- Kundi moja la wataalamu wa mimea wamegundua spishi mpya ya mti wa msitu wa mvua katika Milima ya Udzungwa, Tanzania.
- Takribani miti 100 mikubwa ilipatikana kwenye hifadhi mbili za misitu ya vijiji zilizozungukwa na mashamba yaliyotelekezwa. Tathmini za mwanzo zinaonyesha baadhi ya miti hiyo inaweza kuwa na umri wa hadi miaka 3,000.
- Wataalamu hao wanasema miti hiyo ipo hatarini kutoweka kutokana na idadi yake ndogo na eneo ilipo kuwa finyu.
- Hata hivyo, miti hiyo imepatikana katika eneo linalohusiana na mradi wa urejeshaji wa misitu, jambo linalowapa wengi matumaini kuwa itaendelea kuishi kwa muda mrefu.
Mwanabotania Andrea Bianchi na wataalamu wa mimea wa ndani, Aloyce Mwakisoma na kaka yake, Ruben, walikuwa wakichunguza hifadhi mbili ndogo za misitu ya vijiji katika Milima ya Udzungwa mwaka 2019, walipokutana na miti mikubwa isiyo ya kawaida. Bianchi aliomba ushauri kwa Mwakisoma na kaka yake, lakini hata wao hawakuwa wamewahi kuona miti kama hiyo.
“Huu ulikuwa mshangao mkubwa kwa sababu kama wao hawakuijua (spishi hiyo), basi huenda kulikuwa na kitu cha kipekee kuihusu,” anakumbuka Bianchi.
Kwa sasa miti hiyo imetambuliwa kama spishi mpya na kupewa jina Tessmannia princeps. Inaaminika kuwa baadhi yake huenda ina umri wa hadi miaka 3,000. Bianchi na wenzake walipata takribani miti 100 ya Tessmannia princeps katika Hifadhi za Misitu ya vijiji vya Boma la Mzinga na Uluti. Wamesema kuwa idadi ndogo na eneo finyu la usambazaji vinaweza kuwa vyanzo vya utowekaji wa spishi hiyo.
Jina maalum la spishi hiyo – princeps – linatokana na neno la Kilatini linalomaanisha “wa heshima zaidi” au “mkuu zaidi”, likirejelea matawi yake makubwa yanayopenya juu ya taji la msitu. Miti yenyewe ni mirefu hadi kufikia takribani mita 40 kutoka ardhini, na inapewa nguvu na mizizi yake mikubwa. Miti mingine ya jenasi Tessmannia mara nyingi hupatikana kwenye misitu ya mvua Afrika Magharibi.

Wataalamu hao walipata mti mmoja uliokuwa umeanguka wenyewe na kuchukua sampuli ili kupima uzito wa mbao yake. Ndani ya sentimita moja ya mbao kutoka katikati , Bianchi alihesabu pete 12 hadi 15. Kwa kawaida, miti huweka pete moja kwa mwaka, ikimaanisha kwamba miti hii inaweza kuchukua hadi miaka 15 kuongeza sentimita moja ya kipenyo.
“Hii inaashiria kwamba miti mikubwa inaweza kuwa na umri wa takribani miaka 2,000 hadi 3,000,” anasema Ingawa Bianchi anaonya kwamba kwa kuwa hii ni miti ya misitu ya mvua inayopokea mvua mara mbili kwa mwaka nchini Tanzania, kutathmini umri wake kwa kuhesabu pete si kipimo cha uhakika kila mara.
Timu hiyo sasa inapanga kuchukua sampuli kutoka kwenye moja ya miti hai ili kupata makadirio sahihi zaidi ya umri wake kupitia kipimo cha radiokaboni.
Ikiwa ndiyo safu kubwa zaidi ya milima katika mlolongo wa safu ya milima ya Tao la Mashariki, Milima ya Udzungwa ina makazi ya spishi nyingi – ikiwemo vyura na mimea – ambavyo hupatikana tu katika maeneo madogo kama bonde moja au kipande cha msitu. Inawezekana kuwa miti ya Tessmannia ni michache kwa sababu inahitaji hali maalum inayopatikana pekee katika Bonde la Mngeta, Udzungwa.


Maua ya Tessmannia princeps katika Bonde la Mngeta, Milima ya Udzungwa, Tanzania. Picha na Andrea Bianchi.Kwa bahati nzuri, hifadhi mbili za misitu za ardhi ya vijiji zipo ndani ya uwanda wa Udzungwa, eneo la kilomita za mraba 75 za shamba la zamani ambalo kampuni binafsi ya Udzungwa Corridor Limited, inajitahidi kulirejesha na kulilinda kwa kushirikiana na wamiliki wa ardhi wa eneo hilo. Mradi huu utaunganisha Hifadhi ya Msitu Asilia wa Uzungwa Scarp na Hifadhi ya Msitu Asilia wa Kilombero pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa upande wa Kaskazini-Mashariki.
Arafat Mtui, mhifadhi katika Kituo cha Ufuatiliaji wa Kiikolojia cha Udzungwa (UEMC) kilicho ndani ya hifadhi ya taifa, aliiambia Mongabay kwamba ugunduzi wa spishi mpya kama Tessmannia unatoa msukumo mkubwa wa uhifadhi.
Alitoa mfano wa kinyonga adimu na wa kipekee wa Magombera (Kinyongia magomberae), spishi mpya adimu iliyotambulika mwaka 2009 kutoka katika msitu wa Magombera huko Udzungwa, ambaye alisaidia kuipa nguvu hoja ya kupandisha msitu huo hadhi na kuwa hifadhi rasmi mwaka 2019.
“Wakati spishi mpya zinapotambuliwa, wahifadhi kama mimi hapa UEMC au Kituo cha Udhibiti wa Ikolojia cha Udzungwa, hupewa kipaumbele katika kujifunza ikolojia yao, usambazaji, ukubwa wa idadi yao na vitisho vinavyowakabili, kuhakikisha hatua stahiki za uhifadhi zinachukuliwa,” alisema Mtui.
Picha ya bango: Wataalamu wa misitu wanasema kwa kawaida miti huweka pete moja kwa mwaka, ikimaanisha kwamba mikubwa inaweza kuchukua hadi miaka 15 kuongeza sentimita moja ya kipenyo.
Nukuu:
Bianchi, A., Tomasi, L., Mwakisoma, A., Barbieri, M., & Luke, Q. (2025). Tessmannia princeps (Fabaceae), spishi mpya ya mti wa msitu wa mvua kutoka Milima ya Udzungwa, Tanzania. Phytotaxa, 694(2), 109–118. doi:10.11646/phytotaxa.694.2.1
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 20/03/2025.