- Chura huyu wa kipekee huruka sehemu moja ya ukuaji (tadpole stage). Haruki kama vyura wengine, bali yeye hutembea kama ngo’mbe.
- Juhudi za wanajamii za kuhifadhi mazingira kwa kuzuia ukataji miti, kupanda miti zaidi ya kiasili, kukabiliana na majanga ya moto wa mara kwa mara kwenye misitu, imepongezwa.
- Vyura hao hulinda vyanzo vya maji vinavyosaidia watu 400,000 kunakopita mito kutoka milimani kwa kula algae majini, hivyo kuyaweka maji yawe safi na yenye mtiririko shwari.
- Wataalamu wanasema hakuna data mpya iliyotolewa hivi karibuni, ila bado vyura hao wako katika hatari kubwa ya kuangamizwa, haswa wakati huu kunaposhuhudiwa mabadiliko ya tabianchi, shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira, moto msituni na ukataji miti kiholela.
Kusini mashariki mwa Kenya, kilomita zaidi ya 45 kutoka tambarare za mji wa Voi, katika mwambao wa pwani, kuna kilele cha mlima mrefu kwa jina Vuria, wenye urefu wa zaidi ya mita 2,208.
Pia kuna miinuko ya milima mingine mirefu kiasi inayoshikilia misitu ya kiasili kama vile Ngangao, Mbololo, Chawia, Fururu, Iyale, Mwambirwa, Msidunyi na mengineyo.
Msitu wa Ngangao, wa pili kwa ukubwa kwa zaidi ya hektea 120, baada ya msitu wa Mbololo wenye hektea 220, unashikilia na kuhifadhi viumbe hai wasiopatikana kwingineko ulimwenguni, kama vile ndege, amfibia pamoja na miti ya kiasili.
Kutokana na madhara yanayochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, shughuli za kila siku za binadamu, na moto wa mara kwa mara katika misitu, wanajamii waliamua kuanza kutunza mazingira ya misitu hiyo, baada ya kushawishiwa na wanamazingira, serikali pamoja na asasi za kulinda misitu.
Mwanasayansi wa kutambua viumbe hai, John Maghanga, anakiri kuwa halikuwa jambo rahisi kwa jamii kukubali mabadiliko hayo, hadi wanasayansi na wataalamu wa mazingira walipowahamasisha kuhusu uwepo wa viumbe wengi wasiopatikana kwingineko ulimwenguni, kama vile ndege na chura aina ya “Taita Hills Warty”, ambayo wanasayansi wanasema yuko katika hatari ya kuangamizwa kabisa.

“Wanajamii walichukulia suala hilo uzito, japo shingo upande, kwani kwa miaka mingi wametegemea miti kwa kuni, kuchoma mkaa na pia kujengea nyumba zao kutumia mbao kutoka kwa miti hiyo,” asema Maghanga.
Wanajamii hapa wanatunza mazingira, misitu na kuzuia watu kuchoma moto au kuharibu makazi ya wanyama na viumbe hai katika misitu hii, haswa wanaotambaa. Wanajamii hujihusisha na ushonaji vyondo, ufugaji nyuki na ufugaji vipepeo, ila shughuli hizi huwapatia pato kidogo kiasi, chini ya dola moja kwa siku, japo wanajitahidi kuimarisha rasilimali zilizoko misituni.
Wakiwa wamejiandaa tayari kwa shughuli zao za siku, kama vile kupanda miti, pamoja na kutengeza miche tayari kwa upanzi wakati wa msimu wa mvua, Phidilia Mngolia anainama kando ya gogo la mti lililooza, ambapo huwa makao ya chura Warty, anayetambuliwsa kwa ngozi yake ya gamba na mazoea yake ya kujificha kwenye majani yaliooza ardhini.
“Tulizoea kuwauwa vyura hawa. Na kila tulipowaona, hatukufahamu umuhimu wake kwenye mazingira yetu, hadi wataalamu walipotuelezea,” anasema Phidilia, na kuongeza: “Ila sasa tunamfahamu huyu chura, asiyepatikana kwingineko ulimwenguni, kuwa anatutegemea sisi kuhifadhi mabaki ya misitu iliyosalia ili kumlinda,” anasema Phidilia.

Kando yake ni Jane Chanya, anayekiri kwamba yeye alishangaa kujua kuwa chura wanaweza kupewa umuimu zaidi kuliko binadamu, kiwango cha kuonya watu wasiingie kwenye misitu na wasikate miti, hatua inayoweza kusababisha mtu kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sikuamini eti kuna chura wengi duniani, lakini eti kuna chura spesheli huyu wanamuita Warty Frog. Eti anapatikana hapa kwetu pekee! Ni jambo la kushangaza. “Lakini hatua ya kuungana katika kuboresha mazingira yake ni ya maana kwani nimeona pia watalii wanazuru kuja kuona rasilimali tuliyo nayo,” asema Chanya.
Aidha, Gabriel Mwadime na wenzake, ambao pia ni wanajamii katika muungano wa kutunza mazingira ya misitu, wanasema walishangazwa na utafiti kuwa kuna chura spesheli, anayepatikana Taita pekee. Lakini baada ya hamasa kuhusu chura huyo na viumbe wengine katika misitu ya Taita, waliunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya misitu, si tu sababu ya chura Warty, bali pia kwa manufaa ya viumbe wengine na binadamu kwa ujumla.
“Kuna vikundi 13 kutoka maeneo mbalimbali chini ya mwavuli wa DABICO, Dawida Biodiversity Conservation (CBO), vikiwa na zaidi ya wanajamii 200, wanaojishughulisha na upandaji miche, ushonaji viondo, ufugaji nyuki, ukulima wa vipepeo na utalii wa kinyumbani,” aongeza Maghanga.

Milima ya Taita iliyoko kusini mashariki mwa Taifa la Kenya ni mojawapo ya maeneo anakopatikana huyu chura Taita Hills Warty, anayependela mazingira nyevu kiasi kama makao yake.
Utafiti uliofanywa mwaka 2023 na mwanasayansi wa kutambua viumbe hai na amfibia, Patrick Malonza, unaonyesha kuwa chura huyu ni wa kipekee, kwani huruka sehemu moja ya ukuaji, (tadpole stage). Haruki kama vyura wengine, bali yeye hutembea kama ngo’mbe chini. Ana rangi ya kijivu na hubadili rangi yake kulingana na mazingira ya majani ardhini na magogo yaliyooza. Chura huyo anapenda unyevunyevu na si penye maji mengi.
Malonza anahoji kuwa chura huyu hutaga mayai kama vile kuku na kuyalalia kwa siku 90 hadi yanapoanguliwa. Mayai hayo huwa ni kati ya 30 na 40. Utafiti huo unaonyesha kuwa Warty wa kike huwa mkali sana na hujifurisha mwili, kama ishara yake ya kulinda mayai yake anapoyalalia.
Utafiti huo pia unabainisha kuwa chura Warty wa kike huwa na ukubwa wa milimita 55, ilhali wa kiume huwa na ukubwa wa milimita 35. Ngozi yake ni ya gamba, na hujulikana kwa rangi kadhaa, kama vile rangi ya mchanga, kijivu na manjano ikikaribia rangi ya machungwa.
“Chura huyu ni wa kipekee na yuko hatarini zaidi kuangamizwa. Kama wanasayansi, tumetumia mbinu zote hitajika kumtofautisha na vyura wengine ulimwenguni na kubaini kuwa anapatikana kwenye misitu ya Taita pekee,” anasisitiza Malonza.
“Hata hivyo, chura Warty hula wadudu wadogo wadogo na viumbe wengine, na wao pia huliwa na nyoka wenye maumbo madogo, lakini wadudu hawa hawaweki hatarini vyura hawa hata kidogo,” asema mtaalamu huyo.

Takwimu kutoka halmashauri ya kimataifa inayojihusisha na viumbe hai ulimwenguni, ambayo pia hutoa mustakabali wa viumbe wote, mazingira yao, na idadi ya viumbe hao, kiwango cha hatari na athari zinazowazonga, IUCN Red List ya mwaka 2014, inaonyesha kuwa chura huyo yuko katika hatari kubwa kuangamizwa, kwa kiingereza critically endangered species.
Malonza anasema kuwa hakuna data mpya iliyotolewa hivi karibuni, ila bado vyura hao wako katika hatari kubwa ya kuangamizwa, haswa wakati huu kunaposhuhudiwa mabadiliko ya tabianchi, shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira, moto msituni na ukataji miti kiholela.
Mtafiti huyo anongeza kuwa ni vigumu kutambua idadi kamili ya vyura hao, kwa sababu ya mazingira wanayopendelea kuishi, kwenye majani na maganda ya miti, ila inaweza kubainishwa tu kulingana na wingi wao katika eneo husika.
Kwa sasa chura hao wanapatikana katika misitu ya kiasili iliyoko milimani, kama vile, Ngangao, Fururu, Mbololo, Chawia na nyingine, ikiwa ni asilimia 98 ndani ya miaka 200, kulingana na takwimu kutoka kwa shirika la IBA(Nature Kenya) ya eneo la misitu lililoharibiwa kutokana na shughuli za kila siku za binadamu. Shughuli hizi zimebainika kuwaacha vyura hao kujipambania maisha yao kwa sehemu chache zilizosalia.
Saidi Mwawasi Mahabubu, mlinda mazingira katika shirika la misitu Kenya Forest Service, kwenye mlima wa Ngangao, anasema jukumu lake ni kufanya kazi na jamii inayohusisha vikundi saba eneo la mlimani, wanaojishughulisha na utunzaji mazingira na kulinda misitu, ili kuwahifadhi viumbe hai katika sehemu za misitu iliyosalia, ikiwemo chura huyu adimu.
“Tunachofanya zaidi ni kuzuia uharibifu wa mazingira kama ukataji miti, uchomaji mkaa pamoja na kuwasha moto kwenye misitu iliyosalia, ili kudumisha tamaduni yetu, kuvutia watalii wanaoleta kipato, pamoja na kuendelea kuimarisha faida zinazotokana na chura Taita Hills Warty,” alisema Mwawasi.

John Maghanga, mwanasayansi wa kutambua viumbe hai, na pia mwenyekiti wa Taita Taveta Alliance of Community Forest Associations, anayesimamia miungano yote ya misitu kaunti ya Taita Taveta, anasema misitu iliyosalia ya kiasili, ikiwemo, Fururu, Ngangao, Mbololo, Chawia na msitu wa Msidunyi, inahifadhi vyura Warty.
Maghanga anasema misitu ya kiasili ya Mbololo inayoketi katika hekta zaidi ya 200, na Ngangao, ambayo inashikilia hekta 129, ni kati ya misitu iliyosalia na inahifadhi viumbe hai kama chura Taita Warty, na wengine wasiopatikana kwingineko ulimwenguni.
“Tunahimiza watu kupanda miti ya kiasili. Kwa sasa, msitu wa Ngangao, ambao ni wa pili kwa ukubwa Taita, baada ya msitu wa Mbololo, unahifadhi asilimia 20 ya miti ya kigeni na asilimia 80 ya miti ya kiasili inayohitaji kulindwa kwa dhati,” alihimiza Maghanga. “Isitoshe, chura huyu analeta manufaa kwa kaunti ya Taita na taifa la Kenya kupitia kwa mapato yanayopatikana kwa watalii wanaozuru maeneo hayo ya misitu,” aliongeza Maghanga.
Mshirikishi wa masuala ya misitu kaunti ya Taita Taveta, Kenya Forest Service Joel Nderitu, anasema asilimia zaidi ya 70 ya nyumba eneo la Taita zinategemea kuni kama nishati ya kupikia. Anaongeza kuwa shughuli nyingine kama ukataji miti kiholela, ukulima kwenye misitu pamoja na uchomaji mkaa, zimeendelea kuchangia kupotea kwa makao ya chura huyu.
Nderitu anaelezea kuwa ni hakika kuwa juhudi zinazofanywa sasa na miungano ya kijamii katika maeneo ya misitu ya kiasili iliyosalia katika milima ya Taita, zitazaa matunda, akiwa anatumaini kuwa idadi ya vyura hao itaongezeka ndani ya miaka kumi ijayo na kuendelea.
“Hatua ya serikali kuwapatia nguvu wanajamii kwa ushirikiano na uongozi wa kijamii, mashinani kuyatunza mazingira, kumechochea kuimarika kwa vipande vya misitu iliyosalia milima ya Taita, hivyo idadi ya viumbe hai, wanaopatikana nchini Kenya na hususan milima ya Taita, na walio katika hatari ya kuangamizwa kabisa, wataokolewa na kuongezeka,” alisema Nderitu.
Vile vile, anasema kulingana na data zinazokusanywa kila wakati majumbani, na pia kupitia uchunguzi katika misitu, zinaonyesha kuwa matumizi ya kuni kama nishati nyumbani yamepungua kwa kiwango cha asilimia kubwa. “Wengi wamegeukia njia mbadala za kupikia kama vile gesi na kutumia meko zinazotumia miale ya jua, hivyo kupunguza ukataji miti na uchomaji mkaa ilivyoshuhudiwa miaka iliyopita,” kiongozi huyo aliiambia Mongabay.
Hata hivyo, anashikilia kuwa hili bado ni tatizo kubwa kwa sababu jamii nyingi zingali zikitegemea kuni kama nishati ya kupikia.
Anasema ushirikiano kati ya idara ya misitu, KFS, na shirika la wanyamapori nchini Kenya, KWS, umesaidia kupitia kuwafunza watu zaidi ya 30 wanaohusika na ukusanyaji data ya kila wiki, kupitia kutafuta na kukadiria bila mpangilio, kwa kimombo (Using random time limited search), katika misitu ili kubaini sehemu nane za misitu zilizo na chura huyo.
Mtaalamu Malonza aliambia Mongabay kuwa vyura hao hulinda vyanzo vya maji vinavyosaidia watu 400,000 kunakopita mito kutoka milimani. Hao hutekeleza majukumu hayo kwa kula algae, ambayo humea majini, hivyo kuzuia maji na kuyaweka safi na mtiririko shwari. Pia inasaidia kuimarisha ukulima kupitia kudhibiti wadudu wanaoharibu mimea, kwa sababu chura hao hula wadudu waharibifu, hivyo kuzuia wasiharibu mazingira au hata kufika mashambani.

Matamshi yake yanawiana na maelezo kutoka kwa ukurasa wa Global Humane “Why Frogs Matter”.
Waziri wa Mazingira, Maji, Misitu na Mali Asili kaunti ya Taita Taveta, Granton Mwandawiro, amepongeza juhudi za wanajamii za kuhifadhi mazingira kwa kuzuia ukataji miti, kupanda miti zaidi ya kiasili, kukabiliana na majanga ya moto wa mara kwa mara kwenye misitu, ambayo imeshuhudiwa miezi kadhaa iliyopita, ikiwemo Februari 2026.
Anasema ni dhahiri shahiri kuwa viumbe hai walio adimu ulimwenguni na wanaopatikana milima ya Taita pekee watalindwa na kuhifadhiwa ndani ya miaka kumi ijayo, kutokana na juhudi za sasa zinazotekelezwa na jamii kwa ushirikiano na asasi husika.
“Nimeshirikiana na wanajamii kubuni mpangilio na mwelekeo wa kutunza mazingira, kwa kimombo, Forest Management Plan, ili kuchochea juhudi za kuyatunza mazingira ya viumbe hai misituni,” aliiambia Mongabay. “Kwa sasa, mswaada wa misitu uko bungeni ukisubiri kujadiliwa na kutoa mwelekeo mwafaka wa usimamizi wa mazingira, ili kurudisha hadhi ya misitu asili na kuwapa viumbe hai makao bora,” aliongeza Mwandawiro.
Vile vile, Malonza, ambaye pia ni mwanasayansi wa viumbe hai wanaotambaa katika Hifadhi ya Makumbusho ya Kitaifa nchini Kenya, (National Museums of Kenya), anasema japo rasilimali kutoka kwa serikali si hakika, inashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kupiga jeki juhudi za kulinda misitu na mazingira kwa viumbe hai.
“Itakuwa vyema kwa viumbe hai wote walio katika hatari ya kuangamizwa kuangaziwa pakubwa na jamii kupewa hamasa kuwahusu, ili walindwe pamoja na mazingira yao,” asema Malonza.
Mwanasayansi huyo wa viumbe hai, amesisitiza ushirikiano, hamasa kuhusu viumbe walio hatarini kuangamizwa, kwa kuzingatia kupanda zaidi miti ya kiasili, ili kuongeza eneo la sasa lililo kilomita 4.3km2, na kuwachana na upanzi wa miti ya kigeni, inayoharibu mazingira.
Hatimaye zoezi la kijamii la kuwatunza vyura Warty na mazingira yao, litatiliwa maanani wakati taifa la Kenya litakapoadhimisha siku ya Viumbe Hai Amfibia, kwa mara ya kwanza katika historia yake. Ulimwenguni, hii itakuwa awamu ya 18, (18th Annual Save The Frogs Day), jinsi ilivyoorodheshwa katika wavuti wa SAVE THE FROGS. Lengo kuu ni kuongeza idadi ya vyura hao.
Inakadiriwa kuwa asilimia 39 ya vyura wako katika hatari ya kuangamizwa kulingana na utafiti uliofanywa na wataalamu wanaohusika na utaalam wa Amfibia.
Wataalamu wa masuala ya misitu na mazingira, wanasayansi wa viumbe hai, asasi za kiserikali na zisizo za kiserikali, kwa pamoja, wanakubaliana kuwa kuhusisha jamii moja kwa moja ili kuhifadhi misitu ya kiasili na viumbe hai, kunaleta matumaini na hakikisho la kuongeza idadi ya viumbe hai msituni, akiwemo chura Warty na viumbe wengine walio katika hatari ya kuangamizwa, ulimwenguni kote.
Picha ya bango: Warty Frog, ambaye hupatikana kwenye misitu ya Mlima wa Taita, na si kwingineko duniani isipokuwa Kenya. Picha na (c) mameissner (CC BY-NC) iliyochapishwa katika tovuti ya INaturalist (CC BY-SA).