- Mwanamke wa Kenya, anayejulikana kwa jina Truphena Muthoni, amevunja rekodi yake mwenyewe ya dunia baada ya kuukumbatia mti kwa saa 72 mfululizo katika tukio lililotokea chini ya Mlima Kenya.
- “Maandamano hayo ya kimya kimya” yalilenga kushinikiza uwajibikaji miongoni mwa mamlaka pamoja na umma usiojali kuhusu ukataji holela wa miti, mabadiliko ya matumizi ya ardhi ya misitu, na ulinzi usioridhisha wa maeneo ya vyanzo vya maji.
- Muthoni anawakilisha kizazi kipya cha wanaharakati wa mazingira kinachotumia mbinu bunifu na shirikishi zaidi kugeuza uhifadhi wa mazingira kutoka wazo la kufikirika hadi suala linalogusa maisha ya watu ya kila siku.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 22 amepongezwa baada ya kuukumbatia mti kwa saa 72 mfululizo licha ya hali ya hewa kugubikwa na joto lisilotabirika pamoja na mvua. Tukio hilo lililomfanya mwanamke huyo kuwa kivutio, lilitokea karibu na Mlima Kenya. Kwa ustahimilivu huo, Truphena Muthoni ameivunja rekodi yake ya awali ya kukumbatia mti kwa saa 48 aliyoweka mapema mwaka huu.
Ijumaa, kitabu cha kumbukumbu za maajabu duniani, ama Guinness World Records,kilitambua rasmi rekodi yake ya saa 48, siku moja baada ya kuivunja katika zoezi lililodumu kwa saa 72. “Muda mrefu zaidi wa kuukumbatia mti ni saa 48 na ulifikiwa na Truphena Muthoni (Kenya) huko Nairobi, katika zoezi lililoanza tarehe 31 Januari na kukamilika tarehe 2 Februari 2025,” ilisema taarifa ya Guinness World Records.
Muthoni anasherehekea kutambuliwa huko. “Hatimaye imerejea nyumbani. Saa zangu 48 za rekodi ya kukumbatia mti kwa muda mrefu zaidi imesajiliwa. Asante Mungu. Asanteni Wakenya kwa msaada wenu. Sasa nasubiri saa 72 za kukumbatia mti mfululizo zitambuliwe,” Muthoni aliandika kwenye ukurasa wa Facebook.
Katika mafanikio yake hayo ya hivi karibuni, Muthoni alikuwa imara, aliuzungushia mikono yake mti mkubwa aina ya Roystonea regia, uliokuwa karibu na ofisi za serikali ya Kaunti ya Nyeri. Wananchi wa kawaida, maafisa wa serikali, maafisa wa polisi na wahudumu wa afya walimzunguka na kumshangilia wakati wa zoezi hilo.

Kwa Muthoni, “maandamano hayo ya kimya kimya” ya saa 72 yalilenga kushinikiza uwajibikaji miongoni mwa mamlaka pamoja na umma usiojali kuhusu ukataji holela wa miti, mabadiliko ya matumizi ya ardhi ya misitu, na ulinzi usioridhisha wa maeneo ya vyanzo vya maji. Pia alifanya hivyo kuhamasisha ustawi wa afya ya akili, na kukumbusha watu wote kwamba mfumo wa ikolojia hauwezi kukamilika bila kuwepo kwa misitu asilia yenye afya na vyanzo vya maji vinavyoendelea kujazwa upya.
“Sababu mojawapo ya kukumbatia miti ni kwamba ni tiba kwa nafsi. Tuna changamoto kubwa za afya ya akili duniani ambazo zinahusiana moja kwa moja na uharibifu wa mazingira,” alisema katika video muda mfupi kabla ya kuanza zoezi hilo.
Mwanzoni, juhudi za Muthoni zilionekana kama mzaha au onyesho tu. Watu kadhaa walidiriki hata kumdhihaki kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakijipiga picha wakikumbatia miti kwa sekunde chache tu. Hata hivyo, kwa Muthoni, zoezi lilikuwa mwendelezo wa kampeni yake inayoelezea umuhimu wa uoto wa miti mijini na athari za kutoweka taratibu kwa misitu asilia. Kampeni yake ya kwanza ya aina hiyo ilikuwa mwanzoni mwa mwaka 2025 katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ulio umbali wa takriban kilomita 150 kutoka Nyeri, ambapo aliweka rekodi ya dunia baada ya kuukumbatia mti mmoja kwa saa 48 mfululizo.
Tukio la hivi karibuni lilivuta hisia za vyombo vya habari, kubadilisha mtazamo wa jamii na kuthibitisha kuwa masuala muhimu ya mazingira aliyokusudia kuyaangazia yanawaathiri watu wote, kwa ujumla na mtu mmoja mmoja. Mwisho wa zoezi hilo uliashiria mwanzo wa mjadala mwingine unaoweka msisitizo zaidi kuhusu uhifadhi wa mazingira na nafasi ya misitu katika maisha ya kila Mkenya, hasa ikizingatiwa kuwa misitu ina uhusiano wa moja kwa moja na upatikanaji wa maji.

Uamuzi wa kutekeleza zoezi hilo katika kaunti za Nairobi na Nyeri ulikuwa na ishara maalum, au kielelezo chenye maana kubwa. Nairobi ina msitu wa pili kwa ukubwa duniani kote ulioko ndani ya jiji, yaani Msitu wa Karura, ambao una ukubwa wa zaidi ya hekta 1,000 au ekari 2,470. Msitu huo pia unahusishwa kwa karibu na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Wangari Maathai, ambaye alipigania uhifadhi wake kwa gharama kubwa, hata kumwaga damu. Msitu wa Karura una mapango, maporomoko ya maji, na maelfu ya aina za mimea na wanyama, na unasimamiwa kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi kati ya Shirika la Misitu Kenya Kenya Forest Service na Friends of Karura.
Nyeri, kwa upande mwingine, iko katikati ya Kenya, chini ya Mlima Kenya, ambao ni mnara wa maji unaolisha mto mrefu zaidi nchini, Tana, pamoja na mto Ewaso Ng’iro, na vyanzo vingine vingi vya maji muhimu kwa kilimo na uzalishaji wa umeme unaotokana na nguvu za maji. Kaunti hiyo pia ni makao ya Hifadhi ya Kitaifa ya Mlima Kenya. Marehemu Wangari Maathai pia alitoka Nyeri.
Mara baada ya Muthoni kukamilisha zoezi hili, ilikuwa ni sherehe kubwa katika ofisi ya gavana wa kaunti, ambako harakati za zoezi hilo zilizinduliwa. Muthoni anawakilisha kizazi kipya cha wanaharakati wa mazingira kinachothubutu kubuni mbinu shirikishi na bunifu zaidi za kugeuza uhifadhi wa mazingira kutoka wazo la kufikirika hadi suala linalogusa maisha ya kila siku ya watu.
Waandaaji walisema ushahidi wa ustahimilivu wake utawasilishwa kwa ajili ya uthibitisho, kwenye taasisi husika ikiwemo Guinness World Records. Katika hatua nyingine, wataalamu wa afya wanaendelea kufuatilia afya ya Muthoni ili kujiridhisha kuwa yuko salama baada ya zoezi hilo.
Picha ya Bango: Mwanaharakati wa mazingira mwenye umri wa miaka 22, Truphena Muthoni, baada ya kuanza zoezi lake la kukumbatia mti kwa saa 72 katika Kaunti ya Nyeri, Kenya, chini ya Mlima Kenya. Gavana wa kaunti, Dkt. Mutahi Kahiga (wa pili kulia), alishuhudia kuanza kwa zoezi hilo lililomalizika tarehe 11 Desemba 2025. Picha: Ukurasa wa X wa Mutahi Kahiga.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 18/12/2025