- Craig, tembo aliyetambulika zaidi duniani, alizaliwa mwaka 1972 na kuishi maisha yake yote katika tambarare za Amboseli, alipoashiria uhifadhi mwema.
- Pembe zake zikiwa na uzito wa zaidi ya kilo 45, na zilionekana kupinda chini na kukaribia kugusa ardhi kila alipotembea.
- Mwaka 2021, Craig alitambulishwa rasmi na East African Breweries Limited kupitia chapa ya Tusker, kama balozi wa uhifadhi, dhihirisho la mvuto wake duniani kote.
- KWS ilisema kuwa Craig alikuwa “balozi wa kweli wa Amboseli na ishara ya jinsi uhifadhi wenye mafanikio unavyopaswa kuonekana.”
Tembo mashuhuri Craig, aliyekuwa mmoja wa wachache wanaojulikana kama “super tuskers” barani Afrika, ameaga dunia. Craig alifariki kwenye mbuga ya kitaifa ya Amboseli, kutokana na sababu za kiasili.
Craig alizaliwa mwaka 1972 na tembo jike aliyefahamika kama Cassandra. Aliishi maisha yake yote katika tambarare za Amboseli, na kuwa jitu, pembe zake zikiwa na uzito wa zaidi ya kilo 45. Kila alipokuwa akitembea, pembe hizo zilipinda chini na kukaribia kugusa ardhi, hali iliyompa hadhi adimu ya “super tusker.”
Taarifa ya rambirambi iliyotolewa na Shirika la Huduma za Wanyamapori la Kenya (KWS), ilisisitiza ulinzi maksudi na ushirikiano kati ya washirika wa uhifadhi na jamii asilia. “Ufuatiliaji wa mara kwa mara, juhudi za kupambana na ujangili, ulinzi wa makazi ya wanyamapori, pamoja na usimamizi na ulinzi kutoka kwa jamii, vilihakikisha kuwa Craig aliishi kwa uhuru na usalama,” KWS ilisema katika tovuti yake.
Shirika hilo pia lilimtaja Craig kama “mnara hai wa urithi wa asili wa Kenya na Afrika.”
African Wildlife Foundation (AWF) pia ilitoa heshima zake kupitia mitandao ya kijamii, huku ikigusia hisia za wengi waliomwomboleza. “Leo mandhari ya Amboseli inaonekana kimya zaidi. Kifo cha Craig kinaashiria mwisho wa enzi ya balozi wa kweli wa pori super tusker aliyekumbusha dunia kile kilicho hatarini katika juhudi za uhifadhi,” AWF iliandika.
Hata ingawa mabadiliko ya tabianchi yanazidi kubana mandhari ya asili, na upotevu wa makazi ya wanyamapori kuwasukuma katika maeneo madogo zaidi, simulizi ya Craig ilileta matumaini. Akiwa hai, Craig aliwaunganisha watu.
Tembo huyu amefanya vivyo hivyo hata katika kifo chake kwa jinsi alivyoingia katika fikra za umma. Kabla hajafa, wapiga picha na watalii walivuka mipaka na mabara ili kumwona. Mwaka 2021, Craig alitambulishwa rasmi na East African Breweries Limited kupitia chapa ya Tusker, kama balozi wa uhifadhi, dhihirisho la mvuto wake na umaarufu duniani kote.
Kuishi kwake kwa miaka 54 huku akithaminiwa ni thibitisho kuwa uhifadhi si suala la kuzuia kutoweka tu; bali pia ni kuruhusu viumbe kuzeeka, kuacha alama zao duniani, na kuwa na maana.
Super tuskers, Craig akiwa mmoja wao, ni tembo dume wa savana ya Afrika wenye pembe za uzito wa zaidi ya kilo 45. Tembo hawa wana uwezo wa kuishi muda mrefu. Kwa mujibu wa Tsavo Trust, kuwalinda super tuskers waliobaki kunahitaji maeneo makubwa yaliyounganishwa, utekelezaji madhubuti wa sheria, na ushirikiano wa jamii.
Kulingana na ripoti ya Hesabu ya Taifa ya Wanyamapori 2025 iliyotolewa na Wildlife Research and Training Institute mnamo Desemba ilibaini ongezeko la idadi ya tembo, likifikia takriban 42,000, kutoka zaidi ya 36,000 mwaka 2021. Craig anaaminika kuwa alikuwa amepitisha vinasaba vyake adimu, hivyo kuleta matumaini ya kuona majitu wengine kama yeye katika siku zijazo.
Kwa kila super tusker anayefariki, dunia haipotezi mnyama tu, bali pia historia, kumbukumbu, na uwezekano wa baadaye. KWS ilisema kuwa Craig alikuwa “balozi wa kweli wa Amboseli na ishara ya jinsi uhifadhi wenye mafanikio unavyopaswa kuonekana.”
Mkurugenzi Msaidizi Mkuu wa Mawasiliano ya Shirikisho wa KWS, Duncan Juma Wanyama, aliiambia Dawan Africa kuwa shirika hilo litatoa taarifa punde tu uamuzi wa mwisho kuhusu uwezekano wa kuhifadhi mwili wa Craig utakapofikiwa.
Picha ya bango: Picha isiyo na tarehe ya Craig, Super Tusker, akitembea ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Amboseli nchini Kenya. Picha: KWS, kupitia AP.