- Mamia ya wakazi wa kijiji cha Chesongoch, katika Bonde la Ufa nchini Kenya, bado wanaishi katika kambi za muda miezi mitatu baada ya maporomoko makubwa ya ardhi kuzoa makazi yao.
- Maporomoko haya ya mara kwa mara yana athari kubwa na za muda mrefu kwa mfumo mzima wa ikolojia.
- Msimu mwingine wa mvua umeanza, na kuwatia hofu wale ambao walipoteza wapendwa wao na mali katika matukio ya 2025.
- Wataalamu wameonya kuwa ardhi ambayo imemilikiwa na mamia ya watu walio hatarini ilikuwa misitu.
Hii ni sehemu ya kwanza ya nakala hii kuhusu maporomoko ya ardhi yaliyotokea nchini Kenya baada ya msimu wa mvua Novemba 2025. Soma sehemu ya pili hapa.
KERIO VALLEY, Kenya – Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Kenya tangu Februari zinazidi kuacha alama zisizofutika kwa watu mijini na vijijini, huku jamii zikikabiliana na majanga. Tayari barabara zimezibwa, madaraja yameanguka, huku mashamba yakijaa maji na mafuriko yakizua hofu ya vifo zaidi.
Zaidi ya watu 70 wameripotiwa kufariki kote nchini kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua tangu Februari 2026. Maelfu ya familia pia yamepoteza makazi yao, na wengine wengi kuathirika kwa njia nyingine mbalimbali.
Lakini hata kabla ya mvua na mafuriko ya 2026 ambayo yamegonga vichwa vya habari, Bonde la Kerio lililoko magharibi mwa Kenya, lilikuwa limeshuhudia vifo vya takriban watu 39 katika mazingira ya kutatanisha. Ilikuwa Oktoba 31, mwaka jana, wakati ghafla maporomoko ya ardhi yalisomba nyumba, miti, na mashamba ya wakazi wa kijiji cha Chesongoch, Elgeyo Marakwet na kuwazika wengi wakiwa bado hai.
Hadi sasa, zaidi ya familia 600, ambazo ni baadhi ya wale walioathiriwa, bado zinaishi kwenye makambi ya wahamiaji wa ndani, huku hofu ya mikasa zaidi ikitanda, hasa baada ya Idara ya Hali ya Hewa kutangaza uwezekano wa mvua zaidi.
Hata hivyo, historia ya maporomoko ya ardhi katika eneo hili ni ndefu na yenye mafunzo ya dhahiri. Tukio hilo la mwaka 2025 liliashiria hatari iliyojirudia: mwaka 2010 vifo 14, na mwaka 2012 vifo 26.
Mongabay kwenye eneo la tukio
Mwezi Februari, 2026, timu ya Mongabay ilitembelea nyumbani kwa Mathias Chelimo katika kijiji cha Kwenoi, Chesongoch, na kumkuta akichakura kwenye vifusi kujaribu kuokoa kilichosalia kwenye shamba lake la miembe. Aliinua kichwa kwa muda mfupi kutusalimu, kisha akaendelea na kazi iliyoonekana kana kwamba haina matumaini.
“Ilikuwa takribani saa kumi alfajiri niliposikia mlio mzito kutoka milimani, upande wa magharibi (Mteremko wa Elgeyo Marakwet). Ardhi ilitetemeka kwa nguvu,” aliisimulia Mongabay.


Chelimo alipotoka nje kuangalia hali ilivyokuwa, kulikuwa na giza totoro, lakini sauti kubwa za kishindo na vilio vya watu vilimfanya akimbilie tena ndani ya nyumba yake. “Nilitambua kuwa tulikuwa katikati ya janga la maporomoko ya ardhi,” huyo mstaafu wa utumishi wa umma mwenye umri wa miaka 78 aliiambia Mongabay.
Saa kadhaa baadaye, baada ya giza kupotea, ndipo alielewa ukubwa na athari za maporomoko hayo, ambayo alisema yalidumu takribani dakika 15.
“Makazi matatu upande wa kushoto wa nyumba yangu na matano upande wa kulia yalifagiliwa kabisa. Mahali palipokuwa na mto, sasa kulijaa mawe makubwa, miti na tope. Mazao na uoto mwingine vilitoweka. Jiografia nzima ya eneo ilibadilika,” alisema Chelimo, ambaye sasa nyumba yake imesimama kati ya mto kwa upande mmoja, na vilima upande wa pili, baada ya nyumba za majirani zake kusombwa kwenye bonde.
Baadaye, Chelimo alijiunga na waokoaji katika msako wa kuwatafuta watu waliopotea na miili ya waliokufa. “Mara kwa mara tulikuta kiungo cha mwili hapa, na kingine pale. Miili kamili ilikuwa nadra kupatikana. Ilikuwa vigumu kuwatambua,” alisema.
Zaidi ya vijiji sita, vikiwemo Kasegei, Kaptul, Moror, Kipkirwon, Kwenoi na Central Chesongoch, viliathiriwa. Katika kijiji cha Kwenoi pekee, Chelimo alisema, kufikia Februari watu saba walikuwa hawajulikani waliko.
Pembezoni mwa kijiji, karibu na kanisa la eneo hilo, kulikuwa na makaburi ambako zaidi ya watu 31 waliopoteza maisha kwenye kadhia hiyo ya maporomoko ya ardhi walizikwa. Makaburi hayo yalikuwa yamewekewa misalaba.

Mbali na maumivu ya kihisia na hofu ya uwezekano wa kutokea tena kwa maporomoko mengine makubwa, wakazi wanaendelea kuhesabu hasara za kiuchumi, baada ya miti yao ya miembe na mashamba ya migomba kuharibiwa, pamoja na mifugo, hasa mbuzi, kufa katika janga hilo.
Wakati timu ya Mongabay ilipokutana naye, Chelimo alisema: “Miembe ndiyo ilikuwa pensheni yangu na chanzo cha riziki. Sijui nitafanya nini sasa.”
Ingawa hakupoteza nyumba yake, haingekuwa salama kuendelea kuishi humo. Hivyo alichagua kuhamia katika kambi ya watu waliopoteza makazi yao ili aweze kupata misaada kutoka kwa serikali ya Kenya na taasisi nyingine. Wakati mwingine alipata msaada kutoka kwa wasamaria wema.
Hasara na majonzi kwa mwanamke
Susan Chepchumba, ambaye pia mkazi wa kijiji cha Kwenoi, alipoteza mwanawe katika janga hilo. Kama ilivyokuwa kwa waathirika wengine wengi, mwanawe aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu moja nchini Kenya, alikuwa amelala fofofo wakati maporomoko ya ardhi yalipotokea. Alikuwa miongoni mwa waathirika 31 waliozikwa. Chepchumba sasa amebaki na watoto watatu wengine.

Lakini pia alipata hasara nyingine kubwa: Kati ya miti 75 ya miembe iliyokuwa imepandwa kwenye eneo la ekari tatu, ni miti mitatu tu imesalia. Miti hii ndiyo ilikuwa chanzo chake kikuu cha riziki. “Nilipoteza pia kondoo na mbuzi,” aliiambia Mongabay.
Timu ya Mongabay iliona miti hiyo mitatu ya maembe iliyosalia ikiwa imesimama imara kana kwamba inakaidi uharibifu na taharuki iliyosababishwa na janga hilo. Chepchumba alisema kuwa kila mwaka, wakati wa msimu wa mavuno wa Januari na Februari, alikuwa akipata $400 [KSh60,000] kila wiki kutokana na mauzo ya maembe.
Harufu kali ya matunda yaliyoiva kupita kiasi na kuoza sasa inakukaribisha unapoingia Kwenoi, huku miti mingi ya maembe ikidondosha matunda yake. “Hakuna tena wanunuzi wa maembe kwa sababu mashamba yetu hayafikiki kutokana na maporomoko ya ardhi yaliyoharibu barabara. Tumekwama na matunda yetu, na tunaendelea kuhesabu hasara zaidi,” alisema Chepchumba.
Chepchumba pia huenda mara kwa mara kwenye kituo cha kijiji kupokea misaada ya hapa na pale kutoka serikalini na taasisi nyingine, ingawa misaada hiyo si ya uhakika. Msaada mkubwa zaidi unatoka kwa majirani na ndugu ambao hawakuathiriwa vibaya na maporomoko hayo kama alivyo yeye.
“Ni msimu wa kupanda na hatujaandaa mashamba yetu. Baadhi yetu hata hatujui mashamba yetu yaliko,” alisema.
Wataalamu wanaonya kuwa bila sera madhubuti za kuongoza matumizi ya ardhi na uhifadhi wa mazingira, maporomoko ya ardhi katika eneo la Chesongoch na maeneo mengine yataendelea kujirudia.
“Ni kutowajibika watu kuvamia miteremko mikali katika maeneo kama Chesongoch, wakikata miti na kulima mazao. Na wanafanya vibaya zaidi kwa kulima wakifuata mwelekeo wa mteremko badala ya kulima kwa kuvuka mteremko,” alisema Charles Maina Gichaba, Profesa Mshiriki wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya
Hakuna hifadhidata rasmi ya kitaifa inayoorodhesha matukio yote ya maporomoko ya ardhi nchini Kenya yanayotokea mwaka hadi mwaka. Hata hivyo, hili halikuwa tukio la kwanza kwa eneo la Chesongoch lenye ukubwa wa kilomita za mraba 11.5.
Kumekuwa na ripoti za matukio tofauti kuanzia mwaka 2010 ambapo watu 11 walipoteza maisha, mwaka 2011 kukawa na vifo 14 viliripotiwa, mwaka 2012 watu 26 walifariki, na mwaka 2020 ambapo watu 18 walipoteza maisha.
“Mabadiliko ya tabianchi pia yanachangia kwa kiasi fulani, kwani hali hii mara nyingine husababisha mvua nyingi katika maeneo yaliyoathirika. Lakini pia maporomoko ya ardhi yanaongezeka kwa sababu tumejenga makazi katika maeneo ambayo awali hayakuwa ya makazi,” alisema Gichaba.


Nchini Kenya, maporomoko mengi ya ardhi hutokea katika misimu ya mvua ya Machi hadi Mei (mvua nyingi) na Oktoba–Desemba (mvua za kipindi kifupi), huku maeneo yenye hatari kubwa ikiwa ni Elgeyo Marakwet, West Pokot, Nandi, Nyandarua na sehemu za kaunti za Murang‘a na Kakamega.
Kaunti ya Elgeyo Marakwet ina misimu miwili ya mvua. Mvua nyingi hutokea kati ya Machi hadi Mei, zikifikia kilele chake mwezi Aprili na Mei, wakati mvua za kipindi kifupi hutokea kati ya Oktoba hadi Desemba, huku kiwango cha mvua cha mwaka kikitofautiana kutoka milimita 700 katika nyanda za chini hadi milimita 1,700 katika nyanda za juu, kulingana na takwimu za Kitengo cha Hali ya Hewa cha Kenya. Kipindi cha ukame kawaida ni Januari hadi Februari, na Juni hadi Septemba, ingawa mvua inaweza kunyesha katika miezi hiyo.
Juhudi za kuzuia maporomoko ya ardhi Elgeyo Marakwet hazijaanza juzi. Ripoti ya Uchambuzi kuhusu Maporomoko ya Ardhi ya Bonde la Kerio unaonyesha kuwa eneo hilo linakumbwa mara kwa mara na maporomoko kutokana na “mvua nyingi, ukataji miti na kilimo kwenye vilima vyenye miteremko mikali” na kwenye baadhi ya maeneo ambayo ni “hatari sana kutokana na udongo laini, kuanguka kwa mawe, na ukataji miti wa kihistoria.”
Ripoti hiyo inabainisha baadhi ya juhudi zilizofanywa kuzuia maporomoko katika kipindi cha ukoloni, ambapo afisa wa kikoloni wa Uingereza aitwaye William Spencer “aliweka msitari wa usalama kando ya Mteremko wa Elgeyo, ili kuzuia makazi katika eneo lililokuwa hatarini kutokana na mmomonyoko.”
Hii ilitokea mwanzoni mwa karne ya 1900, na mstari huo ukapewa jina “The Spencer Line” kutambua mchango wa afisa huyo wa kikoloni. Spencer alichunguza usalama wa mteremko na kuangalia mifumo ya mmomonyoko kabla ya kuja na suluhisho hilo.
Mstari huo, uliofanya kazi kama mfumo wa awali wa upangaji wa matumizi ya ardhi Elgeyo Marakwet, uliundwa kwa lengo la kuzuia makazi ya binadamu katika maeneo hatarishi, kulinda misitu ambayo pia ilikuwa inashikilia udongo pamoja, na kuunda eneo la kinga kati ya makazi na sehemu hatarishi zinazopaswa kuepukwa, ripoti inasema.

Lakini utekelezaji wa sheria kuhusu Spencer Line ulidhoofika baada ya Kenya kupata uhuru, na watu walianza kuishi katika maeneo hatarishi. Ukataji miti uliongezeka, watu wakaanza kukata miti ili kuandaa ardhi kwa makazi na kilimo, huku wengine wakitengeneza mkaa.
“Ongezeko la idadi ya watu lilipelekea ujenzi wa nyumba na mashamba katika maeneo hatarishi ambayo awali yalikuwa yamebainishwa kuwa juu ya mistari ya ukomo,’’ ripoti hiyo inasema.
Utafiti huu wa mwaka 2013 pia uliainisha ongezeko la idadi ya watu kama chanzo cha uvamizi wa maeneo hatarishi, upanuzi wa miundombinu ya usafirishaji, na ukataji miti katika maeneo hatarishi kwa maporomoko ya ardhi. Mabadiliko ya tabianchi nayo yalitajwa kama sababu za ongezeko la matukio ya maporomoko.
Utafiti mwingine uliochapishwa katika Natural Hazards mnamo Februari 2026 unaorodhesha shughuli za binadamu kama vile ujenzi wa barabara, uhandisi wa madini, ukataji miti, kilimo, idadi kubwa ya watu, tetemeko la ardhi, na mvua nyingi kama sababu kuu za maporomoko ya ardhi nchini Kenya.
Gichaba anaeleza kuwa kijiolojia, maeneo haya ya milima hayana usalama.

Mawe yaliyoko chini ya ardhi, au mawe yanayojificha chini ya uso wa ardhi, ni yenye mashimo, hivyo hayawezi kushikilia wakati yamejaa maji kutokana na mvua nyingi.
“Unapokata miti, unaondoa mizizi inayoshikilia mawe haya pamoja, hivyo kuongeza uwezekano wa maporomoko ya ardhi wakati wa misimu ya mvua,” anasema.
Anasema maporomoko ya ardhi yanaweza kupunguzwa kupitia sera madhubuti za matumizi ya ardhi, ambazo zinajumuisha uelewa bora na ramani za hatari pamoja na uwezo ulioimarishwa wa kupunguza na kukabiliana na hatari hizo.
Sheria na kanuni za matumizi ya ardhi na mipaka ya makazi nchini Kenya zinakataza makazi katika ardhi zisizo imara kama milima na vilima.
Chelimo aliiambia Mongabay kuwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 na 1970, alipokuwa mtoto, milima ilikuwa imejaa misitu na wanyamapori. “Hata sisi vijana wenye ujanja hatukujaribu kuingia milimani kwa hofu ya kukutana na wanyama,” aliiambia Mongabay.


“Misitu imeanza kuondolewa ili kutengeneza mkaa, kuandaa mashamba kwa ajili ya kilimo, kutokana na ongezeko la idadi ya watu na harakati za kupata rasilimali,” anasema.
Aliiambia Mongabay kuwa juhudi za serikali za mitaa na taasisi kama Kenya Forest Service kuhifadhi misitu hazijazaa matunda kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uhaba wa rasilimali kama magari ya ulinzi, ufisadi wa maafisa wa serikali wanaopokea rushwa kutoka kwa wakazi na kuruhusu ukataji miti, na watu kukosa hamasa ya kuhifadhi misitu.
Tukio la maporomoko ya ardhi halikuwa la kusambaa kwa Kenya peke yake. Miezi mitatu kabla ya yale yaliyotendeka Elgeyo Marakwet, Bulambuli, mashariki mwa Uganda, umbali wa chini ya kilomita 300, angalau watu 20 walipoteza maisha, na wengine 113 kutoweka baada ya maporomoko ya ardhi kuzika nyumba katika vijiji sita.
Ripoti ya hivi karibuni ya IPCC (Sixth Assessment Report) inaonyesha kuwa Afrika Mashariki inakabiliana na changamoto kubwa za tabianchi, ikiwemo hali mbaya ya hewa. Ripoti hiyo inasema kuwa ongezeko la joto limekuwa haraka zaidi katika kanda hii kuliko wastani wa dunia. Hatua za binadamu zinazohusiana na uchimbaji wa mafuta ya kisukuku ndizo zinachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la joto duniani.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa mawimbi ya joto baharini yamekuwa ya mara kwa mara tangu karne ya 20 na inakadiriwa kuongezeka Afrika. Matokeo haya yanaashiria kwamba lazima hatua za haraka zichukuliwe kupunguza madhara na kujenga uwezo wa kustahimili kwa jamii za vijijini zilizo mstari wa mbele kupambana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi katika Afrika Mashariki.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Athari za Majanga inahimiza Anticipatory Action, mpango unaoziwezesha jamii kuwa tayari kwa majanga. Ofisi hiyo ina jukumu muhimu katika kuratibu juhudi hizi, ikijumuisha pia utafiti wa kubaini vichocheo, viwango vya maamuzi, na hatua zinazopimika.

Obed Matundura, mwanasayansi wa masuala ya tabianchi na mtafiti mkuu katika International Institute for Environment and Development, anasema: “Kwa Chesongoch, itakuwa vizuri kuangalia maandalizi ya hatari za majanga nchini Kenya na hatua zinazochukuliwa kupunguza madhara.”
Wito wa kuwa na utu na kuungana katika juhudi za pamoja za kimataifa kushughulikia changamoto za tabianchi wakati wa COP30 nchini Brazili ni hatua nzuri ya kuanzia. Miongoni mwa maazimio yaliyotolewa ni kuanzishwa kwa mpango wa utekelezaji wa teknolojia, ukiwa na ratiba na vipengele maalum, ili kuziwezesha nchi zinazoendelea kutoa kipaumbele kwa teknolojia.
“Hii ni mojawapo ya mambo ambayo Afrika ilikuwa ikipigania kwenye COP30. Katika maandishi ya mwisho, yote yameunganishwa katika “Uhamishaji wa Teknolojia”, ikiwa na kamati ya utendaji kufuatilia na kusaidia vipaumbele vya teknolojia kwa nchi zinazoendelea,” Obed aliiambia Mongabay.
Mpango huu unategemea mifumo ya msaada wa kifedha kama vile Green Climate Fund iliyoanzishwa chini ya Makubaliano ya Paris ya mwaka 2015, ambayo ni chombo kikubwa cha upunguzaji na urekebishaji wa tabianchi cha kusaidia nchi kukabiliana na mabadiliko hayo.
“Nchi zote zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na Kenya, zina fursa ya kupata fedha hizi. Kenya tayari imenufaika na chombo hiki. Lakini je, inatosha? Sidhani. Nchi bado zinahitajika kuwekeza rasilimali zake katika hatua za kurekebisha na kupunguza madhara ya tabianchi kupitia Mchango wa Kitaifa Uliobainishwa kufadhili programu zake za kupunguza madhara,” alisema.
Baadhi ya taasisi barani Afrika pia zinaongoza katika teknolojia mpya zinazolenga kutoa mfumo wa tahadhari ya mapema kwa jamii za wenyeji kuchukua hatua zinazofaa.
Chuo Kikuu cha Nairobi, kwa mfano, kimeunda mfumo maalum wa lugha unaofanya kazi na vipimo vya mvua vya kidigitali ili kutoa tahadhari kwa watu wanaoishi chini ya milima wanapokaribia hatari.

“Tulijiuliza kama uzoefu wa zamani unaweza kutumika kuelewa maporomoko ya sasa na kutabiri yatakayojitokeza katika siku zijazo. Tuliunda mifumo hii inayoshirikiana na mtandao wa vipimo vya mvua vya kidigitali vilivyo katika maeneo hatarishi, vinavyotoa tahadhari pale kiwango hatari cha mvua kinapofikiwa,” Gichaba alieleza.
Ili kuangalia kiwango cha utekelezaji wa sera na upangaji wa bajeti, hasa kwa maandalizi ya majanga, Mongabay iliwasiliana na serikali ya kaunti ya eneo hilo kwa maoni, ikitaka kujua mipango ya matumizi ya ardhi, lakini haikupata majibu kutoka ofisi ya gavana baada ya wiki tatu.
Hata hivyo, kwa waathirika kama Chepchumba na Chelimo, suluhisho la kudumu lingekuwa bora. “Tumechoka kuishi kwa hofu. Kila mvua zinaponyesha, tunatazama milima, tukihofia lini janga kubwa litatokea,” Chepchumba aliieleza Mongabay.
Nukuu:
https://www.scribd.com/document/954095322/Kerio-Valley-Landslides-Analysis-by-Barmoiben