- Ujenzi wa mabwawa madogo na mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua vipewe kipaumbele.
- Mipango ya maji iunganishwe moja kwa moja na tathmini za hatari za mabadiliko ya tabianchi.
- Sheria ya Mita 60 isisitizwe kudhbiti uchafuzi wa maji, kulinda mifumo ikolojia ya mito, maziwa na mabwawa.
- Miundombinu ya maji isasishwe, ubadilishwe na kuweka ile inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Ni usiku mkubwa wa saa nane, Mama Amina ananyakuka kitandani taratibu na kuelekea uani ambako anafungua bomba kuona kama maji yanatoka. Anaambulia patupu na kurudi tena kitandani. Anazinduka tena baada ya saa moja na kukuta hali ni ile ile. Hadi asubuhi, bomba halitatoa hata tone moja ya maji.
Alfajiri pikipiki zilizobeba madumu ya njano ya plastiki yenye maji, zinapishana mtaani. Wanawake, akiwemo Mama Amina, wanazikimbilia kununua maji ambayo yanauzwa kuanzia TSh500 hadi TSh1,000 kwa dumu lenye ujazo wa lita 20. Mama Amina ni miongoni mwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, lenye wakazi karibu 7,000,000, ambao mara kwa mara hukabiliwa na uhaba wa maji.
Wakati viongozi wa Serikali ya Tanzania wanahaha kutembelea vyanzo vikuu vya maji vinavyohudumia Jiji la Dar es Salaam kujionea wenyewe namna vilivyokauka, watalaam wa masuala ya maji wanasema ukame huo ambao kwa kiasi kikubwa unachochewa na mabadiliko ya tabianchi, unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu iwapo ushauri wa kitalaam utafuatwa.
Jiji la Dar es salaam ndilo lenye wakazi wengi zaidi nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, mkoa huo ulikuwa na watu 5,380,000, ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza uliokuwa na watu 3,690,000.
Kuanzia Novemba hadi Desemba mwaka 2025, Jiji la Dar es Slaam limekumbwa na uhaba mkubwa wa maji uliosababishwa na kupungua kwa kina cha maji cha Mto Ruvu – chanzo kikuu cha maji ya jiji hilo. Hali hiyo ilisababisha watu wenye visiwa kuuza maji kwa bei ya hadi TSh1,000 (takriban $0.5) kwa dumu la lita 20.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) iliripoti kuwa uzalishaji wa maji katika mtambo wa Ruvu Chini ulipungua kutoka lita 270,000,000 kwa siku hadi lita 50,000,000 kutokana na kupungua kwa kina cha maji katika Mto Ruvu kulikosababishwa na ukame.
Katika hali ya kawaida, Jiji la Dar es Salaam huhitaji wastani wa lita 500,000,000 za maji kwa siku.
Msimu wa mwaka 2025, katika maeneo ya Pwani na Morogoro, mvua zilipungua kwa asilimia 30 hadi 50 ya wastani wa kawaida.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Morogoro hupata wastani wa maji kuanzia 300-600mm kwa msimu wa masika wakati Pwani hupata mvua kiasi cha 400-800mm kwa msimu wa masika.
Mto Ruvu, ambao hupata maji yake kwa kiasi kikubwa kutoka maeneo ya Pwani ya Tanzania na safu za Milima ya Uluguru, ndio chanzo kikubwa zaidi cha maji katika miji ya Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo, miji ambayo ni kitovu cha uchumi wa viwanda Tanzania.
Miongoni mwa suluhisho lililochukuliwa na serikali ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro. Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkama Bwire, mradi huo unaogharimu takribani TSh335.8 bilioni, utakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 190 za maji kwa ajili ya Dar es Salaam na Pwani.
Bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kusambaza maji takriban lita bilioni 20 kwa siku katika miji ya Dar es Salaam, maeneo ya Pwani na mji wa Morogoro.
Eneo moja wanalia ukame, lingine wanalia mafuriko
Wakati Jijini Dar es Salaam watu wakilia ukame, mwezi mmoja baadaye, macho ya taifa yalielekezwa Kilosa mkoani Morogoro, ambako mvua kubwa zilisababisha mafuriko makubwa yaliyoharibu nyumba, miundombinu na kuathiri shughuli za kiuchumi, hasa kilimo na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Mafuriko ya Kilosa yalitokana na mvua kubwa na ya muda mrefu iliyonyesha mwishoni mwa mwaka 2025, ambayo ilisababisha mito kujaa na maji kuingia kwenye makazi ya watu.
TMA ilisema mvua hizo zilisababishwa na kuimarika kwa mifumo ya mvua za msimu kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambapo kulikuwa na ongezeko la mvua juu ya wastani wa muda mrefu katika maeneo ya Mashariki na kati ya Tanzania. Mvua hizo zilichangiwa na mifumo ya shinikizo la chini la mkondo wa upepo kutoka Bahari ya Hindi iliyosababisha ongezeko la unyevunyevu.
Katika taarifa yake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, alisema zaidi ya nyumba 120 za makazi ziliharibiwa na mvua ulioambatana na upepo mkali, huku kaya zaidi ya 400 zikiathiriwa kwa viwango tofauti.
Mali kama vile mifugo, mashamba na vyombo vya nyumbani viliharibiwa ama kusombwa na maji wakati barabara katika vijiji vya Dumila na Mgaole A na Magole B katika Kata ya Magole, vijiji vya Mamboya, Mabwerebwere, Magomeni na Mkwatani katika Kata ya Kilosa na katika vijiji vya Kidete na Godegode, pia miundombinu ya reli na umeme viliharibiwa na kusimamisha kwa muda usafiri wa treni ya Reli ya Kati kutoka Pwani kwenda mikoa ya Tanzania Bara.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, alisema serikali imeidhinisha miradi ya ujenzi wa bwawa la Kidete pamoja na mabwawa mengine katika Wilaya ya Kilosa ili kuchepusha maji na kudhibiti mafuriko, hasa katika maeneo yanayokumbwa mara kwa mara na maji ya mvua.
Serikali ilipanga kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji katika eneo la Kidete kama suluhisho la kudumu la mafuriko na kujenga kingo za mito na mifereji ya maji kuzuia mafuriko yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi.

Ingawa hakuna takwimu za kiasi cha mvua kilichosababisha mafuriko wilayani Kilosa, madhara ya mvua kubwa kupita makadirio yangeweza kuepukwa kama kungekuwa na miundombinu ya kukinga maji yasiende kwenye makazi ya watu na mindumboni, na badala yake kuvunwa na kuhifadhiwa kwa matumizi ya kilimo, mifugo na majumbani nyakati za ukame.
Kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi: Wataalam wanasema nini
Katika mahojiano na Mongabay yaliyofanyika kwa nyakati tofauti, watalaam wa masuala ya maji walisema athari hizo za ukame na mafuriko, vinaweza kukomeshwa iwapo Serikali itazingatia ushauri wa watalaam.
Ofisa Maabara ya Uoteshaji Tishu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (ZAHILI), Yusuf Abdulrahim Yusuf, anahusisha uhaba wa maji na ubunifu wa miundombinu ya maji usiozingatia hali ya tabianchi ya sasa.
“Ingawa Tanzania ina sera na mipango ya sekta ya maji, changamoto kubwa imekuwa ni kutozingatia hatari zinazochochewa na mabadiliko ya tabianchi katika upangaji na utekelezaji. Mara nyingi, miundombinu ya maji hubuniwa kwa kuzingatia hali ya hewa ya zamani, bila kutathmini kwa kina mabadiliko ya baadaye,” anasema.
Mtaalam huyo anashauri kuwa mipango ya maji iunganishwe moja kwa moja na tathmini za hatari za mabadiliko ya tabianchi, ikijumuisha matumizi ya takwimu za kisayansi, ramani za hatari na mipango ya dharura.
“Changamoto za maji haziwezi kutatuliwa bila usimamizi thabiti na mifumo bora ya ufadhili. Ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha uwekezaji wa muda mrefu. Bajeti za maji zinapaswa kuzingatia gharama za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, badala ya uendeshaji wa kawaida pekee, anasisitiza.
Anatoa wito wa kuwepo kwa miundombinu ya maji inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo linahitaji ubunifu unaojali mazingira na gharama za uendeshaji.
Anataja ulinzi wa vyanzo vya maji asilia kama misitu ya vyanzo vya maji, ujenzi wa mabwawa madogo na mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua, matumizi ya teknolojia zisizohitaji gharama kubwa za nishati na matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu iliyopo, kama mambo yanayotakiwa kupewa kipaumbele.
Kwa mujibu wa Yusuf, athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame na mafuriko haviikumbi Tanzania pekee bali ni suala linalozisumbua hata nchi Jirani na kwamba kuwa na miundombinu ya maji inayozingatia mabadiliko ya tabianchi, ni muhimu sana.
Frederick Mulinda, Mratibu wa Miradi ya Mabadiliko ya Tabianchi wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), anahusisha uhaba wa maji na ukame wa muda mrefu pamoja na ongezeko la joto vinavyochochewa na mabadiliko ya tabianchi.
Anapoulizwa ni jinsi gani mipango ya sasa ya maji inavyoweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mulinda anasema kwa sasa hilo limeanza kuzingatiwa hasa kupitia Sera za Sekta ya Maji na Mipango ya Kitaifa ya Tabianchi.
Hata hivyo, anasema, bado kuna mapungufu katika utekelezaji, utafiti wa hatari za tabianchi kwa vyanzo vya maji, na ujumuishaji wa data za hali ya hewa katika upangaji.
Anasema maboresho yanahitajika katika kufanya tathmini za hatari zatabianchi katika mchakato mzima wa tathmini ya Athari kwa Mazingira kabla ya kufanya uwekezaji kwenye sekta ya maji, kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema, na kujenga uwezo wa taasisi za maji katika kupanga kwa kuzingatia tabianchi.
Mulinda, katika mapendekezo ya nini kifanyike, anasema miundombinu ya maji inapaswa kubuniwa kwa kutumia dhana ya climate-resilient infrastructure. “Hii ni pamoja na kubuni miundombinu inayoweza kuhimili mafuriko na vipindi vya ukame, kutumia teknolojia zinazookoa maji na nishati, na kuchanganya miundombinu ya kijivu (kama mabwawa) na miundombinu ya kijani (kama uhifadhi wa maeneo oevu na misitu ya vyanzo vya maji).
Aidha anasema matumizi ya nishati jadidifu katika mifumo ya maji yanaweza kupunguza gharama za uendeshaji.
Uhifadhi na urejeshwaji wa mazingira ya vyanzo vya maji
Kuhusu mikakati gani ya muda mrefu inayohitajika kukabiliana na ukosefu wa maji unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi, mtaalam huyo anapendekeza uhifadhi na urejeshaji wa mazingira ya vyanzo vya maji (misitu, mabonde ya mito na maeneo oevu) kuimarisha sera, sheria na uongozi wa rasilimali za maji pamoja na uwekezaji katika miundombinu na teknolojia bunifu za maji.
Aidha, anasema kujenga uelewa na uwezo wa jamii kuhusu masuala yanayohusiana na uhifadhi wa maji, ni jambo lingine linalopaswa kufanyika.
“Ni muhimu kutambua kuwa changamoto ya maji na tabianchi si ya sekta moja. Inahitaji ushirikiano wa sekta zote, kuanzia mipango miji, afya, nishati hadi mazingira. Pia, usawa wa kijinsia na makundi yaliyo hatarini unapaswa kuzingatiwa katika suluhisho za maji,” anasema.
Anasisitiza pia matumizi ya nishati jadidifu katika mifumo ya maji ili kupunguza gharama za uendeshaji, pamoja na kuimarisha Usimamizi Jumuishi wa Rasilimali za Maji – Intergrated Water Resource Management of (IWRM), uratibu kati ya taasisi, ushiriki wa jamii na mifumo ya ufuatiliaji wa ubora na wingi wa maji.
Kwa mujibu wa Mulinda, mambo mengine muhimu ili kukabiliana na uhaba wa maji unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi ni kuunganisha vipaumbele vya tabianchi na maji katika bajeti za Serikali, kuimarisha upatikanaji wa fedha za tabianchi pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa ubia na sekta ya umma na binafsi (PPP).
Naye Nyendo Kinyonga, mtaalam wa Mabadiliko ya Tabianchi, Uchumi Endelevu, Elimu na Utetezi wa Sera za Jinsia, anasema nchini Tanzania asilimia kubwa ya maji yanatokana na mvua, hivyo mabadiliko ya joto na mifumo ya mvua yana athari kubwa kwa upatikanaji wa maji.
Akitolea mfano wa Dar es Salaam, Nyendo anasema jiji hilo hutegemea vyanzo vya maji kama Milima ya Uluguru ambayo ni chanzo kikuu cha Mto Ruvu unaotegemewa kwa ajili ya maji jijini Dar es Salaam na Pwani.
Lakini pia hukabiliwa na hatari kubwa za mabadiliko ya tabianchi kama kuongezeka kwa joto kunakochochea kukauka kwa vyanzo vya maji kutokana na uvukizo, huku mvua zisizotabirika na za kiasi kidogo zikipunguza kiwango cha maji.
Nyendo pia anakosoa miundombinu ya maji mijini kutosasishwa kwenye mipango ya muda mrefu ya miundombinu ya maji. Anasema majiji yanakua lakini sehemu kubwa ya miundombinu inayotumika ni ile ile ya zamani.
“Katika mji wa Morogoro, tangu utoto wangu, mfumo wa maji ni ule ule wa zamani, hivyo inaleta ugumu kwa watu wanaoishi nje ya mji kupata maji, kwani miundombinu haiwezi kutosha ikilinganishwa na ukuaji wa mji,” anasema.
Uvunaji wa maji ya mvua
Anashauri uwepo wa mikakati madhubuti zaidi ya kuhifadhi maji ya mvua ili kuziba pengo la upungufu wa maji. “Watu nchini Tanzania wanapata mvua nyingi ambazo wakati mwingine zinasababisha mafuriko. Ni muda muafaka sasa wa kuangalia ni njia gani zitumike kuvuna hayo maji. Inatakiwa kuwepo na uwekezaji wa kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi mbalimbali,” anasisitiza.

Mtaalam wa Rasilimali za Maji jijini Dar es Salaam, Onesmo Zakaria, anapendekeza hatua kuu mbili: Kwanza, kuongeza uwekezaji katika ulinzi wa vyanzo vya maji, ikiwemo usimamizi makini wa utekelezaji wa ‘Sheria ya Mita 60’ kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, 2004 (Sura 191), shughuli za kibinadamu ambazo ni za kudumu haziruhusiwi kufanyika ndani ya umbali wa mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji kama vile bahari, mito, maziwa, mabwawa na maeneo oevu.
Lengo la ‘Sheria ya Mita 60’ ni kuzuia uchafuzi wa maji, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kulinda mifumo ikolojia ya mito, maziwa na mabwawa, na kuhakikisha maji ya mazingira yanaendelea kuwepo.
“Sheria ya Mita 60 hutumika katika nchi mbalimbali kulingana na mazingira kwa hiyo ushauri huu hauihusu Tanzania peke yake bali nchi nyingine zenye changamoto kama zetu,” anasema.
Licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, Waziri mwenye dhamana na mazingira anaweza kutunga kanuni zinazoainisha shughuli zinazoruhusiwa kulingana na mazingira ya eneo husika.
Kwa mujibu wa Zakaria, kuepuka shughuli za binadamu karibu na vyanzo vya maji kutasaidia mito kama Ruvu kuokoa kiwango kikubwa cha upotevu wa maji na kupunguza kushuka kwa kina cha maji.
Shughuli za kibinadamu zinazotakazwa na Sheria ya Mita 60 ni kama vile kilimo, hasa cha umwagiliaji, ambacho kinaweza kutumia kiasi kikubwa cha maji kutoka katika chanzo cha maji. Pia shughuli kama ujenzi, pamoja na mambo mengine yanayoweza kusababisha mmonyonyoko wa udongo.
Kwa mujibu wa Zakaria, hatua ya pili ni kuimarisha uhifadhi wa maji kupitia ujenzi wa mabwawa zaidi, hasa katika maeneo yenye matumizi makubwa ya maji kama Dar es Salaam.
“Pamoja na mpango wa kujenga Bwawa la Kidunda, kuna uwezekano wa kujenga bwawa la kukinga maji ya Mto Ruvu na kuvuna maji ya mvua yatakayoweza kuhifadhiwa na baadaye kutibiwa na kusambazwa kwenye gridi ya maji,” anasema.
Anasisitiza pia kujenga uwezo wa taasisi za watumiaji wa maji kupitia mifumo ya Malipo kwa Huduma za Mazingira (PES), na Malipo Stahiki kwa Huduma za Bonde la Maji (EPWS) ili kuongezwa ukwasi katika sekta ya maji.
Sera, tabia za matumizi ya maji na upotevu wa maji
Almas Mazigo, mtaalam wa Maadili ya Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), anasisitiza umuhimu wa sera madhubuti za matumizi ya maji na udhibiti mkubwa wa matumizi ya maji. Anasema uwepo kwa sheria ndogo ndogo za utunzaji wa maji na mikakati ya kusimamia matumizi endelevu, vitasaidia kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.
Anatoa mfano wa Jiji la Cape Town, Afrika Kusini, ambapo anasema udhibiti mkali wa matumizi ya maji uliwekwa baada ya uhaba mkubwa ambapo watumiaji maji walijengewa uelewa na kusimamiwa kuepuka matumizi holela, na hivyo kupunguza upungufu wa maji.
“Maji mengi hupotea kutokana na miundombinu dhaifu. Kati ya asilimia 38 hadi 49 ya maji yanayosambazwa na DAWASA hupotea kabla ya kumfikia mtumiaji, na hivyo kuongeza pengo lililopo kati ya maji yanayozalishwa kwa ajili ya matumizi na maji yanayomfikia mteja wa mwisho,” anasema Mazigo.
Aidha, anasisitiza ulinzi wa vyanzo vya maji dhidi ya uchafuzi, akitolea mfano wa Ziwa Victoria ambalo alisema kwa sasa maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu bila kutibiwa kutokana na kuchafuliwa kunakochangiwa na shughuli za kibinadamu kando ya ziwa.
Kwa mujibu wa wataalam waliohojiwa, ushauri wao hauihusu Tanzania peke yake kwaniba unaweza kusaidia nchi nyingi zinazokabiliwa na changamoto zinazochochewa na mabadiliko ya tabianchi kama ukame na mafuriko.
Kwa ujumla, wataalam hao wanasisitiza umuhimu wa uhifadhi wa misitu, maeneo oevu na vyanzo vya maji na kuwa na miundomboni inayostahimili mabadiliko ya tabianchi kama nguzo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Picha ya Bango: Sehemu ya mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini. Picha na John Bukuku.