- Hekima ya mapokeo ya uhifadhi inasema kuwa ng’ombe wanaofugwa na wenyeji wa kabila la Maasai waliopo Afrika Mashariki wanashindana na wanyamapori katika kutafuta malisho na hivyo kuharibu maeneo yaliyohifadhiwa kama Maasai Mara nchini Kenya na Ngorongoro, Tanzania.
- Hata hivyo, tafiti zilizofanywa katika eneo dogo la Maasai Mara zinaonyesha kuwa makundi ya ng’ombe hayakupunguza malisho wala hayakuharibu mazingira, na wanyamapori hawakuhama kutoka sehemu zile ambazo ng’ombe walikuwa wakila majani.
- Matokeo ya utafiti huo yameibua ukosoaji kutoka kwa watafiti mbalimbali wakihoji njia zilizotumika katika utafiti huo na kudai kuwa ushahidi thabiti unadhihirisha kuwa ng’ombe wasiruhusiwe kuingia katika maeneo ya hifadhi.
- Lakini watoa hoja wana matumaini kuwa matokeo ya utafiti wao yataibua mawazo mapya kuhusu namna ya wafugaji kama Wamasai wanaweza kuwa washirika wa uhifadhi kuliko kuwatenga kama ilivyokuwa kwa miongo mingi.
Kwa kawaida, ngo’mbe wanaofugwa na wanyama wengine kutoka kwenye hifadhi hawachanganyiki na kwa karne nyingi wafugaji wa Afrika Mashariki walikuwa wakitafuta malisho katika mbuga mbalimbali wakipishana na wanyama kama tembo. Siku hizi, maeneo yaliyokuwa hayamilikiwi na watu na yalikuwa yanaonekana kama hayana wenyewe yamekuwa ranchi, mashamba makubwa na hifadhi za taifa ambako ng’ombe hawatakiwi kuonekana.
Kuruhusu ng’ombe kuingia katika maeneo hayo kunaweza kusababisha mifugo kuuawa kwa kuwa nyasi ambazo huliwa na nyumbu au nyati, kwa mfano, sasa zinaliwa na ngo’mbe ambao kwa sehemu kubwa huharibu mazingira na kuwalazimu wanyamapori kuhamia katika maeneo finyu. Hoja hii ina mashiko siyo tu kwa sababu ya sera zilizopo katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, bali pia tafiti zimethibitisha hivyo.
Lakini kikundi kimoja cha watafiti kinasema kuwa kulingana na takwimu na taarifa mbalimbali ambazo wamezikusanya kwa miezi 19 katika Maasai Mara National Reserve nchini Kenya, zinaonyesha sura tofauti. Matokeo ya utafiti wao yaliyochapishwa mwezi Septemba mwaka huu yamesababisha mkanganyiko siyo tu kwa wanaikolojia wanaofanya kazi katika mbuga ya Maasai Mara bali pia kwa makampuni ya utalii.
Ingawa wafugaji hawaruhusiwi kuingiza mifugo yao katika mbuga hiyo, lakini hulisha huko na wakikamatwa hutozwa faini kubwa. Hata hivyo, hawakomi, hasa wakati wa ukame au kipindi cha kiangazi. Matokeo ya utafiti mpya yanaonyesha kuwa mara nyingi wafanyakazi wa MMNR hawajali sana na wanaendelea na shughuli zao.
“Kulingana na taarifa tulizokusanya tumeona kuwa athari zinazotokana na kuingizwa ng’ombe kwenye hifadhi ni ndogo sana kwa maisha ya wanyamapori na ustawi wa mazingira pia,” anasema Bilal Butt, Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani, ambaye alishiriki katika utafiti huo.
Inaonekana kama kuna kutokubaliana lakini kwa vyovyote vile kunaweza kuwa na athari kubwa kwa wafugaji Kusini mwa Mbuga ya Maasai Mara. Katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro nchini Tanzania, kumekuwa na mvutano wa muda mrefu kuhusu haki za ardhi na uhamishaji wa watu kwa nguvu. Wafugaji wa KiMaasai wanaoishi katika eneo hilo wameshtumiwa na maafisa kuwa ni tishio kwa wanyamapori wa Ngorongoro, pamoja na biashara ya utalii wa safari inayochangia mapato makubwa ya eneo hilo.
Butt anasema utafiti wao unaonyesha kile ambacho wafugaji wa kabila la Maasai wamekiongea kwa miaka mingi; kwamba ufugaji wao hauathiri mazingira. “Kwa namna fulani utafiti wetu unatoa mwelekeo chanya wa kisayansi na kutoa haki za kimazingira,” alieleza.

Kuijenga Mara
Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara ni eneo la hifadhi lenye ukubwa wa hekta 151,000 (ekari 373,000) lililopo kusini mwa Kenya, na linajulikana zaidi kwa tukio la kila mwaka la ”Uhamaji Mkuu’’, ambapo zaidi ya nyumbu milioni moja huvuka kutoka Serengeti ya Tanzania, iliyopo upande wa kusini mwa hifadhi hiyo. Hifadhi hii ya Kenya ilianzishwa kwa mara ya kwanza na serikali ya kikoloni ya Uingereza mwaka 1948, na baadaye ikatambuliwa rasmi na serikali mwaka 1976. Mamia ya familia za wafugaji wa KiMaasai walihamishwa ili kupisha uanzishwaji wa hifadhi hiyo, na malisho ya mifugo ndani ya hifadhi yalipigwa marufuku.
Kwa kujumlisha na maeneo ya hifadhi za wanyamapori yanayomilikiwa na yanayopakana na hifadhi hiyo, mfumo wa ikolojia wa Maasai Mara unachukua karibu hekta 300,000 (ekari 741,000).
Zaidi ya watalii 300,000 hutembelea eneo hilo kila mwaka wakitumaini kuwaona wanyama maarufu wanaojulikana kama “Big Five” — simba, tembo, kifaru, chui, na nyati wa Kiafrika — pamoja na duma, twiga, pundamilia na wengine wengi.
Kati ya mwezi Julai na Desemba 2023, MMNR ilikusanya mapato ya zaidi ya dola za Marekani milioni 20 kama kiingilio kwenye hifadhi. Eneo la Talek lipo karibu na Hifadhi ya Maasai Mara na maisha ya wenyeji yanatokana na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo.

“Katika kijiji cha Talek hakuna malisho. Tunategemea kulisha mifugo yetu katika maeneo jirani, lakini sasa wamejenga uzio karibu kila mahali. Hatuna sehemu nyingine ya kupeleka mifugo isipokuwa ndani ya hifadhi,” anasema Calvin Naurori, mkuu wa Jumuiya ya Vijana wa Talek.
Migogoro kwenye uhifadhi
Katika kipindi cha miezi 19 kuanzia mwaka 2018 mpaka 2019 watafiti walitembelea maeneo 60 wakitumia njia tano zilizoanzia Talek kuelekea mpaka wa Maasai Mara National Reserve na kuingia ndani takriban kilometa 17 (maili saba). Walirudi katika maeneo hayo kila baada ya mwezi mmoja na kuchukua sampuli za kinyesi ili kupima ukubwa, ubora wa lishe na aina ya mimea ambayo mifugo ilikula.
“Tulipima ukubwa wa kinyesi, aina ya mimea iliyoko kwenye kinyesi na ubora wa mimea ambayo mifugo ilikuwa imekula,” alieleza Wenjing Xu, mmoja wa watafiti kutoka Senckenberg Biodiversity and Climate Research Centre, Ujerumani. “Tulipima pia hali ya udongo, ubora na mwonekano wake na tulifanya hivyo kila mwezi.”
Walipochunguza sampuli walizochukua, watafiti waligundua kuwa makundi ya ng’ombe hayakupunguza ubora wala wingi wa malisho kwa ajili ya wanyama pori katika Maasai Mara National Reserve. Wala hapakuwa na ushahidi kwamba kulikuwa na wanyamapori waliohama. Kwa kweli wanyama kama swala, pundamilia na nyumbu walikuwa wakipita katika njia zilezile ambamo ng’ombe walikuwa wanapita.
Matokeo ya utafiti huo yanapingana na tafiti nyingine ambazo zinaunganisha ufugaji wa kuhamahama na shughuli nyingine za kibinadamu pembezoni mwa mfumo wa ikolojia ya Serengeti-Mara na kusababisha wanyamapori kuondolewa. Hata hivyo, waandishi wa utafiti huo wanasisitiza kwamba hawatoi tamko la jumla kuhusu kuruhusu ng’ombe kuingia ndani ya hifadhi.
Idadi ya ng’ombe wanaoingia katika Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara bado ni ndogo kwa kiwango cha jumla; walipotembelea maeneo ya sampuli, walikuta ushahidi wa kuwepo kwa ng’ombe kwa asilimia 6, ikilinganishwa na asilimia 70 kwa nyumbu.
Hata hivyo, matokeo haya yanatoa changamoto kwa mtazamo wa kawaida kuhusu Maasai Mara na mandhari nyingine zinazofanana nayo katika Afrika Mashariki.

Wataalamu wengine wa ikolojia waliowahi kufanya kazi katika eneo la Maasai Mara hawakubaliani na matokeo ya utafiti huo na wanayapinga vikali. Katika mahojiano na Mongabay, Robert Buitenwerf, Profesa Msaidizi wa Baiolojia katika Chuo Kikuu cha Aarhus nchini Denmark, alisema, alikuwa “mkosoaji mkubwa sana wa ujumbe waliotoa.” Hivi sasa anashirikiana na wenzake kuandaa majibu rasmi ya kupinga matokeo ya utafiti huo.
“Eneo walilofanyia utafiti huo ni dogo sana kwa kweli,” alisema. “Ukiyajumlisha maeneo yote waliyoyakagua kwa kuhesabu samadi za wanyamapori na mifugo, ni takriban hekta 3 tu (sawa na ekari 7) zilizotumika katika kipindi chote cha miezi 19.”
Buitenwerf alisema uhusiano kati ya ng’ombe na wanyamapori wengine wanaokula majani ni mgumu kuelewa kwa urahisi. Baadhi ya spishi zinaweza kuishi pamoja na ng’ombe, ama kwa kula aina tofauti ya nyasi, au kwa kunufaika na malisho yenye virutubisho zaidi yanayochipuka tena baada ya ng’ombe kula na kuondoka. Lakini spishi nyingine hazipendelei kabisa kuwepo kwa ng’ombe.
“Tunachogundua ni kwamba wanyama wakubwa zaidi, hasa tembo na nyati, hawahitaji chakula chenye ubora wa hali ya juu sana, bali wanahitaji chakula kingi tu. Hutafuta maeneo ya hifadhi za jamii ambako ng’ombe hawaruhusiwi kuingia,” alisema.
Kupitia simu ya video, Buitenwerf alionyesha picha kutoka kwenye setilaiti zinazoonyesha maeneo ya Talek yaliyochunguzwa kupita kiasi, ambako nyasi zilionekana kuwa haba ukilinganisha na hifadhi jirani ya Mara — jambo ambalo, alisema, ni ushahidi kuwa inaweza kuwa hatari kudai kuwa hakuna haja ya kuweka masharti kwa ng’ombe.
“Kuna hatari kwamba watu wanaofanya maamuzi, watunga sera, wanaweza kuanza kufikiri kuwa hili linaweza kuwa wazo jema. Na nadhani hiyo ni hatari kubwa kwa wanyamapori waliopo na mfumo wa ikolojia kwa ujumla,” aliongeza.

Lakini Xu alisema kuwa kuchagua eneo dogo kijiografia kwa ajili ya sampuli haikuwa bahati mbaya kwa sababu hilo ni moja ya vitu vilivyoupa nguvu utafiti huo. Wakati tafiti nyingi za idadi ya wanyamapori katika Maasai Mara hufanywa kwenye maeneo makubwa kwa kutumia ndege au magari ya angani, wao walitaka kujikita kwenye eneo dogo zaidi ili kupata sampuli za kina na kwa usahihi zaidi.
“Tulitaka kufanya kitu tofauti,” alisema. “Na tulilenga eneo dogo, lakini kwa mpango wa uchunguzi wa kina zaidi, kwa kipindi cha muda kilichopangwa kwa umakini, ili tuone kama tutapata matokeo tofauti au sawa.”
Ukweli kwamba matokeo ya utafiti huu yanazua mijadala kuhusu ng’ombe na Maasai Mara, Xu alisema, ni sehemu ya sababu kwanini yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
“Wakati kunapokuwa na hitimisho moja na simulizi yenye mtazamo mmoja, tunapaswa kila wakati kujiuliza, je, kuna upendeleo wowote? Na je, huu ndio ukweli wa kiikolojia ambao tumeamua kuuamini bila kuhoji?”
Eneo ambalo nyati na ngo’mbe huzurura
Idadi kubwa ya wanyamapori hawapatikani Maasai Mara National Reserve bali katika hifadhi zilizopo kaskazini na hifadhi za jamii ambazo ndizo zinaweza kuupa mashiko utafiti wa Butt na Xu. Kulingana na utafiti uliofanywa na World Wide Fund for Nature (WWF), takribani asilimia 84 ya wanyamapori wako kwenye hifadhi za jamii. Kimsingi, wanaruhusiwa kuingiza mifugo yao huko kwa sababu wao ndiyo wanaomiliki ardhi.
“Tunaruhusu wafugaji kulisha ngo’mbe humu katika nyakati fulani za mwaka kutegemea hali ya malisho,” alisema Alistair Nicklin, Meneja wa Hifadhi ya Nabiosho, yenye ukubwa wa hekta 20,200( eka 50,000) ambayo inapakana na Talek kwa upande wa kakazini.
Hifadhi za jamii za Mara ni mpya zaidi kuliko Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara, zikitokana na mageuzi kutoka kwenye “mashamba ya pamoja” takriban miaka 15 iliyopita. Kama sehemu ya fidia kwa kupokonywa ardhi kihistoria, serikali ya Kenya iliwapatia baadhi ya WaMaasai vipande vidogo vya ardhi. Baadaye, waendeshaji wa shughuli za utalii waliwashawishi kuunganisha hati hizo za umiliki na kuziunda kuwa hifadhi za jamii, ambazo sasa zinakaribisha safari za kifahari.
Hifadhi hizi zimekuwa kivutio kikubwa, zikilenga hasa wageni wanaolipa fedha nyingi na ambao hawataki kushindana na watalii wengine katika hifadhi iliyojaa watu.

Kama sehemu ya makubaliano ya upangishaji ardhi waliyoingia ili kuanzisha hifadhi za jamii, baadhi yao huruhusu wamiliki wa ardhi wa KiMaasai kulisha ng’ombe wao — mradi tu wafuate maelekezo kutoka kwa wasimamizi kama Nicklin.
Katika mahojiano ya simu na Mongabay, Nicklin alisema kwamba mwaka jana alipofanya ukaguzi wa idadi ya mifugo katika Hifadhi ya Jamii ya Nabiosho, alihesabu zaidi ya ng’ombe 16,000. Kundi kubwa kama hilo linaweza kuleta athari kwenye mfumo wa ikolojia, lakini anapoona dalili za kuchunguzwa kupita kiasi, huwaambia wafugaji waelekee maeneo mengine. Kwa njia hiyo, alisema, hifadhi hiyo hubaki kuwa na afya njema na salama kwa wanyamapori pamoja na watalii wanaokuja kuitembelea. Jambo muhimu ni kuwa na mpango wa malisho unaoeleweka — ni lini na wapi mifugo inapaswa kwenda.
“Mwaka huu tumepata mvua nzuri, tuko sawa,” alisema Nicklin. “Lakini tayari tumeanza kuona shinikizo katika maeneo ya kawaida ya malisho, ambako rasilimali zimeisha, na sasa wanaomba nifungue maeneo mengine ya hifadhi — na hapo ndipo unapolazimika kusema, ‘Hapana, haiwezekani.’”
Hata wanasayansi ambao hawajakubaliana kabisa na matokeo ya utafiti wa Xu wanakiri kuwa katika hifadhi hizi za jamii, uwepo wa ng’ombe si tu kwamba unavumilika kwa baadhi ya wanyamapori — bali unaweza kuwa na manufaa kwao.
“Mpango wa malisho wa mzunguko ndio msingi wa kuendeleza ushirikiano kati ya ng’ombe na wanyamapori wanaokula majani katika Mara, kwa sababu unazalisha aina mbalimbali za malisho kwao,” alisema Ask Lykke Herrik, mmoja wa wanafunzi wa zamani wa Buitenwerf na mwandishi mwenza wa utafiti kuhusu malisho ya ng’ombe ndani ya hifadhi za jamii.
“Lakini pia ni muhimu kuhakikisha kuwa kuna maeneo yasiyochunguzwa kabisa — maeneo yasiyo na ng’ombe — kwa sababu baadhi ya spishi kama nyati na tembo wanapendelea sana maeneo yenye nyasi ndefu ambazo hazijaguswa.”
Kwa mujibu wa tovuti ya Nabiosho, hata kama kuna malisho ya ng’ombe yaliyo na udhibiti, bado kuna “makundi ya kushangaza ya tembo” katika eneo hilo. “Kwa sasa, katika hifadhi za jamii kuna wanyama wengi — wawindaji na wala majani — ukilinganisha na hifadhi kuu, kutokana na mpango wa malisho,” alisema Naurori wa Chama cha Vijana cha Talek, ambaye pia anafanya kazi na Kenya Wildlife Trust.
Xu alisema kuwa kutokana na historia ya kiikolojia ya eneo hilo ambayo imehusisha wafugaji kwa mamia ya miaka, hali hii haipaswi kuwa ya kushangaza.
“Unapofikiria kuhusu spishi nyingine pori tunazozisoma ambazo ni walaji wa majani, au wala mimea, hazitofautiani sana na ng’ombe katika jinsi zinavyofanya kazi kwenye mazingira,” alisema. “Watu wanapozungumzia uhusiano kati ya spishi pori zinazokula majani, hawaanzi tu kusema ‘hawa ni wabaya.’ Lakini wanapozungumzia ng’ombe, ghafla wanawaona kama kitu cha kigeni.”
Je, inawezekana kuweka mpango wa malisho katika MMNR unaofanana na ule wa hifadhi za jamii, kwa kushirikiana na wafugaji WaMaasai wa Talek? Na je, hilo linawezekana katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki ambako wafugaji hukatazwa kuingia kwenye maeneo yenye nyasi nyingi?
Si sehemu ya makubaliano
Butt alisema kwamba jibu la swali hili halihusiani kabisa na masuala ya ikolojia, bali linahusiana kikamilifu na uchumi wa Mara.
“Kichocheo kikubwa hapa ni kwamba watalii hawapendi kuona ng’ombe,” alisema.
“Hakuna hoja ya kiikolojia inayotumika hapa — hoja inayotumika ni ya mwonekano tu, kwamba ng’ombe wasiruhusiwe kuingia ndani ya hifadhi.
Cha kushangaza ni kwamba katika baadhi ya hifadhi za jamii, unaweza kwenda kwenye safari, ukasimama kuwaangalia ng’ombe wakilisha na hata kupiga nao picha.”

Buitenwerf alisema ijapokuwa ukosoaji wake kuhusu utafiti huo unalenga mbinu iliyotumika, suala la msingi lina uzito wake. “Kunaweza kuwa na athari kwa utalii wa wanyamapori, ambao ni sehemu muhimu sana ya uchumi wa eneo hili,” alisema.
Mvutano kati ya utalii, uhifadhi wa mazingira, na haki za jamii za asili si jambo jipya, lakini kwa sasa umekuwa ukiongezeka nchini Kenya na kwa upana zaidi Afrika Mashariki. Migogoro ya muda mrefu kuhusu ardhi katika hifadhi za Ngorongoro na Serengeti, pamoja na eneo la Laikipia nchini Kenya, inazua mijadala kuhusu nani anayebeba gharama ya uhifadhi wa wanyamapori. Wafugaji wa kuhamahama, ambao kihistoria wamehitaji kusafiri katika maeneo makubwa ili kuishi, mara nyingi ndio wanaojikuta mstari wa mbele kwenye mijadala hiyo.
Kwa kuchukua nafasi ya kati, hifadhi za jamii za Mara hazikosi wakosoaji wala haziko huru kutokana na migogoro. Lakini kwa kuruhusu malisho yaliyodhibitiwa, huenda zinaonesha kwamba kuna uwezekano wa kuleta usawa wa kiikolojia kati ya kulinda wanyamapori na kuendeleza maisha ya WaMaasai.
“Kama tungeisimamia kama hifadhi za jamii, tungekuwa na hifadhi bora kabisa,” alisema Naurori akizungumzia Maasai Mara.
Xu alisema anatumaini kwamba utafiti wao, pamoja na mvutano uliozuka kuuhusu, utasaidia watu kuwaangalia wafugaji wa KiMaasai wa Talek kwa mtazamo mpya, na kutathmini upya mbinu za kuhifadhi wanyamapori wa eneo hilo.
“Siyo tu Afrika Mashariki, bali kote duniani, jamii za wafugaji zimekuwa zikipuuzwa kama washirika wa kweli wa uhifadhi. Katika Mara, na pia katika maeneo mengine mengi, wamekuwa wakifukuzwa kutoka kwenye maeneo ambayo wameyatumia kwa malisho kwa vizazi. Na kuna mifumo ya kihistoria na mielekeo tunayoiona ikirudiwa tena — Amerika Kaskazini, Afrika Mashariki, na Asia ya Kati,” alisema.
“Kwangu mimi huu ni mwanzo tu — kutumia mbinu ya kisayansi ya kiikolojia, lakini kuihusisha moja kwa moja na muktadha wa kisiasa.”
Picha ya bango: Ng’ombe wakiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Amboseli, Kenya, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara. Picha na GRID/Peter Prokosch kupitia Flickr (CC BY-NC-SA 2.0).
Nukuu:
Wachiye, S., Pellikka, P., Rinne, J., Heiskanen, J., Abwanda, S., & Merbold, L. (2022). Effects of livestock and wildlife grazing intensity on soil carbon dioxide flux in the savanna grassland of Kenya. Agriculture, Ecosystems & Environment, 325, 107713. doi:10.1016/j.agee.2021.107713
Crego, R. D., Ogutu, J. O., Wells, H. B. M., Ojwang, G. O., Martins, D. J., Leimgruber, P., & Stabach, J. A. (2020). Spatiotemporal dynamics of wild herbivore species richness and occupancy across a savannah rangeland: Implications for conservation. Biological Conservation, 242, 108436. doi: 10.1016/j.biocon.2020.108436
Xu, W., & Butt, B. (2024). Rethinking livestock encroachment at a protected area boundary. Proceedings of the National Academy of Sciences, 121(38). doi:10.1073/pnas.2403655121
Veldhuis, M. P., Ritchie, M. E., Ogutu, J. O., Morrison, T. A., Beale, C. M., Estes, A. B., … Olff, H. (2019). Cross-boundary human impacts compromise the Serengeti-Mara ecosystem. Science, 363(6434), 1424-1428. doi:10.1126/science.aav0564
Herrik, A. L., Mogensen, N., Svenning, J.-C., & Buitenwerf, R. (2023). Rotational grazing with cattle‐free zones supports the coexistence of cattle and wild herbivores in African rangelands. Journal of Applied Ecology, 60(10), 2154-2166. doi:10.1111/1365-2664.14493
Kirigia, K., & Riamit, K. (2018). Land injustices in Kenya’s wildlife conservancies. Global-e, 11(50). Retrieved from https://globalejournal.org/global-e/october-2018/land-injustices-kenyas-wildlife-conservancies
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 05/11/2024.