- Kambi inayojulikana kama Ritz-Carlton Masai Mara Safari, hoteli ya kifahari ambayo gharama zake kwa usiku mmoja tu ni Dola za Kimarekani 3500, imejengwa kandokando ya Mto Sand, eneo muhimu la viumbe hai linalotumiwa na makundi ya nyumbu, pundamilia na swala wakati wa uhamaji wao wa kila mwaka.
- Hoteli hiyo imejengwa huku kukiwa na maagizo ya Rais kuzuia ujenzi wa miundombinu mipya katika maeneo nyeti ya uhifadhi,jambo lilioibua maswali kuhusu uhalali kwa mradi huo.
- Kwa mujibu wa Meitamei Ole Dapash, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu, Utafiti na Uhifadhi ya Wamasai, (MERC), mradi huo ulitekelezwa bila kuwashirikisha wananchi wa eneo hilo, kitu ambacho ni kinyume cha sheria na taratibu za ujenzi katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Katika hifadhi ya kitaifa ya Maasai Mara iliyoko nchini Kenya, ujenzi wa hoteli ya kifahari umeibua utata mkubwa. Hoteli hiyo inayojulikana kama Ritz-Carlton Masai Mara Safari Camp, inasimamiwa na kundi la hoteli la Marriott International.
Hoteli hii ya kifahari inayotarajia kufunguliwa katikati ya mwezi Agosti, ina idadi ya vyumba binafsi 20, bwawa la kuogelea lisilo na ukingo, spa na huduma nyingine nyingi. Gharama za chini za kulala kwenye hoteli hiyo ni Dola za Kimarekani 3,500 kwa usiku mmoja tu. Hata hivyo kinacholeta utata hapa si hali ya kifahari ya hoteli hiyo bali mahali ilipojengwa, yaani kandokando ya Mto Sand, kwenye njia muhimu inayotumiwa na wanyamapori katika uhamaji wao.
“Mahali walipojenga ni eneo linalosifika sana kwa uhamaji mkubwa wa wanyama aina ya nyumbu kati ya Tanzania na Kenya. Kila mwaka, kipindi kama hiki, mamilioni ya wanyama wakiwemo pundamilia na swala, huvuka mto huu. Kwa kawaida, wanyama hawa huvuka kupitia maeneo maalum. Kwa hiyo ujenzi wa hoteli hiyo maeneo hayo, unavuruga sana mwenendo wao,” anaeleza Meitamei Ole Dapash, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu, Utafiti na Uhifadhi ya Wamasai (MERC), ambaye pia ni mwanachama wa jamii ya Waamasai.
Uhamaji mkubwa wa wanyama hutokea katika kipindi kinachoanzia mwezi Juni hadi Oktoba kila mwaka ambapo wanyama wanaoishi kwa kula majani, kutoka Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania huhama kwenda kufuata malisho. Ili kufanikisha safari hii, makundi makubwa huvuka mito kadhaa na hatimaye kufika Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara nchini Kenya. Tukio hili la kiasili huvutia maelfu ya watalii, kwa sababu ya muonekano wa makundi makubwa ya wanyama yakisogea kwa pamoja na namna wawindaji wanavyoingilia safari hiyo ya wanyama.
Ni fursa nzuri ya kuingiza fedha. Hata hivyo wingi huu wa watalii wakati mwingine huleta changamoto kama ilivyoelezwa katika mpango rasmi wa usimamizi wa hifadhi hiyo ya taifa ya Kenya: “Kuna kipindi ambapo magari zaidi ya 150 yalionekana kwenye eneo moja la kuvukia… Siku za nyuma, msongamano wa magari umewahi kuvuruga na kusababisha msongamano mkubwa wa wanyama, uliosababisha vifo vya nyumbu wengi walipokuwa wakijaribu kuvuka mto.”

Ili kutafuta ufumbuzi wa suala hili, mamlaka za Kenya zilichukua hatua mbalimbali. Kwa mfano, mwaka 2023, Rais alitoa agizo akiamuru Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kusitisha utoaji wa leseni na vibali kwa miradi katika maeneo muhimu ya uhifadhi hadi sera ya uhifadhi itakapowekwa. Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa katika agizo hilo ni Kaunti ya Narok, ambako Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara inapatikana. “Hoteli hii ilijengwa baada ya kutolewa kwa agizo hili, hali inayoonyesha kuwa agizo la Rais lilipuuzwa,’’ anasema Ole Dapash.
Taasisi ya Elimu, Utafiti na Uhifadhi ya Wamasai (MERC), ilimwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Marriott International, Anthony Capuano, ikiomba kupatiwa nyaraka zote ambazo zinahitajika kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya ujenzi wa hoteli hiyo, ikiwa ni pamoja na ripoti ya tathmini ya athari za mazingira. Hata hivyo hadi muda wa kuchapisha makala hii, MERC walikuwa bado hawajajibiwa.
Mongabay iliwasiliana na idara ya mawasiliano ya Marriott International kwa maelezo zaidi. Waliitumia Mongabay taarifa fupi kwa barua pepe, ambayo sehemu yake ilisema hivi: “Tunaelewa umuhimu wa eneo la Sand River na mandhari yote ya Maasai Mara. Tunafanya kazi kwa karibu na Lazizi Mara Limited, wamiliki na waendelezaji wa kambi hiyo kutoka Kenya, ambao wamethibitisha kuwa wamekamilisha masharti yote muhimu kwa ajili ya ufunguzi wa kambi hiyo. Hii inajumuisha kupata vibali na idhini zinazohitajika kutoka kwa mamlaka husika za Kenya.”
Hata hivyo, licha ya kudai kuzingatia uwazi, Marriott International wilikataa kujibu maswali yetu. Ukosefu huu wa uwazi ni jambo ambalo mtaalamu huyu wa uhifadhi analisikitikia.
“Hatujaelezwa chochote kuhusu namna serikali ya Kaunti ya Narok ilivyoidhinisha ujenzi huu unaokiuka agizo la rais linalokataza maendeleo mapya katika maeneo haya yaliyohifadhiwa. Njia nyingine ambayo Marriott iliweza kupata kibali hiki ni kupitia rushwa, na ninajua rushwa imeenea sana katika Kaunti ya Narok, kama ilivyo katika maeneo mengine nchini hapa,” anasema Ole Dapash.

Wasichana wa Kimasai nchini Tanzania wakiwa wamebeba mizigo ya kuni kupeleka majumbani kwao kwa ajili ya kupikia. Picha na Yulia Avdeeva kupitia Wikimedia Commons ( CC BY-SA 4.0 ).
Baadaye Mongabay iliwasiliana na uongozi wa Kaunti ya Narok, ambao hawakutoa majibu. Jitihada za kuwasiliana na Lazizi Mara Limited, zilishindikana kutokana na kukosekana kwa taarifa za namna ya kuwafikia.
Licha ya mahali ujenzi ulipofanyika, Ole Dapash pia anaibua hoja nyingine kuhusu ujenzi wa hoteli hii. Anasema wahusika hawakuwashirikisha wakazi wa eneo hilo kabla ya kuanza kazi: “Walipaswa kufanya kile ambacho kitaalam kinajulikana kama tathmini ya athari za mazingira.
Huu ni uchunguzi wa kisayansi kuhusu athari za kimazingira zinazoweza kusababishwa na shughuli yoyote katika eneo nyeti kiikolojia kama ilivyo kwa Hifadhi ya Maasai Mara. Moja ya hatua za uchunguzi huu ni kuomba maoni ya jamii inayoishi jirani na eneo husika, yaani kufanya mashauriano na wananchi. Mimi mwenyewe ni mtetezi wa mazingira, ni Mmasai, na mtu ninayefuatilia na kuelewa mambo muhimu yanayoendelea katika jamii. Sijasikia kuwepo kwa mikutano yoyote ya mashauriano. Nilipata taarifa kuhusu hoteli hii wakati mtu mmoja aliponiuliza nini kinaendelea na kama nilikuwa na taarifa zozote.”
Kwa kuwa eneo hilo liko mbali na pia kipindi hicho hakikuwa cha msimu wa uhamaji wa wanyama, hakuna mtu aliyekuwa akienda huko, hivyo hatukubaini kinachoendelea; kila kitu kilifanyika kimya kimya.
Taarifa ya Marriott International kuhusu utata huu, ilitoa maelezo ya jumla ikisema; “Marriott International tunazingatia sana uadilifu, uwazi, na tunaheshimu mazingira na jamii za maeneo tunayofanyia kazi.
Tunachukulia kwa uzito mkubwa uwajibikaji wa hoteli zetu tukihakikisha zinakidhi kanuni za kisheria za eneo husika na viwango vya kimataifa, vikiwemo vile vinavyohusiana na usimamizi wa mazingira, urithi wa kitamaduni, na ushirikishwaji wa jamii.”
Wakati wageni wa kwanza wakijiandaa kuingia kwenye hoteli ya Ritz-Carlton, utata unazidi kuongezeka. Madai makubwa yanayoleta mtafaruku ni matatu; kupuuza maagizo ya Rais, kutotoa nafasi kwa wana jamii kutoa ushauri wao pamoja na mradi huo kuwa tishio kwa moja ya maeneo yenye uhamaji mkubwa zaidi wa wanyama duniani. Upo uwezekano mkubwa wa suala hilo kuishia mahakamani. Taasisi ya MERC imetangaza kwamba inatarajia kufungua kesi dhidi ya Marriott iwapo haitapokea majibu ya barua iliyowatumia.
Picha ya Bango: Ujenzi wa hoteli hii ya kifahari unaathiri uhamaji wa nyumbu kati ya Tanzania na Kenya. Picha na Daniel Rosengren kupitia Wikimedia Commons (CC BY 4.0).
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kifaransa mnamo tarehe 12/08/2025