- Kutoweka kwa kakakuona Tanzania kunatishia mustakabali wake duniani.
- Mwingiliano wa watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, unawapa upenyo majangili hupenyeza.
- Uhaba wa raslimali unakwamisha juhudi za kuelimisha watu vijijini kuhusu kakakuona.
- Kushirikisha wenyeji kwenye ulinzi kutawezesha kutumia maarifa ya jadi na ya kisayansi kwenye ulinzi.
Bweni la wavulana wa shule moja ya sekondari iliyoko karibu na hifadhi ya Misitu ya Minziro Mkoani Kagera, Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania, limezungukwa na miti na vichaka vikubwa. Jioni moja, wakati wanafunzi wameketi nje wakiongea, mara wanaona majani yakitikisika, na taratibu mnyama mdogo kwa umbo mwenye magamba anachomoza.
“Ni kakakuona!” Wote wanalipuka kwa furaha. Furaha yao imebeba mengi, lakini kubwa ni kwamba wana uhakika wa kujipatia pesa nyingi kwa kumuuza mnyama huyu kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani.
Wanafunzi wanamchukua na kumficha bwenini ili kuwasiliana na wateja huku wakimlisha viporo vya wali na ugali. Wanahaha hadi siku ya tatu bila kupata mnunuzi. Kwa hofu ya kukamatwa, wanamsalimisha kwa mwalimu ambaye anawapigia simu maofisa wa Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wanaofika shuleni hapo na kumchukua.
Katika eneo lingine, mwanamume mmoja, akiwa anatokea shambani muda wa jioni, alikutana na kakakuona. Kwa matumaini kwamba akimuuza atapata pesa, alimkamata, kumtia kwenye kiroba na kwenda naye hadi nyumbani kwake ambako alimficha ndani, huku akitafuta wateja. Hata hivyo kutokana na kukosa huduma, mnyama huyo alifia humo ndani.
Kakakuona mwingine alionekana akiwa amekatwa mkia na watu wasiojulikana. Alikufa jioni ya siku hiyo.
Hayo ni matukio ya kweli yaliyofanyika huko mkoani Kagera, karibu na mpaka wa Uganda, kwa nyakati tofauti, kama yalivyosimuliwa na Geofrey Kapinga, Mjumbe wa Kamati ya Mazingira ya kijiji cha Minziro, Wilaya ya Misenyi, Kagera.

Huko mkoani Iringa, Meshack Sanya, Mwenyekiti wa kijiji cha Mafuluto, Wilaya ya Iringa Vijijini, anasema Novemba mwaka 2024, kakakuona alionekana, jamii za makabila tofauti zinazoishi mkoani humo, huku zikipokezana, zilimzungusha kutoka jamii moja hadi nyingine, huku zikifanya mambo yao ya kimila. Wakati maofisa wa wanyamapori walipopata taarifa, mnyama huyo alikuwa anatembea kwa kuchechemea kutokana na uchovu. Kwa bahati alipatiwa huduma ya kwanza na akapona.
Simulizi za Kapinga na Sanya kutoka mikoa ya Kagera na Iringa ni baadhi tu ya mambo yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, na kutishia uhai wa mnyama huyo. Chanzo kikubwa cha matendo hayo ni uelewa mdogo miongoni mwa wanajamii pamoja na mitazamo potofu kuhusu kakakuona.
Vitisho dhidi ya kakakuona vinaathiri mustakabali
Vitisho dhidi ya kakakuona nchini Tanzania vinaathiri mustakabali wa wanyama hao duniani kote, kwani barani Afrika, Tanzania ndio nchi pekee yenye angalau spishi nyingi.
Victor Kakengi, Kaimu Afisa Utafiti Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), taasisi ya serikali inayosimamia na kuratibu utafiti wa wanyamapori nchini, anasema wanyama hao ni adimu sana, na kwamba ulimwenguni kote kuna aina nane tu za spishi za kakakuona. Kati ya hizo, nne zinapatikana katika bara la Asia na nne katika bara la Afrika. Aidha, katika hizo nne za Afrika, tatu zinapatikana Tanzania.
Spishi zinazopatikana Tanzania ni Temminck’s ground pangolin (Smutsia temminckii), White-bellied pangolins (Phataginus tricuspis), na Giant pangolins (Smutsia gigantea). Temminck wanapatikana katika maeneo mbalimbali nchini yenye mifumo ya savana na misitu ya wazi kama mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Tabora, Katawi, Rukwa, Ruvuma, Lindi na Mtwara, pamoja na ndani ya maeneo ya hifadhi kama Serengeti, Ruaha na Nyerere ambako mazingira yake yanamruhusu kupata makazi, uzazi na chakula cha kutosha.
Kakakuona wa aina hii ni yule ambaye huwa anaonekana mara kwa mara, hukaa kwenye mashimo, vichaka, miti iliyoanguka, mapango na hupendelea maeneo yasiyo na mvua nyingi.
White-bellied pangolin na Giant ground pangolin wote wanapatikana zaidi katika misitu ya Kagera na Kigoma.
Kakengi anasema: “Tanzania ndiyo yenye spishi nyingi ukilinganishwa na nchi nyingine za Afrika. Ndiyo maana tunasema kwamba mustakabali wa hawa wanyama duniani uko mikononi mwetu. Tunatakiwa kuwalinda kwa nguvu zote ili waendelee kuzaliana na kuongezeka.”
Nguvu ya kakakuona kimazingira, kiuchumi na kijamii
Kwa mujibu wa Kakengi, kakakuona ana umuhimu sana kwenye mfumo wa ikolojia, ambapo kupitia tabia yake ya kula mchwa na siafu, hudhibiti wadudu hao wanaoleta madhara na hivyo kusaidia kulinda uoto wa asili, kuboresha afya ya udongo na kusaidia kuwepo kwa uwiano wa ikolojia na mnyororo wa ulaji katika mazingira.
Michael Kimaro, Mkurugenzi wa Tanzania Research and Conservation Organization (TRCO), anasema: “Bila kudhibitiwa, mchwa na siafu wangekuwa wengi sana, kiasi cha kuleta madhara makubwa. Lakini uwepo wa kakakuona unasaidia sana kuwapunguza. Fikiria kakakuona mmoja aliyefikia umri wa uzazi anakula wadudu 200,000 kwa siku, au 70,000,000 kwa mwaka mmoja, ni wadudu wengi sana wanaliwa.”
Kimaro anafafanua kuwa kwa vile wanyama hao hutumia kucha kuvunja vichuguu na kufanya udongo uwe laini, huruhusu hewa ya oksijeni kwenda chini kwenye udongo na kusaidia kuhifadhi baadhi ya virutubisho na kuufanya uwe katika hali nzuri ya kuweza kustawisha mazao.
Kiuchumi, Kakengi anasema, kuwepo kwa kakakuona kunaongeza bionuai ya wanyama nchini, kitu ambacho ni muhimu kwa maendeleo ya utalii na uchumi kwa ujumla.
“Tanzania ni nchi yenye utalii wa kila aina, na kuwa na wanyama wa kipekee kama kakakuona ni kivutio kikubwa. Watu wengine hawamfahamu vizuri mnyama huyo kutokana na asili yake ya kuonekana kwa nadra sana,” anasema.
Kwa mujibu wa Kakengi, kijamii, kakakuona anahusishwa na faida nyingi ambazo zinatofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. “Kwenye baadhi ya jamii mnyama huyo anahusishwa na bahati, kielelezo cha heshima, utajiri na fahari, utabiri wa mambo yatakayotokea kama njaa, shibe, mvua, vita, huku wengine wakimtumia kama chakula, mapambo kwa kutumia magamba yake, dawa, hasa kwa waganga wa kienyeji, pamoja na kuongeza mvuto, hasa kwa wanasiasa na watu wanaotaka kuboresha mahusiano yao.
Kukosa uelewa ni mwiba kwa uhai wa kakakuona
Licha ya kakakuona kuwa mnyama adimu mwenye faida zake, wako hatarini kutoweka kutokana na sababu mbalimbali.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Ecology and Evolution mwaka 2025, unaonyesha kuwa kakakuona ni mnyama anayesafirishwa zaidi duniani kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa Kakengi, spishi zote nane zinazopatikana duniani zimeainishwa kwenye kwenye orodha nyekundu ya International Union for Conservation of Nature (IUCN) kuwa ni spishi zilizo katika hatari ya kutoweka. Kwa maana hiyo hakuna spishi ya kakakuona iliyo salama; zote zinakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na vitisho mbalimbali.
Alisema tishio la kwanza ni usafirishaji wake haramu, akipelekwa katika nchi mbalimbali, zikiwemo za bara la Asia akiwa hai, amekufa ama sehemu zake za mwili. Alifafanua kuwa huko anakopelekwa mnyama huyo hutumiwa kwa mambo tofauti tofauti.
Baadhi ya watu hutumia magamba yake kama dawa na mapambo na kucha zake kama hirizi na kinga. Baadhi humla kama kitoweo na wengine humtumia kwenye mambo ya tiba asilia na masuala yanayohusiana na imani na mila.
“Vitisho vingi vinavyomkabili kakakuona, kwa njia moja ama nyingine, vinachochewa na uelewa mdogo wa jamii. Kwa mfano, watu wanaosafirisha mnyama huyo kiharamu wanampata kwa sababu wanapewa ushirikiano na wenyeji wa maeneo anakopatikana, na wengi wanafanya hivyo kwa sababu hawafahamu umuhimu wake,” anasema Hillary Mrosso, mtafiti kutoka TRCO.
Isaack Chamba, Afisa Mhifadhi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), taasisi ya Serikali inayohusika na utekelezaji wa sheria na usimamizi wa raslimali za wanyamapori, anasema Tanzania inahusika kwa namna mbili katika usafirishaji wa kakakuona.

Katika namna ya kwanza, wanyama hupitishiwa nchini Tanzania kupelekwa nchi nyingine. Kesi za ukamataji wa nyara zinazotokea bandarini, uwanja wa ndege au kwenye mipaka, zinadhihirisha kwamba wanyama hao wanaingizwa ndani ya nchi ama wanapita. Pia Tanzania inahusika kama nchi ambayo ujangili unafanyika na wanyama hukamatwa nchini na kuuzwa kwa watu wanaowasafirisha kiharamu.
Chamba anafafanua kuwa wanaonunua wanyama hao kutoka kwa wenyeji ni wafanyabiashara wanaotokea mijini au nchi jirani, ambao huwatumia wenyeji ili kufanikisha malengo yao na kwa vile wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa wanyama hao, hukubali na kushiriki katika biashara hiyo haramu.
Kuna taarifa kwamba kakakuona wanauzwa kwa bei kubwa sana. Kwenye maeneo ya mipakani anaweza kuuzwa kuanzia TSh5,000,000 au ($2,000), huku katika maeneo ya katikati ya nchi bei ikiwa pungufu.
“Kutokana na uelewa mdogo, watu wanaposhawishiwa kwa pesa hukubali na kutoa ushirikiano,” anasema Chamba.
Tishio lingine dhidi ya kakakuona linalochochewa na uelewa mdogo ni ujangili. Geofrey Kapinga, Mjumbe wa Kamati ya Mazingira ya kijiji cha Minziro, Wilaya ya Misenyi, Kagera, anasema katika maeneo yao kuna makundi ya watu wanaojishughulisha na uwindaji haramu ambao maisha yao ni msituni na wanakuwa na taarifa nyingi muhimu kuhusu wanyama hao.
“Ukiwaambia wakutafutie kakakuona kwa fedha nzuri, siku haiishi kabla hawajamleta. Hao jamaa ni hatari sana kwa sababu wako tayari kuwauza ilimradi wapewe fedha nzuri,” anasema Kapinga na kisha kuongeza: “Ili vita hii tuishinde lazima waelimishwe ili wafahamu kwamba hakuna kiasi chochote cha fedha kinacholingana na thamani ya mnyama huyo, ambaye ni urithi wa vizazi vijavyo.”
Kwa mujibu wa Kapinga, tishio lingine ni kitendo cha watu kuendeleza imani na mitazamo ambayo baadhi ni potofu.
Mahojiano na watu mbalimbali yamebaini kuwa mnyama huyo hutumiwa na watu kwa mambo tofauti. Wapo wanaoamini kuwa viungo vya mnyama huyo kama magamba huleta bahati au mafanikio, hutibu maradhi mbalimbali au kuondoa mikosi, na ni kinga dhidi ya majanga.
Kwa wengine, kakakuona ni mtabiri wa mambo yajayo. Waganga wa jadi nao hutumia viungo vyake kwenye madawa yao na matambiko. Wanasiasa wanahusisha mnyama huyo na mvuto wa kisiasa. Kuna jamii nyingine, kutokana na imani zao, wakimuona mnyama huyo, wanamzika akiwa hai.
Wengine humlisha kakakuona unga na tikitimaji
Tishio lingine ni kitendo cha watu wanapomkamata mnyama huyo kumbeba na kwenda kumficha kwenye nyumba zao huku wakimlisha vyakula vinavyoliwa na binadamu.

“Kutokana na asili na tabia ya mnyama huyo, huonekana mida ya jioni kuanzia kwenye saa 11, wakati watu wanatoka kwenye shughuli zao. Hivyo, kukutana na watu ni rahisi na kwa vile hawana uelewa; wanapokutana naye tu, humbeba na kwenda naye majumbani mwao kwa nia ya kumtumia kwenye mambo yao binafsi. Wakiwa naye, wengine humlisha unga na tikitimaji, kitu ambacho kinamletea shida kwenye utumbo na baadaye kumdhuru,” anasema Kimaro.
Anasema kupona kwa mnyama aliyepitia mazingira kama hayo kutategemea ni muda gani walimficha ndani na mhifadhi alifika muda gani baada ya kupewa taarifa. Anasema katika baadhi ya kesi, mnyama anaokolewa lakini akiwa tayari ameathirika.
Kutokana na kuongezeka kwa mwingiliano wa watu kutoka mataifa mbalimbali, wananchi wanajikuta wakiingiliana na makundi tofauti, baadhi yakiwa na nia ovu.
Kwa mujibu wa Chamba, “Kadri siku zinavyosonga mbele, mwingiliano wa watu kutoka sehemu mbalimbali duniani unazidi kuwa mkubwa. Watu wanaingia nchini na kutoka, na huwezi kujua malengo yao. Wengine wana nia ovu ya kufanya ujangili na kuondoka. Kwa vile biashara hiyo haifanyiki kwenye soko la wazi na bei ya nyara iko juu, hayo yanaendelea kuwashawishi wananchi kutoa ushirikiano bila kuelewa madhara yake.”
Mambo mengine yanayochochewa na uelewa mdogo ni vitendo vya wanajamii kuchoma moto maeneo ya misitu wanayoishi wanyama pamoja na kuvamiwa makazi yao wakati wa kufanya shughuli zao za kimaendeleo.
“Hawa wanyama hupendelea kukaa sehemu za kujificha, au maeneo ambayo hayajasumbuliwa lakini watu wanaondoa uoto wa asili ambao ni makazi yao,” anasema Kalengi.
Kwa upande wa Kimaro, ongezeko la idadi ya watu nchini pia ni tishio. Anasema, “Watu wanazidi kuongezeka wakati ardhi ni ileile. Katika harakati za kilimo, kujenga makazi, kuweka miundombinu na huduma za jamii kama shule, hospitali na masoko, watu wanajikuta wakiingia kwenye makazi ya wanyapori, ambao kwa kutojua waelekee wapi, wanaingia maeneo ya watu.’’
Kumlinda kakakuona: Tanzania inakwama wapi?
Licha ya kuwepo kwa sheria na jitihada mbalimbali kufanywa na wadau kudhibiti vitisho dhidi ya mnyama huyo, bado vita hiyo inaendelea kuwa ngumu. Kwa mfano, Sheria ya Wanyamapori ya Tanzania, pamoja na mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Spishi za Wanyamapori na Mimea iliyoko Hatarini Kutoweka (CITES), vimekusudia kusaidia kuzuia biashara haramu ya kakakuona na mazao yake, lakini bado watu wanaendelea kuwasafirisha.
Miongoni mwa sababu kubwa zinazoelezwa kurudisha nyuma juhudi hizo ni ukosefu wa raslimali kwa ajili ya kuwafikia watu wengi zaidi na kuwaelimisha ili wawe na uelewa kuhusu kakakuona, waachane na mitazamo potofu inayohatarisha maisha ya mnyama huyo, lakini pia washiriki kikamilifu katika ulinzi wake.
Katika mahojiano na Mongabay kwa nyakati tofauti, Kakengi, Chamba na Kimaro, wote walieleza namna mipango ya taasisii zao ya kuelimisha wananchi wengi zaidi hasa wale wanaoishi maeneo yanayozunguka hifadhi, inavyokwamishwa na uhaba wa raslimali.
Kwa mujibu wa watalaam hao, viongozi wa vijiji na watendaji ni nguzo muhimu katika harakati hizo kutokana na nafasi zao na pia ukaribu wao na wananchi kwenye maeneo wanayoyaongoza. Hata hivyo, walisema wameshindwa kuwafikia wote kutokana na uhaba wa raslimali na ukubwa wa maeneo husika.
Changamoto nyingine ni upungufu wa tafiti kuhusu kakakuona, hasa katika masuala ya ikolojia yake, uelewa wa jamii, mitazamo na imani zao, mitandao ya biashara, njia za usafirishaji, pamoja na mwenendo wa kibiashara wa kakakuona na mazao yake katika ngazi ya jamii.
Wataalam hao wote walibainisha kwamba mara nyingi kipaumbele kwenye tafiti kimekuwa kikiwekwa kwa wale wanyama wakubwa kama tembo, simba, twiga na nyati, ambao huchukuliwa kama vivutio vya utalii, huku hawa wadogo kama kakakuona wakiachwa nyuma. Waliongeza kuwa kitendo cha mamlaka kutomtangaza vya kutosha mnyama huyo kama zifanyavyo kwa wengine, ni tatizo lingine.
Hadi sasa inaelezwa kuwa hakuna takwimu zinazoonyesha idadi kamili ya kakakuona wanaopatikana nchini Tanzania.
Akizungumzia suala la takwimu, Kimaro alisema njia zinazotumika kuwahesabu zina changamoto kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na kutotoa takwimu halisi. Wakati nyingine zinahitaji vifaa vya kisasa, ambavyo ni vya gharama kubwa.
Changamoto nyingine inayohusiana na takwimu inatokana na asili na tabia ya mnyama huyo. “Kakakuona hubadilisha mashimo kila wakati. Kwa mfano, kwa mwezi mmoja anaweza kubadilisha mashimo 80. Hilo linaleta changamoto kwani mnyama mmoja anaweza kuhesabiwa zaidi ya mara moja na kuleta takwimu zisizo sahihi,” anasema Kimaro.
Nyingine ni ukosefu wa uwezo miongoni mwa wataalamu wa uhifadhi na jamii kwa ujumla katika kushughulikia, kuwaachilia na kuwafuatilia kakakuona waliookolewa kwa njia sahihi, jambo linaloathiri kiwango cha uhai wao baada ya kuokolewa.
Kumlinda kakakuona: Tanzania imefika wapi?
Kuhusu mikakati mbalimbali ambayo wamekuwa wakifanya ili kudhibiti vitendo vinavyotishia maisha ya kakakuona, wataalam hao walitaja utoaji wa elimu, kutilia mkazo suala la tafiti na kutoa hamasa kwa wananchi ili waunge mkono shughuli za uhifadhi, kama baadhi ya mikakati hiyo.
Kwa upande wa TAWIRI, Kakengi alisema wamekuwa wakifanya kampeni zinazohusisha mikutano, mijadala, machapisho, vyombo vya habari na kufanya mafunzo kwenye ngazi mbalimbali kuanzia kwa Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, watendaji wa vijiji hadi wenyeviti wa vijiji, lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa jamii, ingawa hawajaweza kufikia maeneo yote.
Aidha, alisema wameanzisha kundi sogozi lenye wadau mbalimbali kwa ajili ya kupashana habari muhimu, kubadilishana maarifa na uzoefu na pia kujifunza.
Alisema pia wameendelea kufanya tafiti na kutumia matokeo yake kutoa ushauri kwa wadau wengine.
Jitihada nyingine ambazo wamezifanya ni kurekebisha mwongozo unaotumiwa na nchi ya Botswana katika masuala ya kakakuona ili uendane na mazingira ya Tanzania, lengo likiwa kuutumia hadi pale watakapopata uwezo wa kutengeneza wa kwao.

Kukosa mwongozo unaotoa maelekezo kuhusu mnyama huyo ni miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa yalikuwa yakileta changamoto katika juhudi za kumlinda kakakuona.
Hata hivyo changamoto kubwa ni kwa namna gani mwongozo huo utafika vijiji vyote katikati ya changamoto za raslimali ambazo taasisi zote zimelalamikia.
Kwa upande wa TAWA, Chamba alisema wameendelea kutoa mafunzo sehemu mbalimbali nchini kwa kuwashirikisha watendaji wa vijiji na wenyeviti ingawa hadi sasa maeneo ambayo hayajafikiwa ni makubwa zaidi.
Alisema kwa kushirikiana na mamlaka nyingine husika wameweka mikakati ya udhibiti kwenye malango yote, zikiwemo bandari na viwanja vya ndege ambako wameweka mbwa wenye uwezo wa kunusa meno ya tembo, pembe za faru, kucha za simba na magamba ya kakakuona, viumbe ambao wako hatarini kutoweka kutokana na usafirishaji haramu, alisema.
“Tunaendelea pia kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya hifadhi sambamba na kuendelea kuwaelimisha watu wanaoishi maeneo yanayopakana na hifadhi za wanyamapori ili waachane na imani potofu zinazowafanya washawishike kuwakamata wanyama hao,” aliongeza.
Kadhalika alisema kama sehemu ya kushawishi watu waone umuhimu wa uhifadhi, wametoa ajira kwa vijana wenye ujuzi katika masuala ya hifadhi ambao wanafanya kazi kama askari wa wanyamapori wa vijiji.
Kabla ya kuajiriwa, walipelekwa chuoni kujifunza namna ya kudhibiti ujangili na hivi sasa wanashirikiana na askari kutoa ulinzi kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wa TRCO, Kimaro alitaja kampeni, midahalo, mikutano, tafiti, machapisho, taarifa kupitia vyombo vya habari na mafunzo kwa wenyeviti na watendaji wa vijiji katika maeneo zaidi ya 200 kama baadhi ya mikakati yao kuwalinda kakakuona.
“Katika mikutano yetu tulibaini kwamba kuna baadhi ya watu huko vijijini walikuwa hawamfahamu kakakuona. Tulipowaonyesha picha na kuwaeleza umuhimu na hatari inayomkabili, walielewa na kuahidi kutoa ushirikiano,” alisema Kimaro.
Kimaro aliomba taasisi nyingine za ndani na nje pamoja na wadau wa uhifadhi kujitokeza ili kushirikiana nao katika kutekeleza miradi ya kuwalinda kakakuona katika maeneo ambayo wameshindwa kufika kutokana na ufinyu wa bajeti.
Nini kifanyike kuwalinda kakakuona
Kwa upande wa TRCO, Kimaro anasema jambo la kwanza muhimu analoshauri ni kufanyika kwa tafiti za kina na za kutosha kuhusu kakakuona ili kupata takwimu kwa ajili ya kanzidata ya kitaifa.
Anasisitiza pia kuitishwa kwa mkutano wa kitaifa utakaowaleta pamoja watalaam na wadau mbalimbali kujadili na kuweka mkakati wa kitaifa kuhusu ulinzi wa kakakuona nchini na namna ya kushirikiana katika kudhibiti mambo yanayotishia maisha ya mnyama huyo.
Kimaro pia anashauri wananchi wanaozunguka maeneo wanakopatikana wanyamapori, wakiwemo kakakuona, wanaoingia msituni kwa ajili ya kutafuta huduma fulani kama kuni na maji, wasaidiwe kupata mbadala wa kupata huduma hizo ili waachane na kwenda kwenye misitu kuleta usumbufu kwa wanyama na kuathiri makazi yao.
Aidha alishauri kampeni za kuwajengea watu uelewa zipewe kipaumbele ili kusaidia kubadili mitazamo potofu kuhusu kakakuona. Alishauri kampeni hizo zianzie mashuleni.
Kwa upande wa Mrosso, anashauri kushirikisha jamii za wenyeji katika programu zitakazowezesha kutumia maarifa yao pamoja na sayansi ya kisasa kulinda mnyama huyo. Programu hizo zinaweza kuwa zile zinazosaida uhifadhi wa spishi hiyo wakati huohuo zikishughulikia mahitaji ya maisha ya watu.
Anashauri pia kipaumbele kitolewe kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi kwani uelewa wao ukiwa mkubwa, wataachana na mitazamo potofu inayowafanya wawadhuru wanyama hao, lakini pia watatoa ripoti pindi wanapopata taarifa za majangili pamoja na wafanyabishara kutoka mijini au nchi jirani wanaokwenda kwenye maeneo yao kusaka wanyama hao.
Kwa upande wa TAWA, Chamba anashauri kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi zinazopakana na Tanzania ili kusaidia katika udhibiti wa usafirishaji haramu wa kakakuona. Anasema wanaweza kushirikiana katika kubadilishana taarifa pamoja, uzoefu na ujuzi wa namna ya kufanya udhibiti.

Kwa upande wa TAWIRI, Kakengi anaomba serikali ya Tanzania kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa ili kufanikisha ulinzi wa kakakuona. “Tanzania inaangaliwa kwa jicho la kipekee; hatma ya kakakuona duniani iko mikononi mwetu. Ili kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kuwepo na kuwarithisha kwa vizazi vijavyo, lazima tufanye kila linalowezekana kuwalinda,” anasema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Minziro, wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Ladslausi Maiko Richard, anasema uelewa wa watu kuhusu kakakuona na nini wafanye pindi wanapokutana naye, bado ni mdogo. Anashauri elimu zaidi itolewe kupitia njia mbalimbali kuhusu namna wananchi watakavyoshiriki kikamilifu katika kuwalinda.
“Aprili mwaka 2024, nilikutana na kakakuona, nilikimbia nikidhani ni mnyama mbaya anayeweza kunidhuru. Yeye aliishia kwenye misitu. Hawa watetezi wa wanyama walipokuja kwetu kutufanyia mafunzo, wakaonyesha picha, ndipo nikabaini niliyemuona alikuwa kakakuona,” anasema Richard, na kuongeza kwamba wapo wananchi wengi ambao wanashindwa kutoa ushirikiano kwa sababu hawajui la kufanya.
Hizo ni baadhi ya simulizi za kweli zilizotolewa na Geofrey Kapinga, Mjumbe wa Kamati ya Mazingira ya kijiji cha Minziro, wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.
Licha ya jamii, makundi maalum ambayo Kapinga anashauri yapewe kipaumbele katika kupewa elimu ni wawindaji wanaoishi msituni ambao wanakuwa na taarifa kuhusu wanyama hao pamoja na waganga wa kienyeji ambao hutumia viungo vya mnyama huyo kwenye madawa yao.
“Hata ukiangalia chupa zenye dawa zao, nyingine zina picha ya kakakuona, kuashiria kwamba ilitengenezwa kutokana na viungo vya mnyama huyo. Hao inatakiwa waelezwe sheria inasema nini kuhusu kuua au kudhuru wanyama hao, na inatakiwa zitumike mbinu kuwashawishi ili waachane na biashara hizo,’’ anasema Kapinga.
Sanya anashauri mambo mawili yapewe kipaumbele katika kutafuta suluhisho. Jambo la kwanza ni elimu ya kutosha kutolewa kwa wanajamii, na la pili ni wahifadhi kutoa mwongozo kwa watu kuhusu nini wafanye pindi wanapokutana nao.
“Baadhi ya wananchi huogopa kuripoti kutokana na nguvu kubwa inayotumiwa na maofisa wa mamlaka wanaopewa taarifa juu ya kuonekana kwa mnyama huyo. Wanaona wakimpeleka, wataulizwa amefikaje mikononi mwao,” anasema.
Happy Mwampashe, mkazi wa kijiji ya Mafuluto, Wilaya ya Iringa Vijijini, mkoani Iringa, anaona ushirikishwaji wa jamii kwenye ulinzi wa kakakuona utasaidia katika kuhakikisha mnyama huyo anakuwa salama.
Anasema wananchi vijijini ndiyo humuona kakakuona. Wakiwa na uelewa wa nini wafanye, itakuwa rahisi kutomdhuru na kuwapigia simu wahusika ili wafike haraka kumchukua na kumrudisha kunakohusika.
Anasema mara ya kwanza kumuona mnyama huyo ni kijijini kwao ambapo alikuwa amewekewa unga, maji na silaha kwa imani kwamba kitu atakachokigusa ni utabiri wa kitakachotokea siku sijazo.
Kakengi anaomba wadau wote wa uhifadhi wakiwemo wananchi kushiriki kikamilifu katika kumlinda kakakuona. “Mustakabali wa mnyama huyo duniani, uko mikononi mwetu,” anasisitiza.
Picha ya bango: Kakakuona huyu anayeitwa Temminck’s pangolin (Kakakuona wa ardhini), akiwa katika picha aliyopigwa alipoonekana huko mkoani Manyara. Ni aina za kakakuona wanaopatikana sehemu nyingi nchini Tanzania. Picha kwa hisani ya Meritho Katei.