- Miaka kumi iliyopita, korongo wa kijivu, au kwa jina la kisayansi Balearica regulorum, aliyekuwa akikabiliwa na aupotevu wa makazi na hatari ya kutekwa kwa ajili ya biashara haramu, alikuwa akitoweka kimya kimya nchini Rwanda.
- Muungano wa Uhifadhi wa Wanyamapori Rwanda (RWCA), unaoongozwa na daktari wa wanyama Olivier Nsengimana, umekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kukomesha tabia ya kufuga korongo kama wanyama wa kufugwa majumbani, ukiwa umefanikiwa kuwahifadhi tena na kuwaachilia huru ndege wengi waliokuwa mateka.
- Muungano huo pia unawahusisha wanajamii katika kuimarisha ulinzi wa makazi ya korongo dhidi ya uvamizi na uharibifu – mkakati ambao unaenezwa hadi nchi jirani kupitia ushirikiano na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.
- Kwa juhudi hizi, Nsengimana ametunukiwa Tuzo ya Dhahabu ya Whitley ya mwaka 2025, na kumfanya kuwa mshindi mara mbili baada ya kupokea tuzo hiyo kwa mara ya kwanza mwaka wa 2018.
Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori Rwanda (Rwanda Wildlife Conservation Association – RWCA), linaloongozwa na daktari wa wanyama Olivier Nsengimana, limekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kukomesha tabia ya kufuga korongo kama wanyama wa kufugwa majumbani, likiwa limefanikiwa kuwahifadhi tena na kuwaachilia huru ndege wengi waliokuwa mateka.
Shirika hilo pia linawahusisha wanajamii katika kuimarisha ulinzi wa makazi ya korongo kwenye maeneo ya mabwawa dhidi ya uvamizi na uharibifu — mbinu ambayo sasa inaenezwa hadi nchi jirani kupitia ushirikiano na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.
Kwa juhudi hizi, Nsengimana ametunukiwa Tuzo ya Dhahabu ya Whitley ya mwaka 2025, na hivyo kuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mara ya pili baada ya kuipokea kwa mara ya kwanza mwaka 2018.
Miaka 10 tu iliyopita, kuona korongo wa rangi ya kijivu katika maeneo oevu ya Rwanda lilikuwa jambo la kawaida. Ndege hawa wa kifahari – warefu na wenye sura nzuri, wakiwa na manyoya ya dhahabu vichwani mwao – waliwahi kusitawi Afrika Mashariki. Lakini kufikia katikati ya muongo uliopita, idadi yao nchini Rwanda ilikuwa imepungua sana.
“Ilinishtua,” anasema Olivier Nsengimana, daktari wa mifugo na mhifadhi wa Rwanda ambaye alianzisha RWCA. Anasema sensa ya mwaka 2017 ilihesabu chini ya ndege 500 kote nchini. “Tulikuwa na korongo wengi katika nyumba za watu kuliko walivyokuwa porini.”
Wakikabiliwa na upotevu wa makazi, kutekwa kwa biashara haramu kama wanyama wa kufugwa majumbani, na vitisho vingine, korongo wa rangi ya kijivu (Balearica regulorum) alikuwa akitoweka kimya kimya na kutoweka kabisa nchini Rwanda. Hadithi kama hiyo ilikuwa ikitokea katika nchi jirani, zikiwemo Burundi na Uganda, na kwingineko katika safu ya korongo, ambayo inaenea kote Afrika Mashariki na Kusini. Mnamo mwaka 2012, korongo walitathminiwa na IUCN, mamlaka ya kimataifa ya uhifadhi wa wanyamapori, kuwa kwenye hatari ya kutoweka.

Ili kuwalinda Korongo, linda ardhioevu
Uhai wa ndege hawa unategemea uhifadhi wa ardhi oevu. Barani Afrika, maeneo makubwa ya ardhi oevu yanapotea, yanatolewa maji mara kwa mara na kugeuzwa kuwa mashamba au kutoa nafasi ya upanuzi wa pembezoni mwa miji. Takriban asilimia 50 ya mandhari haya muhimu ya ikolojia yalipotea katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
“Korongo hupata chakula na kuzaliana katika maeneo oevu,” Nsengimana anasema. “Katika miongo mitano, tumepoteza karibu asilimia 80 ya korongo, na hiyo ni kwa sababu ya upotezaji wa makazi.”
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), linakadiria kuwa Rwanda ilipoteza takriban asilimia 36 ya ardhi oevu kati ya mwaka 1998 na mwaka 2016. Katika nchi jirani ya Uganda, ambako korongo ni ndege wa kitaifa, asilimia 30 ya ardhi oevu ilipotea kati ya mwaka 1998 na mwaka 2008, kabla hali haijatulia.
“Kama utafuatilia kuporomoka kwa ardhi oevu na kisha kuangalia kupungua kwa idadi ya korongo, ni sawia,” Achilles Byaruhanga, mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la uhifadhi, NatureUganda, anaiambia Mongabay.
“Ikiwa hatutafanya juhudi za kutosha, kuweka hatua nzuri za uhifadhi, kongoro wanaweza kutoweka nchini katika miaka 25 ijayo. Hayo yatakuwa maafa makubwa na aibu kubwa kwa sababu ni alama ya taifa,” anasema.
Zaidi ya uharibifu wa ardhi oevu, korongo pia wanatishiwa na biashara za kitaifa na kimataifa. Ndege hawa wazuri wanahitajika kama ndege wa kufugwa majumbani katika Afrika Mashariki na Mashariki ya Kati.

Chama cha Rwanda kinaongoza njia
Alipoanzisha Muungano wa RWCA mwaka wa 2015, Nsengimana alilifanya jukumu la kuokoa korongo kama kipaumbele. Chama hicho kimekuwa mstari wa mbele katika juhudi ambazo zimeokoa korongo wa kijivu wengi kutoka utumwani katika nyumba binafsi na kufanikiwa kuwarudisha kwenye makazi yao ya asili.
Kwa kuungwa mkono na serikali, muungano huo ulizindua kampeni ya kitaifa ya kuelimisha umma kuhusu masaibu yanayowakuta korongo. Lakini badala ya kuwatia hatiani wale wanaomiliki ndege hao, kampeni hiyo ilitoa msamaha.
“Tuliwaambia, ‘Tunapenda korongo. Tunajua unawapenda. Hebu tuwape nafasi ya pili,” Nsengimana anaiambia Mongabay. “Walikubali.”
Wakazi nchini kote walianza kuiita timu ya Nsengimana, wakiwaalika majumbani mwao kuwasalimisha ndege hao. Kila korongo alisajiliwa kwa uangalifu na kuchunguzwa. Wale waliokuwa na afya njema na manyoya safi walipelekwa katika eneo lenye uzio la urekebishaji kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Akagera, ambako walipewa chakula cha ziada na muda uliohitajika wa kuotesha manyoya na kujifunza upya kupaa.
Wakiwa tayari, waliachiliwa kurudi porini. Kwa wengine – waliojeruhiwa sana kiasi kwamba wasingeweza kuishi peke yao – walihamishwa hadi kwenye hifadhi maalum ya ardhioevu, ambayo sasa inajulikana kama kijiji cha Umusambi, katika mji mkuu, Kigali.
Juhudi hizi zimechangia ongezeko kubwa la idadi ya kongoro nchini Rwanda. “Mnamo mwaka 2017, wakati tunaanza kuhesabu korongo nchini Rwanda, na katika sensa ya kwanza kabisa, tulihesabu korongo 487. Mwaka jana, tulihesabu korongo 1,293,” Nsengimana anaiambia Mongabay kwa simu kutoka nyumbani kwake Kigali.
Anasema sasa wanazingatia zaidi kujenga wahifadhi wa mazingira kutoka katika jamii. Zaidi ya watu 270 sasa wanashirikiana na RWCA, ambapo asilimia 90 kati yao wanatoka katika jamii za wenyeji. Wanaendesha shughuli mbalimbali katika jamii kama vile kampeni shuleni, kutumia baiskeli na mchezo ya mpira wa miguu kueneza uelewa, na kusaidia miradi inayoongozwa na wanawake ili kupunguza utegemezi wa maeneo oevu.
“Tunatengeneza ajira kupitia uhifadhi wa mazingira,” Nsengimana anasema. “Tunataka watu wanufaike na washiriki.”

Korongo bila mipaka
Nsengimana anasema chama cha RWCA kiligundua punde kwamba korongo hawatambui mipaka. Vibandiko vya kiredio vilivyowekwa kwenye korongo nchini Rwanda vilifichua mienendo ya mara kwa mara ya kuvuka mpaka hadi Uganda, Burundi na Tanzania.
“Wanakwenda na kurudi. Wengine wanakaa huko,” Nsengimana anasema. “Hiyo lilituonyesha kuwa hatuwezi kufanya hivi peke yetu.”
Ili kutekeleza hilo, shirika la RWCA lilianza kuunda ushirikiano na vikundi vya uhifadhi kote Afrika Mashariki. Nchini Tanzania na Uganda, mabingwa wa uhifadhi wa jamii – wakazi wa eneo hilo waliofundishwa na kuwekewa programu na simu mahiri – wameajiriwa kufuatilia korongo, kuripoti kuonekana na kulinda maeneo ya kuzaliana. Hii itasambazwa hadi Burundi hivi karibuni.
Byaruhanga, ambaye shirika lake lisilo la kiserikali ni mwanachama wa muungano huu, anasema ushirikishwaji wa jamii ni muhimu. “Njia bora ni kufanya kazi na watu wa ndani: kuwafundisha, kuongeza ufahamu, na kuwawezesha kuwa wasimamizi wa spishi.”
Uganda imeandaa mpango wa kitaifa wa utekelezaji kumuokoa Korongo. Serikali, Byaruhanga anasema, imechapisha kwenye gazeti rasmi la serikali maeneo oevu yote muhimu kwa ajili ya kurejesha idadi ya korongo. “Kama wahifadhi, katika ngazi ya mitaa wametambua maeneo ambayo ni muhimu sana kwa uhifadhi wa korongo na kuyataja kama maeneo ya Ramsar – yaani, maeneo oevu yenye umuhimu wa kimataifa. Ni katika maeneo haya oevu ambapo walinzi wa jamii huwatazama na kuwahudumia korongo kila siku.”
Juhudi hizi zinaleta matokeo chanya. Byaruhanga anasema data za hivi karibuni za sensa, kuanzia mwaka 2022, zilionyesha hakuna kupungua tena – idadi ya korongo inaongezeka.
Matumaini ya siku za usoni
Byaruhanga anataja faida nyingi za kulinda korongo na makazi yao ya ardhioevu. Nchini Uganda, kwa mfano, kutazama ndege ni shughuli ya pili muhimu ya kitalii, baada ya safari ya sokwe.
“Tunakuza ndege na uimarishaji wa ndege kama shughuli muhimu. Tunapata faida kutokana na hilo, sharti tuwalinde ndege,” anasema.
Kwa Nsengimana, juhudi zinazoendelea katika ukanda huu zinampa matumaini. “Katika miaka 10 ijayo, ninatumaini kusikia habari chanya: zile ambazo zinaonyesha kuwa idadi ya korongo haipungui tena bali inaongezeka kutokana na juhudi za kikanda. Nchini Rwanda, tumefanikisha hilo, na naamini linaweza kufanikishwa katika ukanda mzima.”
Anaongeza: “Ninajisikia vizuri sana, imekuwa ni fursa nzuri kufanya kazi nchini Rwanda. Nisingeweza kuifanya peke yangu. Ni sifa kwa Wanyarwanda wote.”
Kwa jitihada zake, Nsengimana ametunukiwa Tuzo ya Dhahabu ya Whitley ya 2025 na Whitley Fund for Nature, shirika la hisani lenye makao makuu yake nchini Uingereza. Tuzo hiyo, ambayo inaambatana na paundi za Uingereza 100,000 ($133,000) katika ufadhili wa mradi, hutolewa kwa mtu ambaye ametoa mchango mkubwa katika uhifadhi. Ni mara ya pili kwa Nsengimana kupokea tuzo inayojulikana kwa jina la “Green Oscars”; alikuwa mpokeaji mnamo mwaka 2018, kupitia kazi yake na kongoro wa kijivu.
Picha ya bango: Olivier Nsengimana, mwanzilishi wa Muungano wa Uhifadhi Wanyamapori wa Rwanda. Picha kwa hisani ya James Rooney/National Geographic Society
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 30/04/2025.