- Popo ni mojawapo ya makundi mbalimbali ya mamalia na huwakilisha sehemu muhimu ya uwiano wa ikolojia. Wanaweza kuwakilisha sehemu kubwa ya utofauti wa mamalia — hasa katika nchi kama Rwanda ambakosehemu kubwa ya misitu ya asili na makazi ya savanna -imepotea, kubadilishwa au kuharibiwa.
- Hivi karibuni watafiti waligundua aina mbili za popo adimu katika Mbuga ya Kitaifa ya Nyungwe nchini humo na shirika la IUCN linasema kuna aina 54 za popo zinazopatikana.
- Utafiti unaonyesha kuwa kuua popo ili kudhibiti magonjwa ya wanyama yanayoathiri binadamu, kunaweza kufanya mambo kuwa mabaya zaidi.
- Tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa popo ni wawindaji muhimu wa wadudu na hivyo, ni raslimali asilia ya uzalishaji wa kilimo,kwa kuwa husaidia kupunguza idadi ya wadudu waharibifu.
KIGALI, Rwanda ― Kufuatia ugunduzi wa hivi karibuni wa popo aina ya farasi walio katika hatari ya kuangamia (au kisayansi Rhinolophus hilli) katika Mbuga ya Taifa ya Nyungwe kusini-magharibi mwa Rwanda, watafiti wanatoa wito wa kuchukua hatua na sera zinazolenga uhifadhi wao.
Wanasayansi wanasema kuwa huu ni ugunduzi wa kwanza wa kuona na kurekodi popo wa aina ya Rhinolophus webalai (horseshoe bat) katika hifadhi hiyo, na pia ni mara ya kwanza kwa Rwanda kushuhudia popo wa Damara woolly bat (Kerivoula argentata) tangu walipoonekana mara ya mwisho mwaka 1981.
Kwa mujibu wa Paul Webala, Mhadhiri Mwandamizi wa Biolojia ya Wanyamapori katika Idara ya Misitu na Usimamizi wa Wanyamapori katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara nchini Kenya, wanasayansi wanachukulia popo kuwa kundi la pili lenye utofauti mkubwa zaidi miongoni mwa mamalia, baada ya panya. Anasema katika nchi kama Rwanda ambapo misitu ya asili na maeneo ya savana yamepotea, kubadilika au kuharibika kwa kiasi kikubwa, popo wanaweza kuwakilisha “angalau asilimia 40 ya utofauti wa mamalia kwa ujumla.”
Kulingana na utafiti wa mwaka mwaka 2022 (utafiti) ambao Webala alishirikiana na mtu mwingine kuufanya, popo wanaokula wadudu nchini Rwanda hutoa huduma muhimu za mfumo wa ikolojia na pia hufanywa kama wadhibiti wadudu katika maeneo ya kilimo.
Hofu za kiafya na upotezaji wa makazi
“Nchini Rwanda, mojawapo ya aina [ya popo] inayotia wasiwasi, ingawa haijatishiwa kulingana na Orodha Nyekundu ya shirika la IUCN, ni popo wa Misri [Rousettus aegyptiacus] kwa sababu ametambuliwa na maafisa wa afya kama hifadhi ya asili ya ugonjwa wa virusi vya Marburg,” Webala anasema.
Mnamo Februari mwaka huu, maafisa wa afya nchini Rwanda waliamua kujenga ukuta katika eneo la uchimbaji madini lililoko Nyamirambo kitongoji cha mji mkuu Kigali kikitenganisha eneo la kufanya kazi na makazi ya popo.
“Kizuizi hiki kinatarajiwa kupunguza mawasiliano ya moja kwa moja kati ya binadamu na popo, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya maambukizi,” ilisema taarifa iliyotolewa wakati huo na Wizara ya Afya mjini Kigali.
Hata hivyo, timu ya watafiti wa uhifadhi kutoka Rwanda na wa kimataifa bado haijabaini uhusiano wa moja kwa moja wa virusi kwa aina ya popo wa Rousettus na virusi vya ugonjwa wa Marburg.
Hii ni kwa sababu mara nyingi popo hutupiwa lawama na kuwekwa katika kundi moja la kibaiolojia na watunga sera, ilhali kwa mtazamo wa wanasayansi wa uhifadhi, ukweli ni kwamba mamalia hawa ni kundi lenye utofauti mkubwa sana lenye zaidi ya spishi 1,482 — wakiwa wa pili kwa wingi wa spishi miongoni mwa mamalia, wakitanguliwa tu na panya.

Popo wanaweza kujumuisha angalau asilimia 40 ya aina mbalimbali za mamalia nchini Rwanda. Picha kwa hisani ya Muungano wa Kuhifadhi Wanyamapori nchini Rwanda – RWCA.Kwa sasa Webala anafanya kazi na timu ya watafiti wa uhifadhi kutoka Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) kupanga ramani ya maeneo ya makazi ya popo wa Misri ili kuhakikisha ulinzi wao na kuwafuatilia kama wana magonjwa.
“Kulinda mapango ya [popo] [nchini Rwanda] ni muhimu, kwani kuwaondoa popo wote hakutakuwa na tija kwa sababu nyingi,” Webala anaiambia Mongabay.
Kulingana na Webala, matatizo ya afya ya umma yanayoletwa na popo ni madogo lakini mara nyingi husababisha hamaki kubwa.
Zaidi ya hayo, Webala anasema kuwa jitihada za kutokomeza magonjwa kupitia udhibiti wa wanyamapori mara nyingi huchochea matatizo zaidi huku zikitishia usawa wa ikolojia. Popo wana jukumu muhimu katika mfumo wa ikolojia ikiwemo kula wadudu, kuchavusha mimea yenye thamani, na kutawanya mbegu muhimu katika kuzalisha upya misitu muhimu.
Spishi hizi haziwezi kabisa kuhusiana na binadamu na [hazina] hatari yoyote ya kusambaza magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, lakini sehemu kubwa ya kusambaa kwa magonjwa hayo hutokana na binadamu kuvamia makazi ya wanyama hawa,” Webala aliambia Mongabay.
Mapango ya Musanze, yaliyoko kaskazini mwa Rwanda, ni kivutio maarufu cha watalii, yakiwa na mahandaki mengi ya volkano na maelfu ya popo, wakiwemo popo wa Misri. Wakati wa matembezi ya watalii yanayoongozwa na waongozaji, wageni hufurahia kuwaona popo wengi wakiwa wamening’inia katika kuta na dari za mapango hayo.
Hata hivyo, serikali ilifunga eneo hilo mnamo Februari mwaka 2025 kufuatia mlipuko wa hivi karibuni wa virusi vya Marburg mjini Kigali. Virusi hivyo vinahofiwa kuwa chanzo chake ni popo wa Misri.

Kupunguza hatari ya ‘magonjwa ya wanyama kuenea’
Ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa, kuua popo wengi ili kudhibiti magonjwa yatokanayo na wanyama kwa bindadamu, yaani zoonotic, kunaweza kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, kama matokeo ya mlipuko wa virusi vya Marburg katika baadhi ya nchi za Afrika, kama Uganda, na kuenea kwa magonjwa mengine yanayoenezwa na popo kama kichaa cha mbwa nchini Peru.
“Hatua zinahitajika ili kupunguza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya wanyama kwa sababu virusi kama Marburg, huruka kutoka kwenye spishi moja, kama vile popo, hadi kwa wanadamu,” Webala anasema.
Orodha Nyekundu ya Spishi Zilizo Hatarini ya Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) ya mwaka 2021-2023 inaorodhesha jumla ya spishi 54 za popo zinazopatikana nchini Rwanda, na inaeleza kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa spishi ambazo bado hazijawahi kurekodiwa rasmi nchini humo.
Kulingana na Webala, upotevu wa makazi na mgawanyiko kutokana na shughuli kama vile uchimbaji madini, ukataji miti, uwindaji, kilimo na moto unaosababishwa na urinaji wa asali ya porini ni tishio kubwa kwa bioanuwai ya eneo hilo.
Kutokana na kiwango cha mabadiliko ya makazi, Webala na kundi lake wanasema, kuendelea kuwepo kwa popo adimu na walio katika hatari ya kupotea, kama vile popo wa Hill’s horseshoe, kunategemea taarifa sahihi na za kisasa zinazotolewa kwa wasimamizi wa rasilimali ambao wanaweza kutumia data hiyo kutekeleza hatua madhubuti za uhifadhi ili kulinda spishi ambazo ziko kwenye hatari kubwa ya kutoweka.
Wanasema wanasadiki kwamba popo ni miongoni mwa wanyama walio na umuhimu mkubwa zaidi, lakini inaeleweka kwa kiwango cha chini sana duniani. “Kutokueleweka huku kunachangiwa zaidi na filamu na vipindi vya runinga vyenye matukio ya kutisha, ambavyo huzua hofu kwa watu wengi. Ingawa popo wanaogopwa sana na kuchukiwa kama viumbe wa kutisha wa usiku, wana umuhimu mkubwa kwa afya ya mazingira yetu na uchumi wetu,” anasema Webala.

Sehemu za mpaka kwa ajili ya kulinda spishi
Mkuu wa Kitengo cha Wanyamapori na Mifugo katika Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) na mshirika wa utafiti wa Webala, Richard Muvunyi, anasema, “Tunaelewa kisayansi kuwa virusi vya Marburg vinatoka kwa popo wa Misri, lakini jambo muhimu ni kuelewa jinsi ya kuishi kwa usalama na spishi hizi kwa kupunguza mwingiliano wa jamii na popo hawa katika makazi yao ya asili.”
Webala na Muvunyi wanasema kuwa kuzielezea spishi zote za popo kuwa chanzo cha Marburg si sahihi, kwa sababu popo ni kundi lenye utofauti mkubwa, zikiwa na zaidi ya spishi 1,400 — na ni ya pili kwa utofauti miongoni mwa mamalia baada ya panya.
Mojawapo ya suluhisho la muda mrefu lililotekelezwa na Kitengo cha Wanyamapori na Mifugo katika Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), katika maeneo 80 yaliyoorodheshwa ya popo nchini Rwanda ili kuhakikisha uhifadhi wa popo ni pamoja na kubuni eneo la mpaka la angalau mita 50 (futi 164) kati ya viota vya popo na shughuli za binadamu.
“Pia tunawahimiza wanajamii kupanda miti karibu na maeneo haya ya hifadhi kama njia ya kuzuia mwingiliano wao na popo,” Muvunyi anaiambia Mongabay.
Muvunyi na Webala wanasema kuwa popo ni wawindaji wa wadudu waharibifu wa mazao, hivyo ni rasilimali ya asili katika kuongeza tija ya kilimo kwa kupunguza idadi ya wadudu waharibifu.
Wanasema kuwa bila huduma zinazotolewa na popo, mimea isingeweza kutoa huduma zake kwa binadamu na wanyama walioko chini kabisa katika mnyororo wa chakula.
“Popo hujumuisha zaidi ya asilia 40 ya wanyama wa aina mbalimbali wa Rwanda, hivyo serikali ina wajibu wa kuwajumuisha katika mipango ya kitaifa ya uhifadhi ,” Webala anasema.
Picha ya bango: Popo wanaweza kujumuisha angalau asilimia 40 ya aina mbalimbali za mamalia nchini Rwanda. Picha kwa hisani ya Chama cha Kuhifadhi Wanyamapori cha Rwanda – RWCA
Nukuu:
Wilkinson, G.S., Adams, D.M. (2019). Recurrent evolution of extreme longevity in bats. Biology Letters, 2019; 15(4): 20180860. doi:10.1098/rsbl.2018.0860
Flanders, J., Frick, W., Nziza, J., Nsengimana, O., Kaleme, P., Dusabe, M. C., Webala, P.W. (2022). Rediscovery of the critically endangered hill’s horseshoe bat (Rhinolophus hilli) na rekodi nyingine mpya za aina ya popo nchini Rwanda. Biodiversity Data Journal, 10. doi:10.3897/bdj.10.e83546
Rocha, P., Aziz, S.A., Brook, C.E., Carvalho, W.D., & Webala, P.W. (2020). Bat conservation and zoonotic disease risk: ajenda ya utafiti ili kuzuia mateso yasiyofaa baada ya COVID-19. Animal Conservation, 24(3). doi:10.1111/acv.12636
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 25/04/2025