- Mbwa wa utambuzi wa uhifadhi wa mazingira ni mbwa waliopata mafunzo ya hali ya juu.
- Wanatumika kubaini sampuli za kibaolojia, kama vile kinyesi, manyoya au hata spishi zenyewe, na hivyo kusaidia katika ufuatiliaji wa ikolojia na juhudi za kupambana na ujangili.
- Nchini Tanzania, nyara za serikali ni sehemu ya mwili au zao la wanyamapori, hivyo ni kosa kisheria kuzmiliki au kuzibeba bila kuwa na kibali maalumu kutoka Idara ya Wanyamapori.
- Barani Afrika, mbwa hawa wanazidi kuthibitisha kuwa si tu nyenzo ya ziada, au zana ya usalama, bali ni nguzo muhimu katika vita vinavyoendelea dhidi ya ujangili.
DAR-ES-SALAAM, Tanzania – Licha ya utajiri wake, ikiwa ni pamoja na uwekezaji wa mamilioni katika uhifadhi, Tanzania inakabiliwa na ongezeko la ujangili na biashara haramu za nyara, kama ilivyofichuliwa na Operesheni Thunder 2025 ya Interpol. Ili kukabiliana na janga hilo, imekuwa muhimu kutumia silaha zaidi, nchi hiyo sasa ikijumuisha ujuzi wa askari wa uhifadhi na mbwa wenye mafunzo maalum ya kunusa nyara.
Takwimu za sensa ya hivi karibuni zinaonesha kuwa Tanzania bado ina idadi kubwa zaidi ya nyati na simba barani Afrika. Mnamo Juni, 2024, Wizara ya Maliasili na Utalii nchini iliwasilisha taarifa katika bunge ikisema kuwa Tanzania ina simba takribani 17,000, nyati 225,000 na chui 20,000.
Hata hivyo, Operesheni Thunder 2025, iliyofanywa kuanzia Septemba 15 hadi Oktoba 15, ilihusisha vyombo vya kutekeleza sheria pamoja na mamlaka za wanyamapori na misitu katika biashara haramu, ambapo maofisa wa nchi jirani ya Kenya walikamata zaidi ya kilo 400 za nyama za twiga, na wa Tanzania kupata nyama na ngozi za pundamilia na swala, zenye thamani ya takriban $10,000.
Mwanzoni mwa Februari 2026, Mongabay ilizuru Shirika la Kuru Conservation Dogs, maarufu shule ya mbwa, iliyopo nchini Tanzania, na kuona jinsi huduma mbalimbali, zikiwemo chakula na matibabu, zilipita kwenye kila chumba cha mbwa. Wahudumu waliwaita kwa majina, nao wakatulia mara moja, na kuacha kubweka, tayari kupokea huduma zao.
Mongabay ilishuhudia makumi ya vyumba ambavyo watoa huduma walipita kufanya usafi na kuwapa mbwa huduma hizo.

Muda mfupi baadaye, William Powell, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, alipotaja jina la mbwa mmoja, mnyama huyo alikimbia kutoka kwenye nyumba yake, na akachuchumaa kama ishara ya heshima. Kila mmoja aliyeitwa alipewa maelekezo tofauti na wenzake, ambayo aliyatekeleza kwa utiifu mkubwa, ikionyesha kuwa wana mafunzo ya hali ya juu na wanafuata maelekezo wanapokuwa kazini.
Sambamba na hao waliokuwa wakipatiwa huduma wakati huo, shirika liliambia Mongabay kuwa wengine zaidi ya ishirini walikuwa katika maeneo tofauti wakitekeleza majukumu yao ya kufuatilia majangili na kudhibiti biashara haramu ya wanyamapori.
“Hauhitaji askari wa uhifadhi 100 kwenye eneo dogo la uhifadhi ili kuokoa wanyamapori au nyara zake. Unachohitaji ni mbwa wa utambuzi wa uhifadhi wachache waliopewa mafunzo ya kiwango cha juu,” Powell alisema.
Mbwa wa Kuru ni wa aina yake nchini Tanzania kwa kuwa ni maalum kwa ajili ya kufuatilia nyara za wanyapori. Kwa pua zao zenye uwezo wa kunusa hata harufu hafifu zaidi ya pembe za ndovu, pembe za faru, magamba ya kakakuona, na bidhaa nyingine za wanyamapori zinazotoroshwa, mbwa hao wenye mafunzo maalum wanazidi kuwa washirika muhimu katika mapambano dhidi ya ujangili na usafirishaji haramu wa nyara za wanyamapori.
Kwa mujibu wa wakufunzi tulioongea nao, kila siku lazima wanyama hao wafanye mazoezi ili wawe kwenye kiwango cha juu cha utendaji kazi.

Kwa kawaida, mbwa wasiokuwa na mafunzo wanapoona sura ngeni za watu, huwa wanaweza kudhuru mtu. Lakini hawa wa Kuru wana mafunzo ya kumgundua mhalifu, na hufuata watu au vitu vingine pale wanapoelekezwa na wakufunzi wao.
Mbwa hawa pia wana uwezo wa kuokoa maisha ya binadamu. Kwa mfano, mwaka 2025, familia moja ilikumbwa na hofu mtoto wao alipopotea katika eneo la malisho mkoani Manyara, Kaskazini mwa Tanzania, kwa siku mbili. Katika muda huo, ndugu na wanakijiji walimtafuta mtoto huyo bila mafanikio, wakipitia vichaka na maeneo ya porini ambako mara nyingi mifugo hulishwa.
Baada ya jitihada hizo kushindikana, waliomba msaada wa timu ya mbwa waliopata mafunzo maalum ya ufuatiliaji. Mbwa mmoja aitwaye Finn aliletwa kusaidia katika zoezi hilo.
Alipofika kijijini, Finn, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka sita, alianza kazi kwa kunusa nguo za mtoto huyo ili kufahamu harufu yake. Kisha akaelekea porini. Safari ya ufuatiliaji ilimchukua umbali wa takribani kilomita nne akipitia vichaka na njia nyembamba za porini. Hatimaye, alifanikiwa kumpata mtoto huyo, anayetoka katika jamii ya wafugaji wa Kimaasai wakati wazazi na wanakijiji walikuwa wameanza kukata tamaa.

Mbwa huyu shujaa ni mmoja wa wale wanaofugwa na kupewa mafunzo na taasisi ya Kuru. Ushiriki huu katika jamii unatajwa na wadau wa uhifadhi kuwa moja ya nguzo kwa shule hii ya mbwa, kwani wanajamii wanafahamu umuhimu wa kutunza wanyamapori na kuacha vitendo vya uhalifu.
“Mara nyingi vijijini tunawaonesha ubora wa mbwa wetu, si kuwatisha. Wengi wakijitathmini wanaona kuwa wataenda kukamatwa watakapotaka kuwinda au kuua wanyama, kwani mbwa hao wanaonekana kuwa bora,” anasema Powell, ambaye wanajamii wengi humuita ‘Will Doggy’.
Taasisi hiyo inasema kuwa mbwa wake hawauzwi kibiashara, bali hutolewa kwa ajili ya kutoa huduma kwa serikali pale wanapohitaji ufuatiliaji wa nyara, na mashirika mengine ya uhifadhi.
Shirika hilo limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi katika utoaji wa huduma za mbwa katika maeneo tofauti nchini Tanzania. Pia hushirikiana na wahisani mbalimbali, na kuwa na makubaliano maalumu na serikali kupitia taasisi zake za wanyamapori kama vile TAWA, na Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania [TANAPA].

Kwa mujibu wa Interpol, ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ni sehemu kubwa ya shughuli zinazofanywa na makundi ya uhalifu. Shirika hilo linadai kuwa biashara hiyo hutengeneza hadi $20 bilioni kwa mwaka.
Taasisi ya Global Environment Facility [GEF] imesema kuwa katika ngazi za chini au kijamii, ujangili na biashara haramu ya nyara husababishwa na umaskini, rushwa, udhaifu wa utekelezaji wa sheria, na ukosefu wa utulivu wa kisiasa.
Hivi karibuni, kuwepo kwa mashirika kama Kuru kumesaidia serikali za Afrika kuimarisha uwezo wa kugundua shehena haramu za wanyamapori na kuwazuia wahalifu katika nchi muhimu zinazotumika kwa usafirishaji haramu.
Powell, ambaye pia ni mkufunzi wa mbwa katika shule hiyo, anasema ufanisi wa mbwa wa kufuatilia nyara hutokana na usimamizi na malezi yaliyo bora. “Kwa saa moja pekee, mbwa wetu mmoja anaweza kunasa mitego takribani 50.”
Mtaalamu huyo anasema mara nyingi mitego huwekwa kwa ajili ya kitoweo cha porini, na huathiri wanyama bila ubaguzi, kujeruhi au kuua tembo na hata vifaru, ambao hata ingawa idadi yao barani Afrika inaongezeka kutokana na kupungua kwa uwindaji haramu, imetishiwa kurudi chini kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na matatizo mengine.
Shule hiyo pia hutoa mafunzo maalumu ya usimamizi wa mbwa kwa askari wa hifadhi. Askari hao hutumia mbwa kama nyenzo ya kutokomeza ujangili. Mafunzo hayo yameshatolewa kwa askari mbalimbali wa hifadhi nchini Tanzania na Kenya.

Kadhalika, wataalamu kutoka mataifa mbalimbali hufunzwa jinsi ya kunasa meno ya tembo, pembe za kifaru, mifupa na meno ya simba, pamoja na magamba ya kakakuona, kwa kutumia mbwa.
Taasisi ya Working Dogs For Conservation ya nchini Marekani, ambayo pia imekuwa ikiendesha miradi ya mafunzo kwa mbwa wa utambuzi wa hifadhi, wanaeleza kuwa mbwa wa aina hiyo wameonyesha mafanikio makubwa katika kugundua wahalifu na nyara mbalimbali.
Megan Parker, mwanzilishi wa taasisi hiyo, aliiambia Mongabay: “Tunaona mabadiliko kwenye uhifadhi. Mbwa wa utambuzi wanaendelea kuthibitisha umuhimu wao mkubwa katika nyanja nyingi, kwa sababu hujengewa uwezo wa hali ya juu wa kunusa, ambao wanaweza kubaini kitu, mnyama, mmea, ugonjwa, dawa za kulevya, vilipuzi au hata kufuatilia harufu kutoka umbali mrefu sana.”
Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania ilieleza kuwa hatua za uhifadhi mbalimbali zimeleta mafanikio, huku idadi ya tembo ikiongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 60,000 mwaka 2023.
Hata hivyo, Mongabay haikupata taarifa kutoka mamlaka za Tanzania kuhusu kiwango cha mafanikio waliyoyapata kila walipotumia mbwa hao.
Uwezo wa mbwa hao
Nchini Tanzania, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama, ikiwemo kampuni binafsi za ulinzi, vimekuwa na vikosi vya mbwa wanaofuatilia wahalifu wa dawa za kulevya, silaha haratarisha kama vile mabomu, na pia wanatumika kwenye doria mbalimbali za kiusalama.
Lakini, kwa mujibu wa Powell, wanapokuwa kwenye eneo la ukaguzi kwenye mpaka wa ardhini, mbwa wa Kuru huwa na uwezo wa kufuatilia nyara kwenye magari kati ya 400 na 600 kwa siku.
“Mbwa wanapopewa mafunzo hawakai wakisubiri, muda wote hutafuta majangili au kushinikiza hao wasiwe na uhuru wa kufanya uwindaji au uchukuaji wa nyara za wanyamapori,” anasema Powell.
Hutambua zaidi kwa harufu
Mtaalamu huyu aliiambia Mongabay kuwa mbwa hao hutumika katika doria za kawaida ndani ya hifadhi. Askari wanapobaini nyayo au dalili mpya za uwepo wa binadamu, mbwa huletwa kufuatilia mwelekeo wa harufu. “Wanaweza kuonesha walipoingia, walikopita na wakati mwingine walipotokea, hivyo kusaidia timu kuelewa mienendo na kuchukua hatua mapema,” anasema.


Mbwa hao wana ufanisi mkubwa katika kubaini mitego ya waya, ambayo ni moja ya tishio kubwa kwa wanyamapori barani Afrika. Wakati waya mmoja unapogunduliwa, mara nyingi mbwa hufuata njia nzima ya aliyefunga mitego hiyo. Mbwa mmoja ana uwezo wa kufanya ufuatiliaji wa mitego kwa takribani kilomita 20 kwenye maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.
“Mbwa hao huwa wanatafuta mitego ya kunasa wanyamapori, pia majangili ambao wengi wamekuwa wakisumbua. Mbwa hao hufuata nyayo na harufu ya majangili na hivyo kuweza kuwagundua kirahisi,” anasema Powell.
Kulingana na ripoti ya watafiti wa masuala ya tiba nchini Marekani, mbwa wana uwezo wa ajabu wa kunusa, ukilinganishwa na ule wa binadamu.
Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti ya National Library of Medicine, inasema hisia ya kunusa kwa mbwa ndiyo hisia yao kuu, inayowawezesha si tu kukusanya taarifa za sasa na za zamani kuhusu mazingira yanayowazunguka, bali pia kubaini chanzo cha harufu hiyo. Uwezo huo ni muhimu katika kutafuta chakula, kugundua hatari, au kupata wenzi kwa ajili ya uzazi.
Tanzania mnufaika mkubwa wa mbwa
Kwa mujibu wa Powell, mbwa kutoka Kuru wanahudumia eneo la kilomita za mraba 30,000 kaskazini mwa Tanzania. Katika hifadhi ya Serengeti, wanalinda kilomita za mraba 14,750, na ya Mkomazi kilomita za mraba 3,245 katika mfumo wa ikolojia wa Manyara, wenye zaidi ya kilomita za mraba 8,000. Powell pia anasema mbwa hao hulinda takriban asilimia 90 ya faru nchini Tanzania.
Ulinzi katika viwanja vya ndege na mipaka ya mataifa ya Afrika
Mbali na porini au hifadhini, mbwa hao wa utambuzi hufanya kazi katika viwanja vya ndege, vizuizi vya barabarani na mipakani.
Powell anasema: “Wamefundishwa kugundua nyara, silaha na bidhaa nyingine za wanyamapori zilizofichwa kwenye magari, na mizigo, hivyo kuwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na uhalifu wa wanyamapori barani Afrika.

Wahifadhi wanasema uhifadhi hupitia changamoto nyingi, lakini kuna kila sababu ya kupambana na majangili barani Afrika. Kuru inabaki kuwa daraja la ulinzi wa nyara katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Msumbiji, Botswana na Uganda.
“Mbwa wachache waliofunzwa vizuri, wenye wahudumu imara na msaada wa kutosha, wanaweza kuwa na athari kubwa kuliko idadi yao inavyoonekana,” anasema Powell, na kuongeza kuwa katika wakati ambao wanyamapori wanakabiliwa na shinikizo kubwa, kazi ya mbwa pia ni kutoa shinikizo kwa wawindaji haramu.
Mafunzo kwa mbwa na watu wanaowasimamia
Shuleni Kuru, ustawi wa mbwa unachukuliwa kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Operesheni Thunder 2025. Wahudumu hufundishwa si tu mbinu za kazi porini, bali pia namna ya kuwatunza mbwa kila siku na kufuatilia afya na hali zao. Uhusiano wa karibu kati ya mbwa na mhudumu wake ni msingi wa mafanikio ya huduma.
Katika maeneo ya jamii, timu hizi huandaa maonyesho ya wazi wakati wa siku za soko au ziara za vijijini. Wananchi hupewa fursa ya kushuhudia mbwa wakifuatilia harufu moja kwa moja. Njia hii inalenga kujenga uelewa na kuzuia uhalifu kwa kuonesha uwezo wa mbwa, badala ya kutumia mbinu za mivutano.
Kupitia shughuli kama hizi, wanajamii huanza kuelewa kwa undani kazi ya mbwa wa ufuatiliaji na nafasi yao katika kulinda wanyamapori na kupambana na ujangili.

Loyce Ledarma, mkazi mmoja wa eneo la Ngorongoro, anasema uwepo wa mbinu hizo mpya za uhifadhi una manufaa makubwa kwa jamii. “Watu wengi wamekuwa wakisema Wamaasai ndio wanaowinda wanyamapori, lakini si kweli,” alisema, na kuongezea; “Kuna watu wenye nia mbaya ambao wamekuwa wakifanya ujangili kisha kutengeneza sifa mbaya dhidi ya Wamaasai.”
Anasema mbwa hao wanaweza kusaidia kubaini wahalifu halisi kwa urahisi zaidi na kupunguza lawama kwa jamii ya Wamaasai. “Sisi tunategemea zaidi mifugo yetu kama vile mbuzi, kondoo na ng’ombe. Kama mbwa hawa watawakamata wanaofanya ujangili, itasaidia kuondoa lawama zisizo za kweli dhidi ya jamii yetu,” alisema mumewe.
Maradhi changamoto kuu kwenye ulinzi
Moja ya changamoto inayotajwa kuwakumba mbwa hao ni magonjwa, hasa ule wa trypanosomiasis, ambao husababishwa na nzi tsetse.
“Hatujawahi kupata changamoto kubwa sana miaka sita iliyopita, lakini maradhi kwa mbwa huwapunguzia ufanisi, na sisi kwa kujua hilo, kila wiki 10 mbwa wetu hupatiwa dawa kinga mbalimbali na tunapanga siku zijazo kuwafanyia vipimo vya damu kila wiki.”
Kwa mujibu wa Kuru, mbwa mmoja anaweza kuhudumu na kufanya kazi hiyo mpaka miaka 14, kulingana na uwezo wake.
“Mbwa huanza kustaafu wakiwa na umri wa miaka nane, lakini huwa tunawanafanyia tathmini kila mara baada ya kutimiza umri huo ili kujua iwapo wana uwezo na furaha ya kuendelea kufanya kazi hiyo kwa viwango vya juu. Ikiwa wataweza basi huweza kukaa mpaka miaka 14, kisha hapo wanastaafu,” anaeleza Powell.
Taasisi hiyo inafanya kazi na wadau wahisani wa uhifadhi wakiwemo mamlaka za hifadhi za wanyamapori za mataifa mbalimbali na mpaka sasa wana makumi ya mbwa wanaoendelea kutoa huduma katika kada mbalimbali za udhibiti wa biashara haramu ya nyara za wanyamapori.
Mamlaka zatambua uwezo wa mbwa kudhibiti hali
TAWA inatambua juhudi za taasisi ya Kuru ikisema kuwa ushirikiano wao unaimarisha juhudi za kulinda wanyamapori nchini humo.
Abraham Jullu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TAWA, anasema: “Siku zote tuko tayari kupokea mafunzo zaidi kuhusu mbinu mpya na bunifu. Mbwa wa uhifadhi wameonyesha thamani kubwa kwenye itikadi zetu za kuimarisha operesheni zetu kwenye maeneo mbalimbali.”
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo inatarajia kuendeleza ushirikiano huo na kushuhudia mafanikio ya pamoja katika kulinda wanyamapori wa Tanzania.
Japokuwa Interpol hawakutaja kiwango ambacho mbwa walijumuishwa katika operesheni yao ya 2025, mamlaka kama za Tanzania zimekuwa zikieleza kuwa zimewatumia kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya operesheni zao dhidi ya majangili na wawindaji wa nyama pori.
Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania, kwa kushirikiana na GEF kupitia mradi wa shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), ilitekeleza mradi wa kupambana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.

Mradi huo ulilenga kulinda spishi muhimu kama tembo na faru, na pia kuchochea ukuaji wa uchumi wa kijani, unawezesha jamii, unaimarisha taasisi, na kutumia ubunifu katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania, mpaka Julai 2025, hali katika hifadhi za nyanda za juu Kusini inaendelea vyema.
Wizara hiyo inaeleza mandhari ya Ruaha–Rungwa yaliyopo kwenye ikolojia ya Ruaha nyanda za juu kaskazini mwa Tanzania, ujangili wa tembo ulipungua kwa kiwango cha asilimia 95.8, huku kukiripotiwa tukio moja tu la ujangili wa tembo kwa mwaka 2024.
Bila kutaja kiasi gani, wizara hiyo pia ilidai kuwa ujangili wa simba umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa nchini kwa miaka ya hivi karibuni.
Ikolojia ya Ruaha ni mfumo wa kipekee na mkubwa wa nyika nchini Tanzania [kilomita za mraba 20,226], ukiwa na kitovu cha Mto Ruaha Mkuu unaovutia wanyama wengi. Eneo hili lina sifa ya misitu ya Miombo, miti ya Commiphora na Acacia, na ni hifadhi muhimu ya tembo, mbwa mwitu, duma, na chui, huku likiwa na mazingira ya kipekee ya nyika na vilima.
TAWIRI inaongoza zoezi la sensa, ambalo lina mchango muhimu katika kupanga mikakati ya uhifadhi wa wanyamapori, kutoa taarifa kwa watunga sera, na kuimarisha usimamizi wa mifumo ya ikolojia.
Maendeleo ya sensa ya wanyamapori ya 2025/26
Mkurugenzi wa utafiti wa wanyamapori TAWIRI, Julius Keyyu, alithibitisha kuwa sensa iliyoanza Septemba 2024 inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika baadaye mwaka huu.
Amesema hadi sasa uchunguzi umekamilika katika maeneo matano kati ya kanda tisa za kiikolojia, ambazo ni Katavi–Rukwa, Ruaha–Rungwa, Nyerere–Selous–Mikumi, West Kilimanjaro–Lake Natron, na Mkomazi. Maeneo hayo yanawakilisha takribani asilimia 65 ya kazi yote ya sensa.
Sensa hiyo inategemea zaidi uchunguzi wa angani, ambapo wataalamu huhesabu wanyamapori kwa kutumia ndege ili kupata takwimu sahihi zaidi. Hadi sasa $1.04 milioni (TSh2.7 bilioni) imetumika katika utekelezaji wa mradi huo.

Mwaka 2024, wakati matokeo ya sensa ya 2022 katika mfumo ikolojia wa Nyerere-Selous-Mikumi yakitangazwa, mamlaka ilidai kuimarika kwa spishi 22 za wanyamapori, wakiwemo nyati 59,878, tembo 20,006, nyumbu 19,060, kongoni 18,361, swalapala 14,031, na ngiri 13,806.
“Katika sensa hii kulikuwa na tembo 20,006 (2022) ikilinganishwa na sensa ya 2018 iliyohesabu 15,501. Viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 16 mwaka 2018 hadi asilimia 0.8 mwaka 2022,″ alieleza Waziri Angela Kairuki, ambaye pia hakutaja moja kwa moja kuhusika kwa mbwa katika kukabiliana na ujangili.
Juhudi za Mongabay kubaini mchango kamili wa mbwa katika jitihada hizo nchini Tanzania hazikufua dafu.
Nchini Kenya, hadi kufikia katikati ya 1980, idadi ya faru ilikuwa imeshuka hadi 400 kutokana na ujangili. Kwa mujibu wa Shirika la Huduma za Wanyamapori, kikosi cha kupambana na ujangili cha Loisaba kinachojumuisha walinzi wa usalama, pamoja na kitengo cha K9 chenye mbwa waliopatiwa mafunzo maalum ya ufuatiliaji, kilisaidia kuzuia uwindaji wa faru ambao mpaka mwaka 2025 idadi yao iliongezeka hadi kufikia zaidi ya 1,000.
Mkazo kwa spishi muhimu za wanyamapori
Mtafiti mkuu wa TAWIRI, Hamza Kija, alisema lengo la kupata takwimu sahihi za idadi ya wanyama hao itasaidia katika utungaji wa sera na kuboresha mifumo ya ikolojia wanamoishi, kuhakikisha wanaendelea kuwepo kwa manufaa ya sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kadri Tanzania inavyoendelea kuimarisha juhudi zake za uhifadhi, sensa ya wanyamapori ya 2025/26 inatarajiwa kutoa taarifa muhimu kuhusu mwenendo wa idadi ya wanyama, hali ya makazi yao, pamoja na changamoto zinazoweza kutishia bioanuwai.

Aidha, biashara haramu ya wanyamapori inavyoendelea kubadilika, ndivyo mbinu za kukabiliana nayo zinavyobadilika pia. Ni dhahiri kwamba matumizi ya mbwa wa kunusa nyara yamekuwa yakiongezeka si Tanzania pekee, bali pia katika nchi nyingine barani Afrika, zikiwemo Kenya, Botswana, Msumbiji na Uganda.
Mbinu hii sasa inachukuliwa kuwa sehemu muhimu ya mikakati ya kisasa ya uhifadhi, ikiunganisha teknolojia, utaalamu wa binadamu na uwezo wa kipekee wa wanyama. Hii ni kwasababu ujangili ni tishio kwa mataifa mengi, ilivyodhihirishwa na operesheni ya Interpol, ambayo ilihusisha mataifa 134 katika kipindi hicho, na kukamata zaidi ya washukiwa 1,000 waliohusika katika biashara haramu ya wanyamapori.
Kwa Tanzania, na bara la Afrika kwa ujumla, mbwa hawa wanazidi kuthibitisha kuwa si tu nyenzo ya ziada, au zana ya usalama, bali ni nguzo muhimu katika vita vinavyoendelea dhidi ya ujangili, na alama ya mwelekeo mpya wa uhifadhi unaochanganya sayansi, jamii na ubunifu.
Picha ya bango: Askari wa usalama hifadhini kaskazini mwa Tanzania wakimtazama afisa wa kikosi cha mbwa nusa akicheza kwa furaha na moja ya mbwa baada ya kuhitimisha shughuli za ufuatiliaji wa rasilimali za wayamapori. Picha na Shirika la Kuru.