- Wafugaji wanaoishi katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha nchini Tanzania, huishi kwa tahadhari kubwa hasa nyakati za usiku, ili kulinda mifugo yao dhidi ya mashambulizi ya simba na chui, katika eneo hilo linalokaliwa na asilimia 10 ya simba wa porini duniani.
- Lakini utafiti umeonyesha kuwa maboma yaliyoimarishwa katika maeneo ya makazi yanaweza kulinda mifugo dhidi ya mashambulizi ya wanyama wala nyama, jambo linaloweza kuwanufaisha wamiliki wa mifugo pamoja na majirani zao.
- Watafiti wamegundua kuwa wanyama wanaowinda hujiepusha na maeneo ya makazi ambapo wafugaji wamejenga maboma kwa kutumia uzio wa nyaya za chuma (chain-link), mbinu ambayo imeonekana kuwa bora zaidi kuliko maboma ya asili ya Kiafrika yanayojengwa kwa kutumia miiba.
- Wanyama wanaokula nyama katika maeneo yenye maboma mengi hukumbana na “kazi zaidi,” jambo linalowawia vigumu kuwatoa wanyama kutoka ndani ya maboma. Uzio huo hupunguza upatikanaji na mvuto wa mawindo, hivyo kuwafanya wanyama wala nyama kuepuka maeneo yenye maboma yaliyowekwa kwa wingi, kwa mujibu wa Jonathan Salerno, mwandishi mkuu wa utafiti huo.
NAIROBI-Kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita, Matambire Mgemaa, mfugaji kutoka kusini mwa Tanzania karibu na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, amekuwa akilazimika kukesha usiku kucha ili kulinda mifugo yake: mbuzi, kondoo na ng’ombe dhidi ya mashambulizi ya simba na chui katika eneo hilo linalokaliwa na asilimia 10 ya simba wa porini duniani.
“Hii ni kazi ngumu sana…Mchana kutwa nakuwa na mifugo nje kuhakikisha wanakula, usiku, badala ya kulala nakesha …siwezi kulala kwa sababu nitawapoteza,” anasema Mgemaa.
Kwa sababu ya uwezo wao mkubwa wa kuona usiku, uwezo ambao huwasaidia kuwinda kwa mafanikio zaidi katika mwanga hafifu, simba, chui na fisi huwa na shughuli nyingi zaidi nyakati za usiku — huwa muda wa mlo wao wa usiku.
Lakini utafiti mpya uliochapishwa mwezi huu katika jarida la Conservation Letters umegundua kuwa, kuwepo kwa maboma mengi yaliyoimarishwa kwa kiwango cha kati au cha juu katika maeneo ya ufugaji, kunaweza kulinda mifugo ili isishambuliwe, kwani wanyama hao hujiepusha na maeneo kama hayo. Watafiti wamebaini kuwa maboma haya ya chuma si tu yanawasaidia wamiliki wake kupunguza mashambulizi kwa mifugo yao, bali pia husaidia hata majirani zao.
Kusini mwa Tanzania, eneo muhimu kwa uhifadhi wa wanyama wala nyama wakubwa, wafugaji huweka mifugo kwenye maboma yenye uzio usiku, na kupeleka mifugo yao kwenye malisho ya jumuiya wakati wa mchana.
Kwa wastani, Mgemaa na majirani zake walikuwa wakipoteza wanyama wawili wa kufugwa kila wiki kutokana na mashambulizi ya wanyama hawa, lakini mashambulizi hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa. Mapema mwaka 2024, Mgemaa alijenga boma la chuma aina ya chain-link ili kuzuia mifugo yake kushambuliwa na wanyama hao usiku.
Winston Mtandamo, meneja wa uendeshaji katika shirika linalojihusisha na mambo ya uhifadhi nchini Tanzania, lijulikano kama Lion Landscapes, anasema kuwa mashambulizi ya wanyama wala nyama — hasa simba na fisi — dhidi ya mifugo ya wafugaji katika maeneo ya Ruaha yalikuwa mengi katika kipindi cha muongo uliopita.

“Nyakati za usiku, wanyama walikuwa wakivamia maboma ya wafugaji na kula mifugo yao. Tuligundua kuwa maboma mengi yalikuwa yamejengwa kwa kutumia miti midogo na dhaifu ambayo wanyama hao walikuwa wakiivunja kwa urahisi au kuruka juu yake na kuwafikia wanyama. Tulipendekeza kuwa wakulima wajenge maboma imara kwa kutumia nyaya za chuma (chain-link) pamoja na nguzo ndefu za mbao au chuma,” anasema Mtandamo.
Wahifadhi kutoka shirika la Lion Landscapes wanashirikiana na wafugaji kujenga maboma imara ili kulinda mifugo na pia kulinda spishi za wanyama hao ambao wako hatarini kutoweka.
Watafiti waligundua kuwa pale mfugaji anapojenga boma la kulinda shamba au mifugo yake, cha kushangaza ni kwamba, wanyama hao badala ya kuhamia kwa majirani wasiokuwa na maboma imara na kuwadhuru, hujiepusha kabisa na maeneo yote. Njia hii imethibitishwa kuwa bora zaidi kuliko uzio wa asili wa Kiafrika unaotengenezwa kwa miiba mifupi.
Mwandishi mkuu wa utafiti huo, Jonathan Salerno, ambaye ni Profesa Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Colorado katika Idara ya Maeneo ya Asili na Rasilimali za Kibinadamu, aliiambia Mongabay kuwa kadri maboma yanavyoongezeka katika eneo fulani, ndivyo ulinzi unavyoongezeka hata kwa majirani ambao hawajajenga maboma hayo.
“Eneo lenye maboma matatu au manne linamfanya mnyama kupata kazi ngumu zaidi kuweza kuwatoa mbuzi au kondoo kutoka kwenye maboma hayo yaliyowekwa vizuizi imara,” anasema. “Uzio huo unawapunguzia upatikanaji wa mawindo (mifugo) ambacho ndiyo chakula chao cha usiku. Zaidi ya hayo, wakishaona ulinzi imara umeweka, wanakosa ujasiri wa kusogea. Ingawa hatuna takwimu kamili kuhusu tabia za wanyama wala nyama, kwa maelezo rahisi ni kwamba maboma mengi yaliyoimarishwa huongeza muda, juhudi, na hatari ya kuwinda katika eneo hilo, hivyo wanyama hao huamua kuepuka kabisa maeneo yenye maboma ya kati au ya kiwango cha juu,” anasema Salerno.
Katika utafiti uliochunguza ripoti 25,000 za kila mwezi kutoka kwa wafugaji zilizokusanywa na taasisi ya Lion Landscapes, matokeo yalionyesha kuwa kaya zilizokuwa jirani na zile zilizo na maboma ya nyaya za chuma, ziliripoti mashambulizi machache ya wanyama wala nyama kwa mifugo yao.
Mgemaa anafurahi kwamba sasa kuna uwezekano mdogo wa kupata hasara kwa mifugo yake, ambayo ndiyo chanzo chake pekee cha mapato . “Ni kama vile ule uzio wa chuma mrefu unawatisha. Hata hawasogei. Na hata wakija, hawajaribu hata kushambulia uzio; wanapita tu,” Mgemaa aliiambia Mongabay kupitia mahojiano ya simu.
Kwa mujibu wa watafiti hao, matokeo haya ndiyo ya kwanza kuonyesha athari chanya za kimazingira zinazotokana na mkakati wa kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyama wala nyama wakubwa, ambao wana nafasi muhimu katika mifumo ya ikolojia. Wanasema kuwa kupotea kwa wanyama hao katika mnyororo wa chakula kunaweza kusababisha athari za mnyororo ambazo huvuruga mfumo wa chakula na kuathiri afya ya mazingira.

Katika utafiti mwingine uliochapishwa mwezi Januari mwaka huu katika Conservation Science and Practice, Ana Grau, mtafiti mshiriki kutoka shirika la Lion Landscapes, pamoja na Salerno na wenzake, walionyesha kuwa maboma yaliyotengenezwa kwa nyaya za chuma (chain-link) yalipunguza sana mashambulizi ya wanyama wala nyama kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Utafiti huo ulitumia takwimu za kila mwezi kutoka kaya 758 za wafugaji kati ya mwaka 2010 hadi 2016, na kubaini kuwa maboma ya chain-link yalikuwa na ufanisi wa asilimia 94 katika kupunguza hatari ya mashambulizi kwa muda mfupi, na asilimia 60 kwa muda mrefu.
“Tunajua kuwa maboma yaliyoimarishwa yana ufanisi mkubwa katika katika kupunguza mashambulizi ya wanyama wala nyama kwa mifugo, na yanaweza kuwa mojawapo ya zana muhimu katika kupunguza migongano katika maeneo ambayo watu huendesha ufugaji karibu na au ndani ya maeneo yanayokaliwa na wanyama hao,” Salerno anaeleza kwa Mongabay.
“Lakini kutathmini ufanisi wa maboma pekee bila kuangalia kinachoendelea katika jamii jirani zisizo na maboma imara kunaacha ombwe. Swali kuhusu athari za kuenea (spillover effects) za juhudi za kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori, halijajibiwa katika mifumo mingi ambako kazi inaendelea — Je, mikakati ya kupunguza migongano inawasukuma tu wanyamapori kwenda kwenye kaya za karibu na kusababisha migongano huko? Kama ni hivyo, basi hakuna upunguzaji wa jumla wa migongano na athari zake kwa wanyamapori na watu.”
Mwandishi mwenza wa utafiti wa Conservation Letters, Kevin Crooks, ambaye pia ni mkurugenzi wa CSU Center for Human-Carnivore Coexistence, anasema utafiti unaonesha kuwa mbinu za tahadhari zisizo za kifo zinaweza kuwa na mafanikio makubwa katika kuzuia mashambulizi kwa mifugo, na kunufaisha si tu familia inayolengwa, bali pia familia za jirani. CSU Center for Human-Carnivore Coexistence ni taasisi ya utafiti na uhifadhi inayolenga kusaidia maisha ya pamoja kati ya binadamau na wanyama wala nyama kwa njia endelevu.
Kwa mujibu wa Mtandamo, wafugaji wa eneo hilo hupata hasara kubwa za kiuchumi kila mwaka kutokana na wanyama wala nyama. “Kwa kutumia uzio huu, simba, chui na fisi hukatishwa tamaa na hujiepusha na maeneo ambayo wakulima wamejenga maboma imara. Tulipopendekeza wazo hili, baadhi ya wakulima hawakukubaliana mara moja, lakini wengi wao sasa wanajenga maboma haya kwa hiari yao. Wafugaji sasa wanaweza kupata usingizi wa kutosha usiku na kufanya kazi mchana,” Mtandamo aliiambia Mongabay.
Shirika la Lion Landscapes lilifadhili asilimia 75 ya gharama ya ujenzi kwa wakulima waliokubali kutumia maboma haya yaliyoimarishwa. Utafiti unaonyesha kuwa baada ya miaka mitano, faida zilizotokana na kuzuia vifo vya mifugo zilikuwa mara 3 hadi 7 zaidi ya gharama walizotumia wakulima kujenga maboma hayo.
Watafiti wanahimiza kuwepo kwa uelewa wa mwingiliano kati ya wanyama wala nyama na binadamu, kwani mienendo hiyo inaweza kusaidia kuongoza matumizi bora ya rasilimali za uhifadhi na kuleta matokeo chanya kwa binadamu, mifugo, na spishi zilizoko hatarini.

Joseph Kaduma, mwandishi mwenza wa utafiti huo na meneja wa utafiti kutoka shirika la Lion Landscapes, anasema kuwa utafiti huu unatoa ushahidi wa kisayansi kuhusu jinsi maboma yaliyoimarishwa yanavyoweza kuendeleza maisha ya pamoja kwa amani kati ya binadamu na wanyama wala nyama. “Kwa kuonyesha jinsi mbinu zisizo za kuua zinavyoweza kunufaisha watu na wanyamapori, utafiti huu unatoa suluhisho la uhifadhi linaloweza kutekelezwa kwa vitendo na kupanuliwa hadi katika maeneo mengine yanayokumbwa na migongano ya aina hii kote duniani.”
Salerno anapinga wazo la kufunga uzio kuzunguka hifadhi kubwa kama Ruaha, akisema kuwa hilo halitakuwa na ufanisi wa kiuchumi na linaweza kuwa na athari hasi kwa ikolojia kwa kuwa litawatenga wanyamapori, jambo ambalo linaweza kuchochea migongano kati ya jamii na juhudi za uhifadhi katika eneo hilo.
Anawahimiza wahifadhi kutenga rasilimali kwa ajili ya kuweka maboma imara kimkakati, au zana nyingine za kupunguza migongano, kwa kuzingatia athari zake kwa maeneo ya jirani, kwani yanaweza pia kutoa ulinzi kwa kaya ambazo hazijaweka maboma hayo.
“Tunahitaji pia kutambua na kuelewa athari za kuenea kwa mikakati ya uhifadhi kwa muktadha wa mahali na muda kwa upana zaidi. Kukusanya na kuhifadhi takwimu hizi kunaweza kuwa na gharama kubwa, lakini ufuatiliaji huu ni muhimu endapo tunataka kutathmini juhudi za uhifadhi na athari zake kwa viwango mbalimbali, jambo ambalo ni la msingi hasa katika mifumo changamano inayochochea migongano kati ya binadamu na wanyamapori,” anasema Salerno.
Picha ya bango: Simba katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Picha kwa hisani ya Richard Mortel kupitia Wikimedia Commons (CC-BY-2.0).
Marejeo
Salerno, J., Warrier, R., Breck, S. W., Carter, N. H., Berger, J., Barrett, B. J., … Crooks, K. R. (2025). Beneficial spillover effects of Antipredation interventions support human–carnivore coexistence. Conservation Letters, 18(2). doi:10.1111/conl.13085
Grau, A., Salerno, J., Hilton, T., Lowasa, A., Cotterill, A., & Dickman, A. J. (2025). Evaluating the effectiveness of fortified livestock enclosures as a human‐carnivore conflict mitigation tool in Tanzania’s Ruaha landscape. Conservation Science and Practice, 7(2). doi:10.1111/csp2.13299
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 31/03/2025.