- Katika miaka miwili iliyopita kumekuwa na matukio matatu makubwa ya mauaji ya tai kwa kutumia sumu katika Mbuga ya Serengeti ambayo yamewaua ndege zaidi ya 400.
- Wahifadhi walibaini vifo hivyo kwa kutumia vifaa vya ufuatiliaji kwa njia ya setilaiti, ambapo waligundua ndege waliokatwa vichwa na miguu, ikidhihirisha wazi kuwa mauaji hayo yanahusishwa na ujangili.
- Matumizi ya sumu yanayohusishwa na imani za kishirikina yamesababisha kupungua kwa idadi ya tai katika maeneo mengine ya bara la Afrika, hasa Afrika Magharibi.
- Wataalamu wa uhifadhi wana hofu kuwa mahitaji ya matumizi ya tai kwa imani hizo huenda pia sasa yanaanza kuongezeka nchini Tanzania.
Mwezi Julai mwaka huu, wahifadhi kutoka Bustani ya Wanyama ya North Carolina nchini Marekani na Mfuko wa Grumeti Tanzania walizunguka kumtafuta tai mgongo mweupe katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tai huyo alikuwa amewekewa kifaa cha ufuatiaji wiki mbili kabla. Taarifa za ufuatiliaji zilionyesha kuwa ndege huyo alikuwa amekufa. Timu ya watafiti iliyojumuisha wataalmu kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ilielekea pembezoni mwa kusini-magharibi mwa hifadhi hiyo kwa kutumia magari ya njia za msituni. Walipofika eneo lilipoashiriwa na kifaa cha ufuatiliaji, walikuta tukio la kutisha. Tai 108 walikuwa wamepangwa kwa safu, wakiwa wamekatwa vichwa na miguu.
Kwa mara ya tatu ndani ya miezi 16, tai ambao wapo hatarini kutoweka katika Hifadhi ya Serengeti wameuawa kwa sumu na viungo vyao huenda vimepelekwa kuuzwa kwa ajili ya matumizi yanayohusishwa na imani za kishirikina.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa watafiti kukutana na tukio kama hilo kwa sababu miezi michache kabla ya hapo, ndege 109 walikutwa wameuawa kwa mtindo huo huo karibu na sehemu hiyo. Mwezi Februari mwaka 2023, ndege 200 walikutwa wameuawa pia. Kwa ujumla wake takriban ndege 400 wameuawa kwa mtindo huu na kwa aina hii ya ndege ambao huzaliana mara chache sana, idaid hii ni kubwa mno.
“Mauaji haya ya kutumia sumu yaliwalenga tai tu na wauaji walihakikisha wanachukua vichwa vyote,” anasema Corine Kendall, ambaye ni mtunza kumbukumbu za uhifadhi na utafiti huko Bustani ya Wanyama ya North Carolina, ambapo wataalamu wake wanaongoza mradi wa kuhifadhi tai nchini Tanzania.
Kendall alikuwa mmoja wa wataalamu waliogundua mauaji ya tai katika tukio la mwezi Julai. Akiongea na Mongabay, alieleza kuwa huenda ushirikina ndiyo sababu kubwa ya mauaji hayo ya kijangili. Viungo vya tai hutumika katika kutengeneza dawa za asili. Lakini pia hutumika katika shughuli za kijadi katika baadhi ya jamii nchini Tanzania. Anasema inawezekana kabisa kuwa kuna baadhi ya mauaji ya ndege hao ambayo hayakugunduliwa.

Kendall anasema: “Kama hakuna ndege waliowekewa vifaa vya ufuatiliaji, na hakuna watu wanaolenga kushughulikia jambo hili, basi matukio mengi ya sumu yataendelea kupita bila kugundulika. Tunachokiona Serengeti kinaonekana kuendeshwa zaidi na biashara inayotokana na imani za kishirikina. Hiyo inaonekana kuwa sababu kubwa, na hivyo tunapata wasiwasi sana.”
Matukio yote ya mauaji ya kutumia sumu yalifuata mtindo unaofanana. Mnyama mkubwa kama nyumbu au pundamilia alinaswa kwenye mtego kisha akauawa na kukatwakatwa na kuwekwa kama chambo cha kuwaita tai. Kisha mzoga ukatiwa sumu ambayo askari wa wanyamapori wanadhani ni carbofuran, ambayo ni dawa ya kuua wadudu yenye sumu kali. Dawa hiyo hairuhusiwi kutumika nchini Tanzania na katika nchi nyingine nyingi duniani.
Kukamatwa kwa majangili na waganga wa jadi kufuatia tukio la mwaka 2023 kulithibtisha kuwepo kwa biashara iliyoandaliwa ya viungo vya tai.
Kwa mujibu wa tafiti zilizopita, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni makazi ya takriban tai 10,000 wa aina mbalimbali. Tukio la hivi karibuni la sumu lilitokea katikati ya msimu wa kuzaliana kwa ndege hao. “Kuna wasiwasi kuwa vifaranga vinaweza kuishi kwa kutunzwa na mzazi mmoja tu,” anasema Claire Bracebridge, meneja wa programu na mtafiti huko Bustani ya Wanyama ya North Carolina.

Mwenendo unaoleta wasiwasi
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni moja ya maeneo ya hifadhi yanayotembelewa sana barani Afrika, maarufu kwa makundi makubwa ya nyumbu wanaohama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Hifadhi hii huvutia mamia ya maelfu ya watalii kila mwaka, wakiwa na matumaini ya kuwaona wanyama watano wakubwa maarufu barani Afrika (“Big Five”). Ingawa tai si miongoni mwa wanyama wanaopendwa sana na watalii, wao ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia ya Serengeti.
Ndege hawa husafisha mazingira kwa kula mizoga na kwa kufanya hivyo huondoa bakteria na virusi ambavyo vingewaathiri wanyama wengine.
Kendall anasema kuwa ndege hao wanalo jukumu muhimu huko porini kwa kuwa inakadiriwa kuwa tai na wanyama wengine wa aina yao hula mizoga mingi inayoachwa nyikani kuliko wanyama wawindaji kama samba na fisi.
Katika maeneo mengine, kutoweka kwa tai kunahusishwa na mifumo ya mazingira na athari za kiafya kwa binadamu. Utafiti uliofanywa huko India ulionyesha kuwa kupungua kwa idadi ya tai kulihusishwa na vifo vya watu 500,000 ambavyo vilisanabishwa na ongezeko la virusi kama vile vya kichaa cha mbwa.
Kama ilivyo maeneo mengine ya Afrika , tai walioko Tanzania wanakabiliwa na tishio la kutoweka. Utafiti wa miaka iliyopita uliofanywa na Kendall na timu yake ulionyesha tishio la kuuawa kwa sumu linalowakabili Tai walioko kusini mwa Tanzania hasa katika maeneo ya hifadhi.
Kwa upande wa kaskazini mwa Tanzania ambako Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ipo, spishi za tai walio hatarini kutoweka kama tai mgongo mweupe (Gyps africanus), tai uso-kunjufu (Torgos tracheliotos), na tai Rüppell (Gyps rueppelli) wote wameuawa.
Biashara haramu ya wanyamapori si tishio pekee linalowakabili ndege hawa kutoka kwa binadamu. Tai pia wamekuwa waathiriwa na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hasa wanapokula mizoga iliyowekewa sumu ambayo inakuwa imelenga kuwaua wanyama walao nyama kama simba au fisi.
Hata hivyo, Kendall anasema ushahidi unaonyesha kuwa mahitaji ya viungo vya tai ndiyo sababu kuu ya matukio hayo matatu ya hivi karibuni.
Mganga wa jadi wa kabila la Wasukuma, Deus Sita, aliambia Mongabay kuwa matumizi ya viungo vya tai kama dawa ni jambo la kawaida miongoni mwa watu wanaoishi karibu na Hifadhi ya Serengeti.
“Mahitaji pia yanaongezeka, hasa kutoka kwa watu wa kabila la Kisukuma, ambao ndiyo watumiaji wakuu wa dawa hizi,” anasema Sita.
Mahitaji haya yanachochewa na imani kuwa dawa zinazotengenezwa kwa ubongo na miguu ya tai zinaweza kuongeza kumbukumbu, husaidia kuona mambo yajayo, na kutabiri mikosi. Kwa mujibu wa Sita, kichwa kimoja cha tai, kikikaushwa, kusagwa na kuchanganywa na mitishamba mingine, kinaweza kutumika kutibu hadi watu 300, kwa kuwa kiasi kidogo tu kinahitajika. Vichwa hivyo huuzwa kwa bei ya chini ukilinganisha na dawa nyingine, lakini faida wanazopata waganga wa jadi ni kubwa.
“Matumizi haya yameenea sehemu nyingi za Tanzania Bara,” anaongeza.
Imani hiyo ni miongoni mwa sababu kubwa za kutoweka kwa tai huko Afrika Magharibi.
Sita anasema kuwa hapo zamani alikuwa akitumia sana dawa za kuchanganya na viungo vya tai lakini kwa sasa ameacha shughuli hizo kwani amebadilika na kujiunga na shirika la mazingira la Nature Tanzania.
Anahamasisha na kuchochea ulinzi wa ndege na matumizi ya viloto (Biophytum crassipes), ambao ni mmea mbadala wa viungo vya tai. Shirika hilo lina wanachama wengi wakiwemo 56 ambao ni waganga wa jadi. Kazi yao ni kuielewesha jamii kuhusu hasara ya kuua tai na kutoa taarifa za biashara haramu ya viungo vya Tai katika maeneo yao.
“Nikiwa kama balozi wa kulinda tai, natumia muda wangu mwingi katika kampeni zinaendeshwa na Nature Tanzania. Nayapenda mazingira na nimejikita katika kuwalinda tai.,” anasema Sita. “Ujumbe wangu ni kwamba watu waache kuwaua tai kwa sababu husaidia kusafisha mazingira.”

Kupambana na biashara haramu
Ili kuwalinda tai walioko Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na sehemu nyingine Tanzania ni muhimu kupambana na biashara haramu ya kishirikina. Lakini mwanasayansi kiongozi anayefanya kazi na Mfuko wa Grumeti, George Lohay, anasema kuwa ni vigumu kupambana na biashara hiyo. Mfuko wa Grumeti ni shirika la kuhifadhi mazingira linalofanya kazi katika eneo la Serengeti.
“Majangili wana uwezo wa kupata aina mbalimabli za sumu, tena kwa urahisi kabisa. Lakini eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni kubwa, hali ambayo inafanya iwe vigumu kuwafikia majangili. Zaidi ya hayo matumizi ya sumu na mitego ambayo inaweza kunasa kila aina ya mnyama inakuwa vigumu kwa askari wa wnayama pori na mamlaka nyingine kuwabaini majangili kabla hawajafanya uhalifu,” anaeleza Lohay.
Kwa upande wake, Kendall anasema kuwa wahifadhi wanatakiwa kuielewa vizuri biashara haramu ya viungo vya tai hasa mtandao wake na jinsi inavyoendeshwa.
“Kama ilivyo kwa Afrika Magharibi, tunatakiwa kuielewa kwa undani biashara hii. Tufahamu ni waganga gani wa kienyeji wanatumia viungo vya tai, nani anayenunua na nani anawaua hawa ndege na ni wapi uhalifu huu unafanyika,” anaeleza. “Tukiweza kuchunguza kwa kina vichwa vya Tai vinaishia wapi itakuwa vizuri zaidi. Tujiulize pia, je hivi vichwa vya Tai wa Serengeti vinatumika wapi hapa Tanzania au katika bara la Afrika?”

Mhifadhi anayefanya kazi na Nature Tanzania, Alpha Mfilinge, aliongea na Mongabay na kueleza kuwa kukabiliana na waganga wa jadi kama Sita na kuwapa askari wa wanyamapori zana zitakazowawezesha kuchukua hatua mara kunapotokea mauaji ya tai kwa sumu, kumeleta matokeo chanya.
Anasema kuwa hakuna matukio ya kuuawa Tai kwa sumu katika miezi sita iliyopita katika kumbukumbu za Makao Wildlife Management Area, hifadhi iliyopo kusini mwa Serengeti ambako Nature Tanzania inafanya kazi.
“Lakini ni muhimu kuongeza jitihada hasa katika maeneo ambayo kumekuwa na matukio ya Tai kuuawa kwa sumu. Ongezko la jitihada lazima liende sambamba na kuimarisha usimamizi na mfumo wa sheria ambao unachochea ulinzi na uhifadhi wa Tai,” anasema Mfilinge.
Mongabay iliwasiliana na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA), ili kupata maoni yao juu ya tukio la kuuawa kwa Tai kwa sumu lililotokea mwezi Julai mwaka huu, lakini hakuna majibu yaliyotolewa.
“Ili kukabiliana na tishio la kutoweka kwa Tai, tunahitaji ushirikiano na watu binafsi, mashirika ya uhifadhi, taasisi za serikali na jamii kwa ujumla,”anasema Lohay. “Ni muhimu kuongeza doria katika maeneo ambako kumekuwa na matukio ya mauaji ya Tai na pia kuongeza kampeni za kuwajengea jamii uelewa hasa katika maeneo ya Wasukuma.”
Kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania, ikishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), inaandaa mpango wa kitaifa wa kuwalinda ambao unajumuisha mikakati ya kukabiliana na biashara ya kishirikina.
“Mpango huo umepata ithibati hivi karibuni na utatoa msukumo na kuchochea utekelezaji wa hatua mbalimbali,” anasema Bracebridge anayefanya kazi na Bustani ya Wanyama ya North Carolina. “Na utahakikisha kuna uhusiano na ushirikiano ili kukabiliana na mauaji ya ndege kwa kutumia sumu na kupunguza kutoweka kwa ndege hao ambao idadi yao inazidi kupungua.”

Picha ya bango: Picha tai akiwa ndani ya mbuga ya Serengeti nchini Tanzania. Picha na Adam Cohn, kupitia Flickr (CC BY-NC-ND 2.0).
Nukuu:
Kendall, C. J., Rubenstein, D. I., Slater, P. L., & Monadjem, A. (2017). An assessment of tree availability as a possible cause of population declines in scavenging raptors. Journal of Avian Biology, 49(1). doi:10.1111/jav.01497
Frank, E., & Sudarshan, A. (2024). The social costs of keystone species collapse: Evidence from the decline of vultures in India. American Economic Review, 114(10), 3007-3040. doi:10.1257/aer.20230016
Peters, N. M., Kendall, C. J., Davies, J. G., Bracebridge, C., Nicholas, A., Mgumba, M. P., & Beale, C. M. (2023). Identifying priority locations to protect a wide-ranging endangered species. Biological Conservation, 277, 109828. doi:10.1016/j.biocon.2022.109828
Peters, N. M., Beale, C. M., Bracebridge, C., Mgumba, M. P., & Kendall, C. J. (2022). Combining models for animal tracking: Defining behavioural states to understand space use for conservation. Journal of Biogeography, 49(11), 2016-2027. doi:10.1111/jbi.14483
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 26/11/2024.