- Mchakato wa kuhifadhi mwili (taxidermy) unajumuisha uhifadhi wa ngozi ya Craig pamoja na sifa zake za kipekee, ili kuunda mfano halisi wa tembo kwa ajili ya elimu, utafiti wa kisayansi na maonyesho kwa umma.
- Kabla ya kuanza kwa mchakato wa kuhifadhi mwili wake, KWS iliondoa pembe za Craig ili zihifadhiwe kiusalama, kulingana na desturi inayofuatwa kila tembo anapokufa kiasili.
- Craig alizaliwa mnamo Januari mwaka1972katika familia inayofuatiliwa kwa karibu ya tembo wa CB huko Amboseli, na alichukua nafasi muhimu kama tembo dume wa uzazi.
- KWS imewahimiza wananchi kuheshimu kumbukumbu ya Craig kwa kutafakari umuhimu wa kulinda wanyamapori nchini Kenya.
NAIROBI, Kenya – Shirika la Huduma za Wanyamapori nchini Kenya (KWS) limeamua kuhifadhi mabaki ya Craig, tembo mashuhuri aina ya super tusker aliyekufa mnamo Januari 3, akiwa na umri wa miaka 54.
Uamuzi huu wa kipekee ulitangazwa rasmi na KWS Januari 13, na Profesa Erustus Kanga, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, akisema: “Kwa kutambua umuhimu wa kipekee wa Craig katika ikolojia, sayansi na utamaduni, tumeanzisha mchakato wa kitaalamu wa kuhifadhi mwili wake kwa njia ya taxidermy ili kuhakikisha urithi wake unabaki hata baada ya kifo chake.”
Craig alizaliwa Januari mwaka 1972 katika familia inayofuatiliwa kwa karibu ya tembo wa CB huko Amboseli, na alichukua nafasi muhimu kama tembo dume wa uzazi. Alikuwa mmoja wa kundi adimu la tembo dume barani Afrika waliotajwa kama super tuskers kulingana na pembe zao zenye uzito wa zaidi ya kilo 45 kila moja.
Profesa Kanga alisema kuwa mchakato wa kuhifadhi mwili (taxidermy) utahifadhi ngozi ya Craig pamoja na sifa zake za kipekee, ili kuunda mfano halisi wa tembo kwa ajili ya elimu, utafiti wa kisayansi na maonyesho kwa umma.
Uamuzi huu ni ukurasa mpya katika namna Kenya inavyokumbuka wanyamapori wake. “Maisha ya Craig yaliakisi mafanikio ya juhudi za pamoja za uhifadhi. Kupitia uhifadhi wa mwili wake kwa njia ya taxidermy, tunahakikisha urithi wake unabaki hata baada ya kifo chake, ukiwapa vizazi vijavyo muunganiko wa moja kwa moja na urithi tajiri wa wanyamapori wa Kenya,” alisema Profesa Kanga, katika taarifa iliyotumwa kwa Mongabay.
Kabla ya kuanza kwa mchakato wa kuhifadhi mwili wake, KWS iliondoa pembe za Craig ili zihifadhiwe kiusalama, kulingana na desturi zinazofuatwa kila tembo anapofariki kiasili. Hatua hii inalenga kuzuia wizi au biashara haramu ya pembe hizo za thamani.
Craig alifariki katika hifadhi ya Kitaifa ya Amboseli kutokana na sababu za kiasili. Uhifadhi wa mwili wake unaashiria ukurasa mpya katika namna taifa linavyokumbuka wanyamapori wake mashuhuri na kutumia urithi wao kwa elimu na utafiti wa kisayansi.
Katika taarifa hiyo, KWS ilisema kuwa ni super tuskers wachache sana ndio wamesalia barani Afrika, ingawa tembo huyo alizaa ndama wengi watakaoendeleza urithi wake wa vinasaba adimu.
Katika taarifa zilizotolewa punde tu Craig alipoaga dunia mwanzoni mwa mwaka, KWS ilimtaja kama “super tusker mashuhuri anayejulikana kwa pembe zake kubwa zinazogusa ardhi na tabia yake tulivu na yenye heshima.” Ilisema utulivu wa mnyama huyo wa kipekee, hata mbele ya watalii na watafiti, ulimfanya awe kipenzi cha wapiga picha na wageni kutoka pembe mbalimbali za dunia.
Kwa mujibu wa KWS, maisha marefu ya Craig yalitokana na miongo ya ulinzi madhubuti, “ufuatiliaji endelevu, juhudi za kupambana na ujangili, ulinzi wa makazi na usimamizi wa jamii”. KWS ilisisitiza umuhimu wa dhamira ya pamoja ya uhifadhi wa wanyamapori.
KWS imeahidi kuarifu umma baadaye kuhusu ratiba na mahali ambapo mabaki hayo yatawekwa kwa maonyesho. Shirika hilo pia limewahimiza wananchi kuheshimu kumbukumbu ya Craig kwa kutafakari umuhimu wa kulinda wanyamapori nchini Kenya.
Picha ya bango: Craig, mmoja wa tembo dume adimu, mashuhuri kama super tuskers, akitembea katika Hifadhi ya Kitaifa ya Amboseli, nchini Kenya. Picha na Elodie Toto wa Mongabay.