- Kwa miaka mingi Ukuta Mkuu wa Kijani (GGW) umekuwa ukisuasua kufikia malengo yake kwa sababu ya kukosa fedha kwaajili ya utekelezaji wa malengo yake na migogoro mbalimbali.
- Ukuta huu wenye lengo la kupambana na kuenea kwa jangwa sasa umepata kasi mpya baada ya programu mahsusi iliyotangazwa mwaka 2021.
- Kupitia program hiyo jitihada zinafanywa kuondoa vikwazo, kuongeza ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali na kutathmini matokeo ya utekelezaji wa juhudi hizo ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kazidata kwenye mtandao.
- Washirika wa utekelezaji wa mpango wa GGW wana matumaini kuwa kuboresha ufuatiliaji wa utekelezaji miradi mbalimbali ya mpango wa GWW utasaidia upatikanaji endelevu wa fedha na hivyo kufikia malengo ya mradi huo wa ukanda wa Sahel.
Mradi wa Ukuta Mkuu wa Sahel (The Great Green Wall in the Sahel), unaojumisha aina mbalimbali za misitu, mashamba na mbuga zilizomo pembezoni mwa jangwa la Sahara, ulianzishwa mwaka 2007 na Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kupambana na ongezeko la jangwa na uharibifu wa ardhi. “Ukuta” huu ambao unaanzia Dakar, upande wa Afrika Magharibi hadi Djibouti upande wa mashariki, kiasi cha urefu wa kilometa 8,000 (maili 5,000) una lengo la kuboresha na kurejesha uoto wa asili katika eneo la hekta milioni 100 (eka 247 milion) za ardhi ambayo imeharibiwa, kutengeneza nafasi za ajira milioni 10, na kuhifadhi tani milioni 250 za kaboni ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2030.
Ingawa kumekuwa na mafanikio ya hapa na pale ya utekelezaji wa programu hiyo katika miaka iliyopita, ucheleweshaji wa fedha, migogoro iliyojitokeza katika eneo hilo na uratibu hafifu, vimechelewesha kukamilika kwa programu hiyo. Ucheleweshaji huo umezua wasiwasi kwamba programu hiyo haitakuwa imefikia malengo yake ifikapo mwaka 2030, ambapo inatakiwa kukamilika. Hadi mwaka 2020, programu hiyo ilikuwa imerejesha takriban hekta milioni 18 (eka milioni 44) na kutengeneza nafasi za ajira 350,000 tu.
Ripoti ya utekelezaji iliyotolewa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Jangwa (UNCCD) ilibainisha changamoto za ziada ikiwemo ufuatiliaji na tathmini hafifu ya mradi huo na kuweka wazi kuwa programu ilihitaji kiasi cha ziada cha dola za Marekani bilioni 33 licha ya makadirio ya awali ya dola bilioni 14 ili kufikia malengo yake.
“Ripoti hiyo ilijaribu kuonyesha mafanikio ya programu ya GGW kwa wakati huo. Huo ndiyo ulikuwa msingi ulioleta taharuki iliyopo sasa kwamba vigezo na vipimo hivyo havipo na inabidi kuvikadiria upya,” anasema Afisa Msimamizi wa Programu hiyo aliyeko UNCCD, Gilles Amadou Ouédraogo,
Kuweka vipimo vipya na kuunda vigezo vipya vitakavyopima utekelezaji wa miradi yote ya GGW, kuanzia kupanda miti na kurejesha uoto wa asili, kutengeneza nafasi za ajira na kuongeza kipato, haya yote yamekuwa kipaumbele cha mradi wa Kuchochea Programu ya Ukuta Mkuu wa Kijani 2021 (Great Green Wall Accelerator in 2021), ukiwemo pia uzinduzi wa Uchunguzi na Usimamizi wa Ukuta Mkuu wa Kijani (Great Green Wall Observatory.)

Uzinduzi wa mradi wa kuchochea utekelezaji wa programu umewavutia wafadhili ambao wametoa dola za Marekani bilioni 19 ili kufidia upungufu wa fedha uliopo na kutatua matatizo mengine yaliyochelewesha utekelezaji wa mradi. UNCCD ndiyo ilipewa jukumu la kufuatilia ahadi za fedha zilizotolewa, kutathmini utekelezaji wa miradi mbalimbali inayohusisha nchi washirika 11 zilizomo katika ukanda wa Sahel na kurejesha kasi ya utekelzaji wa GGW.
“Mradi wa kuchochea utekelezaji wa GGW ni mwitikio wa kutatua matatizo yaliyokuwa yanaukabili. Kwa sasa kuna miradi mbalimbali ya ufuatiliaji ambayo inatuwezesha kuona wazi jinsi programu inavyoendelea,” anasema Ouédraogo.
Meneja Utetezi wa SOS Sahel, Ange Mboneye, anasema kuwa msisimko mpya unaonekana na kutokana na hali hiyo, programu inazidi kutambulika, mawasiliano yameimarishwa huku wafadhili wakivutiwa zaidi na ahadi za kutoa fedha zikiongezeka.


Kuwakutanisha wadau mbalimbali
Baada ya kuanzishwa GGW Accelerator, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuwakutanisha wadau ili kuboresha uratibu wa shughuli zao. Kuanzia mwaka 2022 hadi 2023 ilianza kwa kujenga muungano wa kitaifa katika kila nchi kati ya 11 husika, muungano ambao uliwaleta pamoja watendaji wa serikali, wafadhili mbalimbali, asasi za kiraia, taasisi za utafiti na asasi za kimataifa na kitaifa. Hao walikaa katika ukumbi mmoja na wakala wa utekeleza wa GGW na kutathmini utekelezaji wa kila mradi uliopo chini ya programu ya GGW katika nchi husika.
“Jambo hili lilikuwa muhimu kwani ingawa tulikuwa tukitekeleza programu moja, tulikuwa hatufahamiani. UNCCD imekuwa ikijitahidi kutukutanisha ili tuweze kujadiliana na kuona jinsi gani tunaweza kushirikiana,” anasema Mboneye.
UNCCD pia iliandaa vigezo vya kupima matokeo ya utekelezaji wa kila mradi ili yaweze kufuatiliwa, kupimwa na kulinganishwa. Ouédraogo anasema kuwa kabla ya hapo hapakuwa na utaratibu ulioeleweka na ilikuwa changamoto kutathmini na kufuatilia utekelezaji wa kila mradi kwani vipimo vya utekelezaji na matokeo vilikuwa tofauti.
Kwa sasa utekelezaji wa kila mradi unaweza kufuatiliwa na tunaweza kubaini miradi gani inakidihi viwango na mahitaji, upi haukidhi na tunaweza kufanya maamuzi wapi pa kuelekeza rasilimali ili ziweze kuleta matokeo chanya.
Kutokana na ufuatiliaji unaoendelea, miradi ya asasi za kijamii kama SOS Sahel inaingizwa katika taarifa za utekelezaji wa programu ya GGW, ambayo ripoti iliyotolewa mwaka 2020 haikugusia.

Kuhuisha upatikanaji wa fedha na maendeleo ya programu kwa kutumia takwimu
Muungano wa wadau katika kila nchi ulianza kukusanya takwimu za utekelezaji wa miradi ya GGW. UNCCD ikaanzisha kituo cha kutunza takwimu hizo kupitia mtandao wa Great Green Wall Observatory ambao ulianzishwa mwaka 2024. Hili ni jukwaa kwenye mtandao ambalo hufuatilia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya GGW kutoka kwa wafadhili mbalimbali likiangalia pia maendeleo na matokeo ya utekelezaji wa miradi zaidi ya 350 na kuhakiki hali halisi ya utendaji wa kila nchi kati ya 11 na mchango wake katika kufanikisha malengo ya GGW.
Ufuatiliaj wa takwimu unasaidia kueleza nini kinachoendelea kwa ujumla katika programu yote, anasema, Afisa Mtendaji Mkuu wa Tree Aid, Tom Skirrow, asasi inayofanya kazi kurejesha uoto wa asili na kufuatilia juhudi za kuondoa umaskini katika ukanda wa Sahel.
“Tunataka kila nchi iweze kufuatilia utekelezaji wa miradi yake na manufaa inayopata kutokana na programu ya GGW,” anasema Ouédraogo na kuongeza kuwa uchunguzi na ufuatiliaji vinaweza kuleta rasilimali mbalimbali na kuongeza mwitikio wa kimataifa katika programu ya GGW. “Natamani ifike siku tutakayoweza kuwianisha fedha zote tulizotumia kwa kila heka ambayo tumerudisha uoto wa asili katika programu ya GGW.”
Mongabay ilifanya tathmini ya ubora wa kituo cha kutunzia takwimu na kuona kuwa baadhi ya takwimu hazikuwemo lakini ulikuwa mwanzo mzuri, alisema Skirrow. “Huwezi kupata majibu yanayojitosheleza wakati wote lakini kituo hiki kinakusanya karibu takwimu zote.”


Programu ya GGW yatekelezwa katika maeneo mapya licha ya changamoto zilizopo
Kadiri Programu hii inavyopata kasi mpya ya utekelezaji, ukosefu wa fedha bado ni changamoto hasa kwa watendaji nje ya serikali na asasi za kiraia, anasema Mboneye.
“Wakati mwingine fedha huwa zipo lakini mlolongo wa kuzipata huwa mgumu kwa kuwa taasisi kubwa kama Benki ya Dunia haitoi fedha kwa asasi za kiraia. Tunajitahidi kutafuta fedha kwa kadri tunavyoweza, huku tukianzisha miradi yetu wenyewe,” anasema na kuongeza kuwa inapohusu miradi mikubwa, wafadhili wakubwa hupendelea kufanya kazi moja kwa moja na wakala wa serikali.
Kwa upande wake, Tree Aid hukabiliana na changamoto ya kupata fedha kwa kutafuta masoko ya kaboni. Wakati wa Mkutano wa 16 wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupunguza Kuenea kwa Jangwa (UNCCD’s COP16 ) uliofanyika mjini Riyadh nchini Saudi Arabia mwaka jana, sambamba na Jukwaa la Uchumi Duniani, Tree Aid ilitoa andiko (white paper) juu ya uwezekano wa masoko ya kaboni kuchangia fedha za kuendesha programu ya GGW. Wakati huo ripoti iliyochapishwa mwaka 2020 ilidai kuwa zilihitajika angalau dola za Marekani bilioni 33 ili kutekeleza programu. Lakini kiasi cha dola bilioni 19 tu ndizo zilipatikana mwaka 2021.
Tree Aid inakadiria kuwa GGW ina uwezo wa kuhifadhi tani za ujazo milioni 18 za hewa ya kaboni katika ukanda wa Sahel zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 28, kulingana na soko la 2023.
Endapo utekelezaji wake utatoa kipaumbele kwa jamii, Skirrow anasema kuwa masoko ya hiari ya kaboni yanaweza kuongeza fedha katika utekelezaji wa programu ya GGM na uwekezaji kutoka sekta binafsi, utachochea kurejesha uoto wa asili na kutengeneza nafasi za ajira na hivyo kupunguza umaskini.
Mboneye ana shauku kama hiyo. “Nina matarajio makubwa. Hapa tunaongea kuhusu mamilioni ya watu, kwahiyo lazima tuhakikishe kuwa programu ya GGW siyo maono tu bali ni kitu kinachotekelezeka,” anasema.
Picha ya bango: Wanachama wa ushirika wa Vohoko Est wakiwa na miche ya miti katika kitalu huko Tewaka Burkina Faso. Tree Aid imeanza mradi wa kilimomisitu katika eneo la hekta12,000 ambao unamilikiwa na jamii. Picha na Martha Tadesse wa Tree Aid.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 07/03/2025.