- Mkakati wa uhifadhi kwa miaka 20 ijayo umezinduliwa ili kulinda maeneo yenye utajiri wa kibaiologia.
- Milima ya Udzungwa ni eneo muhimu kwa mimea na wanyama wa asili wakiwemo idadi ndogo ya kipunji ambao wamejulikana hivi karibuni tu kuanzia mwaka 2006.
- Upatijkanaji endelevu wa fedha unatakiwa ili kugharamia mkakakti wa uhifadhi na kuboresha maisha na huduma za jamii katika jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
- Mkakakati unazingitia pia matumizi ya majiko banifu ambayo ni kipaumbele cha wenyeji wanaotumia kuni na mkaa kwa wingi.
Wataalamu wa uhifadha wamezindua mradi wa miaka 20 wenye lengo la kulinda eneo muhimu kibailogia nchini Tanzania: Milima ya Udzungwa. Mkakati huu unatoa kipaumbele kwa jamii za eneo hilo ambapo zaidi ya nusu ya bajeti itatumika kwaajili ya miradi ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutatua mgongano wa wanyamapori na binadamu.
Misitu ya kijani inayopatikana mwaka mzima katika Milima ya Udzungwa, nyanda na maeneo ya miti mtawanyiko inahifadhi mimea na wanyama ambao hawapatikani katika sehemu nyingine yoyote ulimwenguni. Wanasayansi wanakadiria kuwa katika miaka 2,000 iliyopita eneo hilo limepoteza zaidi ya robo tatu ya misitu yake. Katika karne iliyopita, ongezeko la wakulima wadogo, mashamba ya chai na misitu ya kupandwa kwaajili ya mbao na ukataji miti migumu ya asili kwaajili ya mbao bora kumechoachea uharibifu na kupotea kwa misitu.


Kasi ya uharibifu na kupotea kwa misitu katika baadhi ya sehemu ilipungua kuanzia mwaka 1992 baada ya kuanzisha maeneo ya uhifadhi. Hata hivyo Trevor Jones, Mkurugenzi wa Mikakati na Maendeleo wa Mpango wa Kulinda Tembo Kusini mwa Tanzania (Southern Tanzania Elephant Program (STEP), anasema kuwa lengo kuu kwa sasa ni kumaliza kabisa uharibifu na upotevu wa misitu na hatimaye kurejeshe mazingira katika hali yake ya asili.
Mkakati wa Eneo la Udzungwa (The Udzungwa Landscape Strategy (ULS)) ulizinduliwa mwezi Oktoba mwaka wa 2024, ambao ni ushirikiano baina ya makundi ya uhifadhi, wakala wa serikali na jamii za wenyeji, wenye lengo la kulinda maeneo matatu muhimu katika Milima ya Udzungwa ambalo kwa ujumla wake ni eneo kubwa kati ya mengine kumi na mawili yaliyomo kwenye Tao la Milima ya Mashariki, mnyororo wa milima unaounganisha Kenya na Tanzania.
“Fursa ambayo tuliiona na tuliyotaka kujikita huko ni kulinda na kuhifadhi maeneo matatu muhimu, eneo ambalo ni takriban asilimia 60 ya eneo lote la Milima ya Udzungwa,” anasema Jones.
Maeneo hayo muhimu ni Hifahi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ambalo tayari linalindwa na muunganiko wa misitu ya Hifadhi ya Asili ya Kilombero na Udzungwa, ambayo hayajahifadhiwa na kulindwa. (Kilombero and Uzungwa Scarp nature forest reserves).
Mwanzoni kabisa mradi huu ulifadhiliwa na Hempel Foundation na Aage V. Jensen Charity Foundation, lakinu sasa tunataka kukusanya dola za Kimarekani million 3 kila mwaka kwa miaka 20 ijayo, ambapo asilimia 80 ya fedha hizo itagawanywa kwa usawa kati ya kuhifadhi na kulinda Mbuga ya Taifa na misitu ya hifadhi, na kwa upande mwingine kuboresha uchumi na ustawi wa jamii za wenyeji. Asilimia 20 iliyobaki itatumika katika kutatua migangano ya wenyeji na wanyamapori, kukuza ushirikiano na jamii, gharama za uendeshaji na na kutathmini athari na mafanikio ya mradi.
Katika muda mfupi, mradi na washirika wake watatafuta ufadhili na kubuni njia nyingine za kugharamia mradi. Jones anaona kuwa ushirikiano na serikali ya Tanzania ni muhimu katika kupata ufadhili wa kimataifa kama vile kutoka Tropical Forest Finance Facility, mifuko ya fedha ya bioanuai ya dunia, na miradi ya Umoja wa Mataifa inayojishughulisha na uhifadhi.
Kwa siku za baadaye mapato yatakayotokana na biashara ya hewa ukaa na mikopo ya kuendeleza bionuai itasaidia katika shughuli za uhifadhi.
“Milima ya Udzungwa itakuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji kwani tayri ni mojawapo kati ya maenoeo kumi ya ulimwengi yenye bioanuia muhimu na ya kipekee,” anasema Jones.

Eneola Udzungwa ni makazi ya asilimia 6 ya aina za ndege wanaopatikana duniani, asilimai tatu ya aina mbalimabali za mamalia na takriban asilimia moja ya aina za wanyama watambaao na wanaoishi majini na nchi kavu. Hii ni pamoja na vyura wa Kihansi (Nectophrynoides asperginis), chura mdogo mwenye rangi ya njano ambaye huishi kwenye manyuyu ya maji yanayotokana na Maporomoko ya Mto Kihansi. Aina hii ya chura ilitangazwa kutoweka katika mazingira ya asili mwaka 2009, baada ya ujenzi wa bwawa la kufua umeme kukata mtiririko wa maji kwa asilimia 90. Kwa sasa vyura hawa wanafugwa na jitihada zinafanyika kuwarudisha katika makazi yao ya asili.
Wanyama wengine muhimu ni pamoja na nyani, wakiwemo nyani wekundu wa Udzungwa (Udzungwa red colobus monkey (Piliocolobus gordonorum)), Sanje mangabey (Cercocebus sanjei) na kipunji (Rungwecebus kipunji), nyani wa kijivu na kahawia anayeonekana kama amenyoa panki na ambaye yuko hatarini kutoweka, aliyegunduliwa mwaka 2006.
“Kulinda misitu hii adhimu na kuwahakikishia wenyeji maisha bora yaliyo endelevu kunahitaji mipango thabiti, na mikakati imara ya kupata fedha za kugharamia,” anasema Oliver Oliver Beasley, mhadhiri wa sayansi huko Bristol Zoological Society nchini Uingereza.
Shirika lake ambalo limefanya kazi kubwa kuwalinda Sanje mangabeys walioko Udzungwa tangu mwaka 2014, siyo mshirika mtekelezaji wa mradi huu lakini anaona mradi huu utafanikiwa. “Mradi huu unawaleta pamoja makundi mbalimbali ya washirika na wadau na kuwaunganisha ili kutekeleza mambo mbalimbali ya uhifadhi yaliyoandaliwa kwa kushirikiana na wanajamii wenyewe,” anasema Beasley.


Mkazo mkubwa wa Mkakati wa Usangu ni kuboresja maisha ya wakazi wa vijiji 71, ambavyo vinapakana na maeneo yaliyohifadhiwa. Wadau wa uhifadhi wanatarajia kutia saini makubaliano ya hiari na vijiji hivyo ambavyo vitakuwa vikipata malipo kwa shuguli za kulinda misitu na kupambana na ujangili. Vitaundwa pia vikundi vya kuweka na kukopa ili kuwawezesha wanavijiji kuanzisha na kuendesha biashara ndogondogo, kulipia mahitaji ya shule kwaajili ya watoto wao au kugharamia matibabu.
Mathew Mbele, amabye ni mataalamu wa jiografia ya binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, anasema mkakati huu unatoa fursa ya kuona jinsi gani shughuli za uhifadhi zinaendana na mahitaji na matarajio ya wananchi.
Hata hivyo, anatilia shaka kuhusu wajibu wa raia wa kigeni katika kuujenga mkakati huu na ushiriki wa wakala wa ufihadhi wa serikali na wafanya kazi katika hifadhi katika utekelezaji mradi kwa ujumla wake.
“Wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa na misitu ya hifadhi hawana imani na wanavijiji, nao wanavijiji kwa upande wao hawaamini wafanya kazi,” anaeleza Mbele na kudokeza kuwa mvutano huu unatokana na historia ya uhifadhi nchini Tanzania pamoja na sharia sera na muundo wa utendaji.
“Malengo ya mkakati ni lazima yawiane na sera na sheria zilizopo ambazo wakati mwingine hazijengi mahusiano mazuri kati ya wananchi na wafanyakazi wa hifadhi.”
Arafat Mtui, Meneja wa Mkakati huo kwa upande wa Tanzania anakubaliana na maoni ya Mbele, lakini anasisitiza kuwa wale ambao siyo raia wa Tanzania wanachangia utaalamu wa teknologia na utendaji bora wa vigezo vya kimataifa. Mkakati huu umejengwa katika misingi ya vipaumbele vya Tanzania na hali halisi katika jamii husika.
“Lengo kuu ni kuwajengea uwezo watendaji Watanzania na wananchi kwa ujumla, na siyo kupandikiza mambo ya kutoka nje ya nchi,” anasema Mtui.

Ili kujenga imani wanavijiji watashiriki katika doria za kulinda misitu pamoja na wafanyakazi wa hifadhi. Watashiriki kuandaa mafunzo kuhusu haki za binadamu, utii wa sheria kushiriki katika kudumisha tunu za uhifadhi.
Kujumuisha fursa za maisha bora na maendeleo endelevu ya wananchi wa vijiji hivyo 17, na shughuli mbalimbali za uhifadhi ni jambo linalozingatiwa.
Mtui anaona kwamba hali hii itasaidia kupunguza vikwazo vinavyoweza kuletwa na sera na sheria zilizopo.
Jambo jingine muhimu ni kuboresha upatiakanaji wa nishati. Mpaka sasa zaidi ya wakazi 2,400 katika vijiji vitano wamenufaika na majiko ya udongo yapatayo 500 ambayo yamejengwa na mashirika yanayotekeleza mkakati, ikiwemo Mazingira Alliance for Community and Conservation (MACCO), ambalo ni shiriki linalofanya kazi katika eneo la Udzungwa likijihusisha na maendeleo endelevu. Kadhalika wakazi wa vijiji 23 ambao walihudhuria mashauriano yalioandaliwa na shirika la STEP na washirika wake waliweka majiko banifu kama kipaumbele cha kwanza.
Silvia Ricci, mshauri wa idara ya masuala ya jamii na maisha bora katika shirika la MACCO, anasema kuwa kaya nyingi katika eneo la Udzungwa hupika mara tatu au nne kwa siku kwaajili ya watu sita. Hii inaonyesha kuwa gharama ya nishati ni kubwa na ni mzigo kwa familia nyingi.
MACCO imetengeneza jiko banifu kwa kutumia matofali ya udongo kumi na mawili na kufunikwa kwa mchanganyiko wa udongo wa mfinyanzi na vumbi la mbao ambayo husaidia kuingiza hewa ya kutosha na kupunguza moshi na pia kupunguza matumizi ya kuni. “Nishati ya kupikia na matumizi mengine kwa ujumla ni kipaumbele cha Watanzania,” aeleza Ricci, “hata kama haisaidii kupunguza uharibifu wa misitu au uharibifu wa mazingira kwa ujumla.”
Kufikia mwaka 2027, MACCO inatarajia kuvifikia vijiji 15 vinavyozunguka hifadhi. Mradi umeajiri wafanyakazi 30 ambao hutengeneza majiko takriban 450 kila mwezi. Kadhalika wamejenga viwanda vidogo vitatu ambavyo huzalisha mkaa taka kutokana na mabaki ya mazao kama vibunzi, vifuu vya nazi na punba za mpunga. Mkaa huu una bei nafuu kuliko mkaa wa miti.

Jones, ambaye ametumia miaka mingi akifanya utafiti kuhusu mamalia wa Udzungwa anaona kuwa kuna umuhimu na uharaka wa kuhifadhi ambao ameuona katika kazi zake.
Anakumbuka aliwaona kipunji kwa mara ya kwanza mwaka 2004, wakati akifanya utafiti eneo la Ndunduka katika Hifadhi ya Msitu wa Kilombero akichukua taarifa kuhusu Sanje mangabeys.
“Tulikuwa tukiangalia kundi la nayni mchanganyiko, Richard Laizzer, ambaye alikuwa mtafiti msaidizi ghafla akasema kwa sauti, ‘Mangabey!’” Jones anasimulia.
“Nikaelekeza darubini yangu kwa moja wa wale nyani na nilipatwa na msituko kwani niliyemuona hakuwa mangabey. Kwa hakika sikujua ni mnyama gani. Mara yule nyani akatoweka nami nikabaki nimekaa chini kwa mshangao.”
Baadaye nyani yule aliiitwa Rungwecebus kipunji kutokanan na Mlima Rungwe uliopo Nyanda za Juu Kusini ambako mnyama kama huyo aligunduliwa na kundi jingine la watafiti, akiwa amenaswa kwenye mtego wa wawindaji. Kipunji ndiye alikuwa nyani wa kwanza wa aina yake aliyeonekana Tanzania kwa miaka 125 iliyppita.
“Huu ni moja wa uvumbuzi usio wa kawaida katika Milimaya Udzubgwa kwa Zaidi ya miaka 40,” anaeleza Jones. “Na hata sasa bado uvumbuzi unaendelea.”
Picha ya bango: Mmmoja kati ya nyani kipunji wapatao 200 waliopo katika Milima ya Udzungwa. Picha na Anthony Jarrett.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 02/04/2025.