitihada za upandaji wa nyasi za asili unaofanywa katika wilaya za Longido na Monduli, imekuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji.
Wafugaji wengi wa kimasai katika wilaya hii wanaona tofauti baada ya mbinu hii kuboreshwa, juhudi zilizofanywa kwa ushirikiano na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na Serikali.
Faida za mbinu za asili katika Wilaya ya Longido
Zaidi ya kusaidia mifugo, baadhi ya mbinu hizi za jadi ikiwemo Engaroni, zimeonekana kuwa na mchango katika kulinda na kuendeleza malisho kwa wanyamapori.
Jacob Samsoni, mfugaji kutoka kijiji cha Lengoolwa kilichoko wilaya ya Monduli, anasema kwa kudhibiti shinikizo la mifugo katika maeneo fulani na kuruhusu nyasi kurejea, mazingira yanaongeza uwezo wa kuhimili mahitaji ya wanyamapori wanaokula nyasi kama vile nyumbu, pundamlia na swala, huku yakiruhusu kuishi kwa pamoja kati ya mifugo na wanyamapori.
“Majani haya pia yanasaidia wanyama wa porini wanaokula majani. Hawa wanyama tunaishi nao kirafiki. Kwa mfano twiga na pundamlia wanachanganyikana na ng’ombe na wanakula pamoja,” anasema Samsoni.

Elimeleki Ukwai, Afisa Mazingira katika Wilaya Longido, anaongeza kuwa njia hizi za asili zinachangia urejeshaji wa rutuba kwenye ardhi.
Anasema kwa kuacha baadhi ya maeneo bila kutumika kwa muda, udongo hupata fursa ya kujirekebisha kiasili, nyasi huota kwa wingi zaidi, mizizi ya mimea huimarika, na uwezo wa ardhi kushikilia unyevu huongezeka.
Aidha Ukwai anasema kuwa hatua hii pia hupunguza mmomonyoko wa udongo, ambao umekuwa tatizo kubwa katika maeneo mengi ya wafugaji kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayozidisha ukame na mvua zisizotabirika.
Akieleza jinsi mbinu za asili zinavyosaidia katika kutunza ardhi katika jamii hizi za kifugaji, Ukwai anasema, “Kufuga kwa kanda inasaidia katika kudumisha uwiano wa kiikolojia, kwa sababu inalinda maeneo ya asili kubaki na ikolojia yake hasa sehemu za mapito ya wanyama na vyanzo vya maji na pia inasaidia kudhibiti magugu vamizi na kuchangia ukuaji wa nyasi unaoleta rutuba na kuzuia mmomonyoko wa udongo”.

Marcel anazungumzia namna mfumo huo wa asili unavyosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Anasema, “Mifumo ya asili ya utunzaji wa ardhi kama huu unaotumiwa na jamii za Wamasai, husaidia kuongeza uwezo wa mazingira kujirekebisha (uhimilivu)’’.
Anasisitiza kuwa presha inapoongezeka kutokana na mchanganyiko wa mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu, bioanuwai hudhoofika zaidi.
Kwa hiyo, kupunguza au kuondoa baadhi ya shughuli za binadamu kunasaidia kupunguza msukumo kwa viumbe hai, na hivyo mifumo ya asili kuendelea kufanya kazi yake ya kulinda na kuhifadhi bioanuwai hata katika mazingira yanayobadilika.
“Kwa hiyo, kwa namna moja au nyingine, kuacha eneo fulani bila mwingiliano kwa kipindi fulani kunaongeza uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na kutoa nafasi kwa mifumo ya ikolojia kujirejesha na kuanza upya,’’ anasema.
Licha ya kuwa hakuna takwimu za moja kwa moja zinazoonyesha jinsi mbinu hizi za asili zilivyosaidia wanyama kuongezeka, lakini wenyeji wanasema kuwa mbinu yao inasaidia pia wanyama wanaokula nyasi kupata malisho na kuendelea kustawi.
“Majani haya pia yanasaidia wanyama wa porini wanaokula majani. Hawa wanyama tunaishi nao kirafiki. Kwa mfano twiga na pundamlia wanachanganyikana na ng’ombe na wanakula pamoja na tunawaona wakiendelea kuwa na afya nzuri tu,” anasema Nyamyak.
Kijiografia maeneo ya Longido yanapakana na eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambapo wakati mwingine kuna mwingiliano wa wanyamapori katika maeneo haya.
“Majani tuliyopanda chini ya mfumo huu yanasaidia wanyama wa porini wanaokula majani. Hawa wanyama tunaishi nao kirafiki. Kwa mfano twiga na pundamilia wanachanganyikana na ng’ombe na wanakula pamoja tunawaona wakiendelea kuwa na afya,” anasema Nyamyak.
Mfumo huu wa asili, ni jambo linaloweza kufanyika sehemu nyingine nchini.
“Kwenye mafunzo mbalimbali maafisa ugani wanafundishwa kushauri jamii kuacha maeneo ili yarudi katika namna yake ya asili. Kwa hiyo nadhani licha ya maeneo ya Kaskazini mwa Tanzania, mfumo huu unawezekana hata katika maeneo mengine nchini iwapo wananchi watakubali kufuata taratibu zilizowekwa,’’ anasema Marcel.
Kwa kuona umuhimu wa utunzaji wa mazingira, Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido inajaribu kutumia mbinu mbalimbali kushirikiana na jamii za asili. Hadi sasa ushirikiano huo umesaidia katika kupeleka elimu kwa jamii kwa kutumia viongozi wao wa mila.
“Serikali inashirikiana na wazee wa kimila katika kufanya mambo mbalimbali ikiwemo mikutano ya jamii ambayo hutoa elimu kwa wananchi. Pia Serikali inaandaa sheria na sera zinazosisitiza usimamizi shirikishi wa mazingira,” anasema Ukwai.
Mbali na manufaa ya kimazingira, Ukwai anasema utekelezaji wa njia hizi za asili umeanza kuleta mabadiliko ya kijamii, hasa katika nafasi ya wanawake katika usimamizi wa ardhi.
Katika baadhi ya maeneo ya Longido, wanawake sasa wanahusishwa katika mabaraza ya maamuzi kuhusu kanda za malisho, matumizi ya ardhi na ulinzi wa rasilimali za jamii, jambo ambalo kihistoria lilitawaliwa zaidi na wanaume.
Namyak ambaye pia ni mjumbe wa serikali ya kijiji cha Orbamba, Longido anasema siku hizi wanawake nao wanahusika kufanya maamuzi kuhusu ardhi yao.
“Sasa hivi hata mimi mwanamke nina haki ya kusimama mbele ya wanaume na kusema kuwa hii ardhi msipeane kwa sababu ina manufaa kwa jamii yangu ya kifugaji,’’ anasema Namyak na kuongeza kuwa kutokana na namna jamii ilivyobadilika, hivi sasa katika wilaya ya Longido kuna wenyeviti wa vitongoji, wa vijiji na madiwani ambao ni wanawake ukiachana na wale wa viti maalum.
Mchango wa UCRT Longido
Jamboi Baramayagu, Mratibu wa program za UCRT katika wilaya ya Longido, anasema kwa kutambua kuwa ardhi ni nguzo muhimu kwa jamii za Kimasai wanahakikisha wanawasaidia kupanga matumizi bora ya ardhi iliyopo.
Anasema,“Kila kunapokucha maeneo haya yamekuwa yakipungua, yawe maeneo ya wafugaji, wakulima au waokota matunda, wote maeneo yao yamekuwa yakipungua… kwahiyo tunachofanya kama UCRT ni kuwasaidia wananchi kupanga matumizi bora ya ardhi iliyopo,” anasema Jamboi.
Katika Wilaya za Monduli na Longido, shirika la UCRT linashirikiana na jamii ya kifugaji ya Kimasai kupata hati za maeneo yao ili iwasaidie kutunza maeneo haya.
Kwa mujibu wa Jamboi, UCRT pia inashirikiana na jamii katika kutoa elimu kwa mabaraza ya kifugaji kuhusiana na masuala ya utunzaji wa mazingira.
Anafafanua kuwa UCRT pia imewasaidia wafugaji katika wilaya 11, kupata hati za kumiliki eneo lenye ukubwa wa hekta milioni 2.1. Asilimia 25 ya maeneo hayo ni katika wilaya ya Longido.
“Kwa Longido tumesaidia kutoa hati za kimila kwa hekta 500,000. Lakini kama unavyojua mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiathiri sana wafugaji, kwa hiyo kupata hati ni kitu kimoja lakini kuyalinda haya maeneo ili yaendelee kusimamiwa na ili yawe na tija, ni kitu kingine,” anasema Jamboi.
Katika Wilaya ya Longido, zaidi ya vijiji 39 vimeanza kuwa na utaratibu wa mpango bora wa matumizi ya ardhi ili kusaidia ikolojia ya maeneo yao na pia kusaidia mifugo na wanyama wa porini.
Jitihada zinazofanywa kuhakikisha wafugaji wananufaika na ardhi zinapewa nguvu na sera ya taifa ya uhifadhi wa ardhi.
Sera ya Taifa ya Uhifadhi wa Ardhi ya mwaka 1995 toleo la mwaka 2023, inasisitiza kuwa ili kuhakikisha jamii zinanufaika na ardhi, miliki za kimila za ardhi zinatakiwa kutambuliwa. Pia katika malengo yake, sera hiyo inasisitiza matumizi bora ya ardhi ili kuleta maendeleo.

Lengo la pili la sera hiyo ni kuhakikisha kuwa milki za ardhi zilizopo hasa za kimila ambazo ndizo zinazotumika na watu wengi nchini, zinatambuliwa na kulindwa kisheria.
Lengo la nne la sera hiyo ni kuhakikisha kunakuwa na matumizi bora ya ardhi ili kuongeza uzalishaji na kuleta maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi.
Katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, Sera ya Taifa ya Uhifadhi wa Ardhi ya mwaka 1995, toleo la mwaka 2023 inasema kuwa serikali itaandaa mipango ya matumizi ya ardhi yatakayozingatia uhifadhi wa mazingira.
Aidha inasema Serikali itaandaa na kusimamia utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia ya nchi katika ardhi.
Changamoto ya utunzaji wa mazingira kwa wilaya zote
Katika kutunza mazingira yao ya asili, wafugaji wanakutana na changamoto kadhaa. Miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa elimu.
Kwa mujibu wa Laizer, licha ya juhudi ambazo tayari zimefanywa na mashirika mbalimbali pamoja na Serikali, lakini bado kunahitajika juhudi zaidi za kuwafikia wafugaji wengi na kuwaelimisha kuhusu changamoto za mazingira ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ambayo huathiri mifugo yao na hivyo kuathiri vipato vyao.
“Wadau wote bado tunahitaji elimu ya mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi na utunzaji bora wa ardhi na masuala mengine muhimu kwetu kama mbinu za kutuwezesha kunufaika na mifugo yetu,” anasema Laizer.
Kwa wilaya zote mbili za Longido na Monduli wafugaji wanakabiliwa na mimea vamizi ambayo licha ya kukosa faida yoyote kwa mazingira, inaharibu ikolojia ya ardhi.
“Changamoto kubwa ambayo inakabili wafugaji ni mimea vamizi katika maeneo ya malisho. Kuna mmea mmoja unaitwa mrasia, ni mmea hatari ambao umevamia vijiji viwili vya wilaya ya Longido.
Wakati wa kiangazi hustawi sana na ukiota sehemu unazuia mazao mengine yasiweze kuota. Kama jitihada hazitafanyika, mmea huu unaweza kufika Monduli na maeneo mengine ya ardhi ya wafugaji,” anaonya Ukwai.
Kwa upande wa serikali, Ukwai anataja changamoto kubwa kuwa ni pamoja na kutofautiana kwa mifumo ya serikali na jamii husika, lugha inayotumika kwenye mikutano kutoeleweka kwa wadau wote.
“Changamoto nyingine ni uuelewa mdogo wa jamii kuhusu miradi inayohusu utunzaji wa mazingira. Watu wanashindwa kuiunga mkono wakidhani lengo lake ni kuwachukulia ardhi yao,’’ anasema Ukwai.
Changamoto nyingine inatajwa kuwa ni ongezeko la idadi ya watu, jambo linalozidisha uhitaji wa rasilimali na kusababisha migogoro ya matumizi ya ardhi.
“Idadi ya watu inaongezeka lakini ardhi iko vilevile. Kwa hiyo kinachotokea ni kwamba maeneo haya yamekuwa yakivamiwa,” anasema Jamboi wakati akielezea namna ongezeko la watu linavyopunguza upatikanaji wa ardhi kwa kila familia, kwa ajili ya mifugo na huduma nyingine za kijamii.
Kushughulikiwa kwa changamoto hizi kunahitaji elimu, sera na sheria bora, ulinzi wa rasilimali pamoja na ushirikiano wa jamii ili kuhakikisha njia hizi za jadi za usimamizi wa ardhi zinaendelea kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo, anasema Namyak.
Picha ya Bango: Kampeni ya upandaji miti kama njia mojawapo ya kuhifadhi mazingira, inaendelea kupata hamasa katika maeneo ya wafugaji, Kaskazini mwa Tanzania, zikishirikisha wanaume na wanawake. Picha kwa hisani ya UCRT.