- Asasi moja ya kiraia inayofanya kazi na wafugaji wa Kimaasai kaskazini mwa Tanzania inasema juhudi zake za kurejesha uoto wa miti katika eneo la ukame na kuwapatia wakazi mbinu mbadala za kujikimu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuzaa matunda.
- Asasi hiyo inayojulikana kama Tanzania Conservation and Community Empowerment Initiatve (TACCEI) inahamasisha upandaji miti na usimamizi bora wa rasilimali za maji na jamii miongoni mwa wanajamii na pia inawasaidia maafisa wa serikali za mitaa kujumuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika sera na mikakati ya maendeleo.
- Wilaya ya Simanjiro nchini Tanzania ilikumbwa na kipindi cha zaidi ya miaka ishirini cha mvua hafifu kilichoanza mapema miaka ya 2000, ambapo katika kipindi hicho jamii zinazotegemea ufugaji zilishuhudia mifugo yao ikipungua na mingine kufa kabisa.
- Kupitia kusaidia wanajamii kuanza kilimo cha mboga na miti ya matunda, pamoja na ufugaji nyuki na kutengeneza kazi nyingine za mikono, TACCEI inalenga kujenga uwezo wa jamii kuhimili athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi.
Kijiji cha Terrat, ambacho kina wakazi wapatao 14,000 waishio eneo lenye ukame kiasi na misitu ya mikunga katika Ukanda wa Wamaasai, ni miongoni mwa vijiji vingi kaskazini mwa Tanzania vilivyoathiriwa na ukame mkali wa mara kwa mara. Wakazi wa Terrat — wakulima na wafugaji — wanajitahidi kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa msaada wa shirika linalosaidia upandaji miti sambamba na kutoa mbinu mpya za kilimo na fursa za kiuchumi.
Ukame si jambo geni katika wilaya ya Simanjiro, ambako ndiko Terrat ilipo, lakini kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2000, eneo hili la Tanzania lilishuhudia kipindi cha zaidi ya miaka 20 cha upungufu mkubwa wa mvua. Hili lilileta changamoto kubwa kwa takriban asilimia 80 ya wakazi wa Terrat ambao ni wafugaji wanaotegemea mvua kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Terrat, Kone Medukenya, aliiambia Mongabay kuwa kutokana na uhaba wa malisho na vyanzo vingi vya maji kukauka, ng’ombe walidhoofika na wengi kufa, na kwamba ni mbuzi peke yake walioweza kustahimili. Hii ilipunguza chanzo kikuu cha mapato kwa wafugaji. Wafugaji walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta maeneo ya malisho, mara nyingi wakiingia kwenye maeneo ya jamii jirani, jambo lililosababisha migogoro kuhusu rasilimali zinazozidi kupungua.
Ukame pia ulisababisha kupanda kwa bei ya chakula katika sehemu hii ya Tanzania. Bei ya gunia la mahindi la kilo 100 (sawa na pauni 220) ilipanda kutoka dola za Marekani 11 mwaka 2004 hadi dola 66 mwaka 2008, na iliendelea kupanda kwa takriban miaka 10. Kwa mujibu wa wakazi wa Simanjiro, katika kipindi hicho, kuna wakati walilazimika kusafiri zaidi ya kilomita 100 hadi mkoa wa Arusha ili kununua mboga za majani kwa bei nafuu.
“Tulishuhudia hali duni ya maisha kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame, ukosefu wa mvua, uhaba mkubwa wa maji, na upungufu wa chakula na malisho kwa watu wenye mifugo,” alisema Medukenya katika mahojiano kwa njia ya simu. “Tulikosa vyakula vya asili kama mahindi, maharage na nyama, lakini TACCEI imesaidia sana katika eneo letu.”
TACCEI, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake katika kijiji cha Terrat, linaunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uwezo wa jamii wa kustahimili athari zake huko Simanjiro, kwa kuhamasisha upandaji miti, usimamizi bora wa rasilimali za maji na kusaidia maafisa wa serikali za mitaa kujumuisha masuala ya tabianchi katika sera na mikakati ya maendeleo.


Yohana Mollel, Afisa Mshauri wa Jumuiya wa Taasisi hiyo, aliambia Mongabay kwamba kampeni yao ya upandaji miti, ambayo inashirikisha kwa karibu shule za msingi na sekondari katika wilaya ya Simanjiro na wilaya jirani ya Longido, imefanikisha upandaji wa zaidi ya miche 30,000. “Tunapanda aina mbalimbali za miti ya asili, pamoja na miti ya mboga na matunda kama parachichi, limau na machungwa.”
Miti hii husaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo na, inapoendelea kukua, huwawezesha watu kupata kipato cha ziada kutokana na mbao, asali, mafuta ya asili, matunda, dawa za miti shamba na bidhaa nyingine.
TACCEI pia imewasaidia baadhi ya wanajamii kuanzisha mashamba ya mboga ya kibiashara.
“Mpango wao umeboresha sana hali yangu,” alisema Neema Nduya, Mmasai mwenye umri wa miaka 37, ambaye hapo awali alikuwa akiuza kuni ili kuwahudumia watoto wake wanne. “Ninalima mboga, nauza na kupata kipato cha kununulia vitabu, sare za shule na chakula kwa ajili ya watoto wangu. Kupata pesa kumeifanya hali ya maisha iwe rahisi kiasi.”
Shirika hilo pia limewasaidia wanajamii kuanzisha biashara nyingine, kama utengenezaji wa mapambo ya shanga za Kimasai na ufugaji wa nyuki. “Tulitoa dola za Marekani 400 kwa kila kikundi ili kusaidia wanawake wanaoendesha biashara ndogondogo katika kijiji cha Terrat. Tunakusudia kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa mtaji wa kuanzisha biashara mbadala na kuhamasisha watu kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa,” alisema Mollel.
Hata hivyo, mabadiliko haya pia yameleta changamoto. Awali wafugaji walizoea kuachia ng’ombe wao wakizurura kutafuta malisho, sasa mifugo imekuwa ikiharibu mashamba ya wakulima wapya kama Nduya, au kula na kukanyaga miche ya miti iliyopandwa. Baadhi ya wafugaji wenye ng’ombe wengi kupita uwezo wa kuwasimamia mchana kutwa wamelazimika kuwagawia jamaa au marafiki ili wawasaidie kuwatunza.
Kazi ya TACCEI inaongezea nguvu juhudi za maafisa wa ugani wa kilimo wa serikali, ambao nao wanafanya kazi kuwasaidia wakazi wa Simanjiro kukabiliana na hali inayobadilika.
“Tulilazimika kuielimisha jamii kuhusu mabadiliko haya, na kuwafanya watambue umuhimu wa kupanda na kutunza miti kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Petro Mejooli Lukumay, afisa wa kilimo wa serikali. “Kwa kweli wameelewa kampeni hii, na jitihada za upandaji miti zinaendelea kwa kasi.”
Kazi ya TACCEI imeungwa mkono na mashirika kadhaa ya kimataifa, ikiwemo mradi wa GLFx wa Global Landscape Forum, ambao unasaidia juhudi za ndani za kuimarisha sera na kulinda mandhari duniani kote.
Kwa mujibu wa Mollel, shirika hilo tayari limefanikisha kuifanya mandhari ya Simanjiro kuwa na kijani zaidi. Katika kipindi cha miaka 10 ijayo, alisema, anatarajia kuona kuendelea kwa upanuzi wa uoto wa miti, usimamizi bora wa mifugo, na kuimarika kwa njia endelevu za kujikimu zitakazowawezesha wakazi wa Simanjiro kulinda mandhari yao.
Usawa na uendelevu: Kuchukua hatua kurejesha mandhari za Afrika
Mtandao ambao TACCEI ni sehemu yake, GLFx, ni ( mkusanyiko wa miradi huru inayolenga jamii na inayofanya kazi ya kubadilisha mandhari yao na kutetea sera madhubuti). Mtandao huu unalenga kuwaimarisha wachezaji wa ngazi ya jamii kwa kuwapatia maarifa, zana, na mitandao itakayowawezesha kupata matokeo endelevu.
Wanachama wengine wa mtandao wa GLFx wanaofanya kazi barani Afrika pia wamepiga hatua kubwa, ikiwa ni pamoja na nchi za Kameruni ambako urejeshaji wa misitu na vyanzo vya maji unatoa suluhisho endelevu, na nchini Sierra Leone ambako kikundi kimoja kinasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Picha ya bango: Wakazi wa Terrat wakiwa kwenye mafunzo ya ujasiriamali yaliyoratibiwa na TACCEI. Picha kwa hisasi ya TACCEI.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 30/10/2024.