- Pendekezo la kujenga kinu cha nyuklia cha megawati MW 1,000 katika pwani ya kusini mashariki mwa Kenya limekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wakazi na wataalam wa mazingira, ambao wanaonya juu ya madhara yanayoweza kutokea kwa jamii, sekta ya uvuvi na mazingira.
- Mashirika ya serikali sasa yanafanya mashauriano katika eneo lingine linalotarajiwa upande wa pili wa nchi, karibu na Ziwa Victoria, ziwa kubwa zaidi la maji baridi barani Afrika.
- Mahitaji ya nishati ya Kenya leo yanatimizwa zaidi kutoka kwa vyanzo vya kaboni duni, na nchi iko kwenye njia ya kufikia upatikanaji wa nishati kwa wote ifikapo 2030, lakini mamlaka zinasema nishati ya nyuklia inahitajika ili kufikia malengo ya maendeleo ya baadaye.
- Hatahivyo, baadhi ya wataalam, wanaonya kuhusu gharama kubwa, ucheleweshaji, na hatari za kimazingira za muda mrefu zinazohusiana na miradi ya nishati ya nyuklia.
“Ni kamilifu!” anagutuka Anthony Kingi, mwanachama wa jamii ya kijiji cha Uyombo na mwanaharakati wa mazingira. “Kenya haiuhitaji huu. Hata hivyo, kama ni lazima waujenge, ninafurahi kuwa hauko nyuma ya nyumba yangu.”
Anachoashiri “hicho” Kiwanda kinachorejelewa na Kingi ni kinu cha nyuklia cha megawati 1,000 ambacho serikali ya Kenya inapanga kujenga. Serikali imeorodhesha maeneo matatu ambayo yanaweza kutumika kwa mradi huo wenye thamani ya dola bilioni 3.8.
“Kwa sasa Kenya ipo katika awamu ya pili ya maendeleo ya mpango wa nishati ya nyuklia, ikiwa na lengo la wazi la kuunganisha nishati ya nyuklia kwenye gridi ya kitaifa ifikapo mwaka 2034,” Shirika la Nishati ya Nyuklia la Kenya (NuPEA) lilisema katika taarifa kwa Mongabay.
Mashauriano ya awali kuhusu mradi yalijikita katika sehemu ya Uyombo, kijiji cha wavuvi katika Kaunti ya Kilifi kwenye pwani ya kusini mashariki mwa Kenya. Uamuzi huo ulisababisha upinzani mkubwa kutoka kwa wanakijiji wa Uyombo na wataalam wa mazingira. Kwa miaka mingi, maandamano yalipoongezeka, waandamanaji walivamiwa na polisi, na wengine walikamatwa.
Mnamo Juni 27 mwaka huu, kukiwa na shamrashamra ndogo sana, Wizara ya Kawi na Petroli ilitangaza katika Kongamano la Nishati ya Nyuklia katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), kilichoko kaunti ya Siaya kwamba inafikiria kujenga kiwanda hicho huko Luanda Kotieno, katika eneo la Bondo kaunti ya Siaya, upande wa pili wa nchi.

Mbunge wa Rarieda Paul Otiende Amollo, mojawapo ya maeneo bunge sita ya kaunti ya Siaya, alisema wakati wa mkutano huo: “Kukubalika ni muhimu. Huko Kilifi, wana masuala kwa sababu ya kutokubalika. Kwa upande wetu, ninaelewa kutoka kwa shirika la NuPEA kwamba wametambua eneo karibu na Luanda Kotieno. Kama mbunge aliyechaguliwa wa Rarieda, ninaweza kusema kwamba tutakubali, ingawa tutaendelea kushauriana na jamii ili kubali kikamilifu.”
Katika taarifa yake kwa Mongabay, shirika la NuPEA lilisema hakuna uamuzi wa mwisho ambao umefanywa kuhusu sehemu ya mradi.
Shirika hilo liliongeza kusema kwamba “nchi bado iko katika mchakato wa kuendeleza Mpango wake wa Nishati ya Nyuklia na kufanya upembuzi yakinifu, ambao unajumuisha kutambua maeneo yanayoweza kutokea. Hakuna eneo la mwisho ambalo limeidhinishwa, na uamuzi wowote kama huo utakuwa chini ya Tathmini ya Kina ya Athari za Kimazingira na Kijamii (ESIAs), ushiriki wa umma, na vibali vya udhibiti.”
Iliendelea kusema kwamba “msururu wa shughuli zilizopangwa za ushirikishwaji” zimefanyika katika kaunti za Kilifi na Siaya.
Wizara za mazingira na nishati hazikujibu maombi ya Mongabay ya kutaka habari kuhusu eneo la mtambo huo.

Shirika la NuPEA lilichapisha rasimu ya ripoti yake ya Tathmini ya Kimkakati ya Mazingira na Kijamii (SESA) kwa ajili ya mtambo wa nyuklia mtandaoni. Kulingana na waraka huo, kuna maeneo matatu yanayowezekana: nayo ni ya huko Uyombo katika Kaunti ya Kilifi; eneo la Luanda Kotieno katika kaunti ya Siaya; na katika eneo lisilojulikana katika Kaunti ya Turkana, kaskazini-magharibi mwa Kenya. Kaunti hiyo ya Turkana ni mwenyeji wa Ziwa Turkana, ambayo hivi majuzi iligonga vichwa vya habari kwa sababu ya ugunduzi wa mafuta. Luanda Kotieno iko kwenye kingo za Ziwa Victoria.
Uamuzi wa kuzingatia sehemu ya Luanda Kotieno kama eneo linalowezekana ulikaribishwa na viongozi wa kaunti waliokuwepo. Aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya marehemu Raila Odinga, ambaye alitoka katika eneo hilo, alionekana kuunga mkono mradi huo. “Katika enzi ya mabadiliko ya hali ya hewa, nishati ya nyuklia inakubaliwa kama moja ya vyanzo vya nishati safi ambayo haina uzalishaji wa kaboni,” alisema katika mkutano wa Juni uliofanyika katika taasisi ya JOOUST. “Ukweli kwamba tulichukua eneo hili kama mwenyeji wa mtambo wa umeme ni utambuzi wa faida zake za kipekee za kimkakati.”
Mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2023 huko Dubai, COP28, ulitoa wito wa kuharakishwa kwa maendeleo ya nishati ya nyuklia kama chanzo cha umeme cha chini cha kaboni. Lakini baadhi ya wataalam wanahoji haja ya Kenya kugeukia nishati ya nyuklia.
Kenya inaonekana kama kinara wa nishati mbadala katika bara la Afrika. Kulingana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA), nchi iko katika harakati ya kufikia upatikanaji wa umeme kwa wote ifikapo mwaka 2030 ikiwa na mseto wa nishati ambao tayari unajumuisha 90% ya teknolojia za uzalishaji wa chini kama vile jotoardhi, umeme wa maji, upepo na jua. Nchi ina ardhi kubwa zaidi ya upepo katika bara; Mradi wa Upepo wa Ziwa Turkana unaweza kusambaza hadi megawati (MW) 307 kwa gridi ya kitaifa ya Kenya.
Hata hivyo, kulingana na shirika la NuPEA, matarajio ya maendeleo ya taifa yanaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji yake ya umeme, na kufanya uzalishaji wa sasa wa nguvu za umeme kutotosha – hivyo kufanya uamuzi wa kuchunguza nishati ya nyuklia. “Kubadilisha vyanzo vyetu vya nishati na kudumisha mazingira safi ni muhimu kwa ajenda yetu ya maendeleo,” Odinga alisema katika mkutano huo. “Sehemu ya sababu nchi hii haijaweza kuzalisha na kuendeleza kazi zinazolipwa vizuri ni gharama ya nishati.”
Bado, wataalam wanataja vikwazo vikubwa kabla ya mradi kuendelea kwa usalama. “Jambo kuu ni fedha,” alisema Hartmut Winkler, profesa wa fizikia katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini na mtaalamu wa nishati ya nyuklia. “Miradi ya nyuklia ni ghali mno, na hutaona chochote kikitoka humo kwa angalau miaka 10, labda miaka 20. Miradi ya nyuklia inajulikana kwa kuchelewa kila wakati na inagharimu zaidi kuliko ilivyotarajiwa.”

Winkler pia alizungumzia suala la taka za nyuklia: “Hatimaye, utaishia na taka za nyuklia. Na hiyo italazimu ziende mahali fulani. Je, watamuuzia mtu fulani? Hilo ni jambo linalohitaji kufikiriwa; ni tatizo la muda mrefu ambalo halitaisha,” alisema.
Wakati Tathmini ya Kimkakati ya Mazingira na Kijamii (SESA) yenye kurasa 300 ikitaja mara kwa mara taka za nyuklia, inataja tu kuwepo kwa kanuni, za Kenya na kimataifa, bila kutoa mikakati madhubuti ya mradi husika. Toleo la mwisho la SESA halipatikani kwenye tovuti ya shirika NuPEA au kwenye tovuti za wizara za mazingira na nishati.
Lakini kupitia ombi la Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), chombo huru cha ushauri, Tume ya Uholanzi ya Tathmini ya Mazingira (NCEA), ilipitia Tathmini ya kimakakati ya ya Mazingira na Kijamii (SESA). Ilihitimisha kuwa tathmini haifikii viwango vya utendaji mzuri vilivyowekwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), na “kwa hivyo haijumuishi msingi wa kufanya maamuzi yenye ufahamu.” Ripoti ya tathmini ya SESA inahitaji marekebisho muhimu, shirika la NCEA lilisema, ikiita ukosefu wa maelezo kuwa “upungufu.”
Haijulikani kama wizara zinazohusika zimefanyia kazi mapendekezo ya shirika la NCEA. Mongabay aliwasiliana na Wizara ya Kawi na Petroli ya Kenya na Wizara ya Mazingira kwa maelezo zaidi, lakini hakuna aliyejibu maombi yetu ya mahojiano.
Zaidi ya hayo, mradi unaonekana kutozingatia baadhi ya vigezo kutoka kwa tathmini ya SESA yenyewe, kama vile sharti kwamba “tovuti haipaswi kuwa karibu na maeneo yenye thamani ya kiikolojia au hatarishi au maeneo yenye watu wengi.”
Uyombo ipo karibu na mji maarufu wa bahari wa Watamu, mita chache tu kutoka Mida Creek, ambayo mikoko ni sehemu ya Hifadhi ya eneo lenye uhai la Malindi-Watamu, na Msitu wa Arabuko Sokoke, ambao zote zimeorodheshwa kama Maeneo ya turathi ya Dunia ya UNESCO.
“Tuna kasa hapa, viumbe vya baharini vilivyo kwenye hatari ya kutoweka,” alisema Kingi, mwanaharakati wa mazingira. “Pia tuna matumbawe ya aina yake hapa – matumbawe ambayo yanapatikana hapa pekee. Na wanyama katika Msitu wa Arabuko na mikoko ambayo ni ya kawaida. Unaweza kuipata hapa tu. Hatutaki kupoteza viumbe hawa walio kwenye hatari ya kuangamia.”
Bioanuwai hii pia ni muhimu kwa maisha ya jamii za pwani. “Sisi kama wavuvi, hatupendi mradi huo uwe hapa Uyombo,” Elisha Bombosho Mzee, mwenye umri wa miaka 40 ambaye amekuwa akivua samaki sehemu ya Uyombo kwa zaidi ya miaka 25. “Hatupendi kwa sababu tulisikia watatumia maji ya bahari kwa mfumo wa kupoesha. Wanachukua maji, kisha wanarudisha maji yenye vuguvugu baharini, ambayo yatatuathiri. Samaki watahamia maeneo ambayo hatuwezi kufikia. Sio wazo zuri kuwa na mtambo wa nyuklia hapa pwani.”

Uwepo wa kiwanda cha nyuklia karibu na eneo la thamani la kiikolojia la Ziwa Victoria, ziwa kubwa zaidi la maji safi barani Afrika, kunaweza pia kuwa wasiwasi kwa jamii za wavuvi zinazotegemea ziwa Victoria. Kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya shirika la WWF-Kenya, Maziwa Makuu ya Bara la Afrika yana aina nyingi zaidi za samaki wa maji baridi duniani. Lakini viumbe vamizi wamesababisha Ziwa Victoria kukumbwa na kutoweka kwa wanyama wenye uti wa mgongo katika historia ya kisasa, ripoti hio ilisema. Aidha, Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria linaripoti kuwa ziwa hilo hutoa zaidi ya tani 800,000 za samaki kila mwaka – samaki ambao wanaweza kuambukizwa iwapo taka kutoka kwa kinu cha nyuklia zitasimamiwa vibaya au wakati kunatokea ajali.
Zaidi ya hayo, ziwa hilo linaunganishwa na vyanzo vikuu vya maji, ikiwa ni pamoja na chanzo cha Mto Nile, mto mrefu zaidi duniani.
Rasimu ya ripoti ya Tathmini ya Kimkakati ya Mazingira na Kijamii (SESA) inakubali kuwa eneo pana la Ziwa Victoria linajumuisha “zaidi ya mifumo ikolojia 100 muhimu duniani au kikanda, ikiwa ni pamoja na Maasai Mara-Serengeti, Mlima Elgon, Maeneo ya Nabugabo RAMSAR nchini Uganda, na mazingira ya kuvuka mipaka ya Nyungwe-Kibira.”
Mahitaji ya maji kwa ajili ya kupoesha pia yanatarajiwa kuwa ya juu. Kulingana na rasimu ya tathmini ya SESA, “mahitaji ya maji ya kinu cha nyuklia ni karibu 15-25% ya juu kuliko ya mtambo wa makaa ya mawe. Kwa kuzingatia hali ya hewa ya kitropiki ya Kenya, hitaji la maji linaweza kuwa kubwa zaidi kuliko Ulaya Magharibi.”
Pia, Oluwole Olutola, mtafiti wa baada ya udaktari katika mabadiliko ya hali ya hewa na siasa za mazingira katika Chuo Kikuu cha Johannesburg, nchini Afrika Kusini ambaye anajishughulisha na kazi za nishati ya nyuklia, alisema alikuwa na matumaini kuhusu matarajio ya nishati ya nyuklia nchini Kenya. “Ikiwezekana mahali pengine, itawezekana barani Afrika. Kuna viwango vya kimataifa vya kudhibiti upotevu, na nchi za Afrika ni sehemu ya itifaki na makubaliano haya. Ni suala la kufuata tu,” alisema. “Ninahisi hii ndio njia ya kutoka kwa shida kubwa ya nishati ambayo Afŕika imeikabili kwa miaka mingi.”
Lakini wanachosema wenyeji wa sehemu ya Uyombo kinachowatia wasiwasi zaidi ni ukosefu wa mawasiliano kutoka kwa serikali. “Tulisikia walichagua eneo lingine, lakini bado tunasubiri mawasiliano ya wazi kutoka kwa shirika la NuPEA,” alisema Sanita Kitole, mkazi wa Uyombo na mwanachama wa Kituo cha Haki ya Utawala na Mazingira, ambaye alipinga mradi huo katika mji wake wa asili.
“Walikuja tu na kusema, ‘Hapa ndipo tutajenga kituo cha kuzalisha umeme.’ Hawakutuhusisha tangu mwanzo, hawakueleza nishati ya nyuklia ni nini. Tulipouliza maswali, tulikamatwa.”
Tangia wakati huo, Kitole alisema, amekuwa akiishi kwa hofu. “Walininyang’anya simu yangu, wakachukua nambari yangu, kila kitu. Bado sihisi salama. Wakati mwingine ninapozungumza kwenye simu, nasikia usumbufu wa ajabu, kama vile mtu anasikiza mazungumzo katika simu yangu.”
Wakati wa kongamano lililofanyika katika chuo kikuu cha sayansi na teknolojia chaJOOUST, maafisa wa serikali, wanasiasa na wawakilishi wa shirika la NuPEA walisisitiza mara kwa mara hitaji la kushirikisha jamii za mashinani na kuhakikisha wanafahamishwa na kuhusika vyema.
Kulingana na timu ya mawasiliano ya shirika la NuPEA, mashauriano yalifanyika pamoja na wenyeji wa kaunti ya Siaya mwezi wa Septemba hii.
Picha ya bango: Wavuvi wakiwa na nyavu kwenye Ziwa Victoria nchini Kenya. Picha na Zoriah kupitia Flickr (CC BY-NC 2.0).
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 08/10/2025.