- Kampeni za uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia lazima ziende sambamba na maboresho ya gridi.
- Tangu kuanzishwa kwa mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali ya Tanzania imeongeza kasi ya kuunganisha umeme kutoka kaya 500 hadi milioni 1.5 kwa mwaka.
- Ongezeko la matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia lazima yaende sambamba na maboresho ya mfumo wa usambazaji wa umeme.
- Dunia haiwezi kushinda mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi iwapo kila taifa, hasa yaliyo hatarini zaidi, hayatanufaika na maendeleo endelevu.
Hii ni sehemu ya pili ya habari kuhusu Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, mpango uliozinduliwa kwa lengo la kuokoa misitu. Soma sehemu ya kwanza hapa.
Kwa mujibu wa Jiolojia Mkuu katika Wizara ya Nishati, Ngereja Mgejwa, ili kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya majiko ya umeme ya kisasa, serikali ya Tanzania inaendesha kampeni za mawasiliano nchini kote inayogharimu $51,181,102 (TSh bilioni 130), ambazo hadi sasa zimewafikia takribani wananchi milioni 3.2 wa mikoa yote.
Katika kampeni hiyo jamii zinafikiwa kupitia vyombo vya habari vya matangazo, ujumbe mfupi wa simu (SMS), mitandao ya kijamii na mikutano ya hadhara kwa kutoa elimu kwa wananchi ili waelewe umuhimu wa kupikia nishati na namna wanavyoweza kuutumia.
Kampeni imebuniwa ili kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuongeza uelewa wa umma kuhusu faida za kiafya, kimazingira na kiuchumi za kupikia nishati safi, kupinga taarifa potofu kuhusu teknolojia za nishati safi, na kuhamasisha kaya kuacha matumizi ya mkaa na kuni pale kunapokuwa na mbadala.
Mgejwa aliiambia Mongabay kwamba serikali inashirikiana na taasisi za utafiti zikiwemo Modern Energy Cooking Services (MECS) na Tanzania Agricultural Research Institute (TARI) kuchunguza uwezekano wa kutengeneza majiko hayo ndani ya nchi ili kupunguza gharama za ununuzi.
Anasema ushirikiano huo unalenga kupunguza utegemezi wa vifaa vinavyoagizwa kutoka nje, kushusha gharama za uzalishaji, kuboresha teknolojia ili zilingane na mila na desturi za upishi wa ndani, na kujenga uwezo wa kitaalamu nchini, mambo ambayo ni muhimu katika kufikia malengo ya mkakati kuhusu gharama nafuu na upanuzi wa matumizi.
Aidha Mgejwa anakiri kuwa gharama kubwa za majiko hayo na vyombo vyake maalum vya kupikia bado ni kikwazo kikubwa. Anatambua kuwa kwa sasa yanauzwa kati ya $59 na $138 (TSh150,000 na TSh350,000), huku masufuria yakigharimu $23.6 hadi $29.5 (TSh60,000 hadi TSh75,000) kwa seti bei, ambazo kaya zenye kipato cha chini haziwezi kumudu.
Ili kukabiliana na hali hiyo, anasema serikali inaandaa mapendekezo ya msamaha wa kodi na ruzuku kwa vipuri vinavyoagizwa kutoka nje, badala ya kununua bidhaa zilizokamilika, ili kushusha bei za rejareja bila kudhoofisha masoko ya ndani.
Aidha, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, serikali inatoa ruzuku mahsusi kwa baadhi ya wasambazaji binafsi wa majiko, kuwawezesha kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya punguzo. Lengo ni kushusha bei ya rejareja ya majiko ya umeme ili isizidi $19.6 (TSh50,000), lengo likiwa kuziwezesha kaya zenye kipato cha chini kumudu gharama za manunuzi ya papo hapo au mkopo.
Upatikanaji wa umeme
Kwa mujibu wa Neema Mbuja, Kaimu Mkuu wa Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Nishati, tangu kuanzishwa kwa mkakati huo waliongeza kasi ya kuunganisha umeme kutoka kaya 500 hadi milioni 1.5 kwa mwaka. Anasema mkakazi uliopo ni kuhakikisha kufikia mwaka 2030, kaya milioni 8.5 ziwe zimeunganishwa na umeme, malengo yakiwa kuzifikia kaya zote milioni 14.5.

Ingawa upanuzi wa umeme si sehemu rasmi ya mkakati wa upishi safi, Mgejwa anasema serikali inajitahidi kuongeza kasi ya uunganishaji wa umeme ili kuweka mazingira wezeshi yatakayowahamasisha wananchi kuhamia teknolojia za upishi wa umeme pale umeme unapopatikana.
“Serikali inaharakisha uunganishaji wa umeme vijijini kupitia programu za kitaifa za umeme. Ingawa umeme wenyewe hauko chini ya mkakati wa upishi safi, upatikanaji wake unahamasisha kaya kutumia teknolojia za kisasa za kupikia, ikiwemo majiko ya umeme,” anasema.
Anabainisha kuwa upatikanaji wa umeme umeboreshwa kwa kiasi kikubwa. Kati ya Novemba 2020 na Februari 2025, serikali iliunganisha vijiji 4,071 kwa gharama ya $627,165,353.69 (TSh trilioni 1.593) wakati katika mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya kaya 640,747 ziliunganishwa na umeme nchini.
“Hatua inayofuata, baada ya kufikisha umeme katika vijiji vyote, ni kuupanua hadi vitongoji,” anasema Mgejwa. Hadi sasa, vitongoji 33,657 kati ya 64,359 sawa na asilimia 52.3 vimeunganishwa na umeme.
Gharama za kusambaza umeme
Kwa mujibu wa ripoti ya sekta ya nishati ya mwaka 2024, Tanzania inapanga kuwekeza takribani $ bilioni 12.9 ifikapo mwaka 2030 ili kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa umeme na kupanua mitandao ya usafirishaji na usambazaji.
Uwekezaji huu unaungwa mkono na washirika wa maendeleo na sekta binafsi, ikiwemo taasisi kama Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya, wazalishaji binafsi wa umeme pamoja na fedha za ndani. Lengo ni kuharakisha upatikanaji wa umeme nchini kote na kuboresha uhakika wa huduma wakati mahitaji ya umeme yanaendelea kuongezeka kutoka kwa kaya, viwanda, na matumizi mapya yanayoibuka kama upishi wa umeme.
Uhakika wa gridi: Matumaini na tahadhari
Kwa mujibu wa Mgejwa, Tanzania sasa ina mfumo wa umeme wenye uwezo wa kuhimili matumizi ya kupikia, huku uwezo wa kitaifa wa uzalishaji wa umeme ukifikia megawati 3,091.7. Mahitaji ya sasa ni megawati 1,800. Ongezeko hilo linatokana na uwekezaji mkubwa katika miradi ya uzalishaji wa umeme ukiwemo ule wa Bwawa la Julius Nyerere.
Hata hivyo, wataalamu wa nishati wanaonya kuwa uwezo wa uzalishaji pekee hautoshi kuhakikisha uhakika wa upatikaji wa huduma ya umeme katika ngazi ya kaya.
Matthew Josephat Matimbwi, Katibu Mtendaji wa TAREA, anasema kuwa ingawa mitambo ya kuzalisha umeme inaweza kutoa umeme wa kutosha kitaifa, mifumo ya usambazaji kama transfoma na njia za umeme bado ni dhaifu katika maeneo mengi.
Hali hiyo, anasema, inasababisha kukatika kwa umeme na kuyumba kwa viwango vyake, jambo linalopunguza imani ya wananchi katika upishi wa umeme.
“Tunakabiliwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara hata kwa mahitaji ya sasa. Transfoma nyingi ni kongwe na ndogo, na njia za usambazaji zimelemewa. Ikiwa matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia yataongezeka kwa kasi bila kuboresha mfumo wa usambazaji, upatikanaji wa umeme wa uhakika utakuwa kitendawili,” anasema.
Anaongeza kuwa ingawa kampeni za uhamasishaji wa upishi wa umeme ni muhimu, lazima ziende sambamba na maboresho ya gridi, vinginevyo, kukatika kwa umeme mara kwa mara kutazisukuma kaya kurudi kwenye mfumo wa kupikia mkaa na kuni.
Mafunzo kutoka nchi nyingine Afrika
Matimbwi anasema Tanzania inaweza kujifunza kutoka nchi jirani ambazo muundo wa sera ulisaidia kupanua matumizi ya nishati safi kupikia bila kuharibu masoko.
Anasema nchini Uganda, msambazaji wa umeme, Umeme Limited alianzisha tozo maalum ya nishati ya kupikia, inayoruhusu kaya kutumia takribani uniti 30 za umeme kwa mwezi kwa bei nafuu. Baada ya kiwango hicho kufikiwa, mita janja hurudisha watumiaji kwenye tozo za kawaida.
Nchini Tanzania, serikali inatoa majiko ya umeme kupitia mikopo inayolipwa kupitia bili za umeme kwa tozo za kawaida, mpango ambao wananchi wanaona kama hautoi motisha ya kutosha ya kuwafanya waachane na mkaa na kuni. “Huo si ubunifu, ni ukopeshaji wa kawaida tu,” anasisitiza Matimbwi wakati analinganisha utaratibu unaofanywa na Uganda na wa Tanzania.

Pia anaangalia mfano wa Rwanda, ambako serikali hutoa ruzuku ndogo lakini za muda mrefu, zilizobuniwa kulinda masoko badala ya kuyaharibu. “Ruzuku zimeundwa kwa namna ambayo hata zinapopunguzwa, wananchi wanaendelea kutumia teknolojia,” anasema.
Kwa upande mwingine, anataja Kenya kama onyo. Ingawa matumizi ya gesi ya LPG yaliongezeka kwa kasi, kupanda kwa gharama za kujaza mitungi na changamoto za kumudu gharama kulizifanya kaya nyingi zenye kipato cha chini kurejea kutumia mkaa. Kwa mujibu wa Matimbwi, uzoefu wa Kenya unaonyesha hatari ya kuzingatia upatikanaji wa teknolojia bila kuhakikisha uwezo wa watu kumudu kwa muda mrefu.
Kwa sababu hiyo, TAREA inaunga mkono motisha za serikali pale tu zinaposaidia kujenga masoko imara na endelevu. “Hatupaswi kuangalia tu kuongeza idadi leo,” anasema Matimbwi. “Ni lazima tufikirie nini kitatokea pale ruzuku zitakapoondolewa.”
“Serikali inapaswa kuweka ruzuku kwa namna ambayo itahakikisha kaya zinaendelea kutumia suluhisho hilo hata baada ya motisha kuondolewa,” anaongeza.
Sarah Pima, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utu na Mazingira (HUDEFO), anasema Tanzania lazima ielekee kwenye uzalishaji wa ndani ili kuendeleza teknolojia yake yenyewe.
“Majiko haya lazima yatengenezwe nchini ili yauzwe kwa bei nafuu. Kwa sasa yanawafikia wananchi wa kipato cha kati na cha juu pekee, huku watumiaji wa mkaa wa kipato cha chini wakiachwa nyuma,” anasema.
Anaongeza kuwa majiko yanapaswa kuuzwa kwa bei zinazolingana na majiko ya mkaa, gesi au mafuta ya taa ili familia za kipato cha chini ziweze kumudu.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kampuni ya Polistive Ayin Ltd, Atukuzwe Nkya, anaiomba serikali iondoe kodi kwenye majiko hayo ili kuwawezesha wananchi kumudu gharama, akibainisha kuwa kaya nyingi za vijijini haziwezi kumudu jiko la $59 (TSh150,000) au kulikopa kwa $138 (TSh350,000).
Pia anapendekeza serikali ianzishe tozo maalum za umeme kwa watumiaji wa majiko ya umeme, kama ilivyofanyika Uganda, na kusisitiza umuhimu wa kampeni imara za elimu kwa umma ili kuondoa hofu na taarifa potofu.
Uzoefu wa kaya kuhusu majiko ya umeme
Katika eneo la Masaki, Jijini Dar es Salaam, Mariam Mohamed alianza kutumia jiko la umeme la kisasa Oktoba 2024 baada ya kulipata kwa mkopo kutoka kampuni ya ECOA.
Tangu aanze kutumia jiko hilo kwa takribani mwaka mmoja sasa, gharama za nishati ya kupikia zimepungua kwa takribani $7 (TSh18,000) kwa mwezi, tofauti na hapo awali alipokuwa akitumia jiko la gesi na mkaa. Kwa Mariam, mabadiliko hayo si ya kiuchumi tu bali pia kwa afya.
“Jiko hili ni salama kwa afya yangu kwa sababu halitoi moshi, na linapika haraka kuliko gesi au kuni. Awali nilikuwa natumia jiko la kawaida la umeme na nilikuwa natumia $20 (TSh50,000) kwa mwezi, lakini sasa ni $13 TSh32,000). Naokoa $7 (TSh18,000,” anasema.
Hata hivyo, Mariam analalamika kuwa gharama za majiko haya ni kubwa sana, takribani mara 50 zaidi ya jiko la mkaa la ukubwa wa kati, linalouzwa kwa karibu $2 (TSh5,000) tu. “Nilipatiwa jiko la sahani moja kwa mkopo wa $110 (TSh275,000) kwa mwaka mzima, nikilipa $2 (TSh5,000) kila wiki baada ya kutoa amana ya $16.4 (TSh41,000). Hii ni ghali sana,” anasema.
Katika wilaya ya Kinondoni, Kelvin Mlaki, mfanyakazi wa benki, anasema alinunua jiko lake la umeme la sahani moja miezi sita iliyopita kwa $76 (TSh170,000), bei ambayo, anasema, ni ya watu wa kipato cha juu na kati pekee.
“Tangu nianze kutumia jiko hili, sioni tena haja ya kutumia mkaa au gesi kwa sababu linapika aina zote za chakula kwa haraka na kwa kutumia umeme mdogo, lakini sidhani kama mtu wa kijijini anaweza kumudu,” anasema.
Kelvin hutumia takribani $4 (TSh10,000) kwa mwezi kwa ajili ya kupikia, punguzo kubwa ikilinganishwa na $22 (Sh55,000) aliyokuwa akitumia awali wakati anatumia gesi kupikia.
Mteja mwingine, Beatrice Shayo, mkazi wa Mapinga, Dar es Salaam, anaeleza kuwa majiko ya umeme nafuu yanahitaji vyombo maalum vya kupikia ambavyo ni ghali zaidi kuliko vya kawaida.
“Vyombo hivi vya induction hugharimu angalau $30 (TSh75,000) kwa seti. Nilivyopewa pamoja na jiko ni vya lita tatu, nne na tano, vifaa ambavyo ni vikubwa sana kwa mtu mmoja lakini nalazimika kuvitumia kwa sasa kwa sababu siwezi kununua vingine, nina majukumu mengine,” anasema.
Kutoka wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Linda James anasema mifumo ya mikopo ni mzigo mkubwa. “Ninalipa $3 (TSh7,000) kila wiki au $12 (TSh30,000) kwa mwezi. Kulipa zaidi ya $120 (TSh300,000) kwa mwaka kwa jiko la sahani moja ni gharama kubwa sana. Wakati mwingine nikishindwa kulipa, jiko linazimwa kwa wiki nzima,” anasema.
Kupanua upatikanaji katikati ya vikwazo vya kiuchumi
Katarina Aloyce, ambaye ni Meneja wa Kampuni ya Sustainable Energy Services Company (SESCOM), inayouza majiko hayo papo kwa papo na kwa mkopo, anasema gharama za juu za majiko hayo zinasababishwa na ushuru mkubwa wa bandarini kwa sababu bidhaa hizo hazina ruzuku ya serikali isipokuwa pale wafadhili wanapotoa msaada.

“Sasa tunauza majiko ya shinikizo ya lita sita kwa $64 (TSh160,000), ya lita nane kwa $100 (TSh250,000), na air fryer ya lita saba kwa $80 (TSh200,000) kwa sababu hatukupata ruzuku,” anasema.
Mwaka 2023, walipata ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa Cook Fund na kushusha bei hadi $47.2 (TSh120,000) katika baadhi ya maeneo kwa muda, lakini vikwazo vya mikopo vinaendelea kuzitenga kaya zenye kipato cha chini.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kampuni ya Polistive Ayin Ltd, Atukuzwe Nkya, anasema ushuru wa bandarini unaongeza gharama kubwa zinazofanya majiko kuwa ghali. “Gharama za bandarini huongeza thamani ya kila mzigo kwa takribani asilimia 32. Hii humgusa moja kwa moja mnunuzi wa mwisho,” anasema.
Anasema pia kuwa kukatika kwa umeme na kutoshushwa kwa gharama za umeme kunawakatisha tamaa. Katika mikoa kama Mwanza, kukatika kwa umeme mara kwa mara huwakatisha tamaa wateja, huku baadhi wakisubiri bei za umeme zipungue pindi bwawa la umeme wa maji litakaposhusha tozo za kitaifa.
Anasema walianza kuuza majiko ya umeme mwaka 2019 na hadi sasa wamefikia wateja 8,000 katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Dar es Salaam na Mbeya. Bei zao zinaanzia $48 hadi $140 ( (TSh120,000 hadi TSh350,000), na wateja wanaweza kununua kwa fedha taslimu au kwa mkopo. Kwa kaya za kipato cha chini, kampuni hiyo hutoa mikopo kupitia vikundi vya akiba vya VICOBA.
Akizungumza wakati wa kikao cha ufunguzi wa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) Novemba 2025 mjini Belém, Brazil, Katibu Mtendaji wa UN Climate Change, Simon Stiell, alisisitiza kuwa ili kufanikiwa, mpito wa dunia kuelekea nishati safi lazima uwe wa usawa.
Alionya kuwa dunia haiwezi kushinda mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi iwapo kila taifa, hasa yaliyo hatarini zaidi, hayatanufaika na maendeleo endelevu.
“Tutashinda vita dhidi ya changamoto ya tabianchi pale tu ambapo watu wote, katika mataifa yote, watapata sehemu yao ya haki ya manufaa makubwa ya maendeleo endelevu,” alisema.
Picha ya bango: Shughuli za binadamu zinaendelea kuwa kichocheo kikubwa cha ukatazaji miti hapa nchini. Picha na Jenifer Ngilla.