- Oktoba 2023, Mongabay ilisafiri hadi Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth nchini Uganda kama sehemu ya mfululizo wa ripoti kuhusu maeneo yaliyohifadhiwa Afrika Mashariki.
- Tukiwa huko, tulisikia madai kwamba askari wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda (UWA)wamewaua washukiwa wa uwindaji haramu.
- Wiki mbili kabla ya ziara yetu, mwanaume mmoja alipigwa risasi na kufa ndani ya hifadhi; ndugu zake na maafisa wa eneo hilo walidai kuwa aliuawa na walinzi wa wanyamapori wakati akijaribu kujisalimisha.
- Madai hayo yanafuatia kashfa nyingine za hivi karibuni zaukiukwaji wa haki za binadamu zinazohusiana na mbinu kali za utekelezaji wa uhifadhi katika Bonde la Kongo lililo karibu.
Hii ni hadithi ya pili katika mfululizo wa Mongabay – Maeneo Yaliyolindwa Afrika Mashariki. Soma Sehemu ya Kwanza hapa.
KITABU, Uganda — Ni saa sita mchana katika sehemu ya Kitabu, mji mdogo ulio kwenye vilima vya magharibi mwa Uganda chini ya milima ya Rwenzori. Mashamba yaliyotunzwa vyema ya maharage na mihogo yako kando ya barabara inayoelekea huko. Wanawake na watoto wadogo wanaonekana wakiwa wamebeba mizigo ya kuni vichwani mwao chini ya jua kali la Oktoba. Chini kabisa, mandhari ya savanna ya kijani kibichi na kahawia inaambaa kwa umbali, na kuenea hadi upeo wa macho ikiwa na maziwa na mito inayomeremeta.
Hii ni mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth, “kivutio maarufu zaidi cha watalii” nchini Uganda, na mojawapo ya mifumo muhimu zaidi ya ikolojia katika Afrika Mashariki. Misitu yake, mabwawa na nyasi vimeenea katika eneo la karibu kilomita za mraba 2,000 (takribani maili za mraba 765). Kuna tembo wa savanna hapa, pamoja na simba ambao hulala kwenye matawi ya miti, nyati, chui, swala, sokwe, viboko, na zaidi ya aina 600 za ndege tofauti. “Malkia,” kama wasimamizi wa mbuga wanavyoiita, ni “mhifadhi wa binadamu na eneo la uhai” la UNESCO – moja ya makazi machache ya wanyamapori yaliyohifadhiwa kwa kiwango hiki ambacho kimebaki barani Afrika.

Shule iliyoko hapa mji wa Kitabusi ya kawaida. Ilianzishwa mwaka 2018 na kundi la waliokuwa wawindaji haramu, na ni moja ya shule chache zilizo karibu na Mbuga ya Malkia Elizabeth ambazo zinapata usaidizi kutoka kwa wafadhili nje ya nchi au, mara kwa mara, kutoka kwa wakala wanaohusika na usimamizi wa mbuga, yaani Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda (UWA). Madhumuni yake ni kusomesha watoto yatima ambao familia zao haziwezi kumudu ada ya shule. Kati ya wanafunzi wanaohudhuria hapa, 63 hawana baba. Kulingana na katibu wa kikundi hicho, Tadeo Kilolo, baba zao waliuawa katika Hifadhi ya Malkia Elizabeth “kwa sababu ya uwindaji haramu.”
Walipoulizwa namna walivyofariki, Kilolo na wanachama wengine wa kikundi hicho, ambao ni pamoja na baadhi ya wajane wa wanaume waliouawa, walisema kumekuwa na ajali katika hifadhi hiyo: mikuki iliyorushwa vibaya wakati wa harakati za kuwinda viboko ilimpata mwenzao mmoja.
Lakini walipobanwa, walinena, macho yao yakiwa yameshuka chini na sauti kutulia, kwamba wengi walifariki katika hali ambazo ni ngumu zaidi – na hatari – kuongea waziwazi. Wengi wao walipigwa risasi hadi kufa katika mbuga hiyo na walinzi wa mamlaka ya UWA.
Kifo Kyondo
Kama sehemu ya mradi wa kuripoti maeneo yaliyohifadhiwa katika Afrika Mashariki, Mongabay ilitembelea Hifadhi ya Taifa ya Malkia Elizabeth mwishoni mwa Oktoba 2023. Tukiwa huko, tulisikia taarifa za walinzi wa UWA wakiwapiga risasi na kuwaua watu walioingia kwenye hifadhi hiyo kinyume cha sheria.
Watu hawa hawakuwa wawindaji haramu wa tembo waliojihami kwa silaha kubwa. Kwa mujibu wa jamaa zao walionusurika, pamoja na vyanzo vingine vya habari kutoka eneo hilo, walikuwa wawindaji wa kujikimu waliotumia mikuki na mitego katika kutafuta aina za wanyama kama swala na viboko kwa ajili ya kula nyumbani au kuuza mitaani. Baadhi ya watu tuliozungumza nao wanasema watu hao walipigwa risasi na kuuawa bila onyo wakati wakijaribu kujisalimisha. Kwa maelezo yote, ghasia hizi mbaya zimetokea mara nyingi katika Mbuga yaTaifa ya Malkia Elizabeth, pamoja na mbuga nyingine nchini Uganda kwa kipindi cha miongo mingi.
Wiki mbili kabla hatujafika katika mbuga hiyo, Tadeo Bwambale, baba wa watoto sita mwenye umri wa miaka 49, aliingia mbuga hiyo usiku akiwa na mbwa wanne tayari kuwinda akiwa na mkuki. Kundi hilo la Bwambale na wenzake lilimfuatilia na kumuua kiboko, na kumchinja papo hapo. Wakiwa wamebeba vifurushi vya nyama za porini kutoka nje ya hifadhi, inasemekana walikumbana na kile jamaa mmoja alichoeleza kuwa ni doria ya pamoja ya askari wa jeshi la Uganda na askari wa mamalaka ya UWA.

Mashuhuda wa tukio hilo wanasema askari waliokuwa doria walilifyatulia risasi kundi hilo la Bwambale na wenzake na yeye alipigwa risasi kifuani mara nyingi na kuuawa, licha ya kuinua mikono juu na kujaribu kujisalimisha. Wengine walikimbia kabla ya kushuhudia kifo chake.
Mauaji ya Bwambale, yaliyoripotiwa kwa jamaa zake na wanachama waliosalia, yalizua kilio katika kaunti ndogo ya Kyondo, inayopakana na Mbuga ya Malkia Elizabeth.
“Kwa kweli tumehuzunishwa sana na kifo cha kijana wetu,” anasema jamaa mmoja ambaye hakutaka kujulikana. “Tumechanganyikiwa kuhusu nani wa kuuliza au kumwajibisha. Serikali imetukatisha tamaa. Hatujui la kufanya.”
Tukio hilo lilitokea wakati hali ya wasiwasi ikiongezeka ndani ya hifadhi hiyo. Siku chache kabla, watalii wawili walishambuliwa na kuuawa na kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF), lenye mfungamano na ISIS ambalo makao yake yako katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wakati wa ziara ya Mongabay, wanajeshi wa Uganda Peoples’ Defence Forces (UPDF) walisambazwa katika mbuga nzima kuwatafuta washambuliaji.
Lakini familia ya Bwambale, pamoja na kiongozi wa eneo la Kyondo, wanasema ni walinzi wa mamalaka ya UWA waliofyatua risasi.
“Lazima nieleze bayana: Wale wanaouawa katika mbuga ya wanyama wanauawa na walinzi hao wa mbuga,” anasema Jovenal Muke, mwenyekiti wa kaunti ndogo ya Kyondo. “Kesi tulizonazo huwa tunapokea taarifa kutoka kwa mamlaka ya hifadhi za taifa wakitutaka twende tukaone miili ya watu waliokamatwa wakifanya uwindaji haramu.”

Mongabay ilikutana na mke wa Bwambale, Frumera Ithungu, na watoto wao katika nyumba ya wanandoa hao kwenye kilima kilicho na miti eneo la juu la mbuga. Karibu na nyumba ya matofali ya kawaida kuna kaburi la zege, lililomwagwa hivi karibuni, ambalo Bwambale alizikwa.
“Alijisalimisha, lakini wakampiga risasi tena,” jamaa huyo anasema. “Walinzi wa mbuga hawatakiwi kuua watu, badala yake wawafunge.”
Wakati wa ziara ya Mongabay nyumbani kwa Bwambale, mashuhuda wa tukio la risasi walikuwepo, lakini walikataa kunukuliwa kwa sababu ya hofu kwamba wangelengwa na serikali.
Familia ya Bwambale inasisitiza kwamba alikuwa na mkuki tu alipouawa, na kwamba hakuna mtu katika kundi lake aliyekuwa amebeba bunduki. Kifo chake, ambacho kilimwacha mkewe na watoto sita wa kulea peke yake, halikua tukio geni.

Kwenye doria
Sajenti Bob Bernard, afisa wa ulinzi wa mbuga wa UWA mwenye umri wa miaka 38, amesimama kwenye uwanja wenye nyasi ndani ya Mbuga ya Malkia Elizabeth, akitoa maelezo mafupi kwa maafisa wengine watatu wa timu yake. Akiwa amevalia sare za kivita za mamalaka ya UWA, huku bunduki aina ya AK-47 ameitundika mgongoni mwake, Bernard anaeleza kuwa leo wataandamana na mwandishi wa habari kwenye doria.
“Katika doria yetu, tunatarajia kuona mambo mengi – wawindaji haramu na pia wanyama,” anasema. “Na tunachofanya kila mara tunapomwona jangili, tunamkamata. Baada ya kumkamata, huwa tunaita timu ya uchunguzi, ambayo inakuja kuchukua washukiwa, ambao wanafunguliwa mashtaka.”
Wakitembea msituni wakiwa katika mpangilio wa kijeshi uliotawanywa, timu ya watu wanne inakagua upeo kwa macho ili kuona wavamizi au wanyama walionaswa katika mitego. Kwa ujumla, kuna walinzi wa wanyamapori 160 waliopewa jukumu la kuendesha doria katika Mbuga ya Malkia Elizabeth, ambao mara nyingi hutumia wiki kadhaa mfululizo katika mojawapo ya vituo 49 vilivyoenea kwenye mbuga nzima.

Huku askari wa wanyamapori wakitembea kwenye tope lenye kina kirefu kwenye kichaka, wanasikia sauti ya mlio wa ghafla kutoka nyuma ya vichaka. Ni kiboko, akiwaonya watu wa nje wasonge mbele. Viboko ni walengwa wanaopendelewa na wawindaji haramu katika mbuga ya Malkia Elizabeth. Nyama yao ni tamu na hupendwa na baadhi ya jamii zilizo karibu na mbuga hiyo, ambazo mila zao za uwindaji zilianza kwa muda mrefu kabla ya sheria za wanyamapori za Uganda.
Hata hivyo, leo, aina yoyote ya uwindaji ndani ya Mbuga ya Malkia Elizabeth ni marufuku kabisa. Hukumu na adhabu za jela kwa wale waliokamatwa zinaweza kuwa ndefu, zaidi ya muongo. Sheria ya Wanyamapori ya Uganda ya mwaka 2019 inaruhusu hukumu ya maisha kutolewa kwa wakosaji. Licha ya hatari hiyo, wawindaji bado huingia kwenye mbuga mara kwa mara. Mpango mkakati wa UWA wa mwaka 2017 wa kukabiliana na uhalifu wa wanyamapori katika Mbuga ya Malkia Elizabeth unasema kwamba mwaka 2015, wastani wa asilimia 40 ya makazi katika maeneo karibu na mbuga yaliwinda nyama ya porini wakati fulani katika mwaka huo.
“Iwapo labda babu alikuwa mwindaji haramu, hiyo inamaanisha hata mtoto wa kiume wa baba huyo atakuwa jangili. Kwa hiyo, unakuta kwamba ipo katika familia,” Bernard anasema. “Siku zote watakuambia kuwa ni utamaduni wao.”
Kamanda wa Bernard, na mlinzi wa mbuga hiyo Pontius Ezuma, anasema wawindaji haramu na wahalifu wengine wanakamatwa na kushtakiwa kwa kukiuka sheria za Uganda. “Mara tu wanapokamatwa, tunaandaa hati za mashtaka na kuwapeleka mahakamani.”

Lakini vyombo vya habari vya Uganda vimejaa ripoti za wawindaji haramu na wafugaji wanaopotea ndani ya mbuga za wanyamapori. Kila mara, inawekwa wazi kwamba waliuawa na walinzi wa mamlaka ya UWA, lakini mara nyingi zaidi maelezo ya “kuuawa wakati wa ujangili” yanachapishwa. Ripoti hizi zimekuwepo kwa miongo kadhaa , na zinaendelea hadi leo.
Mnamo Septemba 2024, walinzi wa mamlaka ya UWA katika Mbuga ya Taifa ya Mlima Elgon, karibu na mpaka wa mashariki mwa Uganda na Kenya, waliripotiwa kumpiga risasi na kumuua mwanafunzi wa shule ya msingi ambaye alikuwa akichanja kuni kinyume cha sheria.
Taarifa za wafadhili zinarejelea vifo vile vile. Maelezo mradi wa ufugaji nyuki eneo la Kitabu yanayoungwa mkono na shirika lisilo la kiserikali la Uingereza yanataja ujangili kuwa “umepunguza idadi ya wanaume katika kijiji hicho.” Mpango wa kudhibiti uhalifu wa wanyamapori wa UWA wa mwaka 2017-2023, uliotayarishwa na mshauri kwa msaada kutoka kwa serikali ya Uingereza, unakubali kwamba “Mamlaka ya UWA inatuhumiwa kuhusika katika kutoweka kwa wanajamii ndani ya mbuga” na kwamba madai hayo yanaweza kuwa na “athari kubwa, na za muda mrefu katika juhudi za kujenga imani na jamii.”

Kwenye tukio moja kubwa lililotokea mwaka 2018, watu wanne walidaiwa kupigwa risasi na kuuawa na walinzi wa mamlaka ya UWA ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Malkia Elizabeth. Vifo hivyo vilizua tafrani katika eneo hilo, na kumshinikiza Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuikemea mamlaka ya UWA hadharani na kuwaita walinzi waliohusika katika ufyatuaji risasi kuwa “wanyama na wapumbavu.”
Miili ya wawindaji haramu haikupatikana tena, na mamlaka ya UWA ilidai kwamba huenda waliuawa na wanyamapori – licha ya mtu pekee aliyenusurika na shuhuda kurejea nyumbani akiwa na majeraha ya risasi.
Katika taarifa ya mtandao wa X kuhusu tukio hilo, Rais Museveni alisema “hatavumilia kupigwa risasi kwa watu binafsi na walinzi wa wanyamapori. Watu wetu wanahitaji kuhamasishwa, sio kuuawa.”
Mongabay haikusikia madai yoyote kwamba Bernard au kitengo chake walihusika katika kutoweka au ukiukaji mwingine wa haki za binadamu. Sajenti huyo wa mamlaka ya UWA anazungumza kuhusu umuhimu wa kuhifadhi wanyamapori wa Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth kwa ajili ya vizazi vijavyo vya Waganda.

Lakini anakubali kwamba uhusiano kati ya jamii karibu na Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth na walinzi wa mamlaka ya UWA umeharibiwa. Yeye na walinzi wengine wanapotembelea miji ya karibu kununua au kunywa bia, anasema, mapokezi mara nyingi huwa ya chuki. Utafiti unaonyesha kwamba walinzi wasiokuwa kazini wanaogopa kula au kunywa katika baadhi ya miji iliyo karibu na mbuga hiyo kwa sababu ya uwezekano wa kupewa sumu.
“Unajaribu kueleza, lakini hawataelewa kamwe,” anasema Bernard.
Walinzi wa mamlaka ya UWA pia wanakabiliwa na vitisho vyao wenyewe. Katika muongo wa kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2012 pekee, walinzi 17 waliuawa wakiwa kazini, kulingana na takwimu za shirika hilo. Lakini mkakati wake wa kupambana na uhalifu dhidi ya wanyamapori unasema kwamba uwindaji wa kibiashara, ambao ndiyo aina ya ujangili unaotokea kwa wingi katika Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth, mara chache hauhusishi matumizi ya bunduki.
Bernard anasema anawahurumia wawindaji haramu, ambao mara nyingi wanasukumwa na umaskini. Lakini kazi yake ni kutekeleza sheria za hifadhi.
“Wanyama hawa ambao tunajaribu kuwalinda, kuna siku utatoka Marekani na kukuta hakuna kitu hapa,” anasema. “Kwa hivyo, sharti tuwalinde wanyama hawa ipasavyo.”

Mashindano ya silaha kwa ajili ya tembo
Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth iko mbali na eneo pekee lililohifadhiwa barani Afrika ambako walinzi wa wanyamapori wanadaiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Uchunguzi wa Mongabay kuhusu mauaji ya afisa wa mamlaka ya UWA unafuatia ripoti za vyombo vingine vya ukiukaji wa haki za binadamu katika mbuga za Bonde la Kongo na kwingineko.
Msingi mkubwa wa madai haya ni mbinu ya ulinzi wa polisi wa eneo ambalo mara nyingi huitwa “uhifadhi wa kijeshi.”
Mamlaka ya UWA ni wakala wa kujitegemea, lakini inafanya kazi kwa karibu na jeshi la taifa, na kwa umbali, mwanachama wa hao wawili kwa hakika hawatofautiani. Wafanyakazi wa shirika hilo wana safu kali ya kijeshi na huvaa sare hata katika makao yao makuu ya Kampala. Mamlaka ya UWA inafanya doria kwenye viingilio na mito ya Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth kwa kutumia boti za makomando wake, inadumisha mtandao wa kukusanya taarifa za kijasusi karibu na mbuga hiyo, na kufanya uvamizi ndani ya vijiji vya jirani kutafuta hifadhi zilizofichwa za nyama ya porini.
Mtindo huu wa utekelezaji wa sheria za wanyamapori una historia ndefu, na watu wanaouunga mkono wanasema ni jibu la lazima kwa mfululizo na mawimbi makubwa ya ujangili ambayo yalikumba bara la Afrika katika miaka ya baada ya uhuru. Kati ya miaka ya 1960 na 1980, mchanganyiko wa ongezeko la mahitaji ya pembe za ndovu duniani na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe iliyolidhoofisha, ilisababisha mazingira ya kikatili kwa tembo wa Afrika Mashariki, kwa vile mauaji ya awali yaliongozwa na wawindaji wa kikoloni wa Ulaya katika karne ya 19 yalivyokuwa.

Huku kukiwa na machafuko ya migogoro ya kikatili kaskazini mwa Kenya na Uganda, matarajio ya utajiri wa haraka kutokana na pembe za ndovu yaliwavutia maafisa mafisadi na wenyeji. Mwishoni mwa miaka ya 1960, magharibi mwa Uganda ilikuwa na tembo wengi na waliuawa kwa makusudi ili kulinda mazao ya eneo hilo. Kufikia katikati ya miaka ya 1970, asilimia 90 ya tembo hao walikuwa wamekufa. Nchi jirani ya Kenya ilipoteza nusu ya tembo wake kati ya mwaka 1970 na 1977, na kufikia mwishoni mwa miaka ya 1980, inakadiriwa tembo watatu walikuwa wakiuawa kwa siku.
Wahifadhi wengi waliamini kuchukuliwa kwa hatua kali ulikuwa njia mwafaka wa kukabiliana na mauaji hayo. Huko Uganda na kwingineko, faida kubwa ya biashara haramu ya pembe za ndovu ilikuwa inachochewa na watu wakubwa katika jeshi na serikali. Mashinani, mauaji hayo mara nyingi yalifanywa na watu waliojihami kwa silaha ambazo zilizidi sana zile za mamlaka za wanyamapori. Wakiwa wamezidiwa nguvu, mara nyingi walilegea, wakakosa uwezo wa kuwazuia.
Mwishoni mwa miaka ya 1980, watu mashuhuri kama Richard Leakey, Mwenyekiti wa kwanza wa Shirika la Huduma ya Wanyamapori la Kenya (KWS), walifanikiwa kuwashawishi wafadhili na taasisi za magharibi kufadhili upatikanaji wa silaha za kisasa na teknolojia ya uchunguzi kwa walinzi wa wanyamapori. Utekelezaji ulizidi kuwa mgumu, na juhudi za walinzi zikaanza kurudishwa nyuma. Mkakati huu wa kutumia mbinu kali zaidi katika maeneo yaliyohifadhiwa ulienea hadi nchi nyingine, ambapo katika baadhi ya matukio uliendana na maslahi ya wakubwa au wenye mamlaka.

Nchini Uganda, uhifadhi wa kijeshi ulifungua njia mpya za ufadhili, lakini pia ulikuwa muhimu kwa kuweka usalama katika maeneo ya mipakani. Mbuga ya Taifa ya Maporomoko ya Murchison ilikuwa inatumiwa kama maficho ya majeshi ya waasi wenye silaha wa Lord’s Resistance Army katika miaka ya 1990, na waasi wa kundi linaloshabihiana na ISIS lilifanya uvamizi wa mara kwa mara katika Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth katika kipindi hicho. Mwaka 1996, Idara ya Hifadhi za Taifa ya Uganda iliunganishwa na Idara yake ya Michezo na Uvuvi, na kuwa wakala mpya wa UWA.
Kutokana na vitisho vya usalama vilivyopo katika mbuga za wanyamapori za Uganda, jeshi kutoka UPDF walipewa jukumu la kuandamana na maafisa wa UWA kwenye doria, kwa ushirikiano ambao uliimarishwa na mkataba wa makubaliano wa mwaka 2005 ulioweka masharti ya ushirikiano kati ya vikosi hivyo viwili. Msimamo wa kijeshi wa mamlaka ya UWA unaweza kuwa ulihalalishwa na mzozo wa ujangili wa tembo wa bara hilo, lakini pia uliipa serikali ya Rais Museveni safu ya wafanyakazi wenye silaha na wenye nidhamu katika mikoa ya mpaka wa Uganda.
“Miundo ya kijeshi inaruhusu Kampala kufanya ufuatiliaji na, kwa njia fulani, kudhibiti mamlaka ya wanyamapori,” anasema Ivan Ashaba, mwanazuoni ambaye amesomea maendeleo na mafunzo ya mamlaka ya UWA.

Ikitazamwa tu kupitia jicho la uhifadhi wa tembo, mamlaka ya UWA na watangulizi wake, ina mafanikio ya wazi na ya kujivunia. Katika miaka ya 1970, kulikuwa na mamia ya tembo waliobaki katika Mbuga ya Malkia Elizabeth. Sensa ya mwisho ya wanyamapori, iliyofanywa mwaka 2018, ilionyesha idadi ya karibu tembo 4,000, na msimamizi wa mbuga hiyo anasema anakadiria ni karibu 5,000 sasa.
Sababu za mabadiliko ni tofauti. Makazi ya watu sasa yanazuia uhamaji wa makundi ya tembo kati ya Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth na Hifadhi jirani ya Taifa ya Virunga nchini DRC, na bei ya pembe za ndovu duniani imepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni. Ezuma, mlinzi wa Mbuga ya Malkia Elizabeth, anasema juhudi za pamoja za serikali kuvunja mitandao ya ulanguzi zimezaa matunda.
“Uhamasishaji mkubwa ulifanyika kwa miaka mingi katika kuwasaka wahalifu hawa wagumu,” anasema. “Tuna kikosi kazi cha taifa kinachoundwa na jeshi, polisi, maafisa wa idara ya uhamiaji, mamlaka ya UWA, maafisa wa forodha, na vyombo vingine vya usalama.”
Sasa, ni nadra kupata mzoga wa tembo ndani ya Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth. Walinzi wa wanyamapori bado wanakutana na wawindaji haramu wengi katika mbuga hiyo. Lakini huwa ni maskini wanaotafuta tu nyama ya pori.
Hatari na malipo
Mwishoni mwa mwezi wa Oktoba, Mongabay ilihudhuria mkutano wa jamii ya eneo la Kitabu, uliofanyika kwenye kibanda kidogo kinachopakana na shule. Zaidi ya watu 24 walijitokeza kuzungumzia vifo vya wanaume kutoka mji huo na maeneo ya jirani mikononi mwa walinzi wa mamlaka ya UWA.
Baadhi ya waliohudhuria ni wajane ambao wanahangaika kutunza familia zao baada ya vifo vya walezi wakuu. Wengine ni watoto wao, watu wazima na vijana katika miaka yao ya ishirini. Kimya kimya, wengine wakibubujikwa na machozi, wanawake hao walielezea madhara makubwa ya mauaji hayo.
“Mume wangu alikufa mwaka wa 2019,” Vera Uziere anasema kuhusu Emmanuel Baluku, ambaye alikuwa na umri wa miaka 45 alipouawa, na kumwachia watoto wanane anaowalea peke yake. “Ninateseka nao nyumbani. Wale waliokwenda naye (mumewe) walirudi na kuniambia kuwa amekufa.”

Katika ofisi ya zamani ya kundi la wawindaji haramu, kuna orodha iliyoandikwa kwa mkono, na yenye majina ya wanaume kutoka mji huo ambao walitoweka ndani ya mbuga hiyo au kuripotiwa kuuawa. Hadi sasa, orodha hiyo ina majina 25. Baadhi ya wanachama wa kikundi hicho waliiambia Mongabay kuwa walihofia kungekuwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi ikiwa wangezungumza na wanahabari.
“Kumekuwa na matukio ya ghasia, lakini hayajaripotiwa,” anasema Edwin Mumbere, mtetezi wa mazingira. “Sababu ni kwamba watu wanahisi kama hawatapata haki. Wanaogopa kwamba wakikabiliana na serikali, hawatashinda, wanajiambia: ‘Nitashindwa, nahitaji raslimali. Ni bora nikubali yaishe.”
Msukumo wa kuingia mbuga kinyume cha sheria kuwinda ni tofauti. Inaeleweka kuwa ni hatari kubwa, lakini kiboko mmoja anaweza kutoa mamia ya kilo za nyama. Baadhi hutumiwa nyumbani, na nyingine huuzwa, na kuwa chanzo cha pesa katika wilaya ambapo Pato la Taifa kwa kila mtu linakadiriwa kuwa Dola za Marekani 44 kwa mwezi.

Jangili mmoja wa zamani anaiambia Mongabay kwamba mchanganyiko wa tamaa ya ladha za kitamaduni na umaskini huwafanya watu kuwinda katika mbuga hiyo, licha ya kujua kuwa ni kinyume cha sheria.
“Ni tamaa ya nyama, pamoja na umaskini na kutokuwa na uwezo wa kujikimu kunatufanya tuazimie kwenda kupata nyama ambayo ni mali ya serikali,” anasema.
Anasema miaka kumi iliyopita, alikuwa akichinja kiboko aliyeuawa, wakiwa pamoja na kaka yake na kundi la wanaume wengine, walipogunduliwa na walinzi wa doria wa UWA. Anaiambia Mongabay kuwa walinzi walianza kuwafyatulia risasi bila tahadhari. Ndugu yake aliuawa, naye akapata jeraha la risasi mguuni. Baadaye guu hilo lilihitaji kukatwa.
“Baada ya kukusanya vipande vya nyama ili kubeba, walinzi wa mbuga hiyo walituona na kutupiga risasi,” anaeleza mwanaume huyo, ambaye pia aliomba kutotajwa jina. “Ndugu yangu alikufa papo hapo.”
Umaskini sio kichocheo pekee cha uwindaji haramu hapa. Tamaduni za uwindaji karibu na Mbuga yaTaifa ya Malkia Elizabeth zilianzia enzi kabla ya ukoloni nchini Uganda. Kwa upande mwingine wa mbuga, wawindaji wa kabila la Banyaruguru hutoa sadaka kwa mungu wa uwindaji kabla ya kila “misheni.” Kuna miiko ya wanyama ambao wanaweza kuuawa na wasiostahili kuuawa, na mikuki ambayo hutumiwa kuwinda bado hutolewa kwa vijana wengine kila wanapooa.
“Bado wanaishi katika njia zao za jadi,” Mumbere anasema kuhusu jamii ya Banyaruguru. “Wanajua baba zao walikuwa wakienda kwenye mbuga ya wanyama kuwinda na kuleta nyama, kwa hivyo wanahisi bado ni jambo la kawaida.”
Vifo vya wanaume hawa huathiri familia nzima, ambao wengi wao tayari wanatafuta kujikimu.
“Baada ya kufa kwake, sasa nahangaika kuhakikisha watoto wanakwenda shule,” aelezea Masika Melda, mjane mwenye umri wa miaka 46, ambaye anasema mumewe aliuawa na walinzi wa mamlaka ya UWA katika Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth miaka kumi iliyopita. “Baadhi yao hawasomi, kwa sababu ninapokwenda kujaribu kutafuta pesa huwa sifaulu. ”

Kuwaelimisha walinzi
Michael Keigwin ndiye mwanzilishi wa Wakfu wa Uhifadhi wa Uganda, shirika lisilo la kiserikali lenye uhusiano wa karibu na mamlaka ya UWA na lenye uwepo mkubwa katika Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth. Keigwin ni mwanajeshi wa zamani wa jeshi la majini kutoka Uingereza na mshauri wa kimkakati wa zamani wa Deloitte, ambaye mjomba wake aliwahi kuwa mlinzi mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Murchison Falls. Katika mahojiano ya simu, alisema hana muda mwingi wa wahifadhi wa jadi.
“Hawana uelewa wowote kuhusu uhasibu. Hawajui lolote kuhusu ukaguzi au usimamizi. Wanajua ni madoa mangapi yako kwenye mende adimu wakati wa msimu wa mvua, lakini hiyo haisaidii sana usimamizi katika mbuga,” anasema.
Kinyume na kile anachokielezea kama wasomi wanaokwenda polepole na mashirika yasiokuwa ya kiserikali ya uhifadhi, Keigwin anapendelea mbinu madhubuti zaidi ya kusaidia walinzi wa mamlaka ya UWA.
“Ninakuja na mtazamo tofauti sana,” anasema. “A, fanya mambo; na B, acha upuzi.”
Pamoja na kuendesha kozi za mafunzo ya haki za binadamu na programu za kupinga ujangili katika mbuga za kitaifa za Uganda, UCF ya Keigwin inapata pesa kutoka kwa wafadhili kama vile Umoja wa Ulaya ili kujenga “vituo vya amri ya operesheni za pamoja” na miundombinu mingine ya walinzi. Mafanikio yake mengine yamekuwa kuunganisha mamlaka ya UWA na wakufunzi wa kijeshi wa Marekani na Uingereza.
“Tuna kozi zisizo na mwisho na wanajeshi wa Marekani na Uingereza, na washauri wengine wanakuja kuwafundisha walinzi – sio jinsi ya kuua watu kwa penseli, lakini jinsi ya kuwa mtaalamu bora, salama, na kuwa na ustadi zaidi katika uwanja huo,” Keigwin anasema.

Wengine, ingawa wanasema kwamba pamoja na mafunzo yanayoongozwa na jeshi la UPDF ambayo ni ya lazima kwa walinzi wapya wa mamlaka ya UWA, kozi hizo huweka wakala katika mkao unaofaa zaidi kwa mapigano kuliko kukabiliana na wawindaji haramu wanaoishi karibu na mbuga za wanyama.
“Tunachokiona kikifanyika katika mafunzo ya kijeshi ya walinzi nchini Uganda, ni kwamba wanatarajiwa kufanya kazi kama wanajeshi,” anasema Esther Marijnen, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Wageningen ambaye anasomea uhifadhi katika Bonde la Kongo. “Hii ni sehemu ya mwelekeo mpana, na tunaona hii ikitokea pia kwenye mpaka katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga kwa mfano.”
Keigwin anafurahia ukosoaji huo, akisema kwamba iwapo mamlaka ya UWA italegea, wanyamapori wa Uganda watapata madhara.
“Ili kuweka hili katika mtazamo, tumepoteza asilimia 70 ya viboko wetu kote Uganda,” anasema. “Sasa ikiwa tutakomesha ujangili huo, sisi ni adui.”
Viboko waliwekwa kwenye orodha ya wanyama walio hatarini kwenye Orodha Nyekundu ya shirika la kimataifa la IUCN mwaka 2016, na baadhi ya vyanzo vinasema idadi yao inapungua nchini Uganda. Lakini kulingana na takwimu za mamlaka ya UWA, kwa ujumla idadi ya wanyama imeongezeka katika Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth tangu mwishoni mwa miaka ya 1980.
Mnamo mwaka 1989, kulikuwa na viboko 2,200 katika mbuga hiyo. Kufikia mwaka 2018, kulikuwa na viboko 5,875.

“Mamlaka ya UWA inajaribu kuzingatia sheria na moja ya tano ya walinzi wanaowahitaji. Hawana uwezo kutoka kwa serikali kufanya kila kitu na kutatua matatizo yote ya jamii,” Keigwin anasema. “Hayo matatizo yanahamishiwa kwa mamlaka ya UWA, kwa sababu, kwa mfano, wanataka kuchukua, nyama nje ya mbuga na kuiuza.”
Mamlaka ya UWA haikujibu maombi mengi ya maoni kuhusu taarifa hii ya Mongabay. Lakini Keigwin, ambaye anafanya kazi kwa ukaribu na wakala huo, anasema hana huruma hata kidogo kwa hoja zinazowachora wawindaji haramu kama waathirika.
“Usiruhusu watu wakuambie kuwa ni makerubi wanaoelea wakipiga soga na chai ya krimu na kahawa,” anasema. “Hapana, nimefanya doria huko. Nimewatazama wakipigana na kuuana. Nimewatazama wakifanya ujangili bila kikomo.”
Anasisitiza kuwa mamlaka ya UWA haina sera ya “kupiga risasi ili kuua”, akisema shirika hilo linatumia “asilimia 99 ya muda wake kujaribu kuhakikisha kuwa hakuna risasi inayofyatuliwa kamwe.”
“Kusudi lao si kwenda kuua watu,” anasema. “Sio, kwa asilimia mia moja.”

Mzunguko wa ghasia
Tukirejea huko Kyondo, mjane na watoto wa Tadeo Bwambale wameketi uani mbele ya nyumba yao ndogo. Kifo cha Bwambale kimewaweka katika hali ya hatari. Bwambale alikuwa na deni alipofariki, na wadai wake bado wanatazamia kulipwa. Sasa, deni hilo – shilingi milioni 1.5, au karibu dola za Marekani 400 – ni jukumu la mjane huyu. Ikiwa hatapata pesa, familia yake itapoteza nyumba yao.
“Hana usaidizi mwingine wowote,” jamaa yake anasema. “Hawana chochote cha kula, kwa hiyo yeye hunywa uji wa mahindi kama chakula chake cha usiku, bila chochote kingine.”
Mauaji yaliyoripotiwa katika Mbuga ya Malkia Elizabeth ni sehemu ya mabadiliko magumu katika uhifadhi wa kisasa, hasa barani Afrika. Wanyamapori wanakabiliwa na vitisho vya kweli, na bila sheria za kuwalinda, spishi fulani zinaweza kuwindwa hadi kutoweka. Lakini mfumo wa utekelezaji uliopo katika maeneo mengi yaliyohifadhiwa mara nyingi huhitaji vurugu kubwa kudumishwa. Kwa miaka mingi, hiyo imekuwa chanzo cha chuki na maudhi dhidi ya uhifadhi katika jamii nyingi karibu na mbuga.

Pia ni mfumo ambao si rahisi kwa walinzi. Mtafiti mmoja ambaye alizungumza na Mongabay kwa sharti la kutotajwa jina anasema amewahoji baadhi ya watu ambao wana ujuzi wa mauaji. Haishangazi, kuwa nyuma ya bunduki kunaweza kuwaacha na makovu ya kisaikolojia.
“Mlinzi mmoja aliniambia kwamba walinzi wanakabiliwa na madhara,” anasema. “Watu hawa unaowaua wanaomba huruma. Kuna maumivu machoni mwao. Wanakuomba. Wanakuuliza, ‘Tafadhali, nisamehe. Angalau nikamate.”
Hadi mabaliko makubwa yatokee, hata hivyo, anasema hatarajii mauaji hayo kukoma.
“Hizi sio kesi za pekee, kwa bahati mbaya,” mtafiti anasema. “Hili ni jambo ambalo limekuwa la kawaida kwa miaka na miaka. Na vile hakuna kinachotokea kwao, hali ya kutojali inaimarika.”
Kwa upande mwingine, miongo kadhaa ya ukatili na ulinzi mkali haujazuia wawindaji haramu wa eneo hilo kwenda kwenye Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth, hata wakijua matokeo mabaya ambayo wanaweza kukabiliana nayo. Hili lenyewe ni shtaka la mbinu ya uhifadhi kwa vitendo hapa – na katika maeneo mengine mengi yaliyohifadhiwa barani Afrika. Pamoja na unyanyasaji wote huu, hakuna uhakika kama mikakati inayowekwa inafanya kazi.
“Alikuwa akiwatafutia watoto karo,” jamaa wa Bwambale anasema, akiwa amesimama mita chache kutoka kwenye kaburi lake. “Unajua, wakati mtu hana chanzo cha mapato, popote panaposemwa kuna pesa ndipo atakwenda.”

Picha ya bango: Frumera Ithungu akiwa ameshikilia picha ya mumewe, Tadeo Bwambale, ambaye sasa ni marehemu. Picha na Ashoka Mukpo wa Mongabay.
Nukuu:
Moreto, W. D., Brunson, R. K., & Braga, A. A. (2016). ‘Anything we do, we have to include the communities’: Law enforcement rangers’ attitudes towards and experiences of community–ranger relations in wildlife protected areas in Uganda. The British Journal of Criminology, 57(4), 924-944. doi:10.1093/bjc/azw032
Ashaba, I. (2021). Historical roots of militarised conservation: The case of Uganda. Review of African Political Economy, 48(168), 276-288. doi:10.1080/03056244.2020.1828052
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 27/03/2025.