- Mapema mwezi wa Oktoba, kasuku 50 wa rani ya kijivu wa Kiafrika waliachiliwa porini na Wakfu wa Lukuru, baada ya kuokolewa kutoka kwa wawindaji haramu na kurekebishwa kwa mwaka mmoja katika kituo kilichokuwa kikisimamiwa na taasisi hiyo.
- Vituo viwili vya kuwarekebisha asuku vimeunganishwa na cha tatu, katika bustani ya wanyama ya Kisangani, mwezi wa Aprili, ambayo tayari imepokea kasuku 112 wa kijivu wa Kiafrika.
- Wakati DRC inapoanza kutekeleza marufuku ya Julai kwa biashara ya kasuku wa kijivu wa Kiafrika, mamlaka itahitaji kuongeza ufahamu katika jamii, kufuta mitandao ya biashara iliyoimarishwa, na kuhakikisha ndege walioachiliwa hawatakamatwa tena, wahifadhi wa mazingira wanasema.
LUBUMBASHI, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – Kasuku 50 wa Kiafrika wa kijivu wameachiliwa na kurejea porini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia kuokolewa kutoka kwa biashara haramu ya wanyamapori. Kuachiliwa kwao, katika mkoa wa kati wa Maniema mwezi huu wa Oktoba, kulikuja baada ya mwaka mmoja kurekebiswa katika hifadhi inayoendeshwa na Wakfu wa Lukuru wenye makao yake nchini humo, ambao umewatunza na kuwaachilia karibu kasuku 400 waliopatikana kutoka kwa wafanyabiashara haramu. Wakati utekelezaji wa amri mpya iliyochapishwa na wizara ya mazingira ya DRC inapoanza, vituo vya urekebishaji wa taasisi hiyo vinatarajia kazi nyingi zaidi za kufanya.
Mnamo Julai 31, 2025, DRC ilichapisha amri inayokataza kukamata, kumiliki au kufanya biashara ya kasuku wa Kiafrika wa kijivu (Psittacus erithacus). Marufuku hiyo ilitanguliwa na hatua kama hiyo iliyopitishwa awali na mamlaka katika mkoa wa Tshopo, kaskazini mwa DRC, ambao mji mkuu wake, Kisangani, unatumika kama kitovu kikuu cha biashara ya kasuku.
Lakini mwezi mmoja baadaye, kasuku waliokamatwa bado walikuwepo katika jamii za Ngungwa na Kimwachi huko Maniema, kulingana na Corneille Kalume, meneja wa taasisi isiokuwa ya kiserikali ya Action for Environmental Management (Action Communautaire pour la Gestion de l’Environnement) yenye makao yake makuu Kindu, mji mkuu wa mkoa.
“Wawindaji haramu bado wanawawinda na kuwakamata kasuku,” Kalume aliiambia Mongabay kwa njia ya simu. “Ni vizuri kuwa na agizo la mawaziri la kupiga marufuku ujangili, lakini kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kuzuia watu kuwatega ndege.”

Vituo vya urekebishaji wa kasuku waliokamatwa
Biashara ya kasuku ni ya hatari na inaua. Ni thuluthi moja tu ya ndege waliokamatwa wananusurika katika safari kutoka misitu ya DRC hadi kwa wanunuzi katika mataifa ya ng’ambo, kulingana na Wakfu wa Lukuru. Taasisi hiyo inajumuisha wawakilishi wa serikali waliojitolea, wataalam wa sheria, pamoja na John na Terese Hart, wahifadhi wawili kutoka Marekani ambao wamekuwa wakifanya kazi nchini DRC kwa miaka 40.
Mnamo mwezi Aprili mwaka 2025, Wakfu huo na taasisi ya ICCN, wakala wa uhifadhi wa DRC, walianzisha kituo cha uhifadhi wa kasuku katika bustani ya wanyama ya Kisangani. Kufikia mwezi wa Septemba, kituo kipya kilikuwa tayari kimepokea kasuku 112, kulingana na Gentil Kisangani, mkurugenzi wa bustani ya wanyama ya Kisangani.
Kituo kipya kiliongeza uwezo wa ziada wa kupokea na kurekebisha ndege waliopatikana kutoka kwa wasafirishaji, ambao mara nyingi wako katika hali mbaya, na manyoya yao ya mabawa ya kupaa angani yakidhohofika na kuvunjika wakati mwingine. Lukuru alikuwa tayari ameanzisha vituo vya urekebishaji wa kasuku huko Lodja, katika mkoa wa Sankuru, na katika eneo la Dingi, huko Maniema.
Wakati mwingine, shughuli ya urekebishaji wa Kasuku unaweza kuwa wa kasi ya chini na wa gharama ya juu, anasema Terese Hart. Bajeti za vituo vya urekebishaji zinahitaji kusimamia matibabu na chakula kwa ndege, pamoja na matengenezo na ukaguzi. Pia kuna gharama za chakula kwa walezi ambao hawaishi karibu na vituo, kama ilivyo kwa kile kituo kilichopo Dingi, na msaada mwingine kwa wafanyakazi.
“Ili kuwatunza kasuku 100 kwa mwezi mmoja, [gharama yake] ni kati ya dola za kimarekani $1,300 huko Lodja, dola za kimarekani $2,200 katika bustani ya wanyama ya Kisangani, na dola za kimarekani $2,900 huko Dingi,” Hart anasema. “Kujenga nyumba ya ndege ni kiasi cha zaidi ya dola za kimarekani $1,000 na inatofautiana kulingana na gharama ya vifaa na kazi. Tuna ndege saba huko Dingi, ndege watatu Kisangani na ndege moja Lodja.”
Kuachiliwa kutoka kizuizini kwa mara ya kwanza kwa kasuku kutoka kituo cha Kisangani hakutarajiwi hadi mwisho wa mwaka 2025, kulingana na mkurugenzi wa Bustani ya wanyama. Lakini ndege 50 ambao walikuwa wamekamilisha kurekebishwa kwao huko Maniema walikuwa tayari kuachiliwa mapema Omwezi ktoba: “Kasuku 397 wamepata tena uwezo wao wa kuruka na tayari wameachiliwa. Tunatazamia takriban kasuku 50 zaidi kuanza kuruka baadaye wiki hii,” Hart aliandika katika barua pepe kwa Mongabay mwishoni mwa Septemba.

Changamoto kuu: Kuhakikisha ndege walioachiliwa huru wapo salama
Licha ya furaha inayochochewa na kila ndege anayepona na kurudi porini, kuna hatari kwamba ndege hao wanarudishwa kwenye kitanzi cha biashara, kulingana na Bijou Koy, waziri wa mazingira wa Mkoa jirani la Tshopo. “Kuna hatari kubwa kwamba, kufuatia kuachiliwa kwao, ndege hao hao wanaweza kukamatwa tena na watu wale wale. Kwa kusainiwa kwa amri [ya kulinda kasuku], kampeni za uhamasishaji zitakuwa muhimu,” aliiambia Mongabay katika mahojiano ya simu.
Biashara ya kasuku inaonekana kama chanzo cha faida rahisi. Huku baadhi ya maafisa wa umma wakihusika katika hilo, kufuata kanuni mpya za kupiga marufuku biashara zote za kasuku hakutakuwa rahisi, wahifadhi wa mazingira wanasema.
“Ni vigumu kuwa na uhakika kwamba hakuna mfanyakazi katika kituo hicho anayehusika na usafirishaji haramu wa binadamu,” Gentil Kisangani anasema. “Lakini pia hatuwezi kuwashuku wafanyikazi bila idibati yeyote.
“Ni muhimu kuimarisha mifumo mingine inayohusiana na ulinzi wa maeneo ya porini, kama vile kuongeza uelewa miongoni mwa jamii za wenyeji na watu wa kiasili, na kuhusisha mamlaka za kisiasa, kiutawala na kijeshi,” anaongeza.
“Usalama hauwezi kuhakikishiwa baada ya ndege kuachiliwa huru,” Hart anasema. “Vituo vyetu vya Maniema na Tshopo viko kwenye ardhi ya shirika ICCN ambako walinzi wapo. Tutaendelea kutetea utekelezwaji wa sheria kali zaidi za kuwalinda kasuku na kwa ajili ya utekelezaji wake kwa ufanisi.”
Picha ya bango: Kasuku wa Kiafrika wa kijivu kwenye kituo ca uhifadhi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Picha kwa hisani ya WCS.
Taarifa hii ilichapishwa hapa kwa mara ya kwanza kwa Kifaransa mnamo 21/10/2025.