Shirika la kuthibitisha mikopo ya kaboni, Verra, limeuweka Mradi wa Kaboni wa Malisho ya Kaskazini mwa Kenya, kwa lugha ya Kingereza, Northern Kenya Rangelands Carbon Project, chini ya mapitio kwa mara ya pili, jambo ambalo limethibitishwa kwa Mongabay kupitia taarifa ya barua pepe. Kabla ya hayo mapitio kukamilika, huo mradi hautaruhusiwa kuuza hati zozote za kaboni unazozizalisha kupitia modeli yake ya kusimamia njia za malisho ya mifugo. Huu uamuzi umekuwa pigo kwa Northern Rangelands Trust (NRT), shirika la uhifadhi lenye makao yake makuu nchini Kenya, ambalo huratibu mtandao wa hifadhi za wanyamapori za jamii zinazoshiriki katika mradi huo wa kaboni.
Mapema mwaka huu, mwezi Januari, mahakama ya Kenya iliamua kwamba hifadhi mbili zilizohusishwa na NRT zilikuwa zimeanzishwa kinyume cha sheria, na bila ushirikishwaji wa umma ipasavyo. Moja ya hifadhi hizo, Biliqo Bulesa Conservancy, imekuwa ikizalisha mikopo ya kaboni kwa kupangilia njia za misimu ya malisho ya mbuzi, ng’ombe na mifugo mingine kwenye maeneo hayo.
Wateja wakubwa kama Meta na Netflix, wamenunua mikopo ya kaboni ya mamilioni ya dola tangu mradi kuanzishwa mwaka 2012.
Takriban wafugaji 165 kutoka Kaunti ya Isiolo, kaskazini mwa Kenya, walikwenda mahakamani na kudai kuwa viongozi wa hifadhi hiyo hawakufanya mashauriano ya kutosha kabla ya kuisajili mwaka 2007. Verra liliiambia Mongabay kwamba uamuzi wao wa kusimamisha mradi huo ulitokana na ule wa mahakama uliotolewa na jopo la majaji watatu.
“Mwanzilishi wa mradi, ambayo ni NRT, inahusika kwenye kesi ya kisheria iliyopelekea hukumu ya mahakama mnamo Januari 2025. Huku ikiwasilisha rufaa, NRT iliomba kusitishwa kwa uamuzi huo, lakini ombi hilo lilikataliwa. Kwa hiyo, Verra ilichukua hatua rasmi ya kuusitisha mradi huo,” msemaji wa Verra aliiambia Mongabay.
Hii ni mara ya pili sasa kwa mradi huo tata kuwekwa chini ya mapitio na Verra. Mnamo mwaka 2023, jambo hili lilitokea baada ya makundi ya kutetea haki za binadamu kuibua maswali kuhusu mbinu za mradi huo, lakini baada ya miezi michache tu, ulirudishwa tena.
Ingawa hifadhi zingine zinazoshiriki kwenye mradi huo hazikuathiriwa na uamuzi wa mahakama, wachambuzi wengi wamesema kuwa umeweka mfano ambao unaweza kutumika kupinga uhalali wa hifadhi hizo pia. Wale wanaounga mkono mradi huo wa kaboni wanasema kuwa kufungwa kwake kutazuia jamii zinazoshiriki kaskazini mwa Kenya kupata fedha muhimu kwa ajili ya huduma za kijamii kama ufadhili wa masomo na vituo vya afya.
Wanaopinga wanasema mbinu ya uthibitishaji wa kaboni ina upungufu mkubwa kiasi kwamba haiwezi kuthibitisha manufaa kwa tabianchi, na kwamba hifadhi hizo za jamii zilianzishwa bila ridhaa ya watu wanaoishi ndani yake, wengi wao wakiwa jamii za kiasili.
Verra imesema huo mradi kwa sasa unakaguliwa ili kubaini iwapo kuna upungufu mkubwa unaokiuka kanuni zake za uthibitishaji wa mikopo ya kaboni.
Msanifu wa mradi huo, Native, kampuni ya kimataifa inayolenga mabadiliko ya tabianchi, iliieleza Mongabay kuwa inatarajia mapitio ya Verra yatahitimishwa kwa kurudishwa tena kwa mradi huo.
“Kama ilivyokuwa kwa mapitio ya awali ya Sehemu ya 6, yaliyohitimishwa kwa kufungwa kwa matokeo yote na kurejeshwa kwa utoaji wa mikopo ya kaboni, tunashirikiana kwa njia ya kujenga na Verra na tunatarajia mchakato mwingine wa uwazi na wa wakati ufaao,” msemaji wa Native alisema kupitia barua pepe.
Picha ya bango: Mchungaji akilisha mbuzi katika mji wa Gotu, Kaunti ya Isiolo, Kenya. Picha na Ashoka Mukpo wa Mongabay.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 27/04/2024