- Ubunifu unaowawezesha viongozi wa vijiji kupokea taarifa sahihi na kuzitumia kufanya maamuzi yanayozingatia uwiano katika utumiaji wa ardhi kwa ajili ya ulishaji mifugo, uhifadhi wa wanyamaporti na ustawi wa mifumo ya ikolojia, umetambuliwa kimataifa.
- Mpango wa Sustainable Rangelands Initiative (SRI) unatekelezwa katika maeneo ya Kaskazini na Kati mwa Tanzania katika wilaya za Simanjiro, Babati, Longido, Same, Monduli, Ngorongoro na Mwanga, maeneo ambayo ni muhimu kwa shughuli za mifugo na wanyamapori.
- Kupitia mpango huu, kamati za malisho za vijiji zikishirikiana na wafuatiliaji wa maeneo ya malisho waliopatiwa mafunzo, hutumia zana za kidijitali zikiwemo simu za mkononi kukusanya taarifa kuhusu vyanzo vya maji, uoto wa asili, kasi ya ya ukuaji wa majani, afya ya udongo pamoja na uwepo wa vimelea vamizi.
- Taarifa zilizokusanywa hupelekwa kwenye vituo vya teknolojia vilivyowekwa ngazi za vijiji, husomwa ili kubaini hali halisi ya mazingira yaliyopo, na kwa kuzingatia matokeo ya taarifa hizo, huandaa mipango ya malisho inayolingana na hali halisi. Kwa kuwa vijiji vingi hukabiliwa na changamoto ya mara kwa mara ya mtandao, mfumo huu umebuniwa kwa namna ambayo inawawezesha watumiaji kukusanya taarifa hata kama hawajaunganishwa na mtandao na baadaye kuzipakia punde mtandao unapopatikana.
Wafugaji kutoka maeneo ya vijijini nchini Tanzania wametambuliwa kimataifa kwa kufanikiwa kuweka pamoja maarifa ya asili na teknolojia mpya katika juhudi za kurejesha ardhi iliyoharibika na kuhakikisha upatikanaji wa malisho.
Mradi huo unaoongozwa na jamii, ujulikanao kama Sustainable Rangelands Initiative (SRI), ulibuniwa na shirika la African People & Wildlife (APW). Hivi karibuni, ulishinda tuzo katika kipengele cha NatureTech Stewards kwenye uzinduzi wa tuzo za IUCN Tech4Nature, wakati wa Mkutano wa Dunia wa Uhifadhi wa Mazingira wa IUCN, uliofanyika Abu Dhabi Oktoba mwaka huu wa 2025.
Mpango wa Sustainable Rangelands Initiative (SRI) unatekelezwa Kaskazini na Kati mwa Tanzania katika wilaya za Simanjiro, Babati, Longido, Same, Monduli, Ngorogoro, na Mwanga. Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Jamii na Mazingira wa APW, Neovitus Sianga, anasema maeneo haya yalichaguliwa kwa kuwa ni muhimu kwa shughuli za mifugo na wanyamapori.
Kupitia mpango huu, unaotekelezwa na APW kwa kushirikiana na jamii za maeneo husika, kamati za malisho za vijiji pamoja na wafuatiliaji wa maeneo ya malisho waliopatiwa mafunzo, hutumia zana za kidijitali zikiwemo simu za mkononi kukusanya taarifa kuhusu vyanzo vya maji, uoto wa asili, kasi ya ukuaji wa nyasi, afya ya udongo pamoja na uwepo wa vimelea au spishi vamizi.
Nasma Mustafa, mmoja wa wafuatiliaji wa malisho kutoka Kijiji cha Engaluka, anaeleza hatua kuu za zoezi hilo: “Tunatumia kipimo cha tepu ya kupimia, kamba na simu. Kamba hulazwa juu ya ardhi kwa urefu wa mita 100, sambamba na kipimo chenye alama tano. Kisha tunaangalia ni alama zipi kati ya hizo tano zinazogusa uoto wa asili na zipi zinazogusa ardhi iliyo wazi. Tunajaza taarifa tunazokusanya kwenye fomu iliyowekwa kwenye simu. Tunaendelea kufanya hivyo hivyo hadi tutakapokamilisha upimaji wa eneo lililolengwa. Taarifa zilizokusanywa huwasilishwa kwa kamati ya malisho ya jamii kwa hatua zaidi.”
Taarifa hizi hupelekwa kwenye vituo vya teknolojia vilivyowekwa ngazi za vijiji na baada ya kusomwa, huonyesha taswira halisi ya ardhi na hivyo kusaidia kutoa mwongozo wa namna ya kupangilia matumizi ya ardhi.
Kupitia taarifa hizi, wafugaji huweka uwiano wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya mifugo yao na ile ya wanyamapori. Chini ya utaratibu huu, taarifa huwasilishwa kwa lahaja ya wenyeji na pia huzingatia muktadha wa eneo husika, mambo yanayofanya iwe rahisi kwa jamii kuelewa takwimu zinazoakisi maisha yao ya kila siku na kushiriki kikamilifu.

style=”font-size: 10pt;”>Baadhi ya wafuatiliaji wa maeneo ya malisho wakiwa kwenye mafunzo. Picha na Emmily Tunuka-APW.
“Msukumo wa kutumia teknolojia nafuu, rahisi kujifunza na ya kuaminika katika maeneo ya vijijini ulilenga kuhakikisha kwamba wana jamii wenyewe wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa ufuatiliaji,” anasema Sianga.
Kwa kuwa vijiji vingi hukabiliwa na changamoto ya mara kwa mara ya mtandao, mfumo huu umebuniwa kwa namna ambayo inawawezesha watumiaji kukusanya taarifa hata kama hawajaunganishwa na mtandao na baadaye kuzipakia punde mtandao unapopatikana.
Kwa mujibu wa Mwanzilishi Mwenza na Mtendaji Mkuu wa APW, Dkt. Laly Lichtenfeld, kutambua umuhimu wa malisho yenye afya kwa maisha ya wafugaji na uhifadhi wa wanyamapori, viliwapa msukumo kuanzisha mradi huo. Uelewa na uzoefu mkubwa wa jamii kuhusu mazingira unaotokana na ishara na maarifa yaliyorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, vinaendelea kuleta hamasa.
Sam Green, mtaalamu wa uhifadhi aliyebobea katika mifumo ya ikolojia ya maeneo kame, anasisitiza umuhimu wa kuelewa muktadha wa eneo husika kabla ya kutekeleza miradi inayoongozwa na wana jamii. “Ni jambo la msingi kubuni mbinu zinazoendana na mazingira husika,” anasema.
Wana jamii katika maeneo ya mradi wanathamini ushirikishwaji wao katika mradi huu. “Jamii zetu sasa zinafanya kazi kwa ushirikiano. Ardhi ambayo hapo awali ilikuwa wazi sasa imefunikwa na nyasi. Pia tuna usafiri na zana za kufuatilia na kusimamia maeneo ambayo hapo awali yalikuwa hayafikiki,” anasema Yohana Lesirkon, mjumbe wa kamati ya malisho.

Meneja wa Mawasiliano na Uhamasishaji wa APW, Katy Teson, aliiambia Mongabay katika mahojiano ya barua pepe kuwa vituo vya teknolojia pia vinatoa nafasi kwa wanajamii kukutana, kupitia taarifa na kuangalia namna bora maarifa yao ya asili na zana za kidijitali vinavyoweza kufanya kazi pamoja kwenye matumizi ya ardhi.
Matokeo yanayoonekana
“Hadi sasa, zaidi ya ekari 10,000 za malisho yaliyokuwa yameharibika yamerejeshwa katika hali nzuri katika maeneo 29 ya kijamii, huku zaidi ya ekari 800,000 zikiwa zimewekwa chini ya usimamizi wa jamii,” alisema Dr. Lichtenfeld. Aidha, ufuatiliaji wao umebaini kuwepo kwa maboresho mbalimbali, yakiwemo kurejea kwa nyasi katika maeneo ambayo awali hayakuwa na uoto, kuongezeka kwa msongamano wa uoto wa asili, ubora wa malisho, pamoja na kuboreshwa kwa makazi ya wanyamapori.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, mpango huu pia umechangia kuwepo kwa mabadiliko kwenye sera za kitaifa. Mwaka 2021, kwa mfano, APW ilitoa utaalamu wa kiufundi katika uandaaji wa miongozo ya kitaifa ya usimamizi wa malisho, na kuhakikisha kuwa maarifa na uzoefu unaotokana na jamii unajumuishwa katika mifumo ya kitaifa.

Si njia nyepesi
Licha ya mafanikio, mradi huu umekuwa na changamoto kadhaa. Changamoto za upatikanaji wa mtandao huwachelewesha wafuatiliaji wa malisho kutuma taarifa kutoka maeneo yaliyo pembezoni. Kwa kuwa wafuatiliaji wanahitaji mafunzo endelevu ili kukusanya taarifa sahihi na zinazolingana za ikolojia, kujengewa uwezo mara kwa mara ni hitaji muhimu.
Pia, si rahisi kuratibu maamuzi ya malisho kati ya vijiji na kamati nyingi, hususan wakati wa ukame ambapo shinikizo juu ya rasilimali za malisho huongezeka. Aidha, wanakabiliwa na changamoto za kimazingira kama ukame, kuenea kwa mimea vamizi na mmomonyoko wa ardhi, vitu ambavyo husababisha kazi ya urejeshaji kuwa ya dharura na ngumu zaidi.
Baadhi ya wafanyakazi wa APW wanaitazama tuzo ya IUCN Tech4Nature kama ishara ya kutambuliwa, chanzo cha fahari, na ushahidi wa kuongezeka kwa uongozi nchini Tanzania katika uhifadhi unaoongozwa na jamii. “Tuzo hii pia inasisitiza umuhimu wa nafasi ya jamii katika kulinda malisho. Aidha, tuzo hii inaiongezea APW kuaminiwa katika ngazi ya kitaifa na kikanda, na kuipa nafasi kubwa ya kuweza kuathiri sera na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika usimamizi endelevu wa ardhi nchini kote, ” alisema Sianga.
Picha ya Bango: Wafuatiliaji wa malisho wakiwa kazini. Picha na Emmily Tunuka- APW.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa </kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 16/12/2025