- Kongamano lilipendekeza uongozi thabiti, uhifadhi endelevu, ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia bunifu.
- Bara la Afrika linatakiwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu, teknolojia na uendelezaji wa rasilimali watu, ili kuimarisha ushindani wake katika soko la kimataifa.
- Uhifadhi wa wanyamapori pamoja na mifumo ya ikolojia ulitajwa kama nguzo imara ya utalii endelevu.
- Washikadau pia waliangazia umuhimu wa tafiti za kina katika kufanya maamuzi sahihi ya sera.
Kongamano la kimataifa la uhimili wa utalii limependekeza uongozi thabiti, uhifadhi endelevu, ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia bunifu ili kustawi na kuendeleza sekta ya utalii ili iweze kukabiliana na migogoro.
Akitoa hotuba kwenye mkutano wa Nne wa Siku na Kongamano la Ustahimilivu wa Utalii Duniani, uliofanyika jijini Nairobi, Edmund Bartlett, ambaye ni mwanzilishi na mwenyekiti mwenza wa Global Tourism Resilience and Crisis Management Centre (GTRCMC), na pia Waziri wa Utalii wa Jamaica, alisema umefika wakati wa mataifa ya Bara la Afrika kushirikiana katika kuweka mikakati itakayoziwezesha kukabiliana na migogoro inayoikumba sekta ya utalii.
“Mshikamano wa bara la Afrika unaweza kulifanya kuwa kitovu cha utalii chenye ushindani na uthabiti zaidi duniani,” alieleza katika wito wake kwa washiriki.
Waziri wa Utalii na Wanyamapori ya Kenya, Rebecca Miano, ambaye alifungua rasmi mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa sauti ya bara la Afrika kama chombo kinachofaa kuleta uzoefu, kuufanya utalii uwe endelevu pamoja na kubuni sera na uvumbuzi unaotakiwa.
“Bara la Afrika haliendani tu na mienendo ya kimataifa, ila pia huchangia suluhisho kupitia ushirikiano wa kikanda, uthabiti wa kijamii, utalii unaoendelezwa na jamii asilia, ulinzi, ushirikishwaji wa wa vijana, na mifumo ya utawala inayowezesha wadau kutoka taasisi za umma na kibinafsi kufanya kazi kwa uwiano na ushirika,” alisema.
Katika wito wake kwa washiriki, waziri huyo aliitaka Afrika kuongeza uwekezaji katika miundombinu, teknolojia na uendelezaji wa rasilimali watu, ili kuimarisha ushindani wake katika soko la kimataifa.
Katika siku ya pili ya mkutano huo ambao ni wa nne kuandaliwa na GTRCMC, washiriki, chini ya mada, “Ulinzi unaoongozwa na Takwimu: Matumizi ya akili bandia (AI), Takwimu Kubwa na Uchanganuzi Tabanishi kwa Kuzuia Migogoro,” walijadili mbinu kadhaa.

Wataalamu waliohudhuria walielezea jinsi teknolojia inavyoweza kusaidia kutabiri, kuepusha au kupunguzwa kwa migogoro inayoikumba sekta ya utalii. “Ni muhimu pia kwa taasisi za utalii kuwekeza katika mifumo ya utafiti na taarifa,” alisisitiza mwendeshaji wa mjadala huo, Lloyd Waller.
Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Wanyamapori ya Kenya Prof. Erastus Kanja, alisisitiza mabadiliko ya mitazamo kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, hasa kama jukumu la kimazingira, akisema ni mojawapo ya njia tofauti za uwekezaji zinazoweza kustawisha jamii na uchumi wa nchi binafsi kwa njia endelevu.
Kwa mujibu wa Prof. Kanja, ili kufanikisha mikakati kama hii, Afrika lazima ihakikishe mifumo ya ikolojia haitunzwi tu, bali pia imewezeshwa kustahimili majanga tofauti yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Alitoa mfano: “Nchini Kenya, wanyamapori ni urithi wa taifa, chanzo cha utambulisho, msingi wa riziki na nguzo ya uthabiti wa kiikolojia.”
Aliongeza: “Uhimili wa mifumo yetu ya wanyamapori unaamua moja kwa moja uimara wa sekta yetu ya utalii na, kwa upana zaidi, ustawi wa mamilioni ya watu wanaoitegemea.”
Kanja pia alitangaza kuwa hivi karibuni Kenya Wildlife Service (KWS) ilianzisha ukurasa maalum kwenye tovuti yake kwa ajili ya michango ili kuwezesha mashirika na wafadhili binafsi kote ulimwenguni kuchangia uendelezaji wa uhifadhi wa wanyamapori.
Kongamano hilo lililoongozwa na kaulimbiu “Uhimili katika Wanyamapori na Utalii Unaotegemea Asili”, liliwakutanisha washiriki kutoka sekta mbalimbali , wakiwemo wadau wa sekta ya utalii, watunga sera, na wataalamu wa uhifadhi kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Mkutano huo wa siku tatu, uliokamilika Februari 18, pia ulihutubiwa na wataalamu na viongozi katika idara na sekta muhimu duniani.
John L. Ololtuaa, ambaye ni Katibu Mkuu katika Idara ya Utalii nchini Kenya, aligusia mipango ya taifa hilo kuimarisha sera na mikakati itakayostawisha sekta hiyo, maandalizi yake katika kukabiliana na misukosuko kama “mabadiliko ya tabianchi, majanga ya kiafya na changamoto za kiuchumi duniani”.
Silvia Museiya, anayesimamia Idara ya Wanyamapori, alieleza jinsi uhifadhi wa wanyamapori na mifumo ya ikolojia unavyoweza kuwa nguzo imara ya utalii endelevu. “Bila uhifadhi madhubuti, mustakabali wa utalii uko hatarini,” alisema.
Wengine waliochangia mada hiyo ni Norbert Talam, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utalii nchini Kenya. Aligusia udhibiti muafaka ili kuhakikisha viwango na usalama wa watalii vinaimarishwa kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Donovan White, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Utalii ya Jamaica, alieleza namna takwimu zinavyoweza kutumika kufuatilia mienendo ya soko na kubuni mikakati ya masoko yenye tija.
Naye Hesbon Oyiendo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Utalii, aliangazia umuhimu wa tafiti za kina katika kufanya maamuzi sahihi ya sera.
Wengine ni Havar Bauck, mwanzilishi wa HotelOnline, ambaye alionyesha jinsi majukwaa ya kidijitali yanavyoweza kusaidia hoteli na biashara ndogo ndogo kukabiliana na misukosuko kwa kutumia uchambuzi wa takwimu za wateja.
Francis Njue, Mkurugenzi Mtendaji wa Willing Host, alisisitiza umuhimu wa teknolojia pamoja na mafunzo na utamaduni wa ukarimu katika ujenzi wa taswira chanya ya utalii wa Afrika.
Picha ya Bango: Waziri wa Wizara ya Utalii na Wanyamapori ya Kenya, Rebecca Miano na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Wanyamapori ya Kenya, Prof. Erastus Kanja, wakiingia kwenye kongamano la utalii, Nairobi.