- William Ruto alishinda uchaguzi wa urais wa Kenya mwaka 2022 kwa kampeni iliyojumuisha ahadi ya kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032. Kadri nchi inavyokaribia kipindi kingine cha uchaguzi, wachambuzi na wataalamu wa mazingira wanaanza kuhoji ni kwa kiwango gani ahadi hiyo imetekelezwa.
- Kwa mujibu wa Waziri wa Mazingira, Deborah Barasa, hadi sasa, ni takribani miti bilioni 1.5 imepandwa. Licha ya kuwepo kwa changamoto zinazohusiana na mipango, ufuatiliaji na ufadhili, Barasa amesema Kenya bado ina uwezo wa kufikia lengo la kupanda miti bilioni 15.
- Ameongeza kuwa umiliki wa jamii, utunzaji wa muda mrefu na uhai wa miti ni mambo muhimu zaidi kuliko idadi ya miche inayopandwa. Amesisitiza kuwa kampeni ya upandaji miti “inalenga kujenga utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira.”
- Waziri Barasa alizungumza na Mongabay katika mahojiano binafsi yaliyofanyika sambamba na tukio la kuadhimisha urithi wa Wangari Maathai, mwanaharakati wa mazingira kutoka Kenya na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2004. Maathai alianzisha harakati muhimu zilizowahusisha wanawake katika upandaji miti kama njia ya kupambana na ukataji miti.
Mwaka 2022, William Ruto alipochaguliwa kuwa rais wa Kenya, aliahidi kuwa serikali yake itapanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032. Wafuatiliaji wengi waliiona ahadi hiyo kuwa ya kishujaa na yenye malengo makubwa, ahadi inayohitaji mipango ya pamoja, mifumo thabiti ya ufuatiliaji, ufadhili endelevu, pamoja na usimamizi wa muda mrefu kwa kiwango kikubwa sana.
Kulingana na makadirio ya Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Misitu, takribani miti bilioni 1.5 imepandwa hadi sasa. Katika mahojiano ya hivi karibuni na David Akana wa Mongabay Jijini Nairobi, Waziri wa Mazingira wa Kenya, Deborah Barasa, alisema kwamba nchi bado inaweza kufikia lengo la kupanda miti bilioni 15. Hata hivyo, wakati Waziri anatoa kauli hiyo, ripoti za hivi karibuni za vyombo vya habari kuhusu kampeni ya upandaji miti zimeonyesha mpango huo unakabiliwa na changamoto kubwa. Miongoni mwa changamoto hizo ni upungufu wa fedha, uhaba wa wafanyakazi na miche ya miti pamoja na hali ya ukame iliyodumu kwa muda mrefu.
Baadhi ya wataalam wa uhifadhi wanasema kwamba kupanda miti siyo suluhisho la changamoto zote, na kwamba bila mifumo thabiti ya ufuatiliaji na uwajibikaji ulio wazi, juhudi hizi zinaweza kubakia tu kwenye kuhesabu miche badala ya kurejesha mifumo ya ikolojia.
Barasa alikiri kwamba kazi hiyo ni nzito, lakini akasisitiza kuwa utashi wa kisiasa na msukumo mkubwa kutoka ngazi za juu za Serikali, pamoja na kitendo cha jamii kuwa na umiliki wa kweli wa kampeni hiyo, vinaweza kuifanya ahadi hiyo iwe na matokeo endelevu.
Barasa alitoa maelezo haya wakati wa sherehe za kuadhimisha urithi wa Wangari Maathai, mwanaharakati wa mazingira kutoka Kenya ambaye kazi yake kwenye jamii ilisaidia kuleta mtazamo mpya kwenye masuala ya utunzaji wa mazingira nchini na kumfanya ashinde Tuzo ya Amani ya Nobel. Mnamo Desemba 10, 2025, maafisa wa serikali waliungana na wawakilishi wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) na World Resources Institute Africa kusherehekea urithi wa Maathai.
Katika miongo ya hivi karibuni, kampeni za kuhamasisha nishati mbadala zimekuwa pia sehemu muhimu ya ajenda ya mazingira ya Kenya. Nchi hii inajitofautisha miongoni mwa nchi za Afrika kwa kasi ya kueneza nishati mbadala. Kulingana na Mamlaka ya Kimataifa ya Nishati, nishati mbadala sasa inachangia takribani asilimia 90 ya umeme wa nchi. Barasa alisema anaamini Kenya inaweza kufikia hatua ambayo umeme wote utakuwa unatokana na nishati mbadala ifikapo mwaka 2030 na alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mchakato huo unazingatia usawa na unakuwa na manufaa ya kweli kwa Wakenya.
Mahojiano yafuatayo yamehaririwa kidogo kwa urefu na uwazi.

Mongabay: Imepita miaka 20 tangu Wangari Maathai aliposhinda Tuzo ya Amani ya Nobel. Kwa nini ilikuwa muhimu kwa serikali ya Kenya kuwakilishwa katika maadhimisho hayo?
Deborah Barasa: Kwa sababu Wangari Maathai ni chanzo cha msukumo. Yeye ni shujaa. Ni muhimu tufuatilie na kuhakikisha kwamba yale aliyowahamasisha Wakenya kuyafuata yanaendelea hadi leo. Sasa hivi, rais anazungumzia kuhusu kupanda miti bilioni 15. Lakini hiyo kiuhalisia inamaanisha nini? Siwezi kupanda miti bilioni 15 peke yangu. Wewe pia huwezi kupanda peke yako.
Tunachohitaji ni jamii kumiliki kampeni hii. Tunahitaji jamii kutoka nje na kuunga mkono harakati za upandaji miti. Na hili si tu kuhusu kupanda miti. Ni kuhusu kujenga utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira.
Hicho ndicho Mheshimiwa Wangari Maathai alichosimamia. Kwa hiyo, kazi hii inalingana kabisa na kile alichoamini. Tunafurahi sana. Tunajivunia kwamba alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel. Na tunajiuliza ni kwa namna gani tutaendelea kutumia urithi wake na sauti yake kujenga utamaduni huohuo na kulinda mazingira yetu.
Mongabay: Unasemaje kuhusu vipaumbele vya mazingira vya Rais Ruto?
Deborah Barasa: Kwanza ni kupanda miti bilioni 15. Pili ni kuimarisha uchumi. Tumepiga hatua katika kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki lakini pia kuzuia plastiki katika maeneo yanayolindwa, na sasa tumepanua na tunasisitiza uwajibikaji wa wazalishaji.
Mongabay: Hadi sasa ni miti mingapi imepandwa?
Deborah Barasa: Tayari tumepanda takribani miti bilioni 1.5, lakini sasa kipaumbele ni kuzalisha miche zaidi na kuhakikisha kwamba jamii zinashirikishwa kikamilifu katika upandaji na utunzaji wake. Vipaumbele vingine ni pamoja na kuondoa asbestos, kuelimisha watu kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na ujereshaji mkubwa wa mifumo ya ikolojia. Mwaka ujao, Kenya itakuwa mwenyeji wa mikutano kadhaa muhimu ya kimataifa, ukiwemo kuhusu REDD+, uongozi wa misitu katika mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko wa udongo chini ya UNCCD, na bahari. Yote haya yanaonyesha shauku ya rais ya kulinda mazingira kwa vizaji vijavyo.

Mongabay: Niruhusu nikurudishe kwenye lengo la kupanda miti bilioni 15. Ni la kishujaa sana. Linafadhiliwa vipi, na una uhakika gani linaweza kufanikiwa?
Deborah Barasa: Fedha zinatoka vyanzo mbalimbali: Hazina ya Serikali, sekta binafsi, jamii, na washirika wa maendeleo. Huu ni wito kwa Wakenya wote. Wakati wa siku ya Mazingira (Oktoba 10 ni siku ya mapumziko ambayo ilitolewa maalum kwa utunzaji wa mazingira na shughuli nyingine za kulinda na kurejesha asili). Tunawahimiza wananchi kupanda miti ya matunda katika shule za msingi. Mti mmoja wa matunda unaweza kulisha watoto wengi, hivyo tunashughulikia usalama wa chakula huku tukirejesha mifumo ya ikolojia.
Pia tunazingatia maeneo yenye maji, yale yaliyo na ukame kwa kiasi kikubwa na yale ambayo yana ukame kidogo na maeneo ya misitu. Wazo ni kulinganisha upandaji miti katika maeneo tofauti ya ikolojia. Wakati huohuo, hii inaunga mkono ajenda ya rais ya mabadiliko ya kiuchumi kutoka chini kwenda juu: kutengeneza ajira kupitia kilimo-misitu, REDD+ (Kupunguza uchafuzi wa hewa kutokana na ukataji na uharibifu wa) na misitu ya kibiashara hasa kwa vijana.
Mongabay: Kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki Kenya mara nyingi kunatajwa kimataifa. Mpango huu kweli unafanya kazi?
Deborah Barasa: Unafanya kazi. Kama ungetutembelea miaka kadhaa iliyopita, ungeona uchafuzi mkubwa zaidi. Sasa mazingira ni safi na yenye afya. Lakini lazima tuimarishe utekelezaji na utii wa sheria. Kwa sababu mipaka ni yetu ni mipana, plastiki bado zinaweza kuingia nchini. Ndiyo maana Kenya inakuwa sauti yenye nguvu kimataifa kuhusu matumizi ya plastiki. Hizi ni changamoto zinazohusiana, na zinahitaji suluhisho la kimataifa.
Mongabay: Katika nchi nyingi, Wizara za Mazingira hupata ugumu kupata fedha za umma. Imekuwa rahisi kwa kiasi gani kwako kupata msaada kutoka Hazina?
Deborah Barasa: Utashi wa kisiasa ni kila kitu. Unapokuwa na uungwaji mkono kutoka ofisi ya juu kabisa, mambo huenda kwa urahisi zaidi. Kwa miaka mingi, sekta ya misitu ilikuwa imesahaulika. Lakini sasa tuna rais anayeelewa mchango wake katika uchumi na upatikanaji wa ajira. Anatetea upatikanaji wa rasilimali, na hilo limeleta tofauti kubwa. Kitaifa, tunahamasisha rasilimali. Lakini kimataifa, fedha za masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi bado ni changamoto. Nchi za Kusini mwa Dunia zina nafasi ndogo ya kifedha na vipaumbele vingi vinavyoshindana. Kwa kuwa mazingira ni suala la dunia nzima, tunahitaji msaada hasa kutoka kwa nchi zinazotoa hewa ya ukaa kwa kiwango kikubwa ili kurejesha mifumo ya ikolojia na kulinda bayoanuai.
Mongabay: Mnahakikishaje uhamaji wa kuingia kwenye matumizi ya nishati safi unakuwa wa haki na unaowanufaisha Wakenya wa maisha ya chini?
Deborah Barasa: Tunatumia takwimu na majukwaa ya kidijitali kufanya maamuzi. Tunafuatilia kiwango cha upatikanaji, kutambua mapengo, na kuelekeza msaada pale unapohitajika. Nishati mbadala tayari inachangia zaidi ya asilimia 90 ya umeme wetu. Lengo ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030, lakini kwa njia shirikishi na yenye usawa.
Picha ya Bango: Wanachama wa kikundi cha kusaidiana cha Tulinde Mikoko wakipanda miti ya mikoko katika Kaunti ya Mombasa, Kenya. Picha na AP Photo/Gideon Maundu.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kingereza mnamo tarehe 26/01/2026