- Katika viunga vya mji wa pwani wa Mombasanchini Kenya, shirika la wanawake katika eneo la Jomvu Creek limelenga kubadilisha maisha na mazingira kupitia ufugaji wa kaa.
- Ruzuku ya uchumi wa buluu (blue economy) imewawezesha wanawake hao kuanzisha mradi wa kunenepesha kaa na kujenga njia ya mbao (boardwalk) kupitia mkondo wa maji, kwa matumaini ya kukuza utalii wa ikolojia (ecotourism).
- Katika mwezi mzuri, mauzo ya kaa ya wanawake hao hufikia $310, kipato ambacho ni nadra kupata katika eneo hilo ambalo wengi walisema wanaishi maisha ya shida.
- Mbali na kipato, wanawake wa Jomvu wanajiona kama walinzi wa mkondo huo wa maji, kupitia ufugaji wa kaa na urejeshaji wa mikoko. Pia wamepanda karibu miche milioni moja, miti ambayo husaidia kuimarisha ufukwe, kupunguza mmomonyoko wa ardhi, na kuboresha mazalia ya samaki na kaa wadogo.
Mombasa, Kenya — Umbali kama wa dakika tano tu za kutembea kupandisha barabara ya mlimani kutoka mikoko inayozunguka eneo la tambarare la Jomvu Creek, harufu kali ya maji ya bahari imejaa hewani. Kundi la wanawake limeujaza ukumbi mdogo kwa vicheko na mazungumzo. Katika vijiji vya pwani, Kaunti ya Mombasa, mikusanyiko kama hii ya wanawake ya kusimamia vikundi visivyo rasmi vya akiba na mikopo hujulikana kama chama. Lakini hiki si chama cha kawaida.
Hapa, mijadala huzungumzia mawimbi ya bahari, chakula cha kaa pamoja na ukarabati wa vizimba na miche ya mikoko. Wanawake hao, wenye umri wa kati ya miaka 35 hadi 60, ni wanachama wa Jomvu Women in Fisheries and Culture, shirika la kijamii linalolenga kubadilisha maisha na mazingira yao kupitia mradi wa ufugaji wa kaa.
Miaka minne iliyopita, wanawake hawa walikuwa wametawanyika kijijini humo. Wengi wao walifanya kazi inayojulikana kwa wengi kama mama karanga, yaani wanawake wanaokaanga samaki juu ya makaa ya mawe na kuuza karibu na fukwe ambako wavuvi hushusha samaki wao. Baadhi walikuwa wakiuza samaki wabichi huku wengine wakibaki nyumbani wakilea watoto na wajukuu. Hata hivyo, kupungua kwa samaki baharini, matatizo ya kiafya yatokanayo na moshi wa kuni na kutokuwa na uhakika wa mapato ya biashara ndogondogo vilianza kuwaathiri.
Mwaka 2021, mradi wa Kenya Marine Fisheries and Socio-Economic Development (KEMFSED) ulipotangaza ruzuku kwa miradi ya uchumi wa buluu, baadhi ya wanawake hawa waliamua kuchangamkia fursa hiyo.

Dhana Mpya
Ufugaji wa kaa ulikuwa wazo jipya kabisa kwao. Wanawake hao waliandika pendekezo lao la mradi baada ya kuhudhuria mafunzo kadhaa kuhusu usimamizi wa biashara ndogo na uvuvi endelevu.
“Baadhi yetu tulikuwa tumehudhuria warsha, hivyo tulifahamu namna ya kuandika pendekezo,” anasema kwa fahari Charity Baya, mwenyekiti wa kikundi hicho. Anaogeza kuwa baadaye waliomba ushauri wa kitaalamu kutoka kwa maafisa wa uvuvi ili kuboresha mpango wao.
Karibu nusu ya wanachama 30 wa awali walijiondoa, wakihofia kuwa mradi huo usingefanikiwa. Baadhi walihisi mradi wa kaa ulikuwa jambo geni na lenye hatari kubwa. Wengine walikuwa na mashaka kuwa wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 30, wanaokabiliwa na majukumu mengi ya kulea watoto na kusimamia familia, wasingeweza kuendesha mradi huo kwa mafanikio.
Hata hivyo, wanawake 14 pamoja na wanaume watatu, ambao kikundi huwaita kwa upendo “wanaume mashujaa,” waliendelea kusonga mbele. Uvumilivu wao ulizaa matunda wakati mradi wa KEMFSED ulipowapatia KSh2,700,000 (takriban $20,900) kuanzisha biashara ya kunenepesha kaa na kujenga njia za mbao kupitia msitu wa mikoko katika eneo hilo la Jomvu Creek.
Baya akielezea sababu ya kikundi hicho kuchagua kujikita katika ufugaji wa kaa badala ya samaki, anasema: “Samaki walikuwa wanapotea, hawapatikani si kwa ajili ya chakula wala kutuongeza kipato. Kaa wana thamani kubwa na katika eneo la Mombasa hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiwafuga.”
Ruzuku hiyo iligharamia ununuzi wa kreti za plastiki, kamba za kuzifungia na vifaa vingine vya shughuli ya kunenepesha kaa. Pia ruzuku hiyo ilitumika kwenye ujenzi wa awamu ya kwanza ya njia ya mbao kupitia msitu wa mikoko wa Jombu Creek. Kwa sasa, njia hiyo ina urefu wa mita 180 (futi 590), na kuna mipango ya kuirefusha zaidi pindi fedha zitakapopatikana.
Ikikamilika, njia hiyo itatumika kama njia rahisi ya kufikia vizimba vilivyofungwa majini ambako kaa wao hunenepeshwa, na pia itasaidia mradi wa utalii wa ikolojia ambapo wageni watapia misitu ya mikoko.

Sehemu ambayo kaa hustawi
Wanawake wa Jomvu Creek hufuga kaa wa matopeni aina ya Scylla serrata, ambao pia huitwa kaa mkubwa au kaa wa mikokoni. Kaa hao wanaojulikana kwa nyama yao tamu na kuwa na gharama kubwa sokoni, hustawi katika mikondo ya maji ya chumvi yenye mikoko kama Jomvu.
Kikundi hufuga kaa hao katika vizimba vya plastiki vilivyofungwa kwa kamba ndani ya mikondo ya maji ya kupwa na kujaa ambayo ni makazi yao ya asili. Vizimba hivyo ni kreti zilizotumika awali kusafirisha mikate kutoka kwenye maduka hadi masoko ya eneo hilo. Kila kizimba kinaweza kubeba kaa wawili, na kwa sasa kikundi kina takriban vizimba 30.
Kaa wadogo wa porini hukusanywa na wanachama pamoja na wavuvi wa eneo hilo wanaounga mkono mradi. Siku nzuri wanaweza kupata hadi kaa 10 wakati siku mbaya hukosa kabisa. Baada ya kuwekwa kwenye vizimba, kaa hulishwa samaki wadogo, kamba na konokono wa baharini, vitu ambavyo hukusanywa kutoka kwenye mikondo ya maji ya eneo hilo. Ulishaji hufuata ratiba maalum: siku moja wanapewa chakula, siku inayofuata hawapewi. Kaa hula tu wakati vizimba vimezamishwa majini na maji yamejaa.
Huchukua wiki kati ya sita hadi nane kwa kaa kukua kutoka uzito wa takriban gramu 300 za awali wakati anakamatwa hadi kufikia uzito wa kati ya gramu 800 hadi 1,000 wakati amefikia muda wa kuvunwa. Wanawake huuza mavuno yao kwa wanunuzi wakuu wawili: mvuvi wa eneo hilo anayesambaza katika masoko ya Mombasa, na Crab Alive, kampuni ya kuatamia na kusaidia ufugaji wa kaa wa matopeni inayofanya kazi na jamii za Pwani. Kaa hao huuzwa kwa takriban $7 kwa kilo moja.
Katika mwezi mzuri, mauzo yao hufikia kiasi cha $310. Wakigawana zaidi ya wanawake 12, ingawa hawapati kiasi kikubwa sana, lakini ni kipato chenye maana kwa wengi wao waliokuwa wakiishi kwa kubangaiza. Kabla ya kuanza kufuga kaa, samaki walipungua na kusababisha baadhi yao kukosa ajira kabisa.
“Kabla, nilikuwa nikikaanga samaki siku nzima, kazi iliyonifanya nikohoe kwa sababu ya moshi,” anasema Mwanasiti Mwaka Chirima, mweka hazina wa kikundi, ambaye alifanya kazi kama mama karanga kwa miaka 30. “Daktari aliniambia niache, la sivyo ningeathiri afya yangu.”
“Tunawafundisha wanachama wetu kuwa waongoza watalii na waokoaji majini,” anaeleza Baya. “Tunataka wageni wajifunze kuhusu kaa, mikoko na jinsi wanawake wanavyovilinda vyote viwili.”
Kabla ya mabadiliko haya, wanachama waliokuwa na bahati zaidi walipata takriban KSh200 ($1.50) kwa siku kutokana na kukaanga samaki. Kwa sasa, kupitia mauzo ya kaa na mradi uliopangwa wa njia ya mbao, wanatumaini kuzalisha zaidi ya KSh1,000,000 ($8,000) kwa mwaka.

Bahari inapowameza kaa
Hata hivyo, safari yao kuelekea mafanikio imekuwa na changamoto kadhaa. Wiki tatu baada ya kuanzisha mradi, mawimbi makubwa yalikata kamba zilizokuwa zimefunga vizimba vyao. Kwa msaada wa wavuvi wa eneo hilo, wanawake hao walivipata vizimba hivyo vikiwa vimebebwa kwa umbali wa karibu kilomita 2 kutoka vilipokuwa vimefungwa. Mbaya zaidi ni kwamba vilikuwa vitupu. Bahari ilikuwa imemeza kundi lao la kwanza la kaa.
“Hali ilikuwa ya kuhuzunisha sana,” anasema Doris Mwachai, mmoja wa wanachama. “Ndiyo kwanza tulikuwa tumeanza, ghafla tukarudi sifuri.”
Tangu wakati huo, wamejifunza jinsi ya kuimarisha mifumo yao ya kufungia vizimba na kuvichunguza mara kwa mara. Wizi pia umekuwa changamoto, iliyowalazimisha kuanza kufanya ulinzi wa vizimba kwa njia ya kupokezana. “Wakati mwingine watu huiba kaa usiku,” anasema Baya. “Hatuwezi kulinda kila wakati, lakini tunajaribu.”
Changamoto nyingine ni matengenezo ya vifaa vyao vya kazi. Kreti za plastiki, ambazo awali zilikusudiwa kusafirisha mikate, huharibika haraka kwenye mikondo ya maji. Nusu ya kreti za awali zilizonunuliwa miaka minne iliyopita hazitumiki tena. Hivyo wafugaji hao wa kaa wa Jomvu Creek wamelazimika kubuni vifuniko vya vizimba, jambo linalofanya zoezi la kuwalisha kaa wenye makucha yenye nguvu kuwa la hatari.
Mgeni Jumaa zamani alikuwa akivua kaa kwa ajili ya kuuza mara moja. Wakati mmoja alipokuwa akivua, kaa alimkamata mkono kwa nguvu kiasi kwamba alilazimika kushonwa hospitalini. Sasa yeye ni mwanachama muhimu wa kikundi, na ni miongoni mwa wanawake mahiri katika kutafuta kaa wadogo wa kuwekwa kwenye vizimba. “Ninapovua, ninaleta wale wadogo bure kwa kikundi ili wanenepeshwe,” anasema. “Inanipa furaha kuwa sehemu ya jambo kubwa zaidi.”
Anasema kuwafuga kaa kwenye vizimba kumeboresha kipato chake. “Nilipokuwa navua kaa na kuuza moja kwa moja, nilipata labda KSh500 ($3.90) kwa wiki. Sasa, baada ya kuwanenepesha, naweza kuuza kaa mmoja karibu kwa kiasi hicho.”
Kama kikundi, wanawake hao wamejifunza mengi kuhusu kuhudumia kaa wao. Wanajua jinsi ya kuepuka makucha yao, ni wakati gani mawimbi yanafaa kwa ulishaji, ni kaa gani wanenepeshe na ni wapi waachilie.
Hata hivyo Baya anasema bado kuna mengi ya kujifunza. “Baadhi yetu si wavuvi. Tunategemea mafunzo kutoka kwa wataalamu, lakini tunahitaji vifaa bora na maarifa zaidi.”

Mikoko yenye afya, kaa wenye afya
Mbali na kipato, wanawake wa Jomvu Creek wanajiona kama walezi wa mkondo huo wa maji. Tangu mwanzo, waliunganisha ufugaji wao wa kaa na urejeshaji wa mikoko, kwa kupanda karibu miche 1,000,000 ya mikoko. Miti hiyo husaidia kuimarisha ufukwe, kupunguza mmomonyoko wa ardhi na kuunda mazalia ya samaki na kaa.
“Tulipanda miche tukitumaini kuiuza,” anasema mwanachama mwingine wa kikundi, Joyce Rai, “lakini soko la miche ya mikoko halijawa zuri.”
Kila mche huuzwa kwa takriban KSh50 ($0.40), lakini wanunuzi ni wachache. “Hata hivyo, tunafurahi kwa sababu tunasaidia kurejesha mikoko na kaa wanapata chakula humo,” anaongeza huku akicheka.
Kwa kushangaza, mikoko hiyo wanayoipanda wakati mwingine huwa chakula cha kaa. “Changamoto ni kwamba kaa wa matopeni hula miche hii,” Rai anasema. “Kwa hiyo tunalazimika kupanda upya, lakini kwao ni chakula.”
Kikundi kinaelewa kuwa afya ya mkondo huo wa maji ndiyo msingi wa mafanikio yao. Mikoko yenye afya inamaanisha kaa wenye afya. Wanapohudumia vizimba vyao, pia huangalia uwazi wa maji, mzunguko wa mawimbi na mizizi ya mikoko. Ingawa si wanasayansi, mwingiliano wao wa kila siku na mazingira umewaongezea uelewa wa uwiano dhaifu kati ya riziki na mazingira.
Wanawake hao pia wanasema kuwa kuvuna kaa wa porini pekee si endelevu, hasa wakati mawimbi na halijoto vinapobadilika kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Kunenepesha kaa kunawawezesha kuongeza thamani na kudhibiti mzunguko wa mavuno yao wanavyotaka, huku wakipunguza shinikizo la uvuvi wa mara kwa mara katika mkondo huo wa maji, ambao unaweza kuwashawishi wavuvi kuvua kaa kabla hawajakomaa na kuzaa.

Hatua kuelekea pwani endelevu
David Mirera, mwanasayansi mkuu wa utafiti wa Kenya Marine and Fisheries Research Institute (KMFRI), anasema ufugaji wa kaa kama ule wa kikundi cha Jomvu Creek ni hatua muhimu kuelekea riziki endelevu kwa wananchi wa Pwani.
Anasema kunenepesha kaa kunapunguza upotevu baada ya mavuno, hatua inayoathiri mbinu nyingine za uvuvi mdogo wa kaa. “Hapo awali, wavuvi walikuwa wanakusanya kaa na kuwahifadhi kwa siku kadhaa kabla ya kuuza, na wengi wao walikufa. Sasa, wanawake wanawaweka kwenye vizimba moja kwa moja ndani ya mkondo wa maji. Hii inawafanya kaa wabaki hai na kupunguza upotevu.”
KMFRI pia inashirikiana na miradi kama KEMFSED kuanzisha vituo vya kuatamia (hatcheries) vitakavyotoa kaa wadogo, ili kupunguza utegemezi kwa kaa wa porini.
Busolo Bonface, mshauri mkuu wa kiufundi wa ufugaji wa viumbe baharini na uhifadhi wa mazingira nchini Kenya, anasema miradi ya kijamii kama wa wanawake wa Jomvu bado ni midogo mno kuweza kusababisha madhara au kuleta athari kubwa ya kimazingira inayoweza kupimika.
“Kwa sasa, hizi si shughuli za kibiashara kwa kiwango kikubwa,” anasema. “Wanatumia vizimba vya kienyeji na kulisha kwa samaki wadogo au konokono, hivyo kiwango cha virutubisho kinachoingia majini ni kidogo sana. Lakini ikiwa ufugaji wa kaa utapanuka, tutahitaji mwongozo wa wazi kuhusu mazingira ili kuepuka uchafuzi na taka za plastiki.”
Anasema uwepo wa konokono wa baharini katika mikondo ya maji karibu na vizimba vya wanawake hao ni ishara kwamba ubora wa maji bado ni mzuri.
Pia anapongeza juhudi zao za kupanda upya mikoko, akieleza kuwa kuna uhusiano wa asili kati ya kaa na mikoko. Kaa huchimba mashimo yanayolegeza udongo na kusaidia mizizi ya miche ya mikoko kushika. Mikoko nayo hutoa chakula na makazi kwa kaa. “Kwa hiyo, ni manufaa ya pande mbili au uhusiano wa kutegemeana,” anaeleza.
“Mikoko ndiyo uti wa mgongo wa mikondo hii ya maji. Inazuia mashapo, kuchuja uchafuzi na kutoa hifadhi kwa kaa na samaki wadogo. Bila mikoko, ufukwe ungeporomoka tu,” anasema.
“Ukitembelea mkondo wao wa maji na kuona jinsi wanavyosimamia vizimba kwa umakini, na jinsi walivyounganisha mradi huo na urejeshaji wa mikoko, inavutia sana. Wanachohitaji ni mafunzo zaidi na msaada wa kiufundi ili kuufanya mradi uwe endelevu kwa muda mrefu.”

Wanawake wanaoongoza katika uchumi wa buluu
Licha ya kuwa na kiwango kidogo, yaani vizimba 30 tu vinavyotumika kwa sasa, wanawake wa Jomvu Creek wanaona mradi wao kama mfano kwa wengine. “Sisi hatupati tu kipato,” anasema Chirima. “Tunaonyesha kwamba wanawake wanaweza kuongoza katika uchumi wa buluu.”
Njia ya mbao itakapofunguliwa, wanapanga kupokea wanafunzi, watalii na watafiti. Ziara za kuongozwa zitaonyesha makazi ya kaa, ikolojia ya mikoko na nafasi ya wanawake wa eneo hilo katika uhifadhi. Wanatarajia pia kuuza kazi za mikono, vyakula vya baharini na miche ya mikoko kwa wageni.
Kudumisha na kupanua mradi kutahitaji mtaji, mafunzo na masoko ya uhakika. Nusu ya vizimba vinahitaji kubadilishwa sasa; vifaa vipya bora vya kujikinga na kamba ni vya gharama kubwa. Hata hivyo, wanawake hao wanaendelea kuwa na matumaini.
“Tulipoanza, watu walitucheka,” anakumbuka Baya. “Sasa, watu hao hao wanakuja kuuliza jinsi ya kujiunga nasi.”
Mpango wa Jomvu ni sehemu ya harakati pana ya wanawake kujitokeza katika sekta ya uvuvi nchini Kenya. Mercy Mghanga, mwanzilishi wa mtandao wa Coastal Women in Fisheries Entrepreneurship, na mwenyekiti wa muda mrefu wa kitengo cha usimamizi wa fukwe katika eneo hili, ameshuhudia kikundi hicho kikikua.
“Kwa miaka mingi, wanawake walikuwa uti wa mgongo wa mnyororo wa thamani katika uvuvi; wakikausha, kukaanga na kuuza samaki, lakini hawakutambuliwa kama wajasiriamali,” anasema Mghanga. “Utamaduni uliwazuia kumiliki boti au kuchukua mikopo bila idhini ya waume zao.”
Shirika lake sasa linaunganisha zaidi ya wanawake 2,000 katika ukanda wa Pwani, likisaidia upatikanaji wa mikopo, mafunzo na masoko. “Jomvu Women in Fisheries and Culture ni mfano mzuri wa kile wanawake wanachoweza kufanya wakipewa fursa,” anasema.
Mghanga anasisitiza kuwa elimu na ushirikiano vinakwenda pamoja. “Kama mwanamke ameolewa akiwa na miaka 16, je, atarudi shule?” anauliza. “Lazima tumpe njia nyingine za kujifunza, kujipatia kipato na kuongoza.”
Iwapo ufugaji wa kaa unaboresha moja kwa moja mfumo wa ikolojia wa Jomvu Creek, bado haijulikani kwa uhakika, lakini matokeo yasiyo ya moja kwa moja tayari yanaonekana. Miche ya mikoko inashika mizizi, ufukwe unaimarika na wakazi zaidi wanazungumzia uhifadhi.
Wanawake hawa wamekuwa walinzi wa eneo hilo, wakipanda mikoko, kuokoa vizimba vilivyokwama na kuwafundisha watoto wao kuhusu uvuvi endelevu. Kwao, uhifadhi si wazo la kinadharia; umekuwa uhalisia wa maisha yao, uliounganishwa na riziki zao.
“Ikiwa mikoko itakufa, kaa watatoweka,” anasema Baya. “Na kaa wakitoweka, biashara yetu nayo itakufa.”
Maji yanapoongezeka katika Jomvu Creek, mawimbi hupiga taratibu kwenye mizizi ya mikoko. Wanawake hao, wakiwa pekupeku, huingia majini kukagua vizimba vyao. Kazi ni ya matope, ya polepole na wakati mwingine ya kukatisha tamaa. Lakini katika kila kaa wanayemnenepesha na kila mche wa mikoko wanaoupanda kwenye kingo za matope, wanaona ahadi ya mustakabali ambapo mikono ya wanawake inaongeza riziki na kulinda uhai katika pwani ya Kenya.
Picha ya Bango: Picha ya kaa (Scylla sceratta). Picha na titi-uu kupitia iNaturalist (CC BY-NC 4.0)
Taarifa hii ilichapishwa hapa kwa mara ya kwanza kwa Kiingereza mnamo tarehe 11/02/2025.