- Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2004, shirika la Northern Rangelands Trust (NRT) limevutia wengi, na kwa wakati huo huo kukosolewa kwa kuwahimiza jamii wasajili unifadhi wa wanyamapori kaskazini mwa Kenya.
- Mapemma mwaka huu, mahakama Kenya iliamua kuwa hifadhi mbili za wanachama wa shirika hili zilikuwa zimeundwa kinyume cha sheria. Mwezi huo pia NRT ilipoteza mfadhili mkuu,kabla ya ufadhili wa USAID kusimamishwa.
- Kulingana na mwanzilishi wa shirika hilo, ambaye alisukumwa nje na bodi,kusimamishwa kwa mradi wa mkopo wa kaboni, ambayo NRT ilisimamia, kumesababisha ‘kufa’ kwake.
GOTU, Kenya — Ni saa ya alasiri kwenye mji mdogo wa Gotu, kaskazini mwa Kenya. Kivulini mwa mti mmoja wa mkakaya (mwatiko, mgunga), kundi la wazee limekusanyika kujadili masuala ya kijamii.
Mji huu mdogo uliopo umbali wa takribani kilomita 52 kutoka mji wa Isiolo una shughuli nyingi za ulishaji wa mifugo. Kila unapopita, utawaona vijana wakichunga makundi ya ngamia kando ya barabara, huku mbuzi wakila majani mabichi na mimea karibu na makao yaliyojengwa kwa matofali, au udongo, na yenye paa za mabati. Mto uliokuwa karibu sana unaelekea kukauka kufuatia kiangazi. Umebakia mkondo mwembamba tu, huku jamii zikitarajia mvua kila kunapokucha.
Rashid Susa, mwenye umri wa miaka 70, ni mmoja wa wafugaji hawa wanaojadili masuala ya mifugo. Rashid, aliye na ndevu zilizopakwa rangi nyekundu, anaunga mkono shirika moja lisilo la kiserikali, maarufu kama Northern Rangelands Trust (NRT), ambalo linajihusisha na uhifadhi.
Mzee huyu anasema kwa miaka 14 sasa, shirika hili la NRT limesaidia jamii nyingi katika eneo la Gomu. Anaorodhesha faida kama vile mishahara kwa walinzi wa wanyamapori wanaotoka kwenye jamii, ufadhili wa masomo kutokana na malipo ya mikopo ya kaboni, pamoja na usaidizi kuhakikisha kuwa mifugo iliyoibwa baada ya uvamizi wa jamii jirani, imefuatwa na kurudishwa kwa wamiliki.
Wazee wengine wote wanatikisa vichwa vyao, ishara kuwa wanakubaliana na Susa. Mji huo mdogo ni sehemu ya hifadhi ya Nakuprat-Gotu, ambayo ni mojawapo ya hifadhi 45, ambazo pia ni wanachama wa NRT nchini Kenya na Uganda.

Angalau katika kundi hili la wanaume wazee, NRT inapendwa. Wanaume hawa ni wa jamii ya Borana, lakini kwenye hifadhi yao wanashirikiana na wachungaji wa Kiturkana ambao zamani walikuwa adui wao. Vurugu na wizi wa mifugo kati ya jamii hizi mbili ulikuwa mbaya kiasi cha kukomesha kutumika kwa barabara kuu inayopita mjini, kabla ya usimamizi wa pamoja wa Nakuprat-Gotu kuimarisha uhusiano wao.
“Hatimae walijiunga kuunda hifadhi, kisha wakachanganyika,” asema Gallogallo Halkano, ambaye mwaka jana alimaliza muhula wake wa pili kama mwenyekiti mteule wa bodi ya Nakuprat-Gotu. “Walinda-wanyamapori waliajiriwa, wakakaa pamoja na kuwa marafiki. Baadaye jamii zilianza kushirikiana katika mradi huo na hatimaye kukawa na amani”..
Hii ndiyo taswira ya jinsi NRT inavyofanya kazi Kaskazini mwa Kenya, na ambayo inaendana na mtazamo wa shirika lenyewe. Miaka 20 tangu kuanzishwa na mwanahifadhi Ian Craig, NRT imekuwa shirika kubwa. Hifadhi ambazo Craig na NRT walisaidia kuanzisha, sasa zinachukua zaidi ya 10% ya eneo lote la Kenya: hekta milioni 6.37 (ekari milioni 15.74).
Ikiwa kama mbadala wa mtindo wa zamani wa hifadhi za kitaifa — uliokuwa ukihusisha ujenzi wa ngome na ambao ulitawala barani Afrika tangu enzi za ukoloni — NRT inachukuliwa kuwa jaribio lililofanikiwa kwa kiasi kikubwa katika uhifadhi wa jamii barani Afrika. “Sisi, kama hifadhi ya Nakuprat-Gotu, tunaunga mkono NRT,” anasema Susa. Hata hivyo, anaongeza kuwa, kuna baadhi ya wakaaji wa Gotu ambao wanasema NRT inaweza kuanguka wakati wowote.
Tangu 2024, NRT imekumbwa na misukosuko na migogoro ambayo ilifikia kilele mwezi wa tano mwaka huu, wakati Verra – shirika lisilo la kibiashara linalohusika na uthibitishaji wa mikopo ya kaboni, lilipositisha idhini ya mradi inayosimamia, kwa mara ya pili sasa.
Hadi sasa, mradi huo umenufaisha watu wengi kupitia mamilioni ya dola yanayotolewa kusimamia njia za malisho ya mifugo kwa namna ambayo itakawezesha kuongezaka kwa uhifadhi wa kaboni kwenye udongo. Huu mradi pia umekuwa chanzo kikubwa cha fedha kwa NRT na hifadhi zingine ambazo ni wanachama wake.
Kusitishwa huku kulitokana na uamuzi wa mahakama nchini Kenya katika mzozo juu ya uhalali wa hifadhi mbili kubwa za NRT. Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Kenya iliamua kuwa hifadhi hizo mbili zilianzishwa bila kuhusisha umma ipaswavyo, kinyume na sheria.
Isitoshe, ufadhili kutoka Shirika la Misaada la Marekani, USAID, ambao umekuwa nguzo ya fedha katika utendaji wa NRT, ulisimama ghafla wakati utawala wa Marekani ulipobadilika. Kando na haya, Craig mwenyewe aliondoka mwaka jana, baada ya kutofaumzozo mkubwa na bodi ya shirika hilo.
Hali imekuwa ngumu na isiyo ya kawaida huko NRT. Na siyo kila mtu anaitakia mema.

Magharibi mwa Gotu, katika mji wa Biliqo, Hassan Godena, mwenye umri wa miaka 75, ameketi ndani ya nyumba yake ndogo. Mwili wake umedhoofu. Miaka kumi imepita sasa tangu kuuawa kwa mke wake na bintiye kwenye uvamizi wa mifugo. Anaihusisha NRT na vifo vyao, na vya wengine wengi kutoka Biliqo, ambao wameuawa katika mapigano baina ya jamii. Mtazamo huu unashikiliwa na wengine wengi, ambao hawapendezwi na uhusiano mkubwa baina ya NRT na jamii jirani ya Samburu, ambayo kwa muda mrefu imekuwa adui ya wafugaji wa Borana kutoka eneo hili.
Godena anatofautiana sana na wale wazee wa Gotu. Mtazamo wake unasisitiza siasa za chuki kwenye uhifadhi wa jamii kaskazini mwa Kenya, ambapo NRT imechukua majukumu ambayo kwa kawaida huwa ya serikali. Hii inaonyesha kina cha matatizo ambayo NRT inakabiliana nayo. “Tutakomesha yule mnyama aitwaye NRT,” anasema, huku uso wake ukionyesha uchungu mwingi.
Vita mahakamani na kutupiana lawama
Kwa miaka ishirini ambayo NRT imekuwepo sasa, shirika hilo limepata umaarufu haraka sana kaskazini mwa Kenya. Baada ya kuchochewa na upungufu wa idadi ya vifaru na tembo, Craig alihimiza jamii zinazoishi karibu na shamba lake la uhifadhi la Lewa kuanzisha hifadhi zao binafsi za wanyamapori. Hawa ndio walikuwa wanachama wa kwanza wa NRT.
Kila jamii ilipojiunga na mfumo uliotengenezwa na Craig na NRT kama mwanachama, ilitia saini mkataba ili kuruhusu ardhi yake kusimamiwa kwa lengo la uhifadhi. Kama malipo, NRT imekuwa ikisaidia kutoa mafunzo na kuwapa vifaa walinzi wa wanyamapori wa jamii wanaoitwa “skauti”. Pia, shirika hilo huelekeza fedha za wafadhili kwa miradi ya maendeleo kama vile shule na visima vya maji.
Baadhi ya hifadhi hizi zimefuzu kuwa sehemu ya Mradi wa Kaboni wa Northern Kenya Rangelands, na zimezalisha makumi na mamilioni ya dola kutokana na mikopo ya kaboni ya udongo iliyonunuliwa na wanunuzi wa kampuni mbalimbali. Mikopo hiyo inatoka kwa hifadhi zilizokubali kushiriki katika utekelezaji wa sheria za malisho ya mzunguko, ambayo huwezesha nyasi kumea tena, huku ikihifadhi kaboni.
Si kila mtu anayeishi ndani ya maeneo ya hifadhi ana haki ya kushiriki katika uchaguzi wa bodi za uongozi kwa kupiga kura. Hili jambo limekuwa chanzo cha migogoro kuhusu uwakilishaji. Kwa kawaida, hifadhi husajiliwa na mashirika ya kijamii. Ili kuwa kamilifu, NRT inahitaji hifadhi kuthibitisha kwamba imepata ridhaa ya jamii nzima kwanza. Lakini wanachama wengine wamekosoa mchakato huo na kusema kuwa una udhaifu na wa ovyo.

Mwaka 2021, kundi la utetezi la Oakland Institute, lililoko Marekani, lilichapisha ripoti iliyowashutumu walinzi wa NRT kwa kuhusika na vifo vya wafugaji wa Borana huko Biliqo Bulesa, ambayo ni mojawapo ya hifadhi zake kubwa. Ripoti hiyo iliwalaumu walinzi hao kwa kukiuka haki za ardhi za watu wasiounga mkono miradi ya hifadhi. Uchunguzi mwingine huru ulioagizwa na The Nature Conservancy, mojawapo ya wafadhili wa NRT, haukupata ushahidi wowote dhidi ya walinzi hao wa wanyamapori. Hata hivyo, ripoti hiyo ilikiri kuwa uanzishwaji wa Biliqo Bulesa mnamo mwaka 2007 “uliongozwa na viongozi wachache wa jamii wenye uhusiano wa karibu na NRT”.
Mnamo Januari 24, mwaka huu, Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Kenya iliamua kwamba hifadhi za Biliqo Bulesa na Cherab zilianzishwa kinyume na sheria. Zote mbili zinamilikiwa, kwa kiasi kikubwa, na jamii ya Borana iliyoko katika kaunti ya Isiolo, magharibi mwa Gotu kuelekea Somalia. Uamuzi huo ulisababisha maandamano kaunti nzima, kila pande ikilaumu ingine kwa kupotosha maoni ya wakazi wa hifadhi. “Walitupeleka mahakamani bila ridhaa ya jamii na kupunguza kasi ya shughuli za hifadhi,” Mohammed Waka, ambaye ni meneja wa Biliqo Bulesa na pia mfanyakazi wa NRT, alisema. “Sisi kama jamii tilishtuka”.
Mzozo huu unagusa kiini cha maono ya NRT ya uhifadhi wa mazingira. Kundi hilo limesema kuwa kwa muda mrefu sasa jamii zinafaa kuwezeshwa kutunza wanyamapori na mazingira wao wenyewe, bila kutegemea mashirika ya serikali kama Huduma ya Wanyamapori Kenya. Lakini, je, ni nini hutokea kila wanachama wa jamii wanapokosa kukubaliana au kupatana?

Waka anapuuza kesi iliyofika kotini akidai ilifanywa na wachache walioshawishiwa na watu wa nje kupinga NRT. “Wanajamii wengi wanaunga mkono kazi yetu, kwa sababu wanaona faida ya uhifadhi,” anasema.
Lakini Innocent Makaka, ambaye ni wakili mkuu wa walalamikaji 165 kwenye kesi hiyo, anapinga mtazamo huo. “Unamaanisha nini ukisema wengi? Hukuwaalika hata wateja wetu kwenye mikutano ili waamue wanachotaka. Hiyo ni hoja ya kujaribu kupuuza hukumu ya koti”.
Ombi la NRT la kusitisha hukumu katika kesi hiyo lilikataliwa mwishoni mwa Aprili. Shirika hili sasa linaendelea kupitia mchakato wa rufaa nchini Kenya. Iwapo koti itaidhinisha uamuzi huo, hukumu hiyo haitatumika moja kwa moja kwa hifadhi zingine chini ya mwavuli wa NRT. Hata hivyo, Makaka anasema, inaweza kuwa mfano itakayotumika kuibua changamoto kama hizo, ikiwa mtu yeyote anayeishi katika hifadhi hizo atachagua kwenda mahakamani.
Mambo ni mengi. Mnapo mwezi Mei, Verra, shirika ambalo linathibitisha mikopo ya kaboni ili kuuzwa kwenye masoko ya kimataifa, liliweka mradi mkuu wa kaboni wa NRT katika ukaguzi. Biliqo Bulesa ni mmoja wa kundi shirika. Mwaka jana, Mfuko wake wa Kaboni ya Jumuiya ulipata karibu Dola za Kimarekani 200,000 kutokana na mauzo. Sehemu ya mapato hayo yalitumika kuwalipia wanafunzi 550 karo za shule. Kwa ujumla, katika mwaka wa 2024, takriban dola za Kimarekani millioni mbili na nusu zilichukuliwa kutoka kwenye fedha hizo na kugawiwa jamii 22 ambazo zimetoa ardhi kwa ajili ya mradi huo wa kaboni.
Kulingana na taarifa ambayo Mongabay ilipokea kwa barua pepe, Verra ilithibitisha kwamba uamuzi wake ulisababishwa na ule wa mahakama, na hivyo kusitisha uthibitisho wa mradi huo. Ikiwa Verra haitairejesha NRT tena, malipo hayo hayatakuwepo tena. “Shughuli za hifadhi zikisitishwa, hatutapata fedha za kaboni, ambazo zilibadili maisha ya wanajamii,” Waka anasema.

NRT inatarajia mradi huo ufaulu kwenye ukaguzi wa “Kifungu cha 6” wa Verra. “Mradi huu umezingatia mahitaji ya Kiwango cha Kaboni Kilichothibitishwa kikamilifu. Hiki Kifungu cha 6 kitaendelea sambamba na ukamilishaji wa uhakiki ujao wa mradi, ikiwa ni pamoja na uwasilishaji wa maoni ya kisheria ya nje,” NRT ilisema katika taarifa ya pamoja na Native, shirika lililotengeneza mradi huo, iliyotumwa kwa barua pepe kwa Mongabay.
Walalamikaji katika kesi hiyo hawapingi uhifadhi, ila wanataka kuhusika katika kupanga maamuzi yanayozingatia sheria ya ardhi ya jamii Kenya, badala ya kanuni za hifadhi za NRT.
“Tunasisitiza usajili wa ardhi ya jamii, ndiyo kuwe na mwelekeo wa namna ya kuishirikisha jamii,” Makaka anasema.
Hapa Biliqo, mji wenye upepo mkali na wafugaji wengi, uamuzi huo ni pigo kubwa kwa baadhi yao, ingawa kuna wale wanaosherehekea. Wengi wa watu hapa wanaunga mkono madai ya Waka, lakini si vigumu kupata wapinzani wake. “Tangu waje, nimekuwa nikiwapinga,” asema Hadija Jillo, mmiliki wa duka kwenye barabara kuu yenye vumbi Biliqo. Waka ni miongoni mwa watu walioshangilia uamuzi wa mahakama ulipotolewa Januari, na pia anayejieleza kama “mwanzilishi” katika kesi hiyo. “Hatutaki kuona wafanyakazi au magari ya NRT huku kwetu,” anaongeza.
‘Nadhani NRT imekufa’
Kwa sasa, sio Biliqo pekee inayoshuhudia upinzani mkali dhidi ya NRT kule kaskazini mwa Kenya. Tayari kuna pingamizi kutoka pande ambazo hazikutarajiwa: kama vile Lewa, na Ian Craig mwenyewe. Kabla ya mwaka jana, ilikuwa ngumu kutenganisha NRT na Craig akilini mwa wengi kaskazini mwa Kenya. Craig ndiye alifikiria na kuanzisha mradi huu, huku akiwashawishi wafadhili na viongozi wa jamii kaskazini kumwamini na kujiunga naye katika uhifadhi wa aina hii.
“Tulienndeleza shirika kwa miaka 20 kwa lengo moja tu: kutumia uhifadhi kama chombo cha kuziunganisha jamii na kuleta maendeleo,” anasema kwa sauti ya utulivu, akiwa ameketi kwenye benchi ndani ya bustani ya Lewa, huku twiga akipita nyuma yake.

Kwa muda mrefu, sura ya Craig, ambaye ni mzaliwa wa kizazi cha walowezi weupe nchini Kenya, ndiyo imekuwa ikiwakilisha NRT. Chini ya uongozi wake, shirika hilo limepata tuzo mbalimbali kama vile taji la uungwana na Nishani ya Ufalme wa Uingereza. Lakini pia, kuwa kwake maarufu kumemfanya kuwa mlengwa mkuu wa wakosoaji wa shirika hilo. “Mimi ni wa asili ya ukoloni, mimi ni mzungu, mimi ni mzee, mimi ndiye shabaha kamili kwa Survival (International) na Oakland, na wote wanaotaka kutupa mabomu,” anasema Craig.
Bodi ya NRT iko chini ya uongozi wa Julius Kipng’etich, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya bima ya Jubilee Holdings. Bodi hii inajumuisha viongozi wengine wakuu kutoka jumuiya za biashara, uhifadhi na wafadhili wa Kenya. Ruben Lendira, ambaye ni meneja wa hifadhi ya faru ya Sera, anasema kulikuwa na mgogoro mkubwa kati ya Craig na bodi hiyo mwaka jana. “Walitaka kumfukuza ili wachukue usukani,” Lendira alituambia akiwa ofisini mwake karibu na hifadhi.
Juni mwaka jana, NRT ilitoa taarifa ya kushangaza, ikisema kuwa Craig alikuwa amestaafu. Siku chache baadaye, Craig aliishutumu bodi ya shirika hilo kwa “usimamizi mbaya” huku akiikosoa kwa kumuachisha kazi msimamizi wa fedha na pia kuhamisha makao makuu ya shirika hilo kutoka Lewa.
Wote hawa hawakutengana kirafiki, jambo ambalo limegawanya wanajamii kaskazini mwa Kenya na ndani ya baadhi ya hifadhi za NRT.
“Nadhani tangu Ian afukuzwe, mambo yamezorota huku NRT, hasa kwa upande wa shughuli zake na misaada kwa jamii,” asema Lendira.

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya NRT ilinukuu bodi ikisema kuwa uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya shirika hilo kutoka Lewa ulifanywa ili iwe rahisi kufikika. Kuhusu suala la kustaafu, taarifa iliongeza kuwa sera ya shirika hilo linawataka wafanyikazi kustaafu kila wanapofikisha umri wa miaka 60.
Tom Lalampaa, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa NRT, hakujibu ombi la Mongabay la kupata maoni yake kuhusu jinsi Craig alivyotoka kwenye shirika hilo. Kwa upande wake, Craig hakusita kuelezea uchungu alionao kutokana na jinsi alivyotolewa NRT. “Nadhani NRT imekufa,” anasema. “Sio mgogoro, tunasubiri tu sherehe ya mazishi yake”.
Kupoteza msaada wa USAID
Kuongezea matatizo yake ya awali, NRT imelazimika kukabiliana na kupoteza ghafla, wafadhili wake wakuu: USAID. NRT ilikataa kujibu swali kuhusu asilimia ya bajeti yake ambayo ilifadhiliwa na shirika hilo la msaada. Hata hivyo, ni wazi kwamba kati ya mwaka 2015 na 2020, NRT ilipokea karibu Dola za Kimarekani milioni 20 kutoka USAID. Huo msaada uliendelea hadi mwaka wa 2024. Anaponena mwanzoni mwa ripoti ya NRT ya mwaka wa 2024, Kipng’etich alishukuru USAID na kuliita shirika “lenye umuhimu katika kuendeleza dhamira zetu”.
Lendira anasema, kutokana na ukatishwaji wa msaada wa USAID mnamo Januari, NRT ililazimika kuwaachisha kazi wafanyakazi karibu 100. Craig anaongezea kuwa hilo halikuwa pigo pekee la kifedha kwa NRT mwaka huu.
“Mimi ndiye niliyesimama kidete kuhakikisha misaada binafsi inakuja NRT. (Misaada) yote imeambatana nami kwa sababu ya ukosefu wa imani kwa waliobaki,” anasema.

Msemaji wa NRT alikana kuwepo kwa taswira ya kifedha kwao. “Hatujapoteza ruzuku yoyote, au hata michango muhimu, isipokuwa ufadhili wa USAID, ambao ulifutwa kufuatia agizo la utendaji,” aliandika katika barua pepe. “Kama mashirika mengine yote yaliyoathirika, hili lilisababisha kupunguzwa kwa wafanyakazi. Hata hivyo, shughuli zetu na miradi yetu inaendelea bila tatizo”.
Itakumbukwa kwamba katika miaka 20 ambayo NRT imekuwepo, kumekuwa na mabadiliko mengi kaskazini mwa Kenya, ikiwemo kuanzishwa kwa mtandao mpana wa hifadhi za jamii, miradi ya kaboni, vifaa vya utalii, na shughuli za walinzi. NRT pia imekuwa mojawapo ya mipango ya uhifadhi yenye umaarufu sana Africa Mashariki, huku ikiwa na manufaa mengi kwa kila nyanja ya maisha ya wakaaji hapa.
Sasa imechanganyikiwa, kwa upande mmoja ikiwa imempotesa mmoja wa wafadhili wake wakuu, na kwa upande mwingine vita vya maneno vikipamba moto baina yake na mwanzilishi wa shirika hilo. Kinachoendelea hivi sasa ni hali ya kisheria isiyoeleweka kufuatia kesi ya haki za ardhi ambayo pia inaathiri chanzo cha ufadhili unaotokana na mikopo ya kaboni.
Jinsi safari ya NRT itakavyoendelea kutoka sasa itakuwa na athari kadhaa wa kadha kote, ikiwemo uhifadhi unaoongozwa na jamii kote Afrika Mashariki. “Shirika halitafungwa,” Lendira anasema, “lakini litalazimika kupunguza misaada”.
Picha ya bango: Mchungaji akiwa na mbuzi wake katika Kaunti ya Isiolo, Kenya. Picha na Ashoka Mukpo, Mongabay.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 20/05/2025.