- Hifadhi ya mwisho ya barafu ya Mlima Kenya, maarufu kama Ziwa Lewis, inakaribia kufifia, kulingana na Lewis Pugh, Msimamizi wa Mradi wa Bahari katika Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP).
- Muda fulani katika historia ya Jamii ya Wagikuyu, barafu iliyokuwa mlimani (ira) ilitumika kuwapaka vijana watahiriwa wa kiume na wa kike kingoni mwa mito.
- Tathmini za hivi karibuni sasa zinaonyesha kuwa Mto Sagana umekuwa ukipitia mabadiliko makubwa ya mtiririko yanayosukumwa zaidi na mifumo ya mvua, huku uchunguzi wa eneo ukionyesha kuwa maji yalikuwa yakipungua baada ya viwango vya juu awali.
- Pugh alionja kile jamii zinazoishi chini ya milima huvumilia kutokana na kupungua kwa maji kwenye mito wanayoitegemea kwa kilimo, haswa kama mojawapo wa maeneo yanayokuza vyakula kwa wingi nchini.
Hii ndiyo nakala ya kwanza katika Mfululizo wa Mongabay – Kinachotokea mlimani hakisalii mlimani. Soma nakala ya pili hapa.
Juu ya vilele vya Mlima Kenya, ambako barafu iliwahi kuonekana kama ya milele, na mito kutiririka kwa uhakika kuelekea mabonde yaliyojaa uhai, kuna ishara za hatari zinazoonekana wazi leo.
Kupungua kwa barafu za mlima huu wa kihistoria hakumaanishi tu kupotea kwa mandhari ya asili, bali pia kunafungua ukurasa mpya wa changamoto kwa mazingira, mito, na jamii zinazoutegemea.
Safari ya Lewis Pugh, Msimamizi wa Mradi wa Bahari katika Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP), hadi kwenye barafu za mwisho za Mlima Kenya, inatoa taswira ya kusikitisha ya athari halisi za mabadiliko ya tabianchi, zinazotoka juu ya mlima na kushuka hadi mashambani, misituni na vijijini, ambako maji, imani na maisha yenyewe yako hatarini.
Pugh, aliyeshikilia nafasi hiyo katika shirika la UNEP tangu mwaka 2013, aliwasili nchini Kenya kwa matumaini kuwa uwezo wake wa kutoa hotuba zenye mvuto, ulioimarishwa kwa miaka 27 iliyopita, ungezivutia hisia za dunia, kwa namna fulani, kwenye athari mbaya za ongezeko la joto duniani katika eneo la Mlima Kenya.

Huku ulimwengu ukijiandaa kwa sikukuu ya Krismasi, kati ya tarehe 4 hadi tarehe 8 mwezi Desemba 2025, Pugh aliparaga kupitia miamba iliyomikali ya volkeno, baadhi ikiwa na umri wa miaka milioni 4, hadi urefu wa mita 4,985 (futi 16,355) juu ya kilele cha Lenana. Lengo lake kuu lilikuwa kuogelea katika Ziwa Lewis.
Haijalishi uimara wa mkweaji milima, kupanda kwa Kilele cha Lenana, kilichoko kwenye mwinuko sawa na Himalayas, daima huja na hatari ya magonjwa ya mlima. Uzoefu wa kukwea milima na kuogelea baharini kwa Pugh kuliambatana na mvua fupi za mwezi Novemba hadi Desemba wakati hali ya joto mchana ni kati ya nyuzi 5-15, na hushuka kati ya nyuzi 0-4 ifikapo usiku.
Kwenye urefu wa mita 3,000, theluji na baridi kali hujitokeza usiku, huku joto kwenye kilele kikishuka hadi chini ya nyuzi sifuri, kikiweka mlima katika hali ya ukimya na baridi isiyopitisha. Katika baadhi ya sehemu za kupanda, shughuli huanza saa nane alfajiri, wakati ardhi yenye miamba mikali imefunikwa na theluji.
Pugh sio mkweaji mlima wa kawaida. Alikuwa mtu wa kwanza kuogelea kwa umbali mrefu kwenye kila bahari na pia alikuwa mwanzilishi wa kuogelea kwa mara ya kwanza kuvuka Ghuba Kaskazini. Aidha alikuwa mtu wa kwanza kuogelea na kuvuka mkono wa bahari wa Uingereza. Hata aliogelea chini ya barafu ya Antarctic.
Wakati Pugh alipojitosa katika Ziwa Lewis, nia yake kuu ilikua ni kuogelea kwenye barafu na pia kushuhudia kupungua kwa ziwa hilo. Ingawaje ilionekana kuwa rahisi, ilimlazimu Pugh ajadiliane na wasio waaminifu kabla ya kufikia bonde la Teleki chini ya barafu za Lewis na Tryndal. Pana maziwa 12 yenye barafu juu ya mlima, lakini yale maarufu zaidi ni Lewis, Gregory, Alice, Tryndal na Darwin. Pugh aligutushwa na hali ya barafu katika kilele cha Lenana.
“Nimetoka tu kuukwea mlima nikitumai kuogelea chini ya barafu ya Ziwa Lewis, ili kuangazia namna barafu za mwisho za Afrika zinavyotoweka, na kwa nini barafu iliosalia ulimwenguni ni ya thamani sana,” aliiweka taarifa hii kwenye mitandao yake ya kijamii akiwa juu ya mlima huo.
Kile alichokishuhudia Pugh
“Nimezuru maeneo ya barafu kwa miaka mingi, lakini barafu ya Lewis ilikuwa mojawapo ya matukio ya kushangaza sana kuwahi kushuhudia. Kwa sasa iko ndogo sana na hivi karibuni itafifia,” alisema.

Malipo mingine ya Pugh kwa safari hii yenye changamoto yalikuwa ni kufanya matembezi katika hifadhi ambayo imekuwa ya wanyama 81 kwa zaidi ya miaka milioni moja, wakila kutoka kwenye orodha pana ya spishi 800 ya mimea na kutawanyika katika misitu, nyasi, nyanda za juu milimani na hatimaye vilele vya ukame ambako ni viumbe waliozoea pekee vilivyosalia.
Muda wake wa kuukwea Mlima Kenya ulikuwa wa kimkakati. Ulimalizika mwanzo wa mkutano wa saba wa Bunge la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA7), uliofanyika jijini Nairobi, Kenya, kuanzia mwezi wa Desemba tarehe 8 hadi tarehe 12. Kongamano hilo lilihudhuriwa na zaidi ya mawaziri na viongozi 140 wa mazingira kutoka ulimwenguni kote. Mnamo tarehe 11 mwezi huo, Pugh alihutubu kwenye mkutano huo kuhusu hali ya barafu katika Mlima Kenya, na “kwa nini kulinda barafu hiyo sasa ni jambo la dharura”.
Alikuwa na mengi mingine ya kunena: “Kampeni hii haijawahi kuwa kuhusu uogeleaji pekee. Imekuwa daima kuhusu kulinda asili kwa binadamu wanaoitegemea leo na katika siku za usoni.”
Binadamu hao ni kama Gerald Ngatia, afisa mstaafu wa misitu, mwenye umri wa miaka 74, na mmoja wa mashuhuda wa safari ya kishujaa ya Mto Sagana, ambao chanzo chake ni Mlima Kenya, kutoka mlio wa kishindo hadi mtiririko dhaifu. Ngatia ameishi pembezoni mwa Msitu wa Hombe katika mpango wa makazi ya Sagana tangu alipokuwa na umri wa miaka 11.

Anakumbuka utoto wake, ambapo mdundo wa maisha yake na ya jamii yake uliamuliwa na msitu wa karibu pamoja na mto uliokuwa ukinguruma, na uliodhaniwa kuwa hauwezi kushindwa.
Kwa mujibu wa Ngatia, hakuna tembo aliyethubutu kujitosa kwenye maji yaliyofurika ya mto Sagana wakati wa msimu wa mvua. Hata katika hatua ndogo iliokuwa na misukosuko katika Msitu wa Hombe, tembo walizoeshwa kuheshimu mto Sagana na safari zake nyingi zenye misukosuko katika mkondo wake wa kilomita 708 wenye msukosuko kutoka Mlima Kenya hadi katika Bahari Hindi eneo la Kipini.
Nyakati hizo maji yake safi yalitiririka, yakisaidia vishimo vya samaki aina ya trauti, wanaostawi kwenye joto la kati ya nyuzi 17-20. Mababu zake walikuwa wakielekea kuangalia juu mlimani kwa maongozi na miongozi ya kiroho kwa sababu Kirinyaga, kama Mlima Kenya ulivyofahamika kwa heshima kipindi hicho, kulikuwa ni makao ya Mungu wao, afahamikaye kwa jina la Ngai. Wakati fulani katika historia ya Jamii ya Wagikuyu, barafu iliyokuwa mlimani (ira) ilitumika kuwapaka vijana watahiriwa wa kiume na wa kike kingoni mwa mito.
Wakati wowote walipokumbwa na misiba, wazee wa jamii walikusanyika chini ya mti takatifu wa mtini (mugumo), na kumwabudu Ngai. Walifanya hivyo huku wakikabili Mlima Kenya.
Lakini nyakati zimebadilika, bila kutarajiwa. Misimu pia imekorogeka. Mngurumo wa kutia moyo wa Mto Sagana uliowahi kuwapa wakaaji matumaini sasa umebadilishwa na miguno ya njaa kutoka kwenye matumbo ya jamii zilizo chini ya Mlima Kenya. Hamna tena “manyunyu yenye Baraka” kutoka kwa miungu ya mlima huu wenye hasira.
Mto Sagana, unaotokana na kuyeyuka kwa barafu za Mlima Kenya, umekuwa na tabia ya kutotabirika. Kwa wakati mmoja, mtiririko wake wa kila siku ulikuwa wenye mabadiliko yasiyotabirika, kutoka 6,000,000m3 wakati wa msimu wa mvua nyingi mwezi wa Aprili, hadi mtiririko ulioathiriwa na mazingira wa takriban 300,000m3, haswa mnamo mwezi wa Septemba, kisha kuupunguza hadi mkondo wa msimu. Haya ni kwa mujibu wa utafiti wa muda mrefu uliofanywa mwaka 2011 wa Muungano wa watumizi wa rasilimali maji ya Sagana (SWRUA).
“Rekodi za mtiririko zilizopo zinapatikana kuanzia mwaka 1948 hadi leo. Vituo vya kupima maji katika 4AA5 Sagana vinaonyesha kiwango cha chini cha mtiririko wa maji wa 6,048m3 kwa siku, kawaida ya 449,280m3 kwa siku na mtiririko wa mafuriko wa 6,298,560m3 kwa siku.
“Wakati wa msimu wa kiangazi maji mengi hutolewa, bila kuacha mtiririko unaoathiri mazingira. Hii husababisha kuibuka kwa migogoro ya maji. Ili kuweka usawa wa maji ndani ya bonde dogo, kuna haja ya kuanzisha uwezo wa maji ya juu na ya ardhini na kuamua hifadhi,” ripoti iliyotolewa Agosti 2010 inasema.
Tathmini za hivi karibuni pia zinaonyesha kuwa Mto Sagana umekuwa ukipitia mabadiliko makubwa ya mtiririko yanayosukumwa zaidi na mifumo ya mvua. Kwa mujibu wa ripoti za ufuatiliaji wa maji ya juu ya ardhi</ na ziara za kitaalamu eneo hilo, zilizofanywa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) na Mamlaka ya Rasilimali za Maji ya Kenya (WRA), maji yamekuwa yakipungua yakilinganishwa na viwango vya juu awali.
Utafiti huo wa eneo uliofanywa na JICA katika kituo cha kupima mtiririko wa Sagana ulirekodi kina cha maji cha takribani mita 1.19, huku alama kwenye uoto wa kingo za mto zikionyesha kuwa viwango vya maji vilikuwa juu zaidi siku za karibuni, hali inayohusishwa na mvua kubwa zilizoathiri eneo la kati la Kenya mwishoni mwa mwaka 2023.
Ingawa WRA hukusanya takwimu za mara kwa mara za hidrojia kwa Mto Sagana, zikiwemo za viwango vya maji na mtiririko, taarifa za hivi punde za mtiririko wa wakati halisi bado hazipatikani kwa umma.
Kwa mujibu wa Grid Arendal, barafu kwenye vilele vya Mlima Kenya imekuwa ikiyeyuka. Katika matoleo yake ya mwaka 2007, Grid Arendal ilisema: “Barafu ya tropiki ya Lewis ilipungua kwa zaidi ya mita 800 kati ya mwaka 1893 na 2004, na ilipoteza unene unaolingana na takribani mita 16 za maji kati ya mwaka 1979 na 1996.”

Arendal pia iliongelea umuhimu wa Ziwa Lewis, iliyopo kwenye Mlima Kenya: “Hii ni mojawapo ya maeneo machache barani Afrika yenye barafu za kudumu”.
Katika ziara yake, Pugh aliona na kuonja kile jamii zinazoishi chini ya Mlima Kenya huvumilia kutokana na kupungua kwa maji kwenye mito wanayoitegemea kwa kilimo, hasa kwa kuwa eneo hilo ni mojawapo ya maeneo yanayokuza vyakula kwa wingi nchini.
“Nimezungumza na jamii zinazoishi chini ya mlima huu. Wote wanategemea maji yanayotoka hapa kwa kunywa, kilimo na shughuli nyingine za maisha. Maji haya ni muhimu kwa uhai, lakini sasa yanaendelea kupotea. Duniani kote, barafu husaidia kutoa maji kwa karibu watu bilioni mbili,” Pugh alisema.
Akizumgumza akiwa juu ya Mlima Kenya, Pugh alighusia umuhimu wa barafu na kuonya kuwa zinaendelea kuyeyuka kwa kasi. Alizitaka nchi duniani kupunguza haraka utoaji wa gesi chafuzi, ambao unasababisha barafu kuyeyuka.

“Tunahitaji kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi haraka na kusaidia nchi na jamii zinazohitaji msaada zaidi kuhimili mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Aliongeza kuwa Mlima Kenya ni mojawapo ya maeneo matatu pekee barani Afrika ambayo bado yana barafu. “Lazima tuongee na kuangazia kutoweka kwa barafu za mwisho barani Afrika. Huu ni wakati muhimu katika historia, na dunia inapaswa kuutizama kwa makini,” alisema Pugh.
Tarehe 13 Desemba, 2025, alichapisha haya kwenye tovuti: “Jambo moja lipo wazi. Kinachotokea mlimani hakisalii mlimani. Duniani kote, kuyeyuka kwa barafu kunatishia usambazaji wa maji kwa mabilioni ya watu.”
Picha ya bango: Lewis Pugh, Mwakilishi wa Bahari wa UNEP, alipokwea Mlima Kenya kushuhudia upungufu wa barafu na kuangazia athari zake. Picha na Duncan Moore, UNEP.