- Nakala za tathmini za hivi majuzi zimebainisha kemikali zenye sumu, ikiwa ni pamoja na dioksini, kwenye mayai ya kuku wa kienyeji katika mabara matano – huenda ikawa ni matokeo ya uchomaji wa plastiki na taka za kielektroniki zilizo na kemikali zilizopigwa marufuku, pamoja na sumu zisizodhibitiwa.
- Watafiti waliyafanya utafiti mayai yanayotagwa karibu na maeneo ya taka za kielektroniki, mahali pa kutupia taka yaani jaa na vichomea taka na wakapata viwango vya juu vya kemikali zinazozuia moto zilizopigwa marufuku duniani kote, ikiwa ni pamoja na dioksini za bromini ambazo ni sumu na huhatarisha afya ya binadamu na mazingira.
- Wataalamu wanabainisha kuwa ingawa baadhi ya vizuia moto vilivyo na bromini yaani (BFRs) vinadhibitiwa na kupigwa marufuku, vingine havijadhibitiwa. Wakosoaji pia wanaona kuwa sekta ya kemikali mara nyingi hubadilisha kemikali za kibinafsi zilizopigwa marufuku na kemikali zingine ambazo hazidhibitiwi lakini bado zinaweza kuwa na sumu katika familia moja, mchakato unaojulikana kama “badala za kusikitisha.”
- Wataalam wanatoa wito kuwe na udhibiti thabiti zaidi ili kuzuia kutolewa kwa sumu zinazojulikana, si kwa kupiga marufuku kemikali moja kwa wakati mmoja, bali kwa kushughulikia aina zote za kemikali. Lakini mkutano ambao umekamilika hivi punde wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm uliahirisha uorodheshaji na ufuatiliaji wa bromini na bromini zilizochanganywa na dioksini zenye klorini.
Utafiti wa hivi majuzi umepata kuona uwepo wa viwango “vya kutisha” vya kemikali zenye sumu katika mayai ya kuku wa kienyeji ulimwenguni. Ugunduzi huo unatokana na zaidi ya muongo mmoja wa uchanganuzi wa mayai katika mabara matano, ambayo yaligundua mayai yaliyochafuliwa na vizuia moto vilivyopigwa marufuku kimataifa, na haswa dioksini zilizo na bromini, ambazo ni sumu kwa afya ya binadamu na mazingira.
Sehemu za uchafu wa kielektroniki, majaa ya taka na vichomea taka ni vyanzo muhimu vya uchafuzi huu, huku mayai yaliyofanyiwa utafiti katika maeneo jirani yakipatikana kuwa yamechafuliwa sana na kemikali zinazotolewa wakati taka za plastiki zinachomwa.
Sampuli ya mayai yaliyotolewa karibu na maeneo ya taka za kielektroniki nchini Ghana mwaka wa 2019, kwa mfano, yalikuwa na viwango vya dioksini za bromini iliochanganywa na klorini mara 200 zaidi ya kiwango cha usalama cha chakula. Uzalishaji na matumizi ya kimakusudi ya dioksini umeondolewa au kuwekewa vikwazo vikali ulimwenguni kote chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm kuhusu vichafuzi vinavyoendelea vya kikaboni (POPs).
Utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la Emerging Contaminants, uliongozwa na Mtandao wa Kimataifa wa Kutokomeza Uchafuzi (IPEN), pamoja na shirika lisilo la serikali la Czech Arnika na timu ya wanasayansi wa kimataifa. Utafiti huo ulikuwa wa kina, na data ya sumu ya yai iliyokusanywa katika nchi nyingi zinazoendelea, na nchi zilizo na uchumi wa mpito, barani Afrika, Asia, Amerika Kaskazini na Kusini na Ulaya.
Matokeo hayo yanahusu sana, waandishi wa utafiti wanasema, kwani mayai ni chanzo muhimu cha protini katika nchi za kipato cha chini na cha kati, na utafiti unaonyesha kemikali hizi za sumu zinaingia kwenye mzunguko wa chakula.
“Tunajua kutokana na tafiti za miongo kadhaa kwamba dioksini ni baadhi ya kemikali zenye sumu zaidi ambazo tunafahamu,” anasema Therese Karlsson, mshauri wa sayansi na kiufundi katika Mtandao wa Kimataifa wa Kutokomeza Uchafuzi (IPEN). “Ningesema inahusu sana nyanja ya afya ya binadamu.”

Vizuia miale vya bromini na dioksini za bromini vinahusishwa na athari mbalimbali za afya, ikiwa ni pamoja na usumbufu wa endokrini au homoni, sumu ya uzazi, uharibifu wa mtindo wa uimarikaji wa neva, uharibifu wa mfumo wa kinga na saratani.
Wakati dioksini zenye klorini na baadhi ya dawa zinazozuia moto tayari zikiwa zimepigwa marufuku chini ya Mkataba wa Stockholm, wakosoaji wanaona kuwa kwa sasa kuna doa kubwa katika makubaliano ya kimataifa, ambayo yanashindwa kudhibiti na kufuatilia dioksini zenye bromini na bromini na klorini iliyochanganywa.
Waandishi wanatoa wito wa kuorodheshwa kwa bromini na klorini iliochanganywa na bromini na mchanganyiko-wa klorini iliyochanganywa chini ya mkataba, na kusitishwa kwa matumizi ya dawa zote za kuzuia miali ya moto. Baadhi ya vizuia moto vilivyo na bromini, kama vile etha za difenili (PBDEs), hexabromocyclododecane (HBCDD) na Kemikali ya heksabromobifenili(HBB), tayari vimepigwa marufuku.
“Jambo muhimu zaidi ambalo nakala ya stakabadhi inaonyesha ni umuhimu wa kuorodhesha na kudhibiti dioksini za klorini zenye bromini na bromini ilochanganywa na klorini,” anasema Jindřich Petrlík, mwandishi mkuu wa nakala ya tathmini na mwanasayansi wa mashirika ya Arnika na IPEN.
“Katika baadhi ya mayai, tuligundua kuwa dioksini na furani ambayo ni sehemu ya kemikali, zilizo na bromini huchangia zaidi sumu ya dioxin kuliko ya klorini.” Dioksini za klorini ni kati ya vitu vyenye sumu zaidi vinavyojulikana ulimwenguni.
Katika mkutano wa hivi majuzi wa Kamati ya Mapitio ya POP ya Mkataba wa Stockholm, ambao ulihitimishwa Ijumaa, Oktoba 3, 2025 uamuzi wa kuidhinisha maelezo ya hatari ya dioksini za bromini uliahirishwa hadi mwisho wa mwaka ujao. Wasifu wa hatari utakuwa hatua ya kwanza kuelekea kuorodhesha dioksini zilizo na bromini na dioksini zilizochanganywa na klorini chini ya mkataba huo.
Ucheleweshaji huo unamaanisha kemikali hizi hatari huenda zisiwe chini ya udhibiti wa kimataifa na Mkataba wa Stockholm hadi mchakato umalizike kati ya miaka 2-4 kuanzia sasa, Petrlík anasema. Wakati huo huo, mayai na bidhaa zingine za chakula zilizochafuliwa kwa sababu ya ukaribu wao na sehemu za majaa ya takataka visivyofuatiliwa vizuri zitaendelea kuhatarisha afya ya umma.

Ni tatizo pana zaidi?
Juhudi za haraka zinahitajika ili kukabiliana na kutolewa kwa dioksini katika awamu za uzalishaji, uchakatuaji na usimamizi wa taka, wataalam wanasema.
Kwa Lisa Thompson, profesa katika Chuo Kikuu cha California nchini Marekani ambaye hakuhusika katika utafiti huo, utafiti unaonyesha kwamba mayai yanaweza kuwa “chanzo kikuu cha vizuia moto vya bromini,” lakini anasema anaamini kuwa uchafuzi huo unaweza kuwa tatizo kubwa zaidi.
“Kulenga maeneo yaliochafuliwa sana kunaweza kusababisha watu kufikiria kuwa hili ni tatizo iliyojanibishwa,” anaandika katika barua pepe. “Kwa maoni yangu, hatua inayofuata itakuwa kupima mayai kutoka kwa kuku wanaotoka katika makazi ambayo watu wanafanya mazoezi ya kuchoma taka za nyumbani, ambayo mara nyingi hujumuisha chupa za plastiki na mifuko inayotumika mara moja pekee.”
Uchomaji wa wazi wa taka za plastiki na taka nyingine ni tatizo kubwa na ambalo mara kadhaa halitambuliki kuwa tatizo ambalo wataalam wameeleza kuwa “suala la dharura la afya duniani.”
Petrlík anaongeza kusema kwamba zaidi ya taka za kielektroniki na majaa ya taka, Vifaa vya pairolisisi – kwa kutumia njia ya utupaji plastiki iliyotengenezwa hivi majuzi sekta ya petroli na kemikali imeiita “usafishaji wa hali ya juu” – ni chanzo kinachoweza kuwa na shida cha kutolewa kwa kemikali hizi.
Ingawa ushahidi bado ni mdogo, Petrlík anasema vifaa vya pairolisisi vya plastiki “vinaweza kuwa tatizo kuhusiana na uchafuzi wa kikaboni kama vile dioksini za bromini.” Masomo zaidi yanahitajika, hata sekta inapoharakisha kufungua mitambo ya hali ya juu ya kuchakata tena nchini Marekani, Uchina, Japani, Umoja wa Ulaya, Mexico na Brazili.
Suala jingine kubwa la afya ya umma ni usimamizi mbovu wa majivu kutokana na uchomaji moto na uzalishaji wa vyuma. Uchunguzi wa Mtandao wa Kimataifa wa Kutokomeza Uchafuzi IPEN, na wengine, unaonyesha kuwa majivu haya yanaweza kuchafuliwa sana na kemikali. Majivu yalio tuwama, kwa mfano, mabaki yaliyobaki kutoka kwa uchomaji wa taka za manispaa, hutumiwa sana kama nyenzo ya ujenzi.
“Kwa bahati mbaya, majivu yaliotuwama au ya chini yanaweza kueneza uchafuzi wa dioxin iliyo na bromini kwa upana sana,” anasema Petrlík.
Waandishi wa utafiti pia wanaangazia kwamba juhudi za kuchukua nafasi ya vizuia moto vilivyopigwa marufuku na kemikali zingine za “riwaya” za kuzuia moto hazijatatua tatizo; haya, aidha, mara nyingi huwa na sumu lakini bado hayajadhibitiwa yanajulikana kama “badala za kusikitisha.” Kemikali hizi mpya zinaweza kuwa na sumu zinazoonekana kwenye mayai, mara nyingi kwa viwango vya juu.
Kwa sababu asili na vibadala vinafanana kemikali, mara nyingi huja na matatizo sawa ya afya. Matokeo yake, wakosoaji wanasema, ni mchezo wa kupindua madoa huku tasnia ikishindana na kuwashinda vidhibiti kwa kuhama kila wakati kutoka kwa uingizwaji mmoja wa kusikitisha hadi mwingine.

“Hiyo inazua swali kama haingekuwa bora kuangalia kudhibiti kemikali hizi katika vikundi,” Petrlík anasema. “Kwa hivyo, kwa mfano, kupiga marufuku [vyote] vizuia moto vilivyochomwa kunaweza kufikia hatua ya kulenga kemikali hatari sana.”
Zaidi ya kutoa wito wa udhibiti wa dioksini za bromini na dioksini zilizochanganywa za klorini, Mtandao wa Kimataifa wa Kutokomeza Uchafuzi IPEN na washirika wake pia wanasisitiza haja ya kuondokana na matumizi ya kemikali hatari wakati wa uzalishaji na kutekeleza uchakatuaji mzuri wa plastiki na taka za kielektroniki, pamoja na udhibiti mkali wa vizuia moto vyote vya bromini. Wanadai kuwa usafirishaji wa plastiki na taka za kielektroniki kutoka Kaskazini ya Dunia hadi Kusini ya Dunia unapaswa kukomeshwa.
“Kusafirisha taka za plastiki kwa nchi zinazoendelea ni ‘kusafirisha tatizo hilo nje’ ambalo haliwezi kudhibitiwa,” anakubali Thompson. “Kamati ya [Stockholm] inafaa kuchukua hatua kupiga marufuku [vyote] vizuia miale ya moto, ambavyo ni sawa na vichafuzi ambavyo tayari vimepigwa marufuku, na ambavyo vimeonekana kuwa vya kusababisha saratani na kusababisha madhara kwa mifumo ya uzazi na mifumo ya tezi za ndani.”
Roland Weber, mshauri wa mazingira na mwandishi mwenza wa nakala za tathmini hivi karibuni, anasema mkakati wa Umoja wa Ulaya wa kuzuia moto, ambao unalenga kuzuia matumizi ya kemikali hizi, ni hatua “ya ujasiri” katika mwelekeo sahihi.
Anauita uamuzi wa kuahirisha, kuorodhesha na kufuatilia dioksini zilizo na bromini na dioksini zilizochanganywa na klorini kama “bahati mbaya.” Uamuzi huo, anapendekeza, unatokana na baadhi ya wanakamati kuwa na dhana kwamba kuna ukosefu wa takwimu thabiti zinazothibitisha kufichuliwa kwa wanadamu.
“Ufuatiliaji wa ziada unapaswa kuwa na uwezo wa kuleta data inayohitajika [kwenye kamati ya udhibiti], na ninatumai kwamba jumuiya ya watafiti itaweza kufanya utafiti au tafiti kama hizo ndani ya mwaka mmoja.”
Kwa maoni ya Petrlík, kuahirishwa kwa kamati ya POP ya Mkataba wa Stockholm kunahusu kwa sababu ina maana kwamba ukosefu wa uangalizi wa udhibiti wa kemikali hizi za sumu huenda utaendelea kwa miaka. Ni “shida kubwa [inayoongeza] uchafuzi unaoendelea wa sayari yetu.”

Picha ya bango: Kuku wa kienyeji huku kukiwa na karakana chakavu ya chuma nchini Thailand. Usimamizi mbaya wa majivu kutoka kwa uchomaji na utengenezaji wa chuma ni suala lingine kubwa la afya ya umma. Picha kwa hisani ya Jindrich Petrlik/Arnika.
Nukuu:
Petrlik, J., Bell, L., DiGangi, J., Lucero, A., Kuepouo, G., Ochola, G., … Weber, R. (2025). Review of Brominated flame retardants na Polybrominated Dibenzo-P-Dioxins na Dibenzofurans in eggs and contamination sources. doi:10.2139/ssrn.5399284
Sharkey, M., Harrad, S., Abou-Elwafa Abdallah, M., Drage, D. S., & Berresheim, H. (2020). Phasing-out of legacy brominated flame retardants: The UNEP Stockholm convention and other legislative action worldwide. Environment International, 144, 106041. doi:10.1016/j.envint.2020.106041
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 15/10/2025