- Miaka ya data ya safari za tembo inaonyesha njia tofauti ambazo wanyama huchukua ili kupata chakula na maji, lakini ujenzi wa barabara na njia mpya za reli, miji na ua zinazidi kukatiza uwezo wao wa kuzunguka katika mazingira yao.
- Katika kukabiliana na hali hiyo, wahifadhi wanashirikiana na jamii katika mamia ya maili kaskazini mwa Kenya kuainisha shoroba hizi, ili maendeleo yoyote yajayo yalinde njia zao, ambazo pia zinapungua kutokana na mmomonyoko mkubwa wa baadhi ya maeneo kutokana na malisho makubwa na kufuatiwa na matukio ya mvua.
- Katika sehemu ya kitabu chake kipya kwa jina la “ROAM: Wild Animals and the Race to Repair Our Fractured World,” mwandishi Hillary Rosner anajadili masuala haya na jinsi jamii za vijijini zinavyoshirikiana na mashirika yasio ya kiserikaliili kuhakikisha uhamiaji huru wa siku za usoni wa wanyama hawa wa maarufu.
Uwanja wa ndege unaotumika kila mara nje ya mji wa Archers Post, kaskazini mwa Kenya, ulifungwa baada ya kuharibiwa na mvua kubwa, kwa hiyo ndege yangu ilitua katika uwanja mdogo wenye vumbi ulio upande mwingine wa hifadhi ya kitaifa ya Samburu. Kutoka hapo, barabara ilielekea kusini kupitia ardhi ya malisho inayomilikiwa na jamii hadi lango la magharibi la hifadhi, kando ya Mto Ewaso Ng’iro. Ilikuwa ni wiki moja tu kabla ya 2024, na Januari kwa kawaida ni mwanzo wa msimu wa kiangazi, lakini mvua bado ilikuwa haijapungua. Hifadhi hiyo, eneo linalolindwa lenye ukubwa wa Jimbo la Washington DC, – sehemu ya eneo kubwa zaidi la ardhi ya uhifadhi – ilikuwa utafiti wa kijani kibichi, ardhi ya tambarare na vilima vyake vilivyofunikwa na msukosuko wa mimea.
Mara tu tulipovuka mpaka wa hifadhi, tulikuwa miongoni mwa tembo, kuanzia watoto wa umri mdogo wa miezi kadhaa hadi vijana wadogo na wachangamfu, wazee wanaoongoza, na fahali wakubwa. Walitanga huku na huku kwa miguu yao iliyofunikwa na ngozi na kwato za mviringo, wakisinzia, wakinyonyesha, wakipita mtoni, huku wakijimwagia vumbi. Kwenye joto la adhuhuri, walisimama kwenye vivuli vya miti ya migunga na kwa uvivu kung’oa vijiti vya kijani kibichi na vigogo vyao, kisha wakavitupa vinywani mwao. Bila ya wasiwasi na uwepo wa gari aina ya Land Cruiser niliyopanda; walitangatanga hadi kwenye gari, wengine wakiwa na urefu wa chini ya shina moja.
Hizi zilikuwa siku za kutojali kwa tembo wa Samburu. Ilikuwa ni miaka miwili mirefu, migumu, yenye mauti kutokana na ukame uliokithiri, wakati wanyama wenye njaa walipokufa katika mazingira yaliyochakaa. Kati ya mwaka wa 2021 na mwaka 2023, tembo 1,260 walifariki katika eneo pana la Samburu – Laikipia, takriban tembo 563 vifo vyao vikitokana na “sababu za asili” -uwezekano mkubwa wa njaa na kiu kutokana na baa la njaa- na wengine wengi mikononi mwa wanadamu waliochoshwa na wanyama waliokata tamaa, waliokuwa wakivurumiza kwenye uzio na kuiba malisho duni ambayo wafugaji walihitaji kwa mifugo yao iliyokabiliwa na njaa. Lakini hatimaye mvua ilinyesha mwezi wa Novemba, na iliendelea kunyesha, na eneo hilo sasa lilikuwa na hali nzuri ya hewa ya kijani kibichi kama vile mtu yeyote angeweza kukumbuka kuliona kwa miaka mingi. Tembo hao walikuwa wamenenepa na wenye afya nzuri, na ilikuwa ni maajabu kuwatazama wakifurahia kipindi adimu cha maisha rahisi kiasi.

Kwenye upinde wa mto Ewaso, ng’ambo ya nyumba ya kulala wageni ya zamani iliyoharibiwa na mafuriko na ambayo sasa imetolewa kuwa makazi ya nyani, kuna kambi ndogo ya shamba ambako wahifadhi wamekuwa wakisoma na kusaidia kulinda tembo tangu mwaka wa1997. Huko, watafiti huweza kuwatambua zaidi ya tembo 600 wanaoishi kwa kuwaona, kwa msingi wa daftari za kina zenye michoro ya masikio ya wanyama hao. Wamevipa vikundi vya familia za tembo majina ya mada – Maua, Falme, Visiwa vya Hawaii – kusaidia kufuatilia tembo hao katika kila kikundi, kurekodi tarehe za kila mmoja za kuzaliwa na kifo. Na pia wamekuwa wakiwavalisha tembo kwenye ukosi kola za kufuatilia na GPS, wakikusanya data ya miongo mitatu ambayo husaidia kufahamisha mipango ya uhifadhi. Katika uwanja wa kambi ya utafiti, rafu za mbao zilizowekwa kati ya mto na sehemu wazi ya chumba cha kulia huhifadhi kola nyingi za tembo zilizotumika, kamba kubwa za ngozi zilizopambwa kwa masanduku ya mgunga – makavazi ya miundo ya kola za GPS kwa nyakati zote.
Iain Douglas – Hamilton, mtaalamu wa wanyama au mwanazoolojia wa Scotland, alianzisha shirika la Save the Elephants (STE) mwaka wa 1993, baada ya kuwasoma tembo katika Afrika Mashariki kuanzia miaka ya 1960. Kama vile tu Jane Goodall alivyowafungulia wanadamu ufikiaji wa karibu kwa ulimwengu wa tabia na utamaduni wa sokwe, Douglas-Hamilton alifanya vivyo hivyo kwa tembo. Mtaalamu huyo wa wanyama pia aliangazia na kuutoa wazi uwindaji haramu kwa ulimwengu na kusaidia kuchochea marufuku ya kimataifa ya pembe za ndovu na mipango ya uhifadhi.
Katika miaka ya 1970, Douglas- Hamilton alikuwa akitazama tembo kutoka angani, akiendesha ndege ndogo na, huku watu kadhaa waliopata fursa kusafiri na yeye mara kwa mara walivyonisimulia, mara nyingi wakishuka chini kwa kasi kufuata kundi la wanyama ardhini. Tafiti hizi ziliweka msingi wa data ya mwendo wa tembo ambayo ilionyesha jinsi ilivyokuwa muhimu kulinda njia zao. Baadaye, Douglas-Hamilton alianzisha matumizi ya kola za GPS za kufuatilia tembo.
Miaka kadhaa ya data ya mwendo wa tembo inaonyesha barabara kuu za tembo, njia ambazo wanyama wametumia katika historia kupata malisho na maji. Hata hivyo, leo njia hizo zinatoweka. Kwa kujenga barabara na njia za reli, kwa kuanzisha miji na majiji katikati ya njia za tembo, na kuezeka uzio unaofanya wanyama hao wasiweze kuvuka, wanadamu wanakatiza uwezo wa tembo kurandaranda katika mandhari yake. Wakati mamalia hawa wenye akili nyingi wanapofuata njia zao za muda mrefu, zilizoshirikiwa kiutamaduni ili kufikia rasilimali wanazohitaji kwa msimu, wanagongana dhidi ya miundombinu mipya na, mara nyingi, njia mbadala chache zinazohitajika. Hali hii inazua uwezekano wa uhasama baina ya binadamu na tembo, ambao kwa sasa nchini Kenya umekuwa chanzo kikubwa zaidi cha vifo vya tembo, sawia na vile makundi ya wanyama hatimaye yalivyokuwa yanapona kutokana na mzozo mbaya wa uwindaji haramu wa miaka mingi maangamizi makubwa,” kama Douglas-Hamilton amelijadili.
Kaskazini mwa Kenya, idadi kuu ya tembo wanaolisha katika Hifadhi ya Kitaifa ya Samburu ni wahamiaji. Wanafuata chakula kinachopatikana, wakitembea kati ya sehemu kubwa ya maeneo yaliyohifadhiwa, mara nyingi wakisafiri mamia ya maili kila njia kupitia ardhi inayomilikiwa na jamii mchanganyiko wa vyanzo – pamoja na sehemu fulani zimetengwa kimakusudi kwa ajili ya malisho ya mifugo na harakati za wanyamapori na nyingine zisivyo. Samburu kulikuwa tulivu nilipokuja mwezi Januari, lakini baada ya wiki kulianza kukauka. Viwango vya maji vingeshuka, chakula chenye lishe bora kingekuwa vigumu kupata, na tembo wengi wangeanza kujitosa sehemu nyingine.
Mamia ya tembo hao wangehamia magharibi, wakipitia njia mbalimbali zilizochakaa na kisha kupita kwenye vichochoro vyembamba kati ya vilima vyenye miinuko, karibu na makazi ya Oldonyiro, wakielekea kwenye nyanda za Laikipia. Huko, miti ya migunga itakuwa ikichuruzika maganda ya mbegu zake zilizo tamu na yenye lishe ambayo tembo wanatamani. Eneo hilo karibu na Oldonyiro ni kiunganishi muhimu katika safari ya tembo. Pia ni utafiti kuhusu jinsi mambo yanavyobadilika haraka nchini Kenya, na ni kipi kipo hatarini.

Kenya ni taifa lililo katika mabadiliko ya haraka sana. Chini ya mpango uliozinduliwa na rais wa wakati huo Mwai Kibaki mnamo mwaka wa 2006, nchi imekuwa ikijitahidi kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2030. Sehemu kuu ya mpango huu, inayojulikana kama Kenya Vision 2030 au Ruwaza ya Kenya 2030, imekuwa uboreshaji wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na lengo la kuweka lami kilomita 10,000 (zaidi ya maili 6,000) ya barabara na kuimarisha mfumo wa reli iwe ya kisasa, iliojengwa na Wakoloni wa kiingereza karne moja uliopita.
Kuanzia mwaka wa 2014, kama mpango wa awali wa Mpango wa China wa Belt and Road Initiative, serikali ya China ilifadhili kilomita 472 (maili 293) za njia mpya za reli, iitwayo Standard Gauge Railway (SGR), inayoanzia Nairobi kusini mashariki hadi Mombasa, pwani. Njia hiyo ya treni ilipunguza safari kwa reli kutoka kama saa kumi na mbili hadi saa nne, lakini pia iligawanya mbuga mbili za kitaifa kwa njia.
Kinachofuata ni upanuzi wa reli katika upande mwingine, na ujenzi wa njia mpya za barabara ya mwendokasi yenye njia sita, sambamba na SGR, ambapo barabara ya lami ya njia mbili kwa sasa inasonga takribani robo tatu ya bidhaa zote zinazoingizwa Afrika Mashariki. Ambako barabara zinaelekea, ndivyo maendeleo na kutapakaa. Kenya iko katika njia panda, njia moja ikiongoza kwa ukuaji endelevu na njia nyingine katika kuporomoka kwa turathi kubwa ya idadi ya wanyamapori nchini.
Ili kuhakikisha kwamba wanyama hao wanaweza kuvuka vyanzo kwa usalama ni changamoto ya kutisha, muhimu ya uhifadhi, yenye athari nyingi zaidi ya mipaka ya taifa. Ikiwa ni mojawapo ya mataifa yanayoongoza kiuchumi barani Afrika, Kenya inachunguzwa kama kielelezo cha jinsi ya kuendeleza na kuinua viwango vya maisha bila kutoa kafara bayoanuwai yake. Kuipotosha kunaweza kuwa na maana pana zaidi, janga.

Alasiri moja yenye jua kali, nilifunga safari kuelekea Oldonyiro, yapata mwendo wa saa nne kwa kutumia gari kutoka sehemu ya Archers Post kwenye njia nyembamba, zenye vumbi, nikiwa na Benjamin Loloju, ambaye ni wa kabila la Wasamburu na alilelewa akichunga mbuzi katika maeneo hayo. Aliniambia alidhani alikuwa na umri wa karibu miaka 32 au 33 hivi, ila hakujua kwa uhakika kwani hakuna mtu yeyote katika jamii yake aliyekuwa akinakili siku za kuzaliwa. Kama mmoja wa watoto kumi na mmoja, alikuwa mwanafamilia pekee aliyehudhuria shule; kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika katika eneo hilo bado kinaning’inia karibu asilimia 30. Alifanya vizuri shuleni na hatimaye akapata mpango wa “ufadhili wa masomo ya tembo” kutoka kwa Save the Elephants, sehemu ya mpango unaosaidia kufadhili masomo ya watoto katika jamii za wachungaji wanaoishi pamoja na tembo. Barabara mpya ya udongo ilikuwa ikijengwa wakati huo, hatua kubwa ya maendeleo. Barabara zilimaanisha makazi zaidi, miundombinu ya kudumu zaidi, na uwezekano zaidi wa kuongezeka kwa uhasama baina ya binadamu na wanyamapori. Douglas-Hamilton alitaka kufanya kazi na jamii ili kukuza kuishi pamoja.
Kutokana na ufadhili, Loloju alisoma katika shule ya bweni jijini Nairobi. “Sikuamini mara yangu ya kwanza nilipowasili katika jiji hilo,” alikumbuka, akiicheka kumbukumbu. Alipata alama za ‘A’ wastani katika masomo yake yote na kuorodheshwa miongoni mwa wanafunzi mia moja bora nchini kote. Aliendelea kusomea uhandisi wa kijiografia katika Chuo Kikuu cha Nairobi, kisha baadae akapata shahada ya uzamili nchini Uingereza. Nilipokutana naye, alianza kuwazia juu ya programu za PhD za kusomea mmomonyoko wa udongo, ambayo ni shida mmoja katika eneo hili. Loloju alijenga nyumba kwenye kilima nje ya Oldonyiro, aliporejea katika nchi yake ili kusaidia kuunda njia salama na endelevu kwa tembo.
Tulipitia mashariki kupitia nyanda kubwa za ardhi za jamii, mara kwa mara tukikwama kwenye vichochoro vyenye michanga inayovuka mikondo au mito iliokauka. Tulipita kwenye vilima vya kustaajabisha na miamba ambako nyani walitawanyika. Tuliwapita wanyama kama pundamilia na twiga, digidigi wadogo wakiruka vichakani, swara wakiwa malishoni, na makazi ya muda ya binadamu ama maboma, yenye mabanda yalivyojengwa kwa mbao za mgunga.
Kila mara tulipita mchungaji aliye peke yake akitembea na mbuzi wake, au mtoto aliyebeba vyombo kuchota maji. Lakini mara kadhaa tuliendesha gari kwa mda mrefu katika mandhari mapana bila miundombinu ya kudumu ya watu. Saa chache kwenye safari yetu, tulisimama pahali njia ilivuka barabara. Loloju aliruka nje ya gari na kutuonyesha alama ya zege ya mraba iliyowekwa kwenye vumbi. Alama ya chuma kilichopachikwa kwenye zege ilisoma: Livestock + Wildlife Corridor”.

Kulingana na data kutoka kwa tembo wenye kola za GPS, Save the Elephants na shirika a Uswizi la Wyss Academy for Nature, wamefanya kazi na jamii kwenye mamia ya maili kaskazini mwa Kenya kuainisha njia hizi, ili maendeleo yoyote ya siku za usoni, yakitokea, yalinde angalau njia hii kwa wanyama. Wameezeka zaidi ya alama 200 ardhini, wakisaidiwa na jamii. Uwekaji mipaka wa njia hizo husaidia kuhakikisha njia kwa wafugaji kusafirisha mifugo yao, pamoja na njia ya wanyamapori. “Hii imekuwa nzuri,” Loloju alisema kuhusu juhudi. “Watu, jamii, wamekubali kusema, ‘Ni nzuri, iwekeni mipaka.’” Kikundi hicho sasa kinajitahidi ili kuona njia hizi zinawekwa kwenye sheria za kitaifa, na pia kuzieneza mbali zaidi kusini na mashariki, kule Laikipia. Lakini Oldonyiro inawakilisha hali mbaya zaidi. “Tayari tulidhani labda tumechelewa kufika Oldonyiro. Tulipaswa kufika hapa miaka kumi iliopita,” Loloju alilalamika. “Ila sasa, wakati ndio huu.”
Wakati wa alasiri, tulifika kwenye eneo la makazi yenye watu wengi zaidi kuliko tulivyoona siku nzima, ikiwa na miundo ya kudumu – majengo yaliyojengwa kwa vizuizi vya mawe na zege – yakianza kuonekana kando ya barabara. Hii ilikuwa ukingoni mwa Oldonyiro. “Ni hali ngumu sana hapa,” Loloju alisema. “Hii ni njia kubwa sana ya maisha.” Kutoka Samburu hadi Laikipia, kimsingi ni eneo moja kubwa la kuhama kwa tembo, na wanyama wengine wengi, ambao wanahitaji kuhama na misimu. “Lakini hapa” – katika Oldonyiro – “ndio uzi; huu ndio moyo wake. Tukipafunga hapa, basi tutawazuia tembo wanaohama, na wanyama wengine wa porini. Tutakatisha kurandaranda kwao. Na kwa ajili ya kuishi kwao, ni hivyo, muhimu sana kuwa na uhusiano huu.” La sivyo, tembo wengi zaidi wangeweza kufariki kutokana na kukosa chakula au mikononi mwa wanadamu wenye hasira.

Kwenye ramani ya data ya mwendo wa tembo, matone makubwa yanayofanana na tambi ya mistari nyekundu, inayoonyesha njia za wanyama wenye kola za GPS, yanaonyesha mienendo “iliyotulia”, tembo wakila, wakinywa, wakichezacheza, wakipumzika, labda wakijamiana. Wako njiani sehemu fulani, lakini hawako kwenye haraka ya kufika huko. Fikiria uko kwenye gari la masafa marefu, na hapa ndipo unaposimama kwa chakula cha mchana cha burudani, kulala usiku, au hata kutembelea kivutio cha utalii.
Karibu tu na mji wa Oldonyiro, mviringo huo unanyooka hadi kuwa kijiduara kimoja. Hapa, data inaweka wazi; tembo hawazunguki pamoja; hawachezi. Wanajaribu tu kuvuka hadi nafasi inayofuata salama. Hapa ndipo kwenye safari yako ya barabarani; umefikia sehemu isiyopendeza ya barabara kuu, au labda unajaribu tu kupitia na kuweka umbali wake nyuma yako.
Katika ramani hiyo hiyo, miduara ya manjano inaonyesha makazi ya watu. Kundi kubwa zaidi la tawi hili hupishana na miviringo ya tembo ambao hawazunguki hasa katika mji wa Oldonyiro. Kwa karne nyingi, labda milenia, tembo walivuka mazingira ya hapa. Lakini sasa ni kituo kipya cha mji wenye shughuli nyingi, na jengo baada ya jengo linaloinuka kando ya barabara ya vumbi. Eneo ambalo awali lilikuwa na maboma ya wafugaji linabadilika kuwa mji. “Haya yote ni mapya,” Loloju alisema tulipokuwa tukipita katikati ya eneo la maendeleo, ambapo majengo ya mawe ya ghorofa moja – maduka ya nyama, maduka ya bidhaa za kimsingi, vibanda vya simu -yalikuwa yakiendelea kujengwa kwenye pande zote za barabara.

Alionyesha miundo michache ya mbao ambayo ilianzia utotoni mwake. Zaidi ya majengo hayo machache, mengine yote yalikuwa nyongeza za hivi karibuni. “Upanuzi huu unaelekea kule,” alisema, akionyesha kusini. “Na utaenda hadi mahali ninapoishi, katika miaka michache ijayo. Kila kitu ni kipya na bado wanaendelea kujenga, na kwa hivyo, mstari unakaribia ukanda ambao tembo wanatumia kwa sasa.”
Wakizuiliwa kutoka kwa njia zao za kihistoria kwa sababu majengo mapya sasa yameziba njia zao, tembo hao walikuwa wamebuni njia mpya kusini mwa mji. Ramani ya hivi punde ilionyesha wazi korido zao zilizosogezwa. Hata unaweza kuona kutoka kwa njia za GPS kwamba tembo walijaribu kutumia njia yao ya zamani ila wakakutana na ua au maendeleo mengine, wakarudi nyuma, wakatafuta njia ya kuzunguka. Vikundi vichache vya familia vimepata njia hii mpya ya kusini, na “kila tembo sasa atanusianusia, na wanafahamu, hii ndiyo njia sasa,” Loloju alisema.
“Tembo hubadilika kwa haraka,” mwanabiolojia wa tembo Lucy King, aliyelelewa kati ya Kenya, Somalia, na Lesotho, aliniambia kabla ya safari yangu. King anafanya kazi kama mkurugenzi wa shirika la Save the Elephant , mpango wa kuishi pamoja kwa binadamu na tembo, na mwanzilishi wa matumizi ya “uzio wa mizinga ya nyuki” kama njia ya kuzuia tembo kuvamia sehemu za kilimo kusini mwa Kenya na kwingineko. Tembo hawaelewani na nyuki, kwa hivyo kuweka mizinga kwenye uzio kunaweza kusaidia kuwaweka mbali na mazao shambani. “Wana uwezo wa kusonga na kubadilisha mahali wanapotembea, ikiwa wanaweza kupata njia nyingine. Hawajali kubadilika kwa urahisi.” Lakini ni sharti kuwe na hiari zinazopatikana.
Inavyoonekana, njia mpya ya tembo kusini mwa mji pia iko katika hatari kubwa ya kupotea. Miaka miwili ya nyuma, kaunti ilikamilisha ubadilishaji wa ardhi sehemu hii, kutoka kwa ardhi inayomilikiwa na jamii hadi hati miliki za kibinafsi. Watu sasa wanamiliki vipande vyao vya ardhi – na wengi walikuwa wakijenga majengo ya kudumu na kuzingira mali zao kwa uzio wa kuzuia wanyamapori, si tofauti na Marekani Magharibi. “Tembo hawa watakuja na kusema, mungu wangu, uzio huu haukuwepo mwezi mmoja au miwili iliyopita,” Loloju alisema.

Tulisimama sehemu ambayo korido ya tembo ilipishana na barabara, na tukatembea kwa miguu mita 100 hivi kufuata njia hiyo. Vifusi vikavu vya kinyesi vilienea kwenye vumbi la rangi ya kutu. “Hiki ni kiwanja cha mtu,” Loloju alisema kuhusu ardhi tuliokuwa tumesimama. “Bado haijajengwa.” Alituelekeza pande mbalimbali. “Hapa kuna kiwanja cha mtu, ni hati ya umiliki wa mtu. Kwa upande mwingine, ni hati ya umiliki. Kwa hivyo, katika miaka michache ijayo, haya yote yanaweza kujengwa.” Mara tu hilo litatokea, njia itakatizwa kabisa kwa tembo – labda Loloju na baadhi ya wasaidizi wa jamii wangeweza kuwashawishi wamiliki wa ardhi kuzunguka ukanda kutenga sehemu nyembamba za ardhi zao, yadi 20 au 30 tu, hata, kwa ajili ya wanyamapori – kama njia ya uhifadhi. Haijulikani ni umbali gani wanyama wanaweza kutembea kwenye ukanda wa uzio ambao ni mwembamba, lakini uliwakilisha chaguo la kipekee.
Kando ya barabara, tunaweza kuona siku za usoni. Mmiliki mpya wa ardhi aliyeitwa hapo tayari alikuwa amejenga nyumba kubwa, iliyozungukwa na uzio wa nyaya zenye urefu wa futi sita. Sehemu moja ya uzio haikuwepo; tembo waliiangusha hivi majuzi walipokuwa wakijaribu kufuata njia, iliwachukuwa miezi michache iliyopita, na mwenye nyumba alikuwa amerundika matawi ya mgunga ili kuziba pengo hilo kwa muda. Loloju alikuwa akizungumza na wamiliki binafsi wa mali, mkutano wa darzeni kadhaa kati yao ulipangwa kufanyika mwezi uliofuatia – na mmiliki huyu alikuwa amejitolea kwa kauli yake kujenga uzio wake na kutenga mita 30 kwa tembo. Lakini baadae alijenga uzio karibu na mstari wa makazi yake. Na kwa sababu ua huo sasa ulikaa kwenye njia ambayo tembo hao walikuwa wamepita mara ya mwisho, walirudi, wakakaribia sana, na kuiharibu.
Hili halikuwa tatizo peke; sehemu ya sababu iliyofanya tembo hao kukaa karibu sana na uzio huo ni kwamba uliwakilisha njia hatari kiasi ya kusafiri. Katika eneo hilo lote, makorongo makubwa ya mmomonyoko wa udongo, mengine makubwa ya kutosha kuendesha gari, yanafunguka, yakienea, na kuongezeka. Ni tatizo sugu ambapo mifumo ya malisho, mabadiliko ya hali ya hewa, makosa ya zamani ya matumizi ya ardhi, na fizikia tupu vinachanganyika na kuwa kinamasi halisi. Malisho ya mifugo huondoa mimea, ambayo hulegeza udongo, na kisha mvua inaponyesha, maji yanayotiririka huondoa vumbi tupu. “Inaanza kama njia nyembamba,” Loloju alisema. “Na kwa miaka, inaendelea kupanuka tu.” Bila chochote cha kuzuia udongo mahali pake, korongo zinaendelea kukua na kukua. Makorongo mengi ni mapana sana sasa hivi kwa mwanadamu kuruka na kuvuka ng’ambo ya pili, na kina zaidi ya futi sita – kikubwa cha kutosha kwa tembo wachanga kutumbukia ndani.

Tulitembea kwa muda wa saa moja katika ardhi tambarare, tukichungulia kwenye ukingo wa makorongo, tukijaribu kufuata njia za tembo. Makorongo mingine tungeweza kuzunguka, mengine tungeweza kuruka juu, mengine yalikuwa mapana sana na kutulazimu kuruka chini upande mmoja na kurudi juu ya pili. Ilikuwa vigumu kufikiria familia za tembo kufanya safari hii; hata vigumu zaidi kuwazia jinsi wangefunga safari ikiwa uzio lingeacha tu korido nyembamba na kisha kumezwa kwenye shimo.
Hili halikuwa zoezi nadharia la kufikiria kuhusu tembo au kuonyesha njia ya kinadharia. Nilikuwa nimewaona tembo wale wale ambao hivi karibuni wangeelekea njia hii – niliona safu za tembo wakubwa waliozingira ili kuwaweka watoto salama katikati yao, nilimtazama ndugu mmoja mchanga mwenye hasira akijaribu kumwamsha ndugu yake kutoka kwenye usingizi, nikaona makunyanzi na kope zao na jinsi vumbi lilivyoshikamana na meno yao. Hawa walikuwa ndovu ambao, katika majuma au miezi ijayo, wangefika mahali hapa, wakihitaji tu kupita kwa usalama katika njia yao ya kwenda mahali pengine ambapo wangeweza kupata chakula kwa wingi.
Hillary Rosner ameripoti kuhusu masuala ya mazingira kwa National Geographic, The Atlantic, Scientific American, Audubon na mengi mengineyo. Maandiko haya yamenukuliwa kutoka kwa kitabu chake kipya kilichochapishwa na Patagonia, “ROAM: Wild Animals and the Race to Repair Our Fractured World,,” ambapo anawapa changamoto wasomaji kufikiria upya nafasi yetu ulimwenguni, na kutoa hoja ya kuwachukulia wanyamapori kama majirani.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 14/10/2025